“Januari 29–Februari 4: ‘Nitawatayarishia Njia’ 1 Nefi 16–22,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: Kitabu cha Mormoni 2024 (2024)
“Januari 29–Februari 4. 1 Nefi 16–22,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani : 2024 (2024)
Januari 29–Februari 4: “Nitawatayarishia Njia”
1 Nefi 16–22
Wakati Familia ya Lehi ilipokuwa ikisafiri kuelekea nchi ya ahadi, Bwana aliwapatia ahadi hii: “Nitawatayarishia njia, kama mtatii amri zangu” (1 Nefi 17:13). Ni wazi, kwamba ahadi hiyo haikumaanisha kwamba safari ingekuwa rahisi—wanafamilia bado walitofautiana, pinde zilivunjika, watu walihangaika na kufariki na bado walihitajika kujenga merikebu kutokana na malighafi zilizokuwepo. Hata hivyo, wakati familia ilipokabiliana na shida au majukumu yaliyoonekana kutowezekana, Nefi alitambua kwamba Bwana kamwe hakuwa mbali. Alijua ya kwamba Mungu “atawalisha [waaminifu] na kuwatia nguvu, na kuwapatia njia ambayo wao wanaweza kukamilisha jambo ambalo Yeye amewaamuru” (1 Nefi 17:3). Kama umewahi kujiuliza kwa nini mambo mabaya hutendeka kwa watu wema kama Nefi na familia yake, unaweza kupata utambuzi katika milango hii. Lakini pengine muhimu zaidi, utaona kile ambacho watu wema hufanya wakati mambo mabaya yanapotokea.
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Nyumbani na Kanisani
Mwokozi atanisaidia nikabiliane na changamoto za maisha.
Familia ya Nefi ilikabiliana na changamoto ngumu—kama vile sote tunavyokabiliana nazo. Je, ni kipi unaweza kujifunza kutoka kwa Nefi kuhusu kukabiliana na majaribu kwa imani katika Yesu Kristo? Soma kuhusu uzoefu wake kwenye 1 Nefi 16:17–32; 16:34–39; 17:7–16; 18:1–4; na 18:9–22. Fikiria kuandika unachokipata kwa kutumia vichwa va habari kama hivi: “Changamoto”, “Jinsi Nefi Alivyoikabili,” na “Jinsi Bwana Alivyomsaidia.” Je, unajifunza kipi ambacho kingeweza kutumika kutatua changamoto unayokabiliana nayo?
Baada ya kujifunza kuhusu Nefi na familia yake, ungeweza kuandika mawazo ya ziada yenye vichwa hivi vya habari: “Changamoto Zangu.” “Jinsi Nitakavyozikabili,” na “Jinsi Bwana Anavyoweza Kunisaidia.” Ufanyapo hivyo, ungeweza kurejea maandiko kama haya: Mathayo 11:28–30; Yohana 14:26–27; Mosia 24:13–15. Wimbo kama: “Iwapi amani?” (Nyimbo za Dini, na. 62), ungeweza kuimarisha imani yako kwa Mwokozi na msaada Anaoutoa katika nyakati za majaribu.
Ona pia Anthony D. Perkins, “Remember Thy Suffering Saints, O Our God,” Liahona, Nov. 2021, 103–5; “He Will Give You Help,” “The Lord Guides Lehi’s Journey,” “The Lord Commands Nephi to Build a Ship,” na “Lehi’s Family Sails to the Promised Land” (video), Gospel Library; “Life Help,” Gospel Library.
1 Nefi 16:10–16, 23–31; 18:11–22
Bwana huniongoza kupitia njia ndogo na rahisi.
Wakati Mungu alipoiongoza familia ya Lehi kwenda nyikani, Yeye hakuwapa ramani ya kuonesha kila kitu kuhusu safari hiyo. Badala yake, Yeye aliwapa Liahona ili iwaongoze kila siku. Unaposoma 1 Nefi 16:10–16, 23–31, na 18:10–22, fikiria kutengeneza orodha ya kweli zinazoonesha jinsi gani Mungu anawaongoza watoto Wake (kwa mfano, 1 Nefi 16:10 inaweza kufundisha kwamba nyakati zingine Mungu hutuongoza katika njia zisizotarajiwa). Je, ni mifanano ipi unayoiona kati ya Liahona na Roho Mtakatifu? Ni zipi “njia ndogo” ambazo kwazo Yeye amesababisha “vitu vikubwa” katika maisha yako?
Majaribu yangu yanaweza kuwa baraka.
Ingawa Nefi na kaka zake walikuwa na changamoto sawa nyikani, uzoefu wao ulikuwa tofauti sana. Ungeweza kutofautisha maelezo ya Nefi ya safari nyikani (ona 1 Nefi 17:1–6) na yale ya kaka zake (ona 1 Nefi 17:17–22). Nefi alijua nini au alifanya nini ambacho kilimsaidia awe na mtazamo wa uaminifu? Fikiria kuandika kuhusu jaribu la hivi karibuni au ulilonalo sasa kwa mtazamo wa imani na shukrani. Je, unahisi nini au unajifunza kipi kutokana na jaribu hilo?
Ona pia Amy A. Wright, “Kristo Huponya Kile Kilichovunjika,” Liahona, Mei 2022, 81–84; “No Strength without Struggle” (video), Gospel Library.
Naweza “kulinganisha maandiko yote” na mimi mwenyewe.
Kwa sababu maandiko yaliandikwa kipindi kirefu kilichopita, inaweza kuonekana kama si ya muhimu kwetu leo hii. Lakini Nefi alijua vyema zaidi. “Nililinganisha maandiko yote na sisi,” alisema “ili yaweze kutufaidisha na kutuelimisha” (1 Nefi 19:23). Hii ni sababu mojawapo ya Nefi kupata nguvu nyingi za kiroho kwenye maandiko.
Fikiria maswali kama yafuatayo wakati ukisoma 1 Nefi 20–22:
-
1 Nefi 20:1–9.Mistari hii inafundisha nini kuhusu watu katika siku za Isaya? Unapata kipi ambacho ni kwa ajili yako?
-
1 Nefi 20:17–22.Mistarti hii inafundisha nini kuhusu jinsi Baba wa Mbinguni alivyowaongoza watu wa kipindi cha Isaya? Ni kwa namna gani anakualika umfuate Yeye?
Ni kipi kingine unachokipata katika 1 Nefi 20– 22 ambacho unaweza “kukilinganisha” kwako wewe mwenyewe?
Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto
1 Nefi 16:10, 28–29; 18:8–13, 20–22
Wakati ninaposhika amri, Bwana huniongoza.
-
Kama una dira, ramani au kitu kingine chochote ambacho hutusaidia kupata njia, ungeweza kukionesha kwa watoto wako. Hii ingeweza kuwa njia nzuri ya kuanza mjadala kuhusu Liahona, ambapo unaweza kusoma kuhusu hilo katika 1 Nefi 16:10, 28–29 Je, ni zipi baadhi ya sababu ambazo dira au ramani inaweza isifanye kazi? Je, ni kwa nini wakati mwingine Liahona haikutoa uelekeo kwa familia ya Lehi (ona 1 Nefi 18: 9–12, 9–22). Je, Baba wa Mbinguni ametupatia nini hivi leo ili kutuongoza turudi katika uwepo Wake?
-
Ili kuwasaidia watoto wako kutumia wanachojifunza kuhusu Liahona katika 1 Nephi 16:10, 26–31; 18:8–22, ungeweza kuwaalika wafikirie kuhusu uamuzi mgumu au muhimu. Je, Mungu ametupatia kitu gani hivi leo ambacho hufanya kazi sawa na Liahona? (Ona, kwa mfano, Alma 37:38–44.) Fikiria kushiriki uzoefu binafsi ambapo Baba wa Mbinguni alikuongoza.
Ninaweza kuwa mfano mzuri kwa familia yangu.
-
Wakati mkisoma 1 Nephi 16:21–32 pamoja, wasaidie watoto wako wagundue jinsi mfano wa Nefi ulivyoibariki familia yake (ona pia video “The Lord Guides Lehi’s Journey” [Gospel Library]). Hii ingeweza kuongoza kwenye mjadala kuhusu jinsi ambavyo tungeweza kuwa kama Nefi. Waalike watoto wako wapange jambo moja wanaloweza kufanya ili kuwa washawishi wazuri kwa wanafamilia wengine.
Baba wa Mbinguni anaweza kunisaidia nifanye mambo magumu.
-
Watoto hupenda kusimulia hadithi. Ungeweza kuwaalika wakusaidie kusimulia hadithi ya Nefi akiamriwa kujenga merikebu (ona 1 Nefi 17:7–19; 18:1–4; ona pia “Mlango wa 7: Kujenga Merikebu,” katika Hadithi za Kitabu cha Mormoni, 21–22; au video “The Lord Instructs Nephi to Build a Ship” [Gospel Library]). Wangeweza pia kuimba pamoja “Nephi’s Courage” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto,120–21). Nini kilimsaidia Nefi awe na ujasiri wakati kaka zake walipomfanyia mzaha kwa kujaribu kujenga merikebu?
-
Nefi hakujua jinsi ya kujenga merikebu, hivyo alitegemea maelekezo kutoka kwa Bwana. Baada ya kusoma 1 Nefi 18:1 pamoja nawe, watoto wako wangeweza kukamilisha ukurasa wa shughuli ya wiki hii. Wakati wakifanya hivyo, zungumza nao kuhusu jinsi Baba wa Mbinguni anavyoweza kutusaidia tufanye mambo magumu, kama vile alivyomsaidia Nefi.