“Mei 4–10. Mosia 11–17: ‘Nuru … Ambayo Haiwezi Kuwekwa Giza,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Kitabu cha Mormoni 2020 (2020)
“Mei 4–10. Mosia 11–17,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2020
Mei 4–10
Mosia 11–17
“Nuru … Ambayo Haiwezi Kuwekwa Giza”
Maneno ya Abinadi yalisababisha mabadiliko makuu angalau katika mshiriki mmoja wa mahakama ya Mfalme Nuhu (ona Mosia 17:2–4). Soma Mosia 11–17 kwa sala moyoni mwako kwamba uweze kupokea misukumo kuhusu jinsi unavyoweza kubadilika.
Andika Misukumo Yako
Moto mkubwa unaweza kuanzishwa na cheche moja. Abinadi alikuwa mtu mmoja tu ambaye alikuwa akishuhudia dhidi ya mfalme mwenye nguvu na mahakama yake. Maneno yake yalikataliwa kwa sehemu kubwa, na alihukumiwa kifo. Lakini ushuhuda wake wa Yesu Kristo, ambaye ni “nuru … ambayo haiwezi kuwekwa giza” (Mosia 16:9), ulichochea kitu fulani ndani ya kuhani kijana Alma. Na cheche hiyo ya kuongoka ilikua pole pole Alma alipokuwa akiwaleta wengi kwenye toba na imani katika Yesu Kristo. Miale ambayo ilimuua Abinadi hatimaye ilizima, lakini moto wa imani ambao maneno yake yalisababisha ungekuwa na ushawishi mkubwa juu ya Wanefi—na juu ya wale wanaosoma maneno yake leo. Wengi wetu kamwe hatutakabiliana na kile hasa alichokabiliana nacho Abinadi kwa sababu ya shuhuda zetu, lakini sote tunazo nyakati ambapo kumfuata Yesu Kristo ni mtihani wa ujasiri na imani yetu. Pengine kujifunza ushuhuda wa Abinadi kutapuliza miale ya moto wa ushuhuda na ujasiri moyoni mwako pia.
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kibinafsi
Ninaweza kutetea ukweli, hata ninaposimama peke yangu.
Fikiria jinsi ambavyo ilivunja moyo kwa Abinadi kuhubiri toba kwa watu ambao kamwe hawakuonekana kuwa na hamu ya kubadili njia zao za uovu. Ujumbe wake ulikataliwa tena na tena. Lakini Abinadi hakukata tamaa.
Ni lini ulihisi kuwa unasimama peke yako katika kutetea ukweli? Unaposoma Mosia 11–13 na 17, ni nini unachojifunza ambacho kinaweza kukusaidia kuwa tayari wakati ambapo Bwana anakuhitaji utetee injili Yake? Ni kanuni zipi zinginezo unazojifunza kutoka kwenye mfano wa Abinadi?
Nahitaji kuandaa moyo wangu kuelewa neno la Mungu.
Makuhani wa Nuhu walifahamu neno la Mungu—waliweza kudondoa vifungu vya maandiko na walidai kufundisha amri. Lakini amri hizo “hazikuandikwa mioyoni [mwao] ,” na “hawakujitolea mioyo [yao] kwa ufahamu” (Mosia 13:11; 12:27). Kama matokeo, maisha yao hayakubadilika.
Unaposoma Mosia 12:19–30, tafakari maana ya kujitolea moyo kwa ufahamu wa neno la Mungu. Je, hili linakutia msukumo ufanye mabadiliko yoyote katika jinsi unayojifunza injili?
Bwana atawaidhinisha watumishi Wake katika kufanya kazi Yake.
Kwa upande mmoja, tukio la Abinadi linaonyesha mifano mingi ya jinsi ambavyo Bwana anawasaidia watumishi wake—unaweza kupata mifano kadhaa kama hii katika Mosia 13:1–9. Kwa upande mwingine, Bwana pia alimruhusu Abinadi kuteswa, kufungwa, na kuuwawa kwa ushuhuda wake. Ni kipi unachopata katika mistari hii ambacho kinaonyesha kwamba Abinadi alimwamini Bwana? Ni kwa jinsi gani mfano wa Abinadi unaathiri jinsi unavyotazama miito na majukumu yako?
Yesu Kristo aliteseka kwa ajili yangu.
Mfalme Nuhu na makuhani wake waliamini ya kwamba wokovu huja kupitia sheria ya Musa. Abinadi alitaka wafahamu kwamba wokovu huja kupitia kwa Masiya, Yesu Kristo. Katika Mosia 14–15, tambua maneno na virai vinavyomuelezea Mwokozi na mateso aliyopitia kwa ajili yako. Ni mistari gani inasaidia kufanya upendo na shukrani zako Kwake kuwa za kina?
Ni kwa namna gani Yesu Kristo ni wote Baba na Mwana?
Vifungu hivi mara nyingine hukanganya kwa sababu yaweza kuonekana kwamba Abinadi anafundisha kwamba Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo ni Kiumbe mmoja, lakini tunajua kwamba wao ni Viumbe tofauti. Abinadi alimaanisha nini? Alifundisha kwamba Mungu Mwana—Yehova—angekuwa Mkombozi (ona Mosia 15:1), akiwa na mwili, na kuwa sehemu binadamu na sehemu Mungu (mistari 2–3). Alijitolea kikamilifu kwa nia ya Mungu Baba (mistari 5–9). Kwa sababu ya kufanya hivi, Yesu Kristo ni wote Mwana wa Mungu na mfano kamili wa Mungu Baba duniani (ona Yohana 14:6–10).
Abinadi aliendelea kwa kuelezea kwamba Yesu Kristo pia ni Baba kwa namna kwamba wakati tunapokubali ukombozi Wake, tunakuwa “uzao wake” (Mosia 15:11–12). Hi ina maana kuwa, tunazaliwa tena kiroho kupitia Kwake (ona Mosia 5:7).
Ona pia Yohana 5:25–27; 8:28–29; 17:20–23; “Baba na Mwana,” Ensign, Apr. 2002, 12–18.
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kifamilia na Jioni ya Familia Nyumbani
Unaposoma maandiko na familia yako, Roho anaweza kukusaidia kujua kanuni zipi zisisitizwe na kujadiliwa ili kukidhi mahitaji ya familia yako. Haya ni baadhi ya mawazo.
Mosia 11–13; 17
Abinadi na Alma ni mifano ya kutia msukumo wa kuwa mwaminifu kwenye ukweli, hata wakati kufanya hivyo hakupendwi na wengi. Washiriki wa familia yako wanaweza kuwa wakikabiliana na shinikizo la jamii kusaliti maadili yao. Ni nini wanaweza kujifunza kutoka kwa Abinadi na Alma kuhusu kutetea ukweli? Picha inayoambatana na muhtasari huu inaweza kusaidia familia yako kupata taswira ya historia hii. Baada ya kujifunza sura hizi, zingatia kuigiza hali halisi za maisha ili washiriki wa familia yako waweze kufanya mazoezi ya kujibu shinikizo la kusaliti maadili yao. Au mnaweza kushiriki na kila mmoja uzoefu ambao mmepitia katika kutetea ukweli.
Mosia 12:33–37; 13:11–24
Inamaanisha nini kuwa na amri za Mungu zikiwa “zimeandikwa mioyoni [mwetu]? (Mosia 13:11). Pengine unaweza kuandika baadhi ya mawazo (au kuchora picha ya mawazo yako) kwenye karatasi kubwa lenye umbo la moyo. Kwa nini amri ni muhimu kwetu? Tunawezaje kuziandika mioyoni mwetu?
Mosia 14
Katika sura hii utapata maneno na virai kadhaa ambavyo vinamuelezea Yesu Kristo. Pengine familia yako inaweza kuviorodhesha huku ukivitafuta. Washiriki wa familia wanahisi vipi kuhusu Mwokozi tunapojifunza maneno na virai hivi?
Mosia 15:26–27; 16:1–13
Mistari hii inaelezea kile ambacho kingetokea kwa watoto wa Mungu kama Yesu “hangekuja ulimwenguni” (Mosia 16:6) au kama hawangemfuata. Ni mambo gani mazuri ambayo yametendeka kwa sababu alikuja na kutupatanisha? Ona pia video “Why We Need a Savior” (ChurchofJesusChrist.org).
Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kufundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi.