Njoo, Unifuate
Januari 27–Februari 2. 1 Nefi 16–22: “Nitawatayarishia Njia”


“Januari 27–Februari 2. 1 Nefi 16–22: ‘Nitawatayarishia Njia,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Kitabu cha Mormoni 2020 (2020)

“Januari 27–Februari 2. 1 Nefi 16–22,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2020

Lehi akitazama liahona

Lehi na Liahona, na Joseph Brickey

Januari 27–Februari 2

1 Nefi 16–22

“Nitawatayarishia Njia”

Unapojifunza 1 Nefi 16–22, tafuta vifungu vinavyokuvutia. Baadhi ya watu hupendelea kupaka rangi mistari kama hii katika maandiko yao; wengine huandika maelezo pambizoni. Zingatia jinsi utakavyoandika misukumo unayopokea.

Andika Misukumo Yako

Familia ya Nefi ilipokuwa ikisafiri kuelekea nchi ya ahadi, Bwana aliwapatia ahadi hii: “Nitawatayarishia njia, kama mtatii amri zangu” (1 Nefi 17:13). Ni wazi kwamba, ahadi hii haikumaanisha kwamba safari hii ingekuwa rahisi—wanafamilia bado walitofautiana, pinde zilivunjika, na watu walipambana na kufariki, na bado walihitajika kujenga meli kutokana na mali ghafi. Hata hivyo, wakati familia ilikabiliana na shida au kazi zilizoonekana kutowezekana, Nefi alitambua kwamba Bwana kamwe hakuwa mbali. Alijua ya kwamba Mungu “atawalisha [waaminifu], na kuwatia nguvu, na kuwapatia uwezo ili wakamilishe kitu ambacho amewaamuru” (1 Nefi 17:3). Kama umewahi kushangaa kwa nini mambo mabaya hutendeka kwa watu wema kama Nefi na familia yake, unaweza kupata umaizi katika sura hizi. Lakini pengine muhimu zaidi, utaona kile ambacho watu wema hufanya wakati mambo mabaya yanapotendeka.

ikoni ya kujifunza kibinafsi

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kibinafsi

1 Nefi 16–18

Wakati ninapotii amri, Mungu atanisaidia kukabiliana na changamoto.

Sura za 16–18 za 1 Nefi zinaelezea kuhusu changamoto kadhaa ambazo familia ya Nefi ilikabiliana nazo, ikiwa ni pamoja na kukabiliana na upinde uliovunjika (ona 1 Nefi 16:17–32), Kifo cha Ishmaeli (ona 1 Nefi 16:34–39), kujenga merikebu (ona 1 Nefi 17:7–16; 18:1–4), na kutoelewana katika familia (ona 1 Nefi 18:9–22). Ni jinsi gani majibu ya Nefi kwa changamoto hizi yalitofautiana na majibu ya baadhi ya wanafamilia wake? Ni nini kilikuwa matokeo ya majibu haya?

Inaweza kusaidia kuandika kile utakachogundua katika jedwali lenye vichwa vya habari kama hivi: “Changamoto,” “Majibu ya Nefi,” “Majibu ya Wengine,” na “Matokeo.” Unafikiria ni kwa nini Nefi aliweza kusalia mwaminifu wakati wengine walishindwa? Tafakari kuhusu jinsi mfano wa Nefi na familia yake unaweza kukusaidia katika changamoto zako.

Ona pia video zinazohusika katika mkusanyiko wa video za Kitabu cha Mormoni kwenye ChurchofJesusChrist.org au kwenye Gospel Library app.

1 Nefi 16:10–16, 23–31; 18:11–22

Bwana huniongoza kupitia njia ndogo na rahisi.

Wakati Mungu alipoiongoza familia ya Lehi hadi nyikani, hakuwapa mpango mkamilifu kuhusu safari yao ya kuelekea katika nchi ya ahadi. Lakini alimpa Lehi Liahona ya kuiongoza familia yake kila siku hadi mwisho wa safari yao. Ni nini Baba wa Mbinguni amekupa wewe ili kutoa mwongozo na mwelekeo? Je, unafikiri inamaanisha nini kwamba “kwa njia ndogo Bwana anaweza kuleta vitu vikubwa”? (1 Nefi 16:29).

Unaposoma 1 Nefi 16:10–16, 23–31 na 18:11–22, zingatia kutengeneza orodha ya kanuni zinazoonyesha jinsi Mungu anavyowaongoza watoto Wake (kwa mfano, 1 Nefi 16:10 inaweza kufundisha ya kwamba Mungu mara nyingine hutuongoza kupitia njia zisizotarajiwa). Uzoefu gani umekuwa nao kwenye hizi kanuni?

Ona pia Alma 37:7, 38–47; Mafundisho na Maagano 64:33–34.

Lehi akitumia Liahona

Kama Mmejitayarisha Hamtaogopa, na Clark Kelley Price

1 Nefi 19:23–24; 20–22

Naweza “kulinganisha maandiko yote” nami.

Isaya aliandika kwa watoto wote wa Israeli, na Nefi aliona ya kwamba hii ilijumuisha familia yake mwenyewe hasa—na inakujumuisha wewe (ona 1 Nefi 19:23–24). Kuhusu dondoo za Nefi kutoka kwa Isaya, Rais Henry B. Eyring alisema, “Nilisoma maneno ya Isaya … nikiamini ya kwamba Nefi alizichukua zile sehemu za Isaya ambazo mimi, bila ya kuwa na wasi wasi kuhusu matumizi ya tamathali za semi, ningeweza kuzielewa moja kwa moja kana kwamba Bwana alikuwa akisema nami” (“Kitabu cha Mormoni Kitabadili Maisha Yako,” Ensign, Feb. 2004, 10).

Ukiwa na maneno ya Rais Eyring akilini mwako, zingatia maswali kama haya yafuatayo unaposoma sura ya 20–22:

1 Nefi 20:1–9.Ni virai gani katika mistari hii vinaelezea kuhusu wana wa Israeli? Vinawazungumzia namna gani Lamani na Lemueli? Ni maonyo na matumizi gani unapata kwa manufaa yako?

1 Nefi 20:17–22.Ni jinsi gani Bwana aliwaongoza watoto wa Israeli? Ni jinsi gani Aliiongoza familia ya Lehi? Je, Anakuongoza wewe kwa namna gani?

Ni kipi kingine unachopata katika 1 Nefi 20–22 ambacho kinafanya uhisi kana kwamba Bwana alikuwa anazungumza nawe? Ni jinsi gani mawazo ya Nefi katika sura ya 22 yanakusaidia kuelewa utabiri wa Isaya?

1 Nefi 21

Nyumba ya Israeli na Wayunani ni kina nani?

Nyumba ya Israeli ni watu wa uzao wa Yakobo nabii wa Agano la kale, ambaye alipewa jina Israeli na Bwana (ona Mwanzo 32:28; 35:10; ona pia Kamusi ya Biblia, “Israeli”). Bwana alifanya maagano kadhaa pamoja na Israeli, na watu wa uzao wake walichukuliwa kuwa watu wa agano la Mungu. Hata hivyo, vizazi vingi baadaye, wengi wao walimuasi Bwana na hatimaye walitawanywa kote duniani.

Neno Wayunani katika vifungu hivi linahusu watu ambao wangali hawana injili (ona Kamusi ya Biblia, “Myunani”). Isaya alifundisha kwamba katika siku za mwisho Wayunani wangepewa injili na kusaidia katika kufundisha na kukusanya nyumba ya Israeli (ona 1 Nefi 21:22; 22:8–12; ona pia Isaya 60; 66:18–20).

ikoni  ya kujifunza kifamilia.

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kifamilia na Jioni ya Familia Nyumbani.

Unaposoma maandiko na familia yako, Roho anaweza kukusaidia kujua kanuni zipi zisisitizwe na kujadiliwa ili kukidhi mahitaji ya familia yako. Haya ni baadhi ya mawazo.

1 Nefi 17:1–6, 17–22

Pengine familia yako inaweza kutofautisha simulizi ya Nefi ya kusafiri nyikani 1 Nefi 17:1–6) na simulizi ya ndugu zake (ona 1 Nefi 17:17–22). Kwa nini unafikiri waliona matukio yanayofanana katika hali tofauti? Ni nini tunaweza kujifunza kutoka kwa Nefi kuhusu kuwa na mtazamo wa imani?

1 Nefi 17:17–22; 18:9–16

Ni nini matokeo ya wivu, ugomvi, na kunung’unika katika familia? Jinsi gani tunaweza kushinda changamoto hizi?

1 Nefi 19:22–24

Nefi alilinganisha maandiko na familia yake “ili ya[wa]faidishe na ku[wa]elimisha” (1 Nefi 19:23). Kuna hadithi kadhaa katika 1 Nefi 16–18 ambazo familia yako inaweza kuzilinganisha nanyi. Pengine mnaweza kuigiza mojawapo ya hadithi hizi na kujadiliana jinsi inavyofaa familia yenu.

1 Nefi 21:14–16

Ni jinsi gani ujumbe katika mistari hii unaweza kumsaidia mtu ambaye anahisi kwamba amesahaulika?

Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kufundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi.

Kuboresha Kujifunza Kibinafsi.

Muombe Bwana msaada. Maandiko yalitolewa kwa ufunuo, na tunahitaji ufunuo ili kuyaelewa vyema. Bwana ameahidi, “kama … mtaniuliza kwa imani, … kwa kweli vitu hivi vitafanywa vijulikane kwenu” (1 Nefi 15:11).

Nefi na familia yake kwenye merikebu

Na Wakawa Wakali Sana Kwangu, na Walter Rane