Njoo, Unifuate
Mei 18–24. Mosia 26–28: “Waliitwa Watu wa Mungu”


“Mei 18–24. Mosia 25–28: ‘Waliitwa Watu wa Mungu,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Kitabu cha Mormoni 2020 (2020)

“Mei 18–24. Mosia 25–28,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2020

malaika akiwatokea Alma na wana wa Mosia

Kuongoka kwa Alma Mdogo, na Gary L. Kapp

Mei 18–24

Mosia 25–28

“Waliitwa watu wa Mungu”

Baada ya “sauti ya Bwana kumjia [Alma],” aliandika mambo ambayo Bwana alimwambia “ili awe nayo” (Mosia 26:13, 33). Ni kwa jinsi gani utafuata mfano wa Alma?

Andika Misukumo Yako

Baada ya karibia vizazi vitatu kuishi katika nchi tofauti, Wanefi walikuwa kitu kimoja tena. Watu wa Limhi, watu wa Alma, na watu wa Mosia—hata watu wa Zarahemla, ambao hawakuwa wa ukoo wa Nefi—sasa pia wote “walihesabiwa pamoja na Wanefi” (Mosia 25:13). Wengi wao pia walitaka kuwa waumini wa Kanisa ambalo Alma alikuwa ameanzisha. Kwa hiyo wowote “waliotaka kulichukua jina la Kristo” walibatizwa, “na waliitwa watu wa Mungu” (Mosia 25:23–24). Baada ya miaka mingi ya vita na utumwa, ilionekana kwamba hatimaye Wanefi wangelifurahia kipindi cha amani.

Lakini baada ya muda mfupi, wasioamini walianza kuwatesa Watakatifu. Kilichosababisha hasa tukio hili kuwa la huzuni zaidi ilikuwa kwamba wengi wa hawa wasioamini walikuwa watoto wa walio amini—“uzazi mchanga” (Mosia 26:1), ikiwa ni pamoja na wana wa Mosia na mwana mmoja wa Alma. Kisha muujiza ukatokea, na historia ya muujiza huo imewapa matumaini wazazi wenye maumivu makali kwa vizazi vingi. Lakini hadithi ya kuongoka kwa Alma siyo tu kwa ajili ya wazazi wenye watoto wapotevu. Kuongoka kwa kweli ni muujiza ambao, katika njia moja au nyingine, unahitaji kutendeka ndani ya kila mmoja wetu.

ikoni ya kujifunza kibinafsi

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kibinafsi

Mosia 26:1–6

Ninawajibika kwa imani yangu na ushuhuda wangu mwenyewe.

Wale ambao walisikiliza hotuba ya Mfalme Benyamini walihisi kuongoka kwa ajabu (ona Mosia 5:1–7), lakini kuongoka ni tukio la kibinafsi ambalo haliwezi kutolewa kama urithi kwa watoto wa mtu fulani. Ni lazima sote tupate uzoefu wetu wenyewe wa kuongoka kwenye injili ya Yesu Kristo. Unaposoma katika Mosia 26:1–6 kuhusu “uzazi mchanga” wa Wanefi wasioamini, tambua matokeo ya kutoamini kwao. Ungeweza pia kufikiria kuhusu watu ambao unatamani ungeweza kuwaleta kwa Kristo. Huku ukiwa hauwezi kuwapa uongofu wako, Roho anaweza kukunong’onezea vitu unavyoweza kufanya kuwasaidia wapate imani. Unaposoma katika Mosia 25–28 kuhusu namna Alma na waumini wengine wa Kanisa walivyousaidia uzazi mchanga, mawazo mengine yanaweza kukujia.

Ona pia Mafundisho na Maagano 68:25–29.

Mosia 26:6–39

Watumishi waaminifu wa Mungu hutafuta kufanya mapenzi Yake.

Wakati mwingine tunaweza kufikiria kwamba kiongozi wa Kanisa kama Alma daima anafahamu kitu sahihi cha kufanya. Katika Mosia 26 tunasoma kuhusu shida Kanisani ambayo Alma hakuwahi kukumbana nayo na “aliogopa kwamba atafanya vibaya mbele ya Mungu” (Mosia 26:13). Alma alifanya nini katika hali hii? (ona Mosia 26:13–14, 33–34, 38–39). Tukio hili la Alma linapendekeza nini kuhusu jinsi unavyoweza kutatua shida ngumu katika familia yako au katika huduma yako Kanisani?

Ingeweza pia kuwa ya kupendeza kuorodhesha kweli ambazo Mungu alimfunulia Alma, zinazopatikana katika Mosia 26:15–32. Tambua kwamba baadhi ya kweli hizi hazikuwa katika jibu la moja kwa moja kwa swali la Alma. Hii inapendekeza nini kwako kuhusu sala na kupokea ufunuo binafsi?

Mosia 27:8–37

Watu wote waume kwa wake hawana budi kuzaliwa mara ya pili.

Ilikuwa wazi kwamba Alma Mdogo, alihitaji kuzaliwa tena kiroho, kwa kuwa yeye na wana wa Mosia walikuwa “wenye dhambi mbovu zaidi,” ambao walikwenda “ili waangamize kanisa la Mungu” (Mosia 28:4; 27:10). Lakini punde baada ya kuongoka kwake, Alma alishuhudia kwamba uongofu upo—na ni muhimu—kwa kila mtu: “Usishangae,” alisema, “kwamba wanadamu wote … lazima wazaliwe mara ya pili” (Mosia 27:25; msisitizo umeongezwa). Hiyo, bila shaka, inakujumuisha wewe.

Unaposoma kuhusu uzoefu wa Alma, unaopatikana katika Mosia 27:8–37, ungeweza kujaribu kujiweka katika nafasi yake. Siyo kwamba unajaribu kuangamiza Kanisa, lakini hakika unaweza kufikiria juu ya mambo kuhusu wewe ambayo yanahitaji kubadilishwa. Nani, kama baba yake Alma, anakusaidia na kusali kwa ajili yako “kwa imani kubwa”? Ni uzoefu gani umesaidia “kukusadikisha [wewe] kuhusu uwezo na mamlaka ya Mungu”? (Mosia 27:14). Ni “vitu vikuu” gani Bwana amekutendea wewe au familia yako ambavyo mnapaswa “kukumbuka”? (Mosia 27:16). Unajifunza nini kutoka kwenye maneno na vitendo vya Alma Mdogo kuhusu maana ya kuzaliwa mara ya pili? Maswali kama haya yanaweza kukusaidia kutathmini maendeleo yako katika mchakato wa kuzaliwa mara ya pili.

Ona pia Mosia 5:6–9; Alma 36; “Uongofu” (Mada za Injili, topics.ChurchofJesusChrist.org).

Alma Mdogo akibebwa hadi nyumbani kwa baba yake

Baba Yake Alifurahia, na Walter Rane

Mosia 27:14, 19–24

Mungu anasikia maombi yangu na atayajibu kulingana na Mapenzi Yake.

Pengine unamjua mzazi aliye katika hali kama ya Alma Mzee, ambaye mwana au binti yake anafanya chaguzi mbovu. Au wewe ni mzazi huyo. Unapata nini katika Mosia 27:14, 19–24 ambacho kinakupa tumaini? Ni kwa jinsi gani mistari hii inaweza kushawishi sala zako kwa niaba ya wengine?

ikoni  ya kujifunza kifamilia

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kifamilia na Jioni ya Familia Nyumbani

Unaposoma maandiko na familia yako, Roho anaweza kukusaidia kujua kanuni zipi zisisitizwe na kujadiliwa ili kukidhi mahitaji ya familia yako. Haya ni baadhi ya mawazo.

Mosia 25:5–11

Watu wa Mosia walihisi vipi baada ya yeye kuwasomea kumbukumbu za watu wa Zenivu na watu wa Alma? Je, familia yako ina kumbukumbu zozote ambazo mnaweza kusoma? Pengine mngeweza kuongezea kwenye kumbukumbu zenu au uanze kuandika yako mwenyewe. Unaweza kujumuisha nini ambacho kinaweza kuisaidia familia yako, (ikiwa ni pamoja na vizazi vijavyo) “kujazwa na shangwe kuu zaidi” na kujifunza kuhusu “wema wa Mungu ulio kamili”? (Mosia 25:8, 10).

Mosia 25:16

Kwa nini ilikuwa muhimu kwa watu wa Limhi kukumbuka kuwa Bwana alikuwa amewakomboa kutoka kwenye utumwa? Ni nini Bwana ametutendea ambacho tunapaswa kukumbuka?

Mosia 26:29–31; 27:35

Kulingana na mistari hii, ni nini mtu lazima afanye ili asamehewe?

Mosia 27:21–24

Unaposoma mistari hii, fikiria mtu ambaye familia yako inaweza kusali na kufunga kwa ajili yake.

Mosia 27–28

Ili kuisaidia familia yako kupata taswira ya historia zilizopo katika sura hizi, ungeweza kuwaalika kuchora picha za watu waliohusika na kutumia picha hizo kusimulia hadithi hiyo tena. Au wangeweza kufurahia kuigiza hadithi hiyo; ni jinsi gani wanaweza kuonyesha badiliko ambalo Alma na wana wa Mosia walipitia?

Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Msingi.

Kuboresha Ufundishaji Wetu

Tumia sanaa.Kitabu cha Sanaa ya Injili na WSM Maktaba ya Vyombo vya habari kwenye ChurchofJesusChrist.org zina picha nyingi na video ambazo zinaweza kusaidia [familia yako] kupata taswira ya dhana au matukio” (Kufundisha katika Njia ya Mwokozi, 22).

malaika akimtokea Alma Mdogo

Kielelezo cha malaika akimtokea Alma Mdogo na Kevin Keele