2022
Tumaini la Mtoto Aliyezaliwa
Disemba 2022


Ujumbe wa Urais wa Eneo

Tumaini la Mtoto Aliyezaliwa

Yesu Kristo alitimiza misheni aliyopewa na Baba wa Mbinguni. Yeye anatualika tufuate mfano Wake na tutimize misheni ambayo Baba wa Mbinguni ametupatia.

Mwaka huu uliopita nilipata shangwe ya kuwabeba wajukuu watatu ambao walizaliwa mwaka uliopita. Nikitazama macho yao nilistaajabu juu ya kukosa kwao hatia, usafi na ahadi wanayokuja nayo wakati wanapoanza maisha yao katika ulimwengu huu.

Kuzaliwa kwa mtoto kiuhalisia huleta shangwe na kustaajabu, sherehe na tumaini. Tumaini ni kwamba maisha ya mtoto yataleta fursa na furaha na shangwe tele. Kwa familia na marafiki—hasa wazazi—kuna kustaajabu katika kushuhudia muujiza wa maisha mapya pale mtoto aliyezaliwa anapoanza safari yake ya maisha ya duniani.

Kuzaliwa kwa mtoto wa kifalme kunaleta matarajio ya ziada ya ahadi kwa ajili ya fursa mpya. Watu wa ufalme wanatazamia kwenye utawala endelevu, usioingiliwa wa ufalme. Hili ni kweli hususan kwa mfalme na malkia ambao ni wenye hekima, wakarimu na wanaopendwa na watu wao.

Kwa watu wa ufalme wa Baba wa Mbinguni ajuaye yote, mwenye upendo, tangazo la kuzaliwa kwa Mwana Wake wa Pekee katika mwili lilibeba kustaajabu na tumaini kubwa. Manabii wa kale walitabiri misheni ya Mpakwa Mafuta huyu, Mtoto huyu wa Ahadi, Masiya huyu, Mwokozi na Mkombozi huyu wa ulimwengu, mtoto Yesu Kristo:

“Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani” (Isaya 9:6).

Malaika walitangaza usiku wa kuzaliwa Kwake: “Kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote.

“Maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana . . .

“Atukuzwe Mungu juu mbinguni, Na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia” (Luka 2:10–11, 14).

Mtoto Yesu alikuwa na ahadi tele na alileta tumaini kubwa kwa ulimwengu kwa kuzaliwa Kwake. Na Yesu Kristo hakika alitimiza misheni Yake takatifu.

Misheni hiyo ilikuwa nini hasa? Yesu Kristo mwenyewe alishiriki misheni Yake:

“Mimi ni nuru na uzima wa ulimwengu; na nimekunywa kutoka kwa kikombe kichungu ambacho Baba amenipatia, na nimemtukuza Baba kwa kujivika dhambi za ulimwengu ambamo ndani yake nimevumilia mapenzi ya Baba katika vitu vyote kutoka mwanzo” (3 Nefi 11:11).

“Tazama, nimewapatia injili yangu, na hii ndiyo injili ambayo nimewapatia—kwamba nilikuja kwenye ulimwengu kufanya mapenzi ya Baba, kwa sababu alinituma.

“Na Baba yangu alinituma ili nipate kuinuliwa juu kwenye msalaba; na baada ya kuinuliwa juu kwenye msalaba, kwamba ningeleta watu wote kwangu, kwamba kama nilivyoinuliwa juu na watu, hata hivyo watu wainuliwe juu na Baba, kusimama mbele yangu, na kuhukumiwa kwa vitendo vyao, ikiwa vitakuwa vizuri au ikiwa vitakuwa viovu” (3 Nefi 27:13–14).

Alikuja kufanya mapenzi ya Baba.

Kwa kuongezea kwenye kufanya mapenzi ya Baba kama ilivyoelezwa kwenye mistari iliyotangulia, ni kipi kingine Kristo alifanya?

Aliwaponya wengi ambao miili yao ilikuwa na magonjwa, imevunjika au imekufa.

Aliiinua mikono iliyolegea na kuwaimarisha walio dhaifu.

Aliwafukuza pepo wachafu na kuwaweka huru wengi waliokuwa kwenye kifungo cha dhambi.

Alifundisha kweli za milele kwa wafuasi Wake.

Na wakati ulipowadia wa Yeye kukamilisha moja ya sehemu muhimu kabisa ya misheni Yake, uchungu wa Gethsemane, maumivu ya kusulubiwa Golgotha na ushindi juu ya kifo kupitia ufufuo, Yeye kwa ujasiri aliwaambia wafuasi Wake: “je! Kikombe alichonipa Baba, mimi nisikinywee?” (Yohana 18:11).

Kama wafuasi wa Yesu Kristo na watu wa ufalme Wake, je, tunafuata mfano wa Kristo wa kukinywea kikombe ambacho Baba yetu wa Mbinguni ametupatia, kila mmoja binafsi tukitenda mapenzi Yake, hata ikiwa kile tulichoamriwa kufanya ni kigumu? Unapozingatia ni zawadi ipi unaweza kumpa Kristo mwaka huu, ninakusihi utimize misheni ambayo Baba wa Mbinguni amekupatia.

Katika msimu huu wa mwaka tunaposherehekea kuzaliwa kwa mtoto Yesu, Mwokozi wa Ulimwengu, tunaweza kuwa na tumaini kubwa katika maisha yetu. Kristo alitoa mfano mkamilifu kwa wanadamu wote pale kwa ujasiri alipotimiza misheni Mungu aliyomtuma aitimize. Kwa sababu Yake, tunaweza hakika kutamka maneno, “Shangwe kwa ulimwengu, Bwana amekuja; Dunia na impokee Mfalme wake!”1

Ninashuhudia kwamba Yesu Kristo ni Mwana Pekee wa Mungu katika mwili, mtoto aliyezaliwa asiye na hatia kama vile kila mmoja wetu. Yeye aliishi maisha yenye ukamilifu. Alisulubiwa na alifufuka. Yu hai leo na anatualika tuje Kwake Naye atatuponya na kutubadilisha ikiwa tunamtumaini Yeye na kumfuata Yeye.

Muhtasari

  1. “Shangwe Kote,” Nyimbo za Dini, na. 113.

Chapisha