Njoo, Unifuate 2024
Februari 26–Machi 3: “Jina Lake Ataitwa … Mfalme wa Amani.” 2 Nefi 11–19


“Februari 26–Machi 3: ‘Jina Lake Ataitwa … Mfalme wa Amani.’ 2 Nefi 11–19,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani: Kitabu cha Mormoni 2024 (2024)

“Februari 26–Machi 3. 2 Nefi 11–19,” Njoo, Unifuata—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2024 (2024)

Picha
Isaya akiandika kwenye hati za kukunja

Februari 26–Machi 3: “Jina Lake Ataitwa … Mfalme wa Amani”

2 Nefi 11–19

Kuchonga kwenye mabamba ya chuma siyo rahisi na nafasi kwenye bamba ndogo za Nefi ilikuwa ni ndogo. Hivyo ni kwa nini basi Nefi alifanya jitihada ya kunakili kiasi kikubwa cha maandishi ya Isaya katika kumbukumbu yake? Alifanya hivyo kwa sababu alitaka sisi tuamini katika Yesu Kristo. “Nafsi yangu inafurahia,” aliandika, “kuwathibitishia watu wangu ukweli wa kuja kwa Kristo” (2 Nefi 11:4). Nefi alikuwa ameona kile kitakachotokea kwa watu wake katika vizazi vya baadaye. Aliona kwamba, licha ya baraka kuu, watakuja kuwa na kiburi, mabishano na kupenda anasa za dunia (ona 1 Nefi 12; 15:4–6). Pia aliona matatizo sawa na hayo katika siku zetu (ona 1 Nefi 14). Maneno ya Isaya yalionya dhidi ya uovu wa aina hiyo. Lakini pia yalimpa Nefi tumaini kwa ajili ya siku zijazo zenye utukufu—mwisho wa uovu, kusanyiko la waaminifu na “nuru kuu” kwa ajili ya wale “waliotembea katika giza” (2 Nefi 19:2). Haya yote yangetokea kwa sababu “mtoto [alizaliwa]” ambaye angeweza kumaliza maovu yote—“Mfalme wa Amani” (2 Nefi 19:6).

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Nyumbani na Kanisani

Ni kwa jinsi gani ninaweza kuelewa vyema mafundisho ya Isaya?

Nefi alikiri kwamba “maneno ya Isaya si rahisi kueleweka” (2 Nefi 25:4). Lakini alitupatia pia ushauri wa kutusaidia tupate maana katika maandishi ya Isaya:

  • Linganisha maneno yake” kwako mwenyewe (2 Nefi 11:2). Mengi ya mafundisho ya Isaya yana maana na matumizi zaidi ya moja. Kwa mfano, wakati ukisoma kuhusu sehemu za kuishi katika 2 Nefi 14:5–6, fikiria jinsi gani mistari hii inatumika kwenye nyumba yako. Jiulize, “Baba wa Mbinguni anataka nijifunze nini?”

  • Tafuta ishara za Yesu Kristo (ona 2 Nefi 11:4). Mengi ya mafundisho ya Isaya kuhusu Mwokozi yanatolewa kupitia ishara. Kwa mfano, ni kwa jinsi gani Mwokozi amewakilishwa katika 2 Nefi 19:2? Je, ishara hii inakufundisha nini kuhusu Yeye?

  • “Tafuta “kujazwa na roho wa unabii” (2 Nefi 25:4). Unapojifunza, sali kwa ajili ya mwongozo wa kiroho. Yawezekana usielewe kila kitu kwa mara moja, lakini Roho anaweza kukusaidia uweze kujifunza kile unachohitaji kujua.

Pia inaweza kuwa ya manufaa kurejelea kwenye misaada ya kujifunza ndani ya maandiko, ikiwa ni pamoja na tanbihi, vichwa vya habari vya milango na Mwongozo wa Maandiko. Kitabu cha Mormoni na vitabu vya kiada vya chuo vya Agano la Kale, vina maelezo ya ziada ambayo yanaweza kukusaidia ujifunze kuhusu muktadha wa kihistoria wa mafundisho ya Isaya.

2 Nefi 11–19

Isaya alishuhudia juu ya Yesu Kristo.

Kwa sababu Isaya alitumia sana lugha ya ishara, inaweza kuwa rahisi kutotilia maanani ushahidi wake wenye nguvu juu ya Yesu Kristo. Mtafute Mwokozi katika 2 Nefi 13:13; 14:4–6; 15:1–7; 16:1–7; 17:14; 18:14–15; 22:2. Mistari hii inakufundisha nini kuhusu Yeye?

Unabii katika 2 Nefi 19:6 unaorodhesha majina kadhaa ya Yesu Kristo. Ni kwa jinsi gani Yeye ametimiza majukumu haya katika maisha yako?

Ona pia Ulisses Soares, “Yesu Kristo: Mtunzaji wa Nafsi Zetu,” Liahona, Mei 2021, 82–84.

2 Nefi 12–13; 15

Wenye kiburi na wapenda anasa za dunia watanyenyekezwa.

Nefi alikuwa ameona kwamba kiburi kingesababisha maangamizo ya watu wake (ona 1 Nefi 12:19). Kwa hivyo siyo ajabu kwamba Nefi alishiriki na watu wake maonyo ya Isaya yaliyorudiwa mara kwa mara dhidi ya kiburi. Katika mlango wa 12 na 13, tafuta maneno ambayo Isaya aliyatumia kuelezea hali ya kiburi, kama vile kujidai na maringo. Katika 2 Nefi 15:1–24, tafuta lugha ya ishara inayoelezea matokeo ya kiburi. Kisha unaweza kujaribu kufupisha kile ulichokisoma kwa maneno yako mwenyewe. Fikiria kuhusu jinsi utakavyochagua kuwa mnyenyekevu.

Ona pia “Chapter 18: Beware of Pride,Teachings of Presidents of the Church: Ezra Taft Benson (2014), 229–40.

Picha
ikoni ya seminari

2 Nefi 12:2–3

Hekalu ni nyumba ya Bwana.

Isaya alielezea hekalu kama “mlima wa nyumba ya Bwana” (2 Nefi 12:2) Je, ni kwa nini mlima ni ishara nzuri kwa ajili ya hekalu?

Je! unawezaje kumwelezea mtu mwingine kwa nini tunahitaji mahekalu? Ungeweza kutafuta majibu katika 2 Nefi 12:2–3 ujumbe wa Rais Russell M. Nelson “Hekalu na Msingi Wako wa Kiroho” (Liahona, Nov. 2021, 93–96). Kulingana na ulichokisoma, kwa nini Bwana anakutaka ujifunze na upate uzoefu katika nyumba Yake? Je, ni uzoefu upi umewahi kuwa nao huko?

Unaweza kupata maswali kwa ajili ya usaili wa kibali cha hekaluni kwenye kurasa 36–37 za Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana: Mwongozo wa Kufanya Chaguzi. Zingatia kusoma kila swali na ujiulize, je, swali hili linanifundisha nini kuhusu njia za Bwana? Je, linanisaidiaje “nitembee katika njia zake”?

Ona pia Mada za Injili , “Mahekalu,” Gospel Library; “Juu ya Mlima,” Nyimbo za Dini, na 5.

2 Nefi 12–19

Yesu Kristo atawakomboa watu Wake.

Licha ya uovu aliouona, Isaya aliona matumaini kwa ajili ya siku za usoni. Fikiria kusoma kila moja ya vifungu vya maneno vifuatavyo. Andika ukweli mmoja au zaidi ambao kila kifungu cha maneno kinaufundisha kuhusu siku yetu: 2 Nefi 12:1–5; 14:2–6; 15:20–26; 19:2–8. Kwa nini unahisi vifungu hivi vya maneno ni muhimu kwetu kuvielewa?

Kwa mawazo zaidi, ona toleo la mwezi huu la Liahona na magazeti ya Kwa ajili ya Nguvu kwa Vijana.

Tafuta mpangilio. Katika maandiko tunaweza kupata mpangilio ambao hutuonesha jinsi Bwana anavyoifanya kazi Yake. Katika 2 Nefi 11–19, unaweza kupata mipangilio ambayo inaonesha namna Bwana anavyoonya kuhusu dhambi na kusamehe watu wanaotubu.

Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto

2 Nefi 12:2–3

Hekalu ni nyumba ya Bwana.

  • Isaya alielezea hekalu kama “mlima wa nyumba ya Bwana.” Watoto wako wangeweza kufurahia kujifanya kama wanapanda mlima wakati ukisoma 2 Nefi 12:2–3. Wasaidie watafute virai kwenye mistari hii ambavyo vinaelezea kwa nini tunayo mahekalu.

  • Ili kuelezea kwa mifano kifungu cha maneno “tutatembea katika njia zake” kutoka 2 Nefi 12:3, ungeweza kutengeneza njia kwenye sakafu, ikielekea kwenye picha ya hekalu. Wakati watoto wako wakitembea kwenye njia, wangeweza kutaja vitu ambavyo wanaweza kufanya ili kutembea kwenye njia za Bwana.

  • Pengine watoto wako wangeweza kuchora picha zao wenyewe wakienda hekaluni. Pia wangeweza kuimba au kusikiliza wimbo kuhusu hekalu kama vile “I Love to See the Temple” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 95). Wasaidie watafute virai kutoka kwenye wimbo ambavyo vinafundisha hekalu ni nini na nini tunakifanya hekaluni.

2 Nefi 11:4–7; 17:14; 19:6

Yesu Kristo ni Mwokozi wangu.

  • Kuna baadhi ya majina ya Yesu Kristo katika 2 Nefi 11:4–7; 17:14; 19:6. Wasaidie watoto wako wayatafute na zungumza kuhusu kile majina hayo yanachomaanisha. Kwa mfano “Kristo” humaanisha “mpakwa mafuta” na “Emanueli” humaanisha “Mungu pamoja nasi.” Je, majina haya hutufundisha nini kuhusu Yesu?

  • Onesha sehemu ndogo ndogo za video “The Christ Child” (ChurchofJesusChrist.org) ambazo huonesha watu tofauti tofauti wakimwona Yesu kwa mara ya kwanza. Simamisha video kwa muda wakati wa maonesho haya na waulize watoto wako kuhusu nini watu hawa wangeweza kukihisi. Tungehisi vipi ikiwa tungekuwepo pale? Je, tutahisije wakati tutakapomwona tena?

2 Nefi 15:20

Shetani anajaribu kunikanganya kuhusu wema na uovu.

  • Waoneshe watoto wako kitu kilicho kichungu au kichachu, kama vile kipande cha limao, ndani ya karatasi ya peremende. Someni pamoja 2 Nefi 15:20. Ni kwa namna ipi Shetani anajaribu kufanya vitu viovu vionekane vyema? Ungeweza pia kuonesha sekunde 90 za mwanzo za video“You Will Be Freed” (Gospel Library). Kwa nini mvuvi aliipa ndoano yake mwonekano tofauti? Kwa nini Shetani huipa dhambi mwonekano tofauti? Ni kwa jinsi gani Yesu Kristo hutusaidia tuepuke kudanganywa na Shetani?

Kwa ajili ya mawazo zaidi, ona toleo la mwezi huu la gazeti la Rafiki.

Picha
Hekalu la Panama Jijini Panama

Hekalu la Panama Jijini Panama. “Nyumba ya Bwana itajengwa kileleni mwa milima, … na mataifa yote yataitiririkia” (2 Nefi 12:2).

Chapisha