Mlango wa 14
Isaya huzungumza kuhusu Masiya—Manyanyaso na mateso ya Masiya yanafafanuliwa—Anatoa nafsi Yake kama malipo ya dhambi na kutetea wanaovunja sheria—Linganisha Isaya 53. Karibia mwaka 148 K.K.
1 Ndiyo, si hata Isaya anasema: Ni nani ambaye ameamini ujumbe wetu, na ni kwa nani mkono wa Bwana umefunuliwa?
2 Kwani atakua mbele yake kama mmea mwororo, na kama mzizi kutoka nchi kavu; hana umbo nzuri wala urembo; na tutakapomuona hana urembo wa kutuvutia.
3 Amechukiwa na kukataliwa na watu; mtu wa huzuni, na aliyezoea huzuni; na tukaficha nyuso zetu kutoka kwake; alichukiwa, na hatukumheshimu.
4 Kwa hakika amechukua ghamu zetu, na kubeba huzuni zetu; na tulimdhania kuwa amepigwa, na Mungu, na kuteswa.
5 Lakini alijeruhiwa kwa makosa yetu, alichubuliwa kwa maovu yetu; adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake; na kwa mapigo yake tunaponywa.
6 Sisi sote, kama kondoo, tumepotea; kila mmoja wetu amegeukia njia yake; na Bwana amemwekea maovu yetu sisi sote.
7 Alidhulumiwa, na aliteswa, lakini hakufungua kinywa chake; yeye analetwa kama mwanakondoo machinjoni, na kama vile kondoo ni bubu mbele ya wanaokata manyoya yake hakufungua kinywa chake.
8 Alichukuliwa kutoka gerezani na kutoka kwenye hukumu; na ni nani atatangaza uzazi wake? Kwani aliondolewa kutoka nchi ya wanaoishi; kwa makosa ya watu wangu alipigwa.
9 Na kaburi lake lilikuwa pamoja na waovu, na matajiri kifoni mwake; kwa sababu hakuwa ametenda uovu wowote, wala hapakuwa na uwongo wowote kinywani mwake.
10 Lakini Bwana alipendezwa kumchubua; amemhuzunisha; utakapotoa nafsi yake kuwa dhabihu ya dhambi ataona uzao wake, ataongeza siku zake, na mapenzi ya Bwana yatafanikiwa mkononi mwake.
11 Ataona taabu ya nafsi yake, na kuridhika; kwa maarifa yake mtumishi wangu mwenye haki atawafanya wengi kuwa wenye haki; kwani atayachukua maovu yao.
12 Kwa hivyo nitamgawia sehemu pamoja na wakuu, na atagawanya nyara pamoja na mashujaa; kwa sababu ametoa nafsi yake hata kufa; na akahesabiwa na wenye dhambi; na alibeba dhambi za wengi, na kuwatetea wenye dhambi.