Njoo, Unifuate
Februari 3–9. 2 Nefi 1–5: “Tuliishi kwa Furaha”


“Februari 3–9. 2 Nefi 1–5: ‘Tuliishi kwa Furaha,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Kitabu cha Mormoni 2020 (2020)

“Februari 3–9. 2 Nefi 1–5,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2020

Picha
Adamu na Hawa wakiondoka katika Bustani ya Edeni

Adamu na Hawa, na Douglas Fryer

Februari 3–9

2 Nefi 1–5

“Tuliishi kwa Furaha”

Maandiko yanaweza kufungua mlango kwa ajili ya ufunuo binafsi. Unaposoma 2 Nefi 1–5, unaweza kugundua ya kwamba Bwana analo jambo maalum Analotaka kukufundisha.

Andika Misukumo Yako

Kama ungelijua maisha yako kuwa yako karibu kumalizika, ni jumbe gani za mwisho ungeweza kutaka kushiriki na wale uwapendao zaidi? Wakati nabii Lehi alipohisi alikuwa akikaribia mwisho wa maisha yake, aliwakusanya watoto wake kwa mara ya mwisho kutoa unabii na kushiriki kweli za injili alizozithamini pamoja na watu aliowathamini. Alifundisha kuhusu uhuru, utiifu, kuanguka kwa Adamu na Hawa, ukombozi kupitia kwa Yesu Kristo, na shangwe. Sio watoto wake wote walikubali ushuhuda wake wa mwisho, lakini wale ambao walikubali—pamoja na mamilioni wanaousoma leo—waligundua katika ushuhuda wake kanuni za kuishi “kwa furaha” (2 Nefi 5:27).

Picha
ikoni ya kujifunza binafsi

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Binafsi Maandiko

2 Nefi 2

Niko huru kuchagua uzima wa milele.

Mzee D. Todd Christofferson alisema: “Mungu anadhamiria kwamba watoto Wake wanapaswa kutenda kulingana na maadili ya haki ya kujiamulia ambayo Amewapa. … Ni mpango Wake na mapenzi Yake kwamba tuna wajibu mkubwa wa kufanya maamuzi katika matukio ya maisha yetu wenyewe” (“Huru Milele, Kujitendea Wenyewe,” Ensign au Liahona, Nov. 2014,16). Katika mafundisho yake kuhusu haki ya kujiamulia, Lehi alitambua hali muhimu zinazohitajika kuwezesha haki ya kujiamulia na kutuwezesha kufikia uwezo wetu mtukufu, ikijumuisha yafuatayo:

  1. Ujuzi wa wema na maovu (2 Nefi 2:5)

  2. Sheria waliyopewa wanadamu (2 Nefi 2:5)

  3. Chaguzi zenye upinzani, zenye kushawishi (2 Nefi 2:11)

  4. Uwezo wa kutenda (2 Nefi 2:16)

Unaposoma 2 Nefi 2, unajifunza nini kuhusu kila moja ya hali hizi za haki ya kujiamulia na uhusiano wake kati ya moja na nyingine? Ni nini kingetendeka kwa haki yetu ya kujiamulia kama moja au zaidi ya hali hizi haingekuwepo? Unajifunza nini cha ziada kuhusu haki ya kujiamulia kutoka kwenye maneno ya Lehi?

2 Nefi 2:22–29

Anguko na Upatanisho wa Yesu Kristo ni sehemu muhimu za mpango wa Baba wa Mbinguni.

Watu wengi wanaona Anguko la Adamu na Hawa kama tukio la tanzia. Hata hivyo, mafundisho ya Lehi kuhusu Anguko yanafunua ni kwa nini lilikuwa sehemu muhimu ya mpango wa Baba kwa ajili ya kuendelea kwetu milele. Unaposoma mistari hii, tafuta ni kwa nini Anguko lilihitaji kutokea ili sisi—watoto wa Baba wa Mbinguni—tuweze kuendelea. Ni jinsi gani dhabihu ya upatanisho ya Mwokozi ilitukomboa kutoka kwenye Anguko?

Ona pia Musa 5:9–12; 6:51–62; “Anguko la Adamu na Hawa,” Mada za Injili, topics.ChurchofJesusChrist.org.

2 Nefi 3:6–24

Joseph Smith alitawazwa tangu mwanzo ili arejeshe injili.

Sehemu ya mwisho ya 2 Nefi 3 inao utabiri uliotolewa na Yusufu wa Misri kuhusu mwonaji wa siku za baadaye ambaye angekuwa na jina sawa na lake (ona mistari 14–15)—Joseph Smith. Pia ina mengi ya kuzungumzia kuhusu misheni ya Joseph Smith. Ni nini mistari 6–24 inasema kwamba Joseph Smith, “mwonaji bora,” angefanya ili kuwabariki watu wa Mungu? Ni kwa namna ipi ya Joseph Smith imekuwa “yenye thamani kubwa” kwako?

Sehemu moja muhimu ya misheni ya Joseph Smith ilikuwa ni kuleta maandishi ya uzao wa Yusufu, ambayo yanapatikana katika Kitabu cha Mormoni. Unaweza kujifunza nini kutoka sura hii kuhusu umuhimu wa Kitabu cha Mormoni?

Ona pia Tafsiri ya Joseph Smith, Mwanzo 50:24–38 (katika Kiambatisho cha Biblia).

Picha
nabii Joseph Smith

Nabii wa Bwana, na David Lindsley

2 Nefi 4:15–35

Ninaweza kumgeukia Mungu katika udhaifu wangu.

Nefi alikuwa punde tu amempoteza baba yake. Jukumu la kuiongoza familia yake sasa lilikuwa juu yake. Alihisi amezingirwa na majaribu na alivunjika moyo kwa sababu ya dhambi zake. Hata kama hali yako ni tofauti na ya Nefi, unaweza kujihusisha na baadhi ya mawazo na hisia zake zilizoandikwa katika 2 Nefi 4:15–35. Ni nini kilichomsaidia Nefi katika mateso yake? Ni kwa namna ipi majibu ya Nefi kwa changamoto zake yanaweza kukusaidia kukabiliana na mapambano yako?

2 Nefi 5

Furaha inapatikana kutokana na kuishi injili.

Je, ni kwa namna ipi unaweza kufafanua furaha? Nefi aliandika kwamba watu wake waliishi “kwa furaha” (2 Nefi 5:27). Unaweza kutafuta chaguzi Nefi na watu wake walizifanya ambazo zilileta furaha—njia ambazo walisaidiana pamoja na familia zao, kile walichothamini katika jamii yao, na kadhalika. Ni nini unajifunza ambacho kinaweza kukusaidia kujenga maisha yenye furaha, jinsi watu wa Nefi walivyofanya?

2 Nefi 5:20–21

Ni laana ipi iliyokuja juu ya Walamani?

Katika wakati wa Nefi laana ya Walamani ilikuwa kwamba wao “waliondolewa kutoka uwepo [wa Bwana] … kwa sababu ya uovu wao” (2 Nefi 5:20–21). Hii ilimaanisha kwamba Roho wa Bwana aliondoka katika maisha yao. Wakati Walamani walipoikubali injili ya Yesu Kristo baadaye, “laana ya Mungu haikuwa kwao tena” (Alma 23:18).

Kitabu cha Mormoni pia kinasema kwamba alama ya ngozi nyeusi iliwekwa juu ya Walamani baada ya Wanefi kujitenga nao. Asili na mwonekano wa alama hii havijajulikana kikamilifu. Mwanzoni alama hiyo iliwatofautisha Walamani kutoka kwa Wanefi. Baadaye, wote wawili Wanefi na Walamani wakati kila mmoja alipopitia nyakati za uovu na haki, alama haikuwa na maana kama kiashirio cha hadhi ya Walamani mbele za Mungu.

Manabii wanathibitisha katika siku zetu kwamba ngozi nyeusi sio ishara ya kutopendwa au laana. Kanisa linashikilia mafundisho ya Nefi kwamba Bwana “hamkatazi yeyote anayemjia, weusi kwa weupe, wafungwa na walio huru, wake kwa waume” (2 Nefi 26:33). Rais Russell M. Nelson alitangaza: “Bwana amesisitiza fundisho Lake muhimu la fursa sawa kwa watoto Wake. … Tofauti za kitamaduni, lugha jinsia, rangi, asili na utaifa hufifia kuwa zisizo muhimu wakati waaminifu wakiingia kwenye njia ya agano na kuja kwa Mkombozi wetu mpendwa” (“Maneno ya Rais Nelson katika Maadhimisho ya Ukuhani Ulimwenguni Kote” [Juni 1, 2018], newsroom.ChurchofJesusChrist.org).

Ona pia “Till We All Come in the Unity of the Faith” (video, ChurchofJesusChrist.org).

Picha
ikoni ya kujifunza kifamilia

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kifamilia na Jioni ya Familia Nyumbani

Unaposoma maandiko na familia yako, Roho anaweza kukusaidia kujua kanuni zipi zisisitizwe na kujadiliwa ili kukidhi mahitaji ya familia yako. Haya ni baadhi ya mawazo.

2 Nefi 1:13–25

Je, aya hizi zinatufundisha nini kuhusu matamanio makuu ya mzazi mwenye haki kwa watoto wake?

2 Nefi 3:6

Someni kwa pamoja “Mwonaji” katika Kamusi ya Biblia. Je, ni jinsi gani Joseph Smith alikuwa mwonaji? Ni kwa nini tuna shukrani kwa kazi ambayo Joseph Smith aliitekeleza? (ona 2 Nefi 3:6–24).

2 Nefi 4:20–25

Mnaposoma 2 Nefi 4:20–25 kwa pamoja, subiri baada ya kila mstari, na waalike wanafamilia washiriki wakati ambapo wamekuwa na uzoefu au wamehisi kile ambacho Nefi anaelezea. Je, Mungu amefanya nini kwa ajili ya familia yetu?

2 Nefi 5

Je, ni baadhi ya njia zipi ambazo familia yako inaishi “kwa furaha”? Familia yako inaposoma 2 Nefi 5, mnaweza kujadiliana vitu ambavyo Wanefi walivithamini: familia (mstari wa 6), amri (mstari wa 10), maandiko (mstari wa 12), elimu (mstari wa 15), mahekalu (mstari wa 16), kazi (mstari wa 17), na miito ya Kanisa (mstari wa 26). Njia moja ya kufanya hivi ni kutafuta vitu ambavyo vinawakilisha baadhi ya vitu hivi na kuzungumza kuhusu jinsi tunavyoonyesha kwamba sisi, kama Wanefi, tunathamini vitu hivyo pia.

Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Msingi.

Kuboresha Ufundishaji Wetu

Kuwa makini. Unapokuwa na usikivu kwa kile kinachotokea maishani mwa watoto wako, utapata fursa nzuri sana za kufundisha. Maoni ambayo watoto hutoa au maswali ambayo wao huuliza yanaweza pia yakawa ni fursa za nyakati za kufundisha. (Ona Kufundisha katika Njia ya Mwokozi,16.)

Picha
Familia ya Lehi ikiwa imepiga magoti ufukoni.

Lehi na Watu Wake Wanawasili katika Nchi Mpya, na Clark Kelley Price

Chapisha