Njoo, Unifuate
Aprili 27–Mei 3. Mosia 7–10: “Kwa Nguvu za Bwana”


“Aprili 27–Mei 3. Mosia 7–10: ‘Kwa Nguvu za Bwana,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Kitabu cha Mormoni 2020 (2020)

“Aprili 27–Mei 3. Mosia 7–10,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2020

Amoni akimfundisha Mfalme Limhi

Minerva K. Teichert (1888-1976), Amoni mbele ya Mfalme Limhi, 1949-1951, mafuta juu ya ubao, inchi 35 15/16 x 48. Jumba la Makumbusho ya Sanaa la Brigham Young, 1969.

Aprili 27–Mei 3

Mosia 7–10

“Kwa Nguvu za Bwana”

Unaposoma, Roho anaweza kuvuta usikivu wako kwenye virai au vifungu fulani vya maandiko. Andika jinsi unavyohisi kwamba vifungu hivyo vya maandiko vinakuhusu.

Andika Misukumo Yako

Wakati watu wa Mfalme Mosia walikuwa wakifurahia “kuendelea kuwa na amani” kule Zarahemla (Mosia 7:1), mawazo yao yaligeukia kundi lingine la Wanefi, ambalo miaka mingi iliyopita walikuwa wameondoka kwenda kuishi katika nchi ya Lehi-Nefi. Vizazi vingi vilikuwa vimepita, na watu wa Mosia hawakuwa na habari zozote kuwahusu. Kwa hiyo Mosia alimuomba Amoni akiongoze kikundi cha watafutaji kwenda kuwatafuta Wanefi ambao walikuwa wameondoka. Kikundi cha watafutaji kiligundua ya kwamba wale Wanefi, “kwa sababu ya uovu” (Mosia 7:24), walikuwa katika utumwa kwa Walamani. Lakini kwa kuwasili kwa Amoni na ndugu zake, ghafula kulikuwa na matumaini ya ukombozi.

Wakati mwingine tuko sawa na Wanefi hawa waliokuwa katika utumwa, tukiteseka kwa sababu ya dhambi zetu, tukiwaza ni kwa jinsi gani tutapata amani tena. Wakati mwingine sisi ni kama Amoni, tunahisi kutiwa msukumo kuwafikia wengine na hatimaye kugundua kwamba juhudi zetu zimewatia msukumo “kuinua vichwa [vyao], na kusherehekea, na kuweka imani [yao] kwa Mungu” (Mosia 7:19). Haijalishi hali zetu, sisi sote tunahitaji kutubu na “kumrudia Bwana kwa moyo wa lengo moja,” tukiwa na imani kwamba “ata … tuokoa [sisi]”(Mosia 7:33).

ikoni ya kujifunza kibinafsi

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kibinafsi

Mosia 7:14–33

Ikiwa nitamgeukia Bwana, kumwamini, na kumtumikia, atanikomboa.

Kukutana na Amoni, ambaye alikuwa Mnefi kutoka Zarahemla, kulimpa Mfalme Limhi cheche ya matumaini, na alitaka kuwapa watu wake matumaini hayo. Unaposoma Mosia 7:14–33, tilia maanani kile ambacho Limhi aliwaambia watu wake ili kuwatia moyo, kuimarisha imani yao, na kuwapa matumaini kwamba Mungu angewasaidia. Ingawaje haujatenda dhambi sawa na zile za watu wa Limhi, ni jinsi gani maneno yake yanaweza kukusaidia kumrudia Bwana? Utatambua, kwa mfano, kwamba Limhi aliwakumbusha watu wake kuhusu historia ya nyuma ya ukombozi wa Mungu (ona mistari 18–20). Ni jinsi gani historia hizi, vile vile historia nyingine katika maandiko au za kibinafsi, zinakusaidia kumwamini Mungu?

Mosia 8:5–12

Zile bamba 24 zilizopatikanana watu wa Limhi zilikuwa nini?

Wakati kundi dogo la watu wa Limhi walikuwa wakitafuta na kushindwa kuipata nchi ya Zarahemla, walipata bamba 24 za dhahabu zenye michoro katika lugha ambayo haikufahamika. Bamba hizi, ambazo hatimaye zilitafsiriwa na Mfalme Mosia, zilizungumzia kuwahusu watu ambao waliitwa Wayaredi, ambao walikuja katika nchi ya ahadi kutoka katika Mnara wa Babeli na mwishowe waliangamizwa (ona Mosia 28:11–19). Baadaye Moroni alitengeneza ufupisho wa bamba hizi (ona Etheri 1:1–2), ambao ulikuja kuwa Kitabu cha Etheri. Zingatia katika Mosia 28:18 athari za kumbukumbu hii juu ya watu wa Mosia.

Mosia 8:12–19

Bwana anatupatia manabii, waonaji, na wafunuzi kwa faida ya binadamu.

Wakati Limhi aliposikia ushuhuda wa Amoni kwamba Bwana alikuwa amemwinua mwonaji, Limhi, “alifurahia sana, na akamshukuru Mungu” (Mosia 8:19). Kwa nini unafikiri alihisi hivyo? Unajifunza nini juu ya waonaji kutokana na maneno ya Amoni katika Mosia 8:13–19? Katika siku yetu, “Urais wa Kwanza na Akidi ya Mitume Kumi na Wawili wanaidhinishwa kama manabii, waonaji, na wafunuzi” (Kamusi ya Biblia, “Mwonaji”). Ni lini ilikuwa mara ya mwisho ulipotafakari kuhusu baraka ya kuwa na manabii, waonaji, na wafunuzi duniani? Pengine ungeweza kuandika jinsi ambavyo manabii, waonaji, na wafunuzi wamekuwa “faida kubwa” kwako (Mosia 8:18).

Nabii Joseph Smith ndiye mwonaji mkuu anayesimama kileleni mwa kipindi chetu cha maongozi ya Mungu (ona M&M 21:1; 124:125; Joseph Smith—Historia ya 1:62). Je, ni kwa jinsi gani aliweza kuonyesha kwa mfano maelezo ya Amoni kuhusu mwonaji wakati wa huduma yake?

Mosia 9–10

Ninaweza kukabiliana na changamoto zangu “kwa Nguvu za Bwana.”

Zenivu alikiri ya kwamba alikuwa amefanya makosa. Wakati mwingine alikuwa mwenye ari kubwa sana, na alikuwa amewaweka watu wake—mababu wa watu wa Limhi—katika hali ngumu kwa kufanya maafikiano mabaya na Mfalme Lamani. Lakini baadaye, wakati alipokwenda kupigana dhidi ya Walamani, aliwasaidia watu wake kukabiliana na changamoto zao kwa imani. Unaposoma Mosia 9–10, angalia kile watu wa Zenivu walichofanya ili kuonyesha imani yao. Je, Mungu aliwaimarishaje? Je, inamaanisha nini kwako kusonga mbele “kwa Nguvu za Bwana”? (Mosia 9:17; 10:10–11).

Mosia 10:11–17

Chaguzi zangu zinaweza kuathiri vizazi.

Kulingana na Mosia 10:11–17, ni kwa jinsi gani vitendo na tabia za mababu wa Walamani viliwazuia Walamani kutojua ukweli? Ni kwa jinsi gani vitendo vya mababu wa Walamani viliathiri vizazi vya siku za baadae? Fikiria kuhusu watu ambao wanaweza kuathiriwa na imani na chaguzi zako; unafanya nini kuwasaidia kikamilifu ili wawe na imani katika Kristo?

ikoni ya kujifunza kifamilia

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kifamilia na Jioni ya Familia Nyumbani

Unaposoma maandiko na familia yako, Roho anaweza kukusaidia kujua kanuni zipi zisisitizwe na kujadiliwa ili kukidhi mahitaji ya familia yako. Haya ni baadhi ya mawazo.

Mosia 7:19–20

Tilia maanani mifano ambayo Limhi alitoa ili kuwahimiza watu wake wawe na imani. Ni mifano gani kutoka katika maandiko inatutia msukumo ili “tuweke imani yetu kwa Mungu”? Inamaanisha nini kuweka imani yetu kwa Mungu? (ona pia Mosia 9:17; 10:19). Ni simulizi gani kutoka maishani mwetu au maishani mwa mababu zetu tunaweza kushiriki ili kuchochea imani kubwa kwa Mungu?

Mosia 7:26–27

Ni nini tunajifunza kuhusu Mwokozi kutoka kwenye mistari hii? (ona pia M&M 130:22). Je, ni kwa nini tuna shukrani kuyafahamu mambo haya?

Mosia 8:13–18

Ili kuweza kuwasaidia wanafamilia kuelewa mwonaji ni nani, pengine ungeweza kuwaonyesha picha za vifaa ambavyo vinatusaidia kuona vitu ambavyo vinginevyo hatungeweza kuviona, kama vile darubini, au hadubini. Je, ni kwa jinsi gani vifaa hivi ni kama mwonaji? (ona Musa 6:35–36). Ni nini waonaji wanaweza kuona ambacho sisi hatuoni? Ni ushahidi gani tunao kwamba Joseph Smith alikuwa mwonaji?

Ungeweza kuonyesha picha za manabii, waonaji, na wafunuzi wetu walio hai na uwaulize wanafamilia wako kile wanachofahamu kuwahusu. Je, ni kwa jinsi gani tunawafuata?

Mosia 9:14–18; 10:1–10

Wakati Walamani walipofanya uvamizi, watu wa Zenivu walikuwa tayari kimwili na kiroho. Je, tunaweza kujifunza nini kutoka kwa Zenivu na watu wake kuhusu kujitayarisha kwa ajili ya changamoto?

Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Msingi.

Kuboresha Kujifunza Kibinafsi.

Tafuta umaizi wako mwenyewe wa kiroho. Muhtasari huu unapendekeza vifungu na kanuni unazoweza kuzifokasia, lakini usiruhusu mapendekezo haya yakuwekee mipaka kwenye kujifunza kwako. Ungeweza kuvutiwa na mistari au kugundua kanuni ambazo hazijatajwa hapa. Mruhusu Roho akuongoze.

Joseph Smith na Moroni

Ono kwa Joseph Smith, na Clark Kelley Price