Mlango wa 20
Bwana anafunua makusudi Yake kwa Israeli—Israeli imechaguliwa kutoka katika tanuri la masumbuko na linapaswa kuondoka kutoka Babeli—Linganisha Isaya 48. Karibia mwaka 588–570 K.K.
1 Sikilizeni na msikie haya, Ee nyumba ya Yakobo, ambao wanajulikana kwa jina la Israeli, na wametoka katika maji ya Yuda, au kutoka kwenye maji ya ubatizo, ambao wanaapa kwa jina la Bwana, na kutaja Mungu wa Israeli, walakini hawaapi kwa ukweli wala kwa haki.
2 Walakini, wanajiita wakaazi wa mji mtakatifu, lakini hawamtegemei Mungu wa Israeli, ambaye ni Bwana wa Majeshi; ndiyo, jina lake ni Bwana wa Majeshi.
3 Tazama, nimetangaza vitu vilivyokuja awali kutoka mwanzoni; na yalitoka kinywani mwangu, na niliyadhihirisha. Niliyadhihirisha kwa ghafla.
4 Na niliitenda kwa sababu nilijua kwamba wewe ni mkaidi, na shingo yako ni ngumu kama chuma, na paji lako kama shaba nyeupe;
5 Na nimekutangazia hata tangu mwanzo, kabla hayajakuwa niliyaonyesha kwako; na nilikuonyesha usije ukasema—Sanamu yangu imezitenda, na mfano uliochongwa wangu, na mfano ulioyeyushwa wangu ndiyo imeziamuru.
6 Umeona na kusikia haya yote; na je wewe hutayatangaza? Na kwamba nimekuonyesha vitu vipya tangu wakati huu, hata vitu vilivyofichwa, na wewe hukuvijua.
7 Yameumbwa sasa, na si tangu mwanzo, hata kabla ya ile siku ambayo hukuyasikia yalikuwa yametangazwa kwako, ili usiseme—Tazama niliyajua.
8 Ndiyo, na wewe hukusikia; ndiyo, wewe hukujua; ndiyo, tangu ule wakati sikio lako halikufunguliwa; maana nilijua kwamba ungetenda uhaini, na ulikuwa mvunja sheria kutoka tumboni.
9 Walakini, kwa sababu ya heshima ya jina langu nitazuia ghadhabu yangu, na kwa sababu ya sifa zangu nitajizuia kutokana nawe, kwamba nisikuangamize.
10 Kwani, tazama, nimekutakasa, nimekuchagua kutoka karibu ya masumbuko.
11 Kwa heshima yangu, ndiyo, kwa heshima yangu nitatenda hii, kwani sitakubali jina langu lichafuliwe, na sitampatia mwingine utukufu wangu.
12 Nisikilize mimi, Ee Yakobo, na Israeli wateule wangu, kwani Mimi ndimi yeye; Mimi ndimi wa kwanza, na pia Mimi ndimi wa mwisho.
13 Mkono wangu pia umejenga msingi wa dunia, na mkono wangu wa kuume umetandaza mbingu. Naziita na zinasimama pamoja.
14 Ninyi nyote, kusanyikeni, na msikie; ni nani miongoni mwao amewatangazia vitu hivi? Bwana amempenda; ndiyo, na atatimiza neno lake ambalo amesema kupitia kwao; na atatendea Babilonia nia yake, na mkono wake utanyoshewa Wakaldayo.
15 Pia, Bwana asema; mimi, Bwana, ndiyo, nimesema; ndiyo, nimemuita kutangaza, nimemleta, na atafanikiwa katika njia zake.
16 Njooni karibu na mimi; sijazungumza kwa siri; tangu mwanzo, tangu ilipotangazwa nimezungumza; na Bwana Mungu, na Roho yake, amenituma.
17 Na hivyo ndivyo asemavyo Bwana, Mkombozi wenu, Mtakatifu wa Israeli; nimemtuma, Bwana Mungu wenu anayekufundisha kufaidika, ambaye anakuongoza katika njia inayokupasa, ameitenda.
18 Ee kwamba ungesikiliza amri zangu—basi amani yako ingekuwa kama mto, na haki yako ungekuwa kama mawimbi ya bahari.
19 Uzao wako ungekuwa pia kama mchanga; na kizazi cha matumbo yenu ingekuwa kama changarawe yake; jina lake halingetupiliwa mbali wala kuangamizwa kutoka mbele yangu.
20 Tokeni kutoka Babilonia, waondokeeni Wakaldayo, kwa sauti ya kuimba tangazeni ninyi, semeni haya, ambieni hadi mwisho wa ulimwengu; semeni ninyi; Bwana amemkomboa mtumishi wake Yakobo.
21 Na hawakuona kiu; aliwaongoza katika majangwa; akasababisha maji kutiririka kutoka kwenye mwamba kwa sababu yao; alipasua mwamba pia na maji yakatoka.
22 Ingawa ametenda haya yote, na makuu pia, hakuna amani, asema Bwana, kwa waovu.