“Mei 11–17. Mosia 18–24: ‘Tumeingia Kwenye Agano na Yeye,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Kitabu cha Mormoni 2020 (2020)
“Mei 11–17. Mosia 18–24,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2020
Mei 11–17
Mosia 18–24
Tumeingia kwenye Agano na Yeye
Rais Thomas S. Monson alifundisha, “Tunaposoma na kutafakari maandiko, tutahisi minong’ono mitamu ya Roho katika nafsi zetu” (“Kamwe Hatutembei Peke Yetu,” Ensign au Liahona, Nov. 2013, 122).
Andika Misukumo Yako
Historia ya Alma na Watu Wake katika Mosia 18; 23–24 inaonyesha maana ya “kujiunga na zizi la Mungu” (Mosia 18:8). Wakati walipobatizwa, waliingia katika agano na Mungu la “kumtumikia na kutii amri zake” (Mosia 18:10). Huku hii ikiwa ni ahadi yenye wajibu wa kibinafsi, pia ilihusu jinsi walivyotendeana mmoja kwa mwingine. Ndio, safari ya kurudi kwa Baba wa Mbinguni ni ya binafsi na ya mtu mmoja mmoja, na hakuna anayeweza kutunza maagano yetu kwa niaba yetu, lakini hilo halimaanishi kwamba tuko peke yetu. Sisi sote tunategemeana. Kama waumini wa Kanisa la Kristo, tunaahidi kumtumikia Mungu kwa kusaidiana na kutumikiana katika hii safari, “[tuki]beba mizigo ya mmoja na ya mwingine” (Mosia 18:8–10). Watu wa Alma bila shaka walikuwa na mizigo ya kubeba, jinsi sisi sote tulivyonayo. Na njia moja Bwana hutusaidia “kubeba mizigo [yetu] kwa urahisi” (Mosia 24:15) ni kwa kutupatia jamii ya Watakatifu ambao wameahidi kuomboleza nasi na kutufariji, jinsi ambavyo sisi tumeahidi kuwatendea.
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kibinafsi
Ubatizo unajumuisha agano la kumtumikia Mungu na kusimama kama shahidi Wake.
Mosia 18:8–10 ina mafundisho ya Alma kuhusu agano la ubatizo, au ahadi tunayompa Mungu wakati wa ubatizo. Unaposoma mistari hii, tafakari maswali yafuatayo:
-
Unajifunza nini kutoka kwenye mistari hii kuhusu ahadi ulizofanya wakati wa ubatizo? Mungu anakuahidi nini?
-
Ni kwa jinsi gani agano la kumtumikia Mungu (ona mstari wa 10) linahusiana na juhudi zetu za kumhudumia kila mmoja wetu? (ona mstari wa 8–9).
-
Je, unafanya nini kutunza ahadi zako?
-
Ni kwa jinsi gani kutunza agano lako la ubatizo kunakuwezesha “kujazwa na Roho”? (Mosia 18:14). Je, ni kwa jinsi gani Roho hukusaidia kutunza agano lako?
Historia hii pia inaweka wazi namna sahihi ya kubatiza. Ni nini unajifunza katika mistari 14–17 kuhusu jinsi ubatizo unavyopaswa kufanywa? Ni kipi tena unajifunza kuhusu ubatizo kutoka Mathayo 3:16; Warumi 6:3–5; 3 Nefi 11:21–28; na Mafundisho na Maagano 20:72–74?
Ona pia Mafundisho na Maagano 20:37, 77, 79.
Watu wa Mungu wanapaswa kuungana.
Kama Alma na watu wake walivyogundua, kumfuata Yesu Kristo wakati mwingine ina maanisha kuacha mwenendo wa maisha uliouzoea kwa ajili ya kitu kipya na tofauti. Lakini watu wa Alma walipata nguvu kutoka kwa kila mmoja kama sehemu ya “Kanisa la Kristo” (Mosia 18:17). Ni kwa jinsi gani mafundisho katika Mosia 18:17–30 yanakutia msukumo kuwa muumini mzuri wa Kanisa? Unaweza kufanya nini kusaidia washiriki wa kata au tawi lako “kuunganishwa pamoja kwa umoja na kwa upendo”? (Mosia 18:21).
Ona pia Henry B. Eyring, “Mioyo Yetu Ikiunganishwa kwa Umoja,” Ensign au Liahona, Nov. 2008, 68–71.
Maneno ya manabii yatatimizwa.
Abinadi alitoa unabii maalum kuhusu kile ambacho kingemtokea Mfalme Nuhu na watu wake kama wangekataa kutubu. Hata hivyo, kwa baadhi unabii huu ulionekana usio wa kuaminika (ona Mosia 12:1–8, 14–15), hasa kwa sababu Wanefi walikuwa wamefanikiwa kujilinda wao wenyewe dhidi ya Walamani kwa takribani miaka 50 (ona Mosia 9:16–18; 11:19). Lakini maneno ya manabii yote yatatimizwa—katika siku zetu kama ilivyofanyika katika siku za Abinadi.
Unapata nini katika Mosia 19–20 ambacho kingemsababisha Gideoni kutangaza kwamba unabii wa Abinadi ulikuwa umetimizwa? (ona Mosia 20:21). Ni kwa jinsi gani historia hii inaimarisha imani yako katika maonyo na ushauri wa manabii wa Mungu na kujitolea kwako kufuata maneno yao? Ni wakati gani umeshuhudia maneno ya manabi yakitimizwa katika siku yetu?
Mungu anaweza kufanya mizigo yangu iwe miepesi.
Watu wa Limhi na watu wa Alma wote walijikuta katika utumwa, ingawaje kwa sababu tofauti na katika hali tofauti. Unaweza kujifunza nini kwa kulinganisha historia za watu wa Limhi katika Mosia 19–22 na watu wa Alma katika Mosia 18; 23–24? Ungeweza kuona jinsi kila moja ya makundi haya yalivyoathirika kwa utumwa au jinsi kila moja mwishowe walivyokombolewa. Unapofanya hivyo, tafuta jumbe ambazo zinafaa katika maisha yako. Kwa mfano, unajifunza nini kutokana na historia hizi ambacho kitakusaidia kubeba mizigo yako?
Ninaweza kumwamini Bwana.
Ingawaje walikuwa wametubu dhambi zao, Alma na watu wake bado walijikuta katika utumwa. Uzoefu wao unaonyesha kwamba kumwamini Bwana na kuishi maagano yetu hakutazuia changamoto kila wakati, lakini kunatusaidia kuzishinda. Unaposoma Mosia 23:21–24 na 24:8–17, tilia maanani maneno na virai ambavyo vinaweza kukusaidia kujifunza kumwamini Mungu, bila ya kujali hali zako.
Ona pia Thomas S. Monson, “Sitakupungukia, Wala Sitakuacha,” Ensign au Liahona, Nov. 2013, 85–87.
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kifamilia na Jioni ya Familia Nyumbani
Unaposoma maandiko na familia yako, Roho anaweza kukusaidia kujua kanuni zipi zisisitizwe na kujadiliwa ili kukidhi mahitaji ya familia yako. Haya ni baadhi ya mawazo.
Mosia 18:1–4
Kuna usemi kwamba unaweza kuhesabu mbegu zilizoko ndani ya tufaha, lakini hauwezi kuhesabu matufaha yanayotokana na mbegu moja. Ni mtu mmoja tu alikubali ushuhuda wa Abinadi, lakini mtu huyo mmoja—Alma—alishawishi vizazi vya Wanefi. Pengine ungeweza kutumia tunda lililo na mbegu kuelezea kanuni hii. Je, ushauri huu unatumika vipi katika familia yetu? Tunaweza kufanya nini ili kushiriki shuhuda zetu na wengine?
Mosia 18:8–10
Nini tunaweza kujifunza kuhusu agano letu la ubatizo kutoka kwenye mistari hii? (Ona pia M&M 20:73, 77–79). Je, tunafanya nini ili kujitayarisha kwa ajili ya kufanya au kutunza agano letu la ubatizo?
Mosia 18:30
Ni mahali gani pana maana maalum kwetu kwa sababu ya matukio ya kiroho tuliyokuwa nayo mahali pale?
Mosia 21:11–16; 24:10–15
Tunajifunza nini kwa kulinganisha utumwa wa watu wa Alma na watu wa Limhi?
Mosia 21:15; 24:11–15
Ni nini mistari hii inatufundisha kuhusu baadhi ya njia ambazo Bwana hujibu sala?
Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Msingi.