Njoo, Unifuate
Juni 23–29: “Thamani … Kuliko Utajiri wote wa Dunia”: Mafundisho na Maagano 67–70


“Juni 23–29: ‘Thamani … Kuliko Utajiri wote wa Dunia’: Mafundisho na Maagano 67–70,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: Mafundisho na Maagano 2025 (2025)

“Mafundisho na Maagano 67–70,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2025

muswada wa Kitabu cha Amri

Juni 23–29: “Thamani … Kuliko Utajiri wote wa Dunia”

Mafundisho na Maagano 67–70

Kutoka 1828 mpaka 1831, Nabii Joseph Smith alipokea mafunuo mengi kutoka kwa Bwana, ikiwa ni pamoja na ushauri wa kiungu kwa ajili ya watu binafsi, maelekezo juu ya kuongoza Kanisa, na maono ya siku za mwisho na kweli nyingi za milele zenye mwongozo. Lakini Watakatifu wengi hawakuwa wamezisoma. Mafunuo yalikuwa bado hayajachapishwa, na nakala chache zilizokuwepo zilikuwa zimeandikwa kwa mkono kwenye karatasi ambazo hazikufungwa pamoja ambazo zilisambazwa kwa waumini na kuchukuliwa kila mahala na wamisionari.

Kisha, mnamo Novemba 1831, Joseph aliitisha baraza la viongozi wa Kanisa ili kujadili kuhusu uchapishaji wa mafunuo haya. Baada ya kutafuta mapenzi ya Bwana, viongozi hawa walifanya mipango ya kuchapisha Kitabu cha Amri—utangulizi wa Mafundisho na Maagano ya leo. Punde kila mtu angeweza kujisomea wao wenyewe neno la Mungu lililofunuliwa kupitia nabii aliye hai, ushahidi hai kwamba “funguo za siri za ufalme wa Mwokozi wetu zimekabidhiwa tena kwa mwanadamu.” Kwa sababu hii na zingine nyingi, Watakatifu wakati huo na sasa wanachukulia mafunuo haya kuwa “ni ya thamani … kuliko utajiri wote wa dunia” (Mafundisho na Maagano 70, kichwa cha habari cha sehemu).

Ona Saints, 1:140–43.

ikoni ya kujifunza

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Nyumbani na Kanisani

Mafundisho na Maagano 67:1–9; 68:3–6

Watumishi wa Bwana wanazungumza mapenzi Yake pale wanapokuwa wameongozwa na Roho Mtakatifu.

Uamuzi wa kuchapisha mafunuo uliopokelewa na Joseph Smith ulionekana kama rahisi, lakini baadhi ya viongozi wa mwanzo wa Kanisa hawakuwa na uhakika kama lilikuwa wazo zuri. Wasiwasi mmoja ulikuwa ni juu ya mapungufu katika jinsi Joseph Smith alivyoandika mafunuo haya. Ufunuo katika sehemu ya 67 ulikuja kama jibu la wasiwasi huo. Ni kipi unajifunza kuhusu manabii wa Bwana na ufunuo kutoka mistari 1–9? Je, ni umaizi upi wa ziada unaupata kutoka 68:3–6?

Umekuja kujua vipi wewe mwenyewe kwamba mafunuo ambayo Mungu huwapa watumishi Wake ni ya kweli? Ungeweza pia kutafakari uzoefu wa wakati ulipohisi Bwana akizungumza na wewe kupitia mmoja wa watumishi Wake (ona Mafundisho na Maagano 68:4). Ni lini ambapo ulihisi “uliongozwa na Roho Mtakatifu” (mstari wa 3) kusema au kufanya jambo? Ni kwa jinsi gani Bwana “alisimama nawe”?(mstari wa 6).

Kabla ya Kitabu cha Amri kuchapishwa, viongozi kadhaa wa Kanisa walitia saini ushuhuda wa maandishi kwamba mafunuo katika kitabu ni ya kweli. Ili kuona nakala ya ushuhuda wao, ona “Testimony, circa 2 November 1831,” Revelation Book 1, 121, josephsmithpapers.org.

Mafundisho na Maagano 67:10–14

“Endeleeni katika uvumilivu.”

Ni kwa jinsi gani wivu, hofu, na kiburi vinatuzuia kusogea karibu na Bwana? Ni kwa jinsi gani tunamshinda “mtu wa asili” au “akili ya kimwili” ili kwamba tuweze “kumwona [Yeye] na kujua kuwa [Yeye ndiye]”? (mstari wa 12; ona pia Mosia 3:19). Ni kipi unakipata katika mistari hii ambacho kinakuvuvia “kuendelea katika uvumilivu hadi mtakapokuwa mmekamilika”? (mstari wa13).

Mafundisho na Maagano 68:25–31

ikoni ya seminari
Ninaweza kujenga msingi wa nyumba yangu juu ya Yesu Kristo.

Maneno ya Bwana katika Mafundisho na Maagano 68:25–31 yanarejelea mahususi kwa wazazi, lakini iwe wewe ni mzazi au la, unaweza kutumia ushauri Wake kufanya sehemu yako kuweka mafundisho ya Yesu Kristo yawe kiini cha nyumba yako. Zilizoorodhesha ni baadhi ya kanuni ambazo Bwana alisema zinapaswa kufundishwa nyumbani. Fikiria jinsi unavyoweza kufanya kila moja ya sehemu hizi ziwe msingi wa nyumba ambayo kiini chake ni Kristo—nyumba unayoishi sana au nyumba yako ya siku za usoni. Nyenzo na maswali yaliyotolewa vinaweza kusaidia.

  • Toba: Jifunze Alma 36:17–20, na ugundue jinsi Alma alivyobarikiwa katika wakati muhimu kwa sababu baba yake alikuwa amemfunza kuhusu huduma ya Mwokozi ya kulipia dhambi. Ni kwa jinsi gani unaweza kuipatia familia yako msukumo wa kumgeukia Yesu Kristo na kutubu? (ona pia 2 Nefi 25:26).

  • Imani katika Kristo: Soma mapendekezo matano ya Rais Russell M. Nelson kwa ajili ya kukuza imani katika “Kristo Amefufuka; Imani Kwake Itahamisha Milima” (Liahona, Mei 2021, 103). Tafakari jinsi ambavyo mapendekezo haya yangeweza kuanzisha utamaduni wa imani katika familia yako.

  • Ubatizo: Pitia tena agano la ubatizo kama lilivyoelezwa katika Mosia 18:8–10, 13. Ni kwa jinsi gani juhudi zako za kushika agano hili zimeiimarisha familia yako?

  • Kipawa cha Roho Mtakatifu: Jifunze mialiko kwenye kurasa 17–19 za Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana: Mwongozo wa Kufanya Chaguzi. Je, unahisi kuongozwa kufanya kipi ili kualika ushawishi wa Roho Mtakatifu katika nyumba yako?

  • Sala: Unajifunza kipi kuhusu nguvu ya sala katika nyumba yako kwenye wimbo “Love Is Spoken Here”? Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 190–91). Ni baraka zipi Mwokozi alizitoa katika 3 Nefi 18:15–21?

  • Kanuni zingine unazozipata katika Mafundisho na Maagano 68:25–31:

Ni ushauri upi ungeweza kuutoa kwa mtu ambaye wanafamilia wake hawaungi mkono juhudi zao za kujenga imani katika Kristo?

Ona pia “Familia: Tangazo la Ulimwengu, “Maktaba ya Injili; Topics and Questions, “Parenting,” Maktaba ya Injili; Dieter F. Uchtdorf, “Yesu Kristo Ni Nguvu kwa Wazazi,” Liahona, Mei 2023, 55–59.

familia ikijifunza pamoja

Mafundisho na Maagano 69:1

Marafiki wa “kweli na waaminifu” hunisaidia nimfuate Yesu Kristo.

Kwa nini unafikiri ilikuwa “hekima kwa [Bwana]” kwa mtu “mkweli na mwaminifu” kuambatana na Oliver Cowdery kwenye kazi iliyoelezwa katika mstari huu? Ni kwa jinsi gani kanuni hii inatumika kwako?

Wasaidie wanafunzi wainuane. Kila mtu katika darasa lako au familia ni chanzo kikubwa cha ushuhuda, umaizi, na uzoefu kutokana na kuishi injili. Waalike washirikishane na wainuane.

Mafundisho na Maagano 70:1–4

Ninawajibika kwa ajili ya mafunuo ambayo Bwana ameyatoa?

Bwana aliwapa baadhi ya wazee jukumu la kusimamia uchapishaji wa mafunuo. Hata kama huna jukumu hilo mahususi, utumishi wako au majukumu yako ni yapi “juu ya mafunuo na amri”? (mstari wa 3).

Kwa mawazo zaidi, ona toleo la mwezi huu la majarida ya Liahona na Kwa ajili ya Nguvu kwa Vijana..

ikoni ya 01 ya sehemu ya watoto

Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto

Mafundisho na Maagano 67

Mafundisho na Maagano hunifundisha kuhusu Yesu Kristo.

  • Waambie watoto kuhusu jinsi mafunuo ya Joseph Smith yalivyochapishwa kuwa kitabu (ona “Sura ya 23: Mafundisho na Maagano,” Hadithi za Mafundisho na Maagano,, 90–92, au video inayohusiana kwenye Maktaba ya Injili). Wasaidie wakumbuke baadhi ya vitu mlivyojifunza kuhusu Yesu Kristo kutoka kwenye Mafundisho na Maagano hadi kufikia hapa mwaka huu. Mngeweza pia kushiriki mmoja na mwingine baadhi ya mistari yenu pendwa kutoka kwenye Mafundisho na Maagano.

    2:2

    Chapter 23: The Doctrine and Covenants: August–November 1831

  • Ungeweza pia kuwaonesha watoto wako Biblia, Kitabu cha Mormoni, Mafundisho na Maagano, na Lulu ya Thamani Kuu na uzungumze nao kuhusu jinsi vilivyo tofauti na jinsi vinavyofanana (ona maelezo ya vitabu hivi katika Mwongozo wa Maandiko). Ni kwa jinsi gani tunaweza kujua kwamba maandiko ni ya kweli? Tunajifunza nini kutoka Mafundisho na Maagano 67:4, 9 kuhusu mafunuo Bwana aliyoyatoa kwa Joseph Smith?

watoto wakisoma maandiko

Mafundisho na Maagano 68:25–31

Ninaweza kubatizwa wakati nitakapokuwa na umri wa miaka minane.

  • Katika Mafundisho na Maagano 68:27, Bwana alieleza bayana umri wa mtu kuweza kubatizwa. Wasaidie watoto wako wagundue kile Yeye alichokisema. Kwa nini Yesu anatutaka sisi tubatizwe? Wimbo kama vile “Baptism,” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 100–101) ungeweza kusaidia. Ukitumia picha au mistari 25–31 (au vyote), wasaidie watoto wako wagundue vitu Bwana anavyowataka watoto wajifunze.

  • Soma pamoja na watoto wako kuhusu kazi Bwana aliyompa Oliver Cowdery katika kichwa cha habari cha sehemu cha Mafundisho na Maagano 69. Ni ushauri upi Bwana aliutoa katika mstari wa 1? Kwa nini ni muhimu kuwa pamoja na watu “ambao watakuwa wakweli na waaminifu”? Pengine watoto wako wangeweza kusimulia kuhusu mtu fulani wanayemjua ambaye wanajua ni “mkweli na mwaminifu.” Imbeni pamoja wimbo ambao unawatia moyo watoto kuwa wakweli na waaminifu kama Mwokozi, kama vile “I’m Trying to Be like Jesus” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto,, 78–79). Ni kwa jinsi gani tunaweza kuhakikisha kwamba tu wakweli na waaminifu kwa Bwana? Ni kwa jinsi gani Yeye anaweza kututumia sisi kuwabariki wengine wakati tunapokuwa wakweli na waaminifu?

Kwa mawazo zaidi, ona toleo la mwezi huu la jarida la Rafiki.

kiwanda cha uchapishaji

Kitabu cha Amri, utangulizi wa Mafundisho na Maagano, kilichapishwa kwenye kiwanda cha uchapishaji kama hiki.

ukurasa wa shughuli kwa ajili ya watoto