Njoo, Unifuate
Juni 29–Julai 5. Alma 23–29: “Hawakuanguka Kamwe”


“Juni 29–Julai 5. Alma 23–29: ‘Hawakuanguka Kamwe,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Kitabu cha Mormoni 2020 (2020)

“Juni 29–Julai 5. Alma 23–29,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2020

Waanti-Nefi-Lehi wanazika silaha zao

Waanti-Nefi-Lehi Wanazika Silaha Zao za Vita, na Jody Livingston

Juni 29–Julai 5

Alma 23–29

“Hawakuanguka Kamwe”

Unapojifunza Alma 23–29, ni jumbe zipi unapata kwa ajili yako na familia yako? Nini ungeweza kushiriki katika madarasa yako ya Kanisani?

Andika Misukumo Yako

Kuna wakati unashangaa kama kweli watu wanaweza wakabadilika? Pengine una wasiwasi kuhusu kama unaweza kushinda chaguzi mbaya ulizozifanya au tabia mbaya ulizozijenga, au unaweza kuwa na wasiwasi sawa na huu juu ya wapendwa wako. Kama ni hivyo, hadithi ya Waanti-Nefi-Lehi inuaweza kkusaidia. Watu hawa walikuwa maadui wa jadi wa Wanefi. Wakati Amoni na ndugu zake walipoamua kuhubiri injili kwao, Wanefi “[waliwacheka] kwa dharau.” Kuwaua Walamani kulionekana kama suluhu yenye kukubalika kuliko kuwaongoa. (Ona Alma 26:23–25.)

Lakini Walamani walibadilika—kupitia nguvu ya kuongoa ya Bwana. Ambapo wakati mmoja walijulikana kama “watu wagumu na wakali” (Alma 17:14), walikuja “kutambulika kwa juhudi yao kwa Mungu” (Alma 27:27). Kwa hakika, “hawakuwahi kuanguka kamwe” (Alma 23:6).

Pengine unazo desturi za uwongo za kuacha au “silaha za … uasi” za kuweka chini (Alma 23:7). Au pengine unahitaji tu kuwa na ari zaidi katika ushuhuda wako na kidogo usiyeelekea kuanguka. Haijalishi ni mabadiliko ya aina gani unahitaji, Alma 23–29 inaweza kukupatia tumaini kwamba, kupitia kwa nguvu za upatanisho wa Yesu Kristo, mabadiliko ya kudumu yanawezekana.

ikoni ya kujifunza kibinafsi

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kibinafsi

Alma 23:1–5

Wakati watoto wa Mungu wanapoikubali injili, baraka kuu huja.

Wakati mfalme wa Walamani alipotangaza kwamba neno la Mungu “lisizuiliwe” miongoni mwa watu wake (ona Alma 23:1–5), alifungua mlango wa baraka kuu kwa ajili yao. Unaposoma Alma 23–29, tafuta baraka hizi. Unawezaje kuhakikisha ya kwamba neno la Mungu “halizuiliwi” katika maisha yako au ya familia yako?

Alma 23–25; 27

Kuongoka kwangu kwa Yesu Kristo na injili Yake kunabadilisha maisha yangu.

Walamani ambao walitembelewa na Amoni na ndugu zake walionekana kuwa watu wasiofaa kwa uongofu—walikuwa wamenaswa na tamaduni za baba zao na uovu wao wenyewe. Ilhali wengi wao walikubali injili ya Yesu Kristo na kufanya mabadiliko makuu katika maisha yao. Kama ishara ya uongofu wao, hawa Walamani walijiita Waanti-Nefi-Lehi. (Maana ya “anti” katika jambo hili si sawa na “kupinga” katika “mpinga-Kristo.”)

Kufikiria kuhusu uongofu wa Walamani hawa kunaweza kukuchochea kutafakari uongofu wako “kwa Bwana” (Alma 23:6). Njia moja ya kujifunza sura hizi yaweza kuwa kutambua jinsi kuongoka kwa Wanti-Nefi-Lehi kulivyobadili maisha yao. Mistari ifuatayo inaweza kukuwezesha kuanza.

Unapotafakari mabadiliko ya Waanti-Nefi-Lehi, fikiria kuhusu jinsi kuongoka kwako kwa Kristo kunavyokubadili. Ni nini unahisi bado ungali unahitaji kubadilika ili kwamba injili iweze kuwa na uwezo mkubwa katika maisha yako?

Alma 23:6–7

Alma 23:17–18

Alma 24:11–19

Alma 25:13–16

Alma 27:26–30

Alma 24:7–19; 26:17–22

Mungu ni mwenye rehema.

Ingawa dhambi ambazo Amoni na Wanti-Nefi-Lehi walihitaji kuacha huenda zilikuwa tofauti sana na kitu chochote maishani mwako, sisi sote tunategemea rehema za Mungu. Ni nini unapata katika Alma 24:7–19 na 26:17–22 ambacho kinakusaidia kuelewa Rehema Zake? Unaposoma, unaweza kufikiria kuhusu vitu hivi: njia ambazo umealikwa kutubu, uzoefu wako kwenye toba, jinsi ambavyo umejaribu kuepuka kutenda dhambi tena, na baraka ambazo umezipata kupitia toba. Wakati unaposoma mistari hii kwa njia hii, unajifunza nini kuhusu rehema za Mungu katika maisha yako?

Alma 2629

Kumtumikia Bwana kunaleta shangwe.

Licha ya uzoefu wao tofauti, Amoni na Alma walionyesha hisia sawa kuhusu kazi yao ya umisionari. Fikiria kusoma Alma 26 na 29 na kuwalinganisha. Umegundua mifanano ipi? Je, ni maneno na virai gani vilivyorudiwa? Unaweza kujifunza nini kutoka kwa Alma na Amoni kuhusu jinsi ya kutafuta shangwe ya kweli licha ya changamoto zako? (Kufanya mapitio ya changamoto ambazo Alma alipitia, ona vichwa vya habari vya sura za Alma 5–16. Kufanya mapitio ya changamoto za Amoni na kaka zake, ona vichwa vya habari vya sura za Alma 17–28.)

Alma 26:5–7

Miganda na maghala ni nini?

Wakati wa mavuno, nafaka kwa kawaida hukusanywa katika vifungu vinavyoitwa miganda na kuhifadhiwa katika jengo la kuhifadhi, wakati mwingine huitwa maghala. Mzee David A. Bednar alishiriki ufafanuzi wa matumizi ya uashiriaji katika Alma 26:5: “Miganda katika analojia hii inawakilisha washiriki wapya wa Kanisa waliobatizwa. Maghala ni mahekalu matakatifu” (“Honorably Hold a Name and Standing,” Ensign au Liahona, Mei 2009, 97). Fikiria kile ambacho analojia katika Alma 26:5–7 inakufundisha kuhusu umuhimu wa maagano ya hekaluni.

ikoni ya kujifunza kifamilia

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kifamilia na Jioni ya Familia Nyumbani

Unaposoma maandiko na familia yako, Roho anaweza kukusaidia kujua kanuni zipi zisisitizwe na kujadiliwa ili kukidhi mahitaji ya familia yako. Haya ni baadhi ya mawazo.

Alma 24:6–19

Ni kwa nini Waanti-Nefi-Lehi walizika silaha zao “chini ardhini ? (Alma 24:16). Pengine wanafamilia wanaweza kufurahia kuandika kwenye vipande vya karatasi vitu ambavyo wangependa kushinda au kuacha. Wangeweza kisha kuchimba shimo na kuzika karatasi hizo.

Alma 24:7–12

Kujifunza mistari hii kunaweza kuisaidia familia yako kuelewa karama ya ajabu ya toba. Wanti-Nefi-Lehi walifanya nini ili kutubu dhambi zao? Ni kwa jinsi gani Bwana aliwasaidia kutubu? Tunaweza kujifunza nini kutokana na mfano wao?

Alma 24:20–27

Ni nini tumeona ambacho kinashuhudia ukweli wa matamshi ya Mormoni: “Hivyo tunaona kwamba Bwana hutumia njia nyingi ili kuokoa watu Wake”? (Alma 24:27).

Alma 26:2

Ni kwa jinsi gani familia yako ingejibu maswali ya Amoni katika Alma 26:2? Pengine unaweza kutengeneza orodha ya majibu yao kwenye karatasi kubwa na kuibandika mahali ambapo kila mtu anaweza kuiona. Watie moyo wanafamilia waongezee kwenye orodha hiyo wanapofikiria juu ya baraka zingine ambazo Mungu “ametupatia sisi.”

Alma 29:9

Ni kwa jinsi gani Amoni na Alma walikuwa vyombo katika mikono ya Mungu? Fikiria kuvitazama vyombo au vifaa katika nyumba yako na kujadili jinsi ambavyo kila kimoja ni msaada kwa familia yako. Ni kwa jinsi gani hili linatusaidia kuelewa jinsi kila mmoja wetu anavyoweza kuwa “chombo katika mikono ya Mungu”?

Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kufundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi.

Kuboresha Ufundishaji Wetu

Tumia utofauti. Kufanya utofauti kwenye jinsi ya kujifunza maandiko kifamilia kunaweza kuwasaidia wanafamilia kuwa na moyo wa kupenda na kujihusisha. Kwa mfano, baada ya mwanafamilia kusoma aya, anaweza kuwaomba wanafamilia wengine kuelezea tena kwa maneno yao kile kilichosomwa.

Waanti-Nefi-Lehi wanazika silaha zao

Kielelezo cha Waanti-Nefi-Lehi wakizika silaha zao na Dan Burr