“Februari 19–25: ‘Ee Jinsi Gani Ulivyo Mkuu Mpango wa Mungu Wetu.’ 2 Nefi 6–10,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani: Kitabu cha Mormoni 2024 (2024)
“Februari 19–25. 2 Nefi 6–10,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2024 (2024)
Februari 19–25: “Ee Jinsi Gani Ulivyo Mkuu Mpango wa Mungu Wetu”
2 Nefi 6–10
Ilikuwa takribani miaka 40 tangu familia ya Lehi itoke Yerusalemu. Walikuwa katika nchi ngeni, umbali wa nusu ya dunia kutoka Yerusalemu. Lehi alikuwa amefariki na uzao wake ulikuwa tayari umeanza kile ambacho kingekuwa vita vya karne nyingi kati ya Wanefi—“wale ambao waliamini katika maonyo na ufunuo wa Mungu”—na Walamani, wale ambao hawakuamini (2 Nefi 5:6). Yakobo, ambaye alikuwa kaka mdogo wa Nefi na sasa akiwa ametawazwa kama mwalimu kwa Wanefi, aliwataka watu wa agano wafahamu ya kwamba Mungu kamwe asingewasahau, kwa hivyo nao kamwe hawakupaswa kumsahau Yeye. Huu ni ujumbe ambao hakika tunauhitaji hivi leo (ona Mafundisho na Maagano 1:15–16). “Hebu tumkumbuke, … kwani hatujatupiliwa mbali. … Kubwa ni ahadi za Bwana,” Yakobo alitamka (2 Nefi 10:20–21). Miongoni mwa ahadi hizo, hakuna iliyo kubwa kuliko ahadi ya “upatanisho usio na mwisho” ili kushinda mauti na jahanamu (2 Nefi 9:7). “Kwa hivyo,” Yakobo alihitimisha, “changamsheni mioyo yenu”! (2 Nefi 10:23).
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Nyumbani na Kanisani
Bwana ni mwenye rehema kwa watu Wake na atatimiza maagano Yake.
Ili kuwasaidia watu wake waelewe kwamba walikuwa sehemu ya nyumba ya Israeli na kwamba wangeweza kumtumainia Mungu na ahadi Zake, Yakobo alinukuu unabii wa Isaya, ulioandikwa katika 2 Nefi 6–8. Ujumbe huo ni kwa ajili yako pia, kwa sababu Watakatifu wa Siku za Mwisho pia ni sehemu ya watu wa agano wa Mungu. Wakati ukisoma milango hii, fikiria kuhusu maswali kama yafuatayo:
-
Ninajifunza kipi kuhusu upendo wa ukombozi wa Mwokozi kwangu mimi? Je, ni maneno yapi au virai vipi vinaelezea upendo huu vizuri zaidi?
-
Je, Mwokozi anatoa nini kwa watu wanaomtafuta Yeye?
-
Ninaweza kufanya nini ili kwa uaminifu zaidi “nimngojee” Mwokozi na baraka Zake zilizoahidiwa?
Yesu Kristo huniokoa kutokana na dhambi na kifo.
Njia mojawapo ya kuongeza shukrani zetu kwa Yesu Kristo ni kufikiria kuhusu nini kingetokea kwetu bila Yeye. Unaposoma 2 Nefi 9:1–26, zingatia kuorodhesha au kupaka rangi ya aina moja kwenye kile ambacho kingetokea kwetu bila Upatanisho wa Yesu Kristo. Kisha, kwa orodha nyingine au rangi tofauti, unaweza kuwekea alama kile tunachoweza kupata kupitia Upatanisho wa Mwokozi. Kulingana na kile ulichokisoma, ungeelezeaje sababu ya sisi kuhitaji Upatanisho wa Yesu Kristo? Je, ulipata kipi ambacho kilikusukuma kusifu “hekima ya Mungu, huruma zake na neema yake”? (2 Nefi 9:8).
Kama ziada kwenye kufundisha Yesu Kristo alituokoa kutokana na kipi, Yakobo pia alitoa utambuzi kuhusu jinsi Mwokozi Alivyotuokoa. Zingatia kuandika kile ambacho unakipata katika 2 Nefi 9:11–15, 20–24.
Yakobo alishangazwa sana na mpango wa Mungu wa ukombozi kiasi kwamba alisema “Ee jinsi gani ulivyo mkuu mpango wa Mungu wetu.” Tazama mshangao wake katika 2 Nefi 9 (zaidi inapatikana kwenye mistari 8–20). Je, unajifunza kipi kutoka kwenye mistari hii kuhusu mpango wa Mungu? Je, ni uzoefu upi umekusaidia uhisi kiasi fulani cha kile ambacho Yakobo alikihisi? Kama sehemu ya kuabudu na kujifunza, zingatia kutafuta wimbo wa dini ambao ungeweza kuelezea jinsi ambavyo unahisi kuhusu Yeye, kama vile “How Great Thou Art” (Nyimbo za Dini, na. 86).
Ona pia “Where Justice, Love, and Mercy Meet,” “Jacob Teaches of the Resurrection” (videos), Gospel Library; Mada za Injili, “Upatanisho wa Yesu Kristo,” Gospel Library.
Upatanisho wa Mwokozi hauna mwisho.
Je, ungeweza kufanya nini ili kuweza kuelewa vyema upatanisho wa Mwokozi “usio na mwisho”? (2 Nefi 9:7). Pengine ungeweza kutazama au kufikiria vitu ambavyo vinaonekana kutokuwa na kipimo kwa idadi—nyasi katika kiwanja, chembe za mchanga kwenye ufuko wa bahari au nyota katika anga. Ni kwa jinsi gani Upatanisho wa Mwokozi hauna kipimo? Ni kwa jinsi gani upatanisho huo ni binafsi pia? Ni virai gani katika 2 Nefi 9 vinakusaidia uwe na shukrani za dhati kwa ajili ya kile Mwokozi alichofanya kwa ajili yako?
Ninaweza kuja kwa Kristo na kufuata mpango wa Mungu.
Katika 2 Nefi 9, Yakobo alitumia virai viwili vyenye nguvu na vinavyotofautiana: “mpango wa huruma wa Muumbaji mkuu” na “mpango ule wa hila wa yule mwovu” (2 Nefi 9:6, 28). Pengine ungeweza kuchora njia na kuipa jina Mpango wa Baba wa Mbinguni. Kisha soma 2 Nefi 9:27–52. Tafuta maonyo na mialiko ambayo Yakobo aliitoa ili kutusaidia sisi tufuate mpango huu. Andika kile unachokipata pembeni mwa njia hiyo. Je, Shetani anajaribu kwa namna ipi kutuweka mbali na mpango wa Mungu? Je, unahisi msukumo wa kufanya nini ili kuitikia maonyo na mialiko ya Yakobo?
Dhabihu ya Yesu Kristo inaweza kuniletea shangwe.
Ujumbe wa Yakobo ulikuwa wa shangwe. “Nawazungumzia vitu hivi,” alisema, “ili kwamba mshangilie, na muinue vichwa vyenu juu milele” (2 Nefi 9:3). Unaposoma 2 Nefi 10:20, 23–25, ni kipi unakipata kinachoufurahisha moyo wako? Utafanya nini ili kukumbuka vitu hivi wakati unapohisi kuvunjika moyo?
Ona pia Yohana 16:33; D. Todd Christofferson, “Shangwe ya Watakatifu,” Liahona, Nov. 2019, 15–18; “Jacob Encourages the Nephites to Be Reconciled with God” (video), Gospel Library.
Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto
Yesu Kristo ni Mwokozi wangu.
-
Unawezaje kuwasaidia watoto wako waelewe na wahisi kwamba wanamhitaji Mwokozi Yesu Kristo? Ukurasa wa shughuli ya wiki hii pia unaweza kusaidia. Unatumia analojia rahisi ya shimo na ngazi. Fikiria kutumia 2 Nefi 9:21–22 kuzungumza na watoto wako kuhusu kwa nini una shukrani kwa ajili ya Yesu Kristo.
-
Moja ya njia za kuwasadia watoto wako waelewe kwa nini tunamhitaji Mwokozi ni kwa kuwafundisha kuhusu Anguko. Ungeweza kuonesha picha ya Adamu na Hawa, kama vile Leaving the Garden of Eden (Gospel Library), na picha ya Mwokozi msalabani. Fikiria kuwaomba wafafanue ni kitu gani kinafanyika katika kila picha. Je, ni kwa namna gani nasi ni kama Adamu na Hawa? Pengine 2 Nefi 9:6–10 inaweza kuwasaidia waone ni kitu gani Yesu Kristo anakifanya kwa ajili yetu sisi. Fikiria kuwaalika watoto kushiriki hisia zao kuhusu Yesu Kristo. Wimbo kama: “I Feel My Savior’s Love,” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 74–75) ungeweza kusaidia.
“Moyo wangu unafurahishwa na utakatifu.”
-
Ili kuwahamasisha watoto wako “[wafurahie] katika haki” au kwa furaha wamtii Bwana (2 Nefi 9:49), pengine ungeweza kushiriki mifano ambapo mtoto anafanya uchaguzi mzuri au uchaguzi mbaya. Waalike watoto wasimame wakati uchaguzi unaleta furaha, na kuketi wakati uchaguzi unaleta huzuni. Ni lini tulihisi furaha kwa sababu tulifanya uchaguzi wa kumfuata Yesu Kristo?
-
Watoto wako wana uwezekano wa kuchangamana na watu (kama bado hawajawahi kuchangamana nao) ambao wanahisi kwamba amri za Bwana ni upumbavu au zimepitwa na wakati. Pengine wewe na watoto wako mngeweza kuzungumza kuhusu jinsi ya kufafanua kwa nini tunafurahia kushika amri. Kwa nini ni muhimu kutumaini ushauri wa Mungu hata kama hatuuelewi kikamilifu? Ungeweza kuwahimiza watafute katika 2 Nefi 9:20, 28–29, 42–43 kwa ajili ya msaada wa kutafakari na kujadili maswali haya.