2022
Masomo ya Krismasi
Disemba 2022


Ujumbe wa Kiongozi wa Eneo Husika

Masomo ya Krismasi

Krismasi Hii, fungua muujiza wa kuzaliwa kwa Yesu Kristo kwa kutafakari umuhimu wake kwako na kwa familia yako.

Mwezi Desemba upo mbele yetu na ni msimu ulioje wa kusherehekea. Watoto wanaonekana kuwa na tabasamu mwanana na wingi wa mapenzi mema hupenya anga. Hakika ni msimu wa kuwa na furaha. Kama wewe, mimi na Dada Arden tunaipenda Krismasi na shangwe ya msimu huo. Kuna miti ya kupendeza iliyopambwa ya Krismasi ya kuweza kutazamwa, mapambo ya kumetameta yakipendezesha maduka, taa zikimetameta na viitikio vya nyimbo za Krismasi vikijaza nyumba, mioyo, masoko na maduka makubwa. Sijaishi Afrika ya Kati kwa muda wa kutosha kufahamu ni chakula gani kitaandaliwa wakati familia zinapokusanyika kusherehekea, lakini ninajua itakuwa yenye kupendeza.

Lakini hebu ngoja! Vipi kuhusu Kristo wakati wa Krismasi? Mwokozi pamoja na misheni yake ya Kimasihi ndiyo mawe ya msingi ya maana ya kweli ya Krismasi na kwa hivyo lazima tuhakikishe kwamba mapambo na taa za kumetameta havizuii nafasi Yake. Nimejiuliza ni nini zaidi tunaweza kufanya ili kukumbuka kwamba ‘Kristo ndiye sababu ya msimu wa Krismasi.’ Hapa kuna mawazo rahisi matano ambayo yanaweza kukusaidia.

  1. Kabla ya kusherehekea vyakula vya kifahari Siku ya Krismasi, ninashauri uikusanye familia yako ili kusherehekea hadithi ya Krismasi kama ilivyosimuliwa katika sura ya pili ya Luka. Kabla ya zawadi ndogo lakini za thamani kufunguliwa, fungua muujiza wa kuzaliwa kwa Kristo kwa kusoma na kutafakari umuhimu wake kwako na kwa familia yako.

  2. Kumbuka kwamba maisha ya Kristo yalikuwa ya huduma kwa wengine. Msimu huu wa Krismasi ungekuwa wakati unaofaa kuwahudumia wengine katika njia ambazo huonesha upendo kwa wengine kama vile Yeye alivyoonesha upendo Wake kwa ajili yetu. Fikiria furaha inayoletwa na mafunzo yanayopatikana pale mtoto anapokuwa Santa wa siri kwa marafiki na majirani. Bado ninaweza kusikia shangwe za furaha pale watoto wangu wadogo walipoonesha matendo ya siri ya huduma kwa kuweka biskuti, matunda au kadi zilizotengenezwa nyumbani kwenye mlango wa mtu aliyehitaji upendo.

  3. Mimi si mwimbaji mzuri, lakini ninapenda shairi lililoandikwa vizuri. Nyimbo za Krismasi kiuhalisia ni kama shairi lililowekwa kwenye muziki, hivyo ikiwa huwezi kuimba, furahia shairi. Pia kuna masomo ya thamani ya Krismasi yanayoweza kupatikana wakati familia, matawi na kata zinapokusanyika pamoja kuimba nyimbo za kusifu na kuabudu za Kristo. Na ikiwa wewe si mwimbaji mzuri, bado ni sawa tu kuimba!

  4. Usipuuzie masomo ya Krismasi yanayopaswa kufunzwa wakati unapopamba mti mdogo au pengine chumba katika nyumba yako. Nyota ni ishara ya nyota mpya ambayo iliwaongoza mamajusi (ona Mathayo 2:2), taa ndogondogo hutusaidia kukumbuka kwamba Kristo ni nuru ya kweli (ona Yohana 1:9) na ndiyo, kuna malaika (ona Luka 1:26) ambaye alitangaza ujio wa kuzaliwa kwa Mwokozi.

  5. Na bado somo lingine la Krismasi ni zawadi ya utoaji. Zawadi kuu ya Kristo kwetu ni uwezekano wa uzima wa milele uliopatikana kupitia Upatanisho Wake Usio na Mwisho ambao ulianzia Gethsemane, ukaendelea msalabani Kalvari na kufikia ukomo wakati alipoyatoa maisha yake kwa hiari na alifufuka ili kwamba sisi, kaka Zake na dada Zake wa kiroho, tuweze pia kufufuka na kuishi tena.

Masomo ya Krismasi na yafundishwe na kueleweka vyema msimu huu wa Krismasi.

Krismasi njema kwa kila mmoja wenu.