2022
Uzinduzi wa Mkutano wa KNV katika Eneo la Kati la Afrika
Disemba 2022


Habari za Eneo

Uzinduzi wa Mkutano wa KNV katika Eneo la Kati la Afrika

Takriban vijana 700 na vijana wakubwa waseja 80 kutoka Nairobi, Kenya walifurahia siku tano za madarasa, ibada fupi na shughuli.

Kuanzia tarehe 4 hadi 8 Julai 2022, Eneo la Kati la Afrika la Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho lilifanya mkutano wake wa kwanza wa Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana (KNV). Mkutano huu wa ufunguzi ni wa kwanza katika mfululizo wa mikutano ya KNV iliyopangwa kufanyika kwenye eneo. Dhima ya mkutano ilikuwa “Mtumaini Bwana” kama inavyopatikana kwenye Mithali 3:5–6.

Waliohudhuria mkutano walikuwa vijana 695, vijana wakubwa waseja 77 na wanandoa watatu waliokuwa wakisimamia mambo yote pamoja na vikao. Mkusanyiko wa wazungumzaji ulijipanga katika mstari kutoa mahubiri yenye kuzungumzia masuala mbalimbali yenye athari kwa vijana.

Mikutano ya KNV ni matukio ya siku tano yanayojumuisha shughuli, ibada fupi na madarasa yanayokusudiwa kuwasaidia vijana kuimarisha imani yao katika Yesu Kristo na kutoa fursa kwa vijana kukua kiroho, kijamii, kimwili na kiakili. Mikutano ya KNV imekuwa ikifanyika kwa wingi nje ya Marekani na Kanada kwa miaka kadhaa na imekuwa ikiandaliwa kwa kuzingatia mikutano ya Mahususi kwa Vijana (EFY) ya Chuo Kikuu cha Brigham Young. Katika Eneo la Kati la Afrika, vijana kutoka Nairobi Kenya walipata nafasi ya kupata uzoefu wa tukio hili la kuvutia ambalo liliahirishwa baada ya mlipuko wa UVIKO-19. Nchi zingine ndani ya eneo zitakuwa na mikutano yao hivi karibuni.

Kaka na Dada Mukasa, wanandoa waongoza vipindi wa KNV walifafanua malengo ya mkutano, walitoa maana halisi ya dhima na waliwaalika vijana kuchangamana, kuburudika na zaidi ya yote kuinuliwa kiroho.

“Vijana wanapopitia KNV, tunatumaini kwamba wanaimarisha imani yao kwa Mwokozi wetu Yesu Kristo na wanaweza kufahamu kwa uhakika kwamba daima wanaweza kumtumaini Bwana,” alisema Dada Eunice Mukasa.

Washiriki walikuwa ni pamoja na Kaka na Dada Badu, Kaka Carlos na Dada Harlaine, Kaka na Dada Mukasa, Vijana 695 na washauri 77 chini ya uongozi wa Kaka Hillary Okoth na Dada Cynthia Trinity. Wazungumzaji waalikwa walikuwa ni pamoja na Dada Emma Mbithi, Dada Lilian Odiero, Kaka na Dada Andika pamoja na Kaka Erick Onyango. Kutoka kwenye kibanda cha Family Search, tulikuwa na Mzee na Dada Spackman, Mzee na Dada Staffler pamoja na Kaka Robert Opiyo.

Tukio la kilele cha mkutano lilikuwa ni ibada fupi maalum kutoka kwa Mzee na Dada Sitati. Dada Sitati alishiriki na vijana uzoefu wake akiwa kama kijana ambapo aliweza kushinda majaribu kwa kuwa mtiifu na kuwa imara katika kutii amri, alishiriki jinsi ambavyo mara kwa mara alikimbia zaidi ya km 3 wakati alipotumwa na wazazi wake na kama vile Nefi hakulalamika. Aliwaalika vijana kuwa wasafi kimwili, majasiri na watiifu katika kutii amri za Mungu akiweka msisitizo kwenye sheria ya usafi wa kimwili.

Mzee Sitati alisisitiza umuhimu wa kutumia haki ya kujiamulia kuchagua yaliyo mema, kwani kufanya hivyo huleta usalama wa nafsi. “Amri zote za Mungu zimekusudiwa kulinda furaha yako ya milele ambayo hujumuisha kuwa na amani duniani, Mungu amekuachia uchague, usidanganywe, fuata maandiko, wafuate viongozi, mfuate nabii, wafuate wazazi na hutaongozwa kufanya makosa au kuvunja sheria ya usafi wa kimwili”. Alihitimisha kwa kuwaomba vijana waepuke udanganyifu, wawe imara na majasiri ili waweze kuitunza sheria ya usafi wa kimwili.

“Haki ya kujiamulia ni nguvu ya kuchagua, Moroni 7:12–17 inafundisha kwamba vitu vyote vilivyo vizuri vinatoka kwa Mungu. Tafadhali kumbukeni andiko hili na mlitumie wakati mnapokuwa kwenye mashaka.”

Chapisha