Mlango wa 6
Mfalme Benjamini anaandika majina ya watu na kuwateua makuhani wa kuwafundisha—Mosia anatawala akiwa mfalme wa haki. Karibia mwaka 124–121 K.K.
1 Na sasa, mfalme Benjamini alifikiria ni vyema, baada ya kumaliza kuongea kwa watu wake, kwamba achukue majina ya wale wote ambao walikuwa wameingia kwenye agano na Mungu kutii amri zake.
2 Na ikawa kwamba hapakuwa yeyote, ila tu watoto wadogo, ambao hawakuingia kwenye agano na kujitundika jina la Kristo.
3 Na tena, ikawa kwamba wakati mfalme Benjamini alipomaliza vitu hivi vyote, na kumtawaza mwana wake Mosia kuwa mtawala na mfalme wa watu wake, na kumpatia masharti yote kuhusu ule ufalme, na pia kuteua makuhani wafundishe watu, ili wasikie na kujua amri za Mungu, na kuwachochea ili wakumbuke kile kiapo walichofanya, akalikiza ule umati, na wakarejea, kila mmoja, kulingana na jamii zao, manyumbani kwao.
4 Na Mosia akaanza kutawala badala ya baba yake. Na alianza kutawala alipokuwa na umri wa miaka thelathini, ikatimia, miaka mia nne, sabini na sita tangu Lehi aondoke Yerusalemu.
5 Na mfalme Benjamini akaishi miaka mitatu na kufariki.
6 Na ikawa kwamba mfalme Mosia alifuata njia za Bwana, na kufuata hukumu zake na maagizo yake, na kutii amri zake katika vitu vyote alivyomwamuru.
7 Na mfalme Mosia akasababisha watu wake kulima ardhi. Na pia yeye, mwenyewe, akalima ardhi, ili asiwe mzigo kwa watu wake, na kwamba atende kulingana na vile baba yake alivyotenda katika vitu vyote. Na hapakuwa na ubishi miongoni mwa watu wake wote kwa kipindi cha miaka mitatu.