“Juni 1–7. Alma 5–7: ‘Mmeshuhudia Mabadiliko Haya Makuu Katika Mioyo Yenu?’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Kitabu cha Mormoni 2020 (2020)
“Juni 1–7. Alma 5–7,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2020
Juni 1–7
Alma 5–7
“Mmeshuhudia Mabadiliko Haya Makuu Katika Mioyo Yenu?
Alma 5–7 inaweza kukusaidia kutafakari juu ya kuongoka kwako kwa Kristo ambako kunaendelea. Unaposoma, andika kile ambacho Roho anakufundisha.
Andika Misukumo Yako
Alma hakujua kuhusu upasuaji wa kisasa wa kuhamisha viungo vya mwili na unaookoa maisha, ambao unabadili moyo ulioharibika au uliougua kwa ule ulio na afya nzuri. Lakini alijua kuhusu muujiza mkubwa wa “mabadiliko ya moyo” (Alma 5:26)—muujiza ambapo Mwokozi anatupatia upya wa maisha ya kiroho, kama “kuzaliwa tena” (ona Alma 5:14, 49). Alma angeweza kuona kwamba mabadiliko haya ya moyo ndicho hasa Wanefi wengi walichohitaji. Baadhi walikuwa matajiri na wengine masikini, baadhi walikuwa na kiburi na wengine walikuwa wanyenyekevu, baadhi ya wadhalimu na wengine waliteseka kwa mateso (ona Alma 4:6–15). Lakini wote walihitaji kuja kwa Yesu Kristo ili waponywe—jinsi sote tunavyohitaji. Tuwe tunatafuta kushinda kiburi au kuvumilia mateso, Ujumbe wa Alma ni mmoja: “Njooni na msiogope” (Alma 7:15). Mruhusu Mwokozi abadili moyo ulioshupazwa, wenye dhambi, au uliojeruhiwa kuwa mnyenyekevu, safi, na mpya.
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kibinafsi
Ni lazima nihisi—na niendelee kuhisi—mabadiliko makuu ya moyo.
Maswali ya kujichunguza ambayo Alma aliwauliza watu wa Zarahemla, yanayopatikana katika Alma 5:14–33, yanaweza kukusaidia kujichunguza nafsi yako na kuelewa maana ya kuwa na “mabadiliko makuu ya moyo” maisha yako yote. Rais M. Russell Ballard alielezea thamani ya maswali haya: “Ninahitaji mara kwa mara kutenga muda wa kujiuliza, ‘Hali yangu ikoje?’ Ni kama kuwa na usaili binafsi, wa siri na nafsi yako. … Kama mwongozo kwangu wakati wa tafakari hii ya siri ya binafsi, ninapenda kusoma na kutafakari maneno ya kujichunguza yanayopatikana katika sura ya tano ya Alma” (“Kurudi na Kupokea,” Ensign au Liahona, Mei 2017, 64).
Zingatia kusoma maswali ya Alma kana kwamba ulikuwa unajifanyia usaili na kuuchunguza moyo wako. Unaweza kutaka kuandika majibu yako kwa maswali hayo. Je, unahisi kutiwa msukumo kufanya nini baada ya usaili wako?
Ona pia Dale G. Renlund, “Kuhifadhi Mabadiliko Makuu ya Moyo,” Ensign au Liahona, Nov. 2009, 97–99.
Naweza kupata ushahidi wangu mwenyewe wa Mwokozi na injili Yake kupitia Roho Mtakatifu.
Alma alitoa ushuhuda wenye nguvu juu ya Mwokozi na Injili Yake, na alielezea pia jinsi alivyopata ushuhuda huo. Alipokuwa akishuhudia, hakutaja tukio lake la kumuona na kumsikia malaika (ona Mosia 27:10–17) badala yake alielezea gharama aliyolipa ili kuujua ukweli mwenyewe. Unajifunza nini kutoka Alma 5:44–51 kuhusu jinsi Alma alivyokuja kujua ukweli? Ni kwa jinsi gani unaweza kufuata mfano Wake katika juhudi zako za kutafuta au kuimarisha ushuhuda wako? Unajifunza nini kuhusu Mwokozi kutoka kwenye mafundisho ya Alma katika Alma 5:33–35, 48–50, na 57–60?
Utiifu kwa bidii utanisaidia kubaki katika “njia ile inayoelekea katika ufalme wa Mungu.”
Watu wa Gideoni hawakuwa wakihangaika na shida sawa na zile za watu wa Zarahemla, kwa hivyo Roho alimsaidia Alma kuhisi mahitaji yao na kuwafundisha kwa njia tofauti (ona Alma 7:17, 26). Ungeweza kugundua tofauti kadhaa kati ya jumbe za Alma kule Zarahemla (ona Alma 5) na kule Gideoni. Kwa mfano, Alma alihisi kwamba watu wa Gideoni walikuwa “katika njia ile inayoelekea katika ufalme wa Mungu” (Alma 7:19). Katika mahubiri yake yote kwao, Alma aliwafundisha vitu vingi kuhusu jinsi ya kubakia kwenye njia (ona Alma 7). Ni ushauri gani aliwapatia? Ni kipi ambacho unaweza kutumia katika maisha yako kwa wakati huu?
Mwokozi alijichukulia juu Yake dhambi zangu, maumivu, na mateso.
Je, umewahi kuhisi kwamba hakuna anayeelewa mapambano au changamoto zako? Kama ni hivyo kweli zilizofundishwa katika Alma 7:7–16 zinaweza kusaidia. Mzee David A. Bednar alishuhudia: “Mwana wa Mungu anajua kikamilifu na anaelewa, kwa kuwa amehisi na amevumilia mizigo yetu binafsi. Na kwa sababu ya dhabihu Yake ya milele na isiyo na mwisho (ona Alma 34:14), Yeye ana uwezo mkamilifu wa kuhisi hisia zetu na anaweza kutunyooshea mkono Wake wa rehema” (“Wabebe Mizigo yao Kwa Urahisi,” Ensign au Liahona, Mei 2014, 90).
Unaposoma Alma 7:7–16, tafakari juu ya kile mistari hii inachotusaidia kuelewa kuhusu malengo ya dhabihu ya Mwokozi. Tunawezaje kupata nguvu Zake katika maisha yetu? Fikiria kuandika mawazo yako.
Ona pia Isaya 53:3–5.
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kifamilia na Jioni ya Familia Nyumbani
Unaposoma maandiko na familia yako, Roho anaweza kukusaidia kujua kanuni zipi zisisitizwe na kujadiliwa ili kukidhi mahitaji ya familia yako. Haya ni baadhi ya mawazo.
Alma 5:6–13
Ni kwa nini Alma aliwataka watu wake wakumbuke rehema za Bwana kwa mababu zao? Ni hadithi gani kutoka kwenye historia ya familia yako zinakufundisha kuhusu rehema Yake? Pengine ungeweza kutembelea familysearch.org/myfamily kuandika hadithi hizi.
Alma 5:14–33
Washiriki wa familia yako wanaweza kujua jinsi ilivyo kujitayarisha—au kutokujitayarisha—kwa ajili ya safari ya kwenda kupiga kambi, mtihani shuleni, au mahojiano ya kutafuta kazi. Ni uzoefu gani wa hivi karibuni wanaweza kushiriki ili kuonyesha umuhimu wa kujitayarisha? Ungeweza kuwaalika wanafamilia wafanye mapitio ya Alma 5:14–33 na watafute maswali ambayo Alma aliuliza kuwatayarisha watu wake kukutana na Mungu. Pengine kila mwanafamilia angeweza kuchagua swali na kushiriki jinsi linavyoweza kutusaidia kujitayarisha kukutana na Mungu. Familia yako ingeweza pia kuweka baadhi ya maswali ya Alma kote nyumbani ili wanafamilia waweze kutafakari.
Alma 6:4–6
Ni nini baadhi ya sababu za sisi kukutana kama Watakatifu? Ni kwa jinsi gani tunaweza kufanya muda wetu kanisani kuwa wenye msaada kwetu na kwa wengine?
Alma 7:9–16
Tunajifunza nini kutoka kwenye mistari hii ambacho kinatusaidia “tusiogope” (Alma 7:15) wakati tunapohitaji kutubu na kubadilika? Ni nini mistari hii inatufundisha kuhusu kumrudia Mwokozi wakati tunahitaji msaada? Ni vitu gani vingine tumefanya kwa ajili ya kupokea msaada Wake? Ni kwa namna gani Ametusaidia?
Alma 7:23
Ni nani tunayemjua ambaye ni mfano mwema wa moja au zaidi ya sifa zilizoorodheshwa katika mstari huu? Kwa nini ni muhimu kukuza sifa hizi?
Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Msingi.