Njoo, Unifuate
Novemba 16–22. Etheri 6–11: “Kwamba Uovu Utupiliwe Mbali”


“Novemba 16–22. Etheri 6–11: ‘Kwamba Uovu Utupiliwe Mbali,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Kitabu cha Mormoni 2020 (2020)

“Novemba 16–22. Etheri 6–11,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2020

Picha
Mashua za Wayaredi baharini

Nitawarudisha Juu Tena Kutoka kwenye Kilindi cha Bahari, na Jonathan Arthur Clarke

Novemba 16–22

Etheri 6–11

“Kwamba Uovu Utupiliwe Mbali”

Akizungumza kuhusu kumbukumbu ya Wayaredi, Mormoni alitoa maoni kwamba “ni muhimu watu wote kujua vitu ambavyo vimeandikwa katika historia hii” (Mosia 28:19). Hifadhi hili akilini mwako unaposoma Etheri 6–11. Ni kwa nini vitu hivi ni muhimu—au vyenye manufaa—kwako na wapendwa wako?

Andika Misukumo Yako

Mamia ya miaka baada ya Wayaredi kuangamizwa, Wanefi waligundua mabaki ya ustaarabu wao wa kale. Miongoni mwa mabaki haya kulikuwa na kumbukumbu—mabamba ya “dhahabu kamili” yaliyaliyokuwa “yamejaa michoro” (Mosia 8:9). Mfalme Mnefi, Limhi, aliweza kuona kwamba kumbukumbu hii ilikuwa muhimu: “Bila shaka kuna siri kuu iliyo katika haya mabamba,” alisema (Mosia 8:19). Leo hii unao ufupisho wa kumbukumbu hii, ikiwa imetafsiriwa katika lugha yako, na inaitwa Kitabu cha Etheri. Inatoka kwenye kumbukumbu sawa na ile ambayo Wanefi “walitamani sana” kuisoma, na wakati walipoisoma, “walijawa na huzuni; walakini iliwapa ufahamu mwingi, ambao uliwafurahisha” (Mosia 28:12, 18). Unaposoma kuhusu kuinuka na anguko kuu la Wayaredi, utapata nyakati nyingi za huzuni. Lakini usikose kutilia maanani shangwe ya kujifunza masomo kutoka kwenye historia hii. Baada ya yote, kama Moroni alivyoandika, “ni hekima kwa Mungu kwamba vitu hivi vionyeshwe kwenu” (Etheri 8:23), kwa kuwa kama tunaweza kujifunza kutokana na kufeli na mafanikio ya Wayaredi, “uovu ungeondolewa mbali, na … wakati ungekuja ambapo Shetani hawezi kuwa na uwezo kwa mioyo ya watoto wa watu” (Etheri 8:26).

Picha
ikoni ya kujifunza kibinafsi

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kibinafsi

Etheri 6:1–12

Bwana ataniongoza hadi kwenye nchi yangu ya ahadi.

Unaweza kupata umaizi wa kiroho kama utalinganisha safari ya Wayaredi kuvuka bahari na safari yako ya maisha ya hapa duniani. Kwa mfano, ni nini Bwana ametoa ambacho kinamulika njia yako kama yale mawe ndani ya zile mashua za Wayaredi? Ni nini mashua zaweza kuwa zinawakilisha, au upepo ambao “unavuma kuelekea nchi ya ahadi”? (Etheri 6:8). Je, unajifunza nini kutokana na vitendo vya Wayaredi kabla, wakati wa, na baada ya safari? Je, ni jinsi gani Bwana anakuongoza kuelekea kwenye nchi yako ya ahadi?

Picha
Wayaredi wakisafiri pamoja na wanyama

Safari ya Wayaredi kuvuka Asia, na Minerva Teichert

Etheri 6:5–18, 30; 9:28–35; 10:1–2

Bwana ananibariki ninapokuwa mnyenyekevu.

Ingawa majivuno na uovu unaonekana kutawala historia ya Wayaredi, ipo pia mifano ya unyenyekevu katika sura hizi—hasa katika Etheri 6:5–18, 30; 9:28–35; na 10:1–2. Kutafakari maswali yafuatayo kunaweza kusaidia kujifunza kutokana na mifano hii: Kwa nini Wayaredi hawa walijinyenyekeza katika hali hizi? Walifanya nini ili kuonyesha unyenyekevu wao? Je, walibarikiwa vipi kama matokeo yake? Tambua kwamba katika hali fulani, watu walilazimishwa na hali zao kuwa wanyenyekevu. Fikiria kile unachoweza kufanya kwa hiari yako “kujinyenyekeza mbele ya Bwana” (Etheri 6:17) badala ya kulazimishwa kuwa mnyenyekevu (ona Mosia 4:11–12; Alma 32:14–18).

Ona Pia “Unyenyekevu,” Mada za Injili, topics.ChurchofJesusChrist.org.

Etheri 7–11

Viongozi wenye haki hubariki watu wanaowaongoza.

Sura za 7–11 za Etheri zinajumuisha angalau vizazi 28. Ingawa si maelezo mengi yanaweza kutolewa kwenye nafasi ndogo kama hii, mpangilio unajitokeza kwa haraka: uongozi wenye haki unasababisha baraka na mafanikio, huku uongozi mbovu unasababisha utumwa na uharibifu.

Hapa chini ni baadhi tu ya wafalme waliotajwa katika sura hizi. Soma aya zinazohusika, na uone kile unachoweza kujifunza kutokana na mifano yao—chanya na hasi—kuhusu uongozi. Unapofanya hivyo, fikiria kuhusu nafasi ambazo unaweza kuwa nazo kuongoza au kuwashawishi wengine nyumbani kwako, katika jumuia yako, wito wako kanisani, na kadhalika.

Etheri 8:7–26

Kundi ovu la siri ni nini?

Wakati watu wawili au zaidi wanapanga njama kuweka siri vitendo vyao vya uovu, wanahusika katika kundi ovu la siri. Mara nyingi wanatiwa motisha na tamaa ya mamlaka au utajiri. pamoja na kundi ovu la siri lililoelezewa katika Etheri 8:7–18, mifano mingine yaweza kupatikana katika Helamani 1:9–12; 2:2–11; 6:16–30, na Musa 5:29–33. Katika Etheri 8:18–26, Moroni anaelezea matokeo ya makundi maovu ya siri (ona pia Etheri 9:4–12) na anatuonya tusiyaunge mkono.

Picha
ikoni ya kujifunza kifamilia

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kifamilia na Jioni ya Familia Nyumbani

Unaposoma maandiko na familia yako, Roho anaweza kukusaidia kujua kanuni zipi zisisitizwe na kujadiliwa ili kukidhi mahitaji ya familia yako. Haya ni baadhi ya mawazo.

Etheri 6:2–12

Je, familia yako inaweza kufurahia kuigiza safari ya Wayaredi kuelekea kwenye nchi ya ahadi? Pengine mnaweza kutumia chumba chenye giza kama mashua na tochi kuwakilisha mawe yanayong’aa. Mnaweza kuzungumza kuhusu jinsi Wayaredi walivyoonyesha imani yao katika Bwana kwa kuingia ndani ya mashua licha ya kujua ya kwamba “wangezikwa kwenye vilindi vya bahari” (Etheri 6:6). Baada ya kusoma mstari wa 9, wanafamilia wanaweza kushiriki nyimbo za kuabudu wanazozipenda zaidi na kuziimba pamoja. Ni jinsi gani nyumba zetu zinaweza kufananishwa na mashua za Wayaredi? Ni nini nchi ya ahadi ambayo Bwana anaongoza familia yetu kuifikia?

Etheri 6:22–23

Katika wiki hii, familia yako inaweza kuangalia jinsi onyo la kinabii la kaka wa Yaredi kuhusu utumwa lilivyotimizwa. Ni maonyo gani viongozi wetu wa Kanisa wametoa kwa ajili yetu? Ni kwa namna gani kupuuza ushauri wao kunaweza kusababisha utumwa?

Etheri 8:23–26

Kulingana na aya hizi, ni kwa nini Moroni aliamriwa kuandika “vitu hivi” kuhusu makundi maovu ya siri ? (Etheri 8:23). Tunaweza kujifunza nini kutoka katika kitabu cha Etheri ambacho kinaweza kutusaidia kupata baraka zilizoelezewa katika mstari wa 26?

Etheri 9:11

Matamanio yetu yanaathiri vipi chaguzi zetu? Tunaweza kufanya nini kama familia kuhakikisha ya kwamba tuna matamanio ya vitu vya Mungu?

Etheri 11:8

Ili kujifunza zaidi kuhusu rehema za Mungu kwa wale wanaotubu, unaweza kusoma Mosia 26:29–30; 29:18–20; Alma 34:14–16; au Moroni 6:8. Pengine wanafamilia wanaweza kushiriki mifano ya rehema za Mungu kutoka kwenye maandiko au kutoka kwenye maisha yao wenyewe.

Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kufundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi.

Kuboresha Kujifunza Kibinafsi

Fanyia kazi kile unachojifunza. Kujifunza injili kunajumuisha zaidi ya kusoma na kutafakari. Kawaida tunajifunza zaidi kwa kutenda kulingana na kweli katika maandiko (ona Yohana 7:17). Utafanya nini ili kutumia mafundisho uliyosoma katika Etheri 6–11?

Picha
Mashua za Wayaredi baharini

Mashua za Wayaredi, na Gary Ernest Smith

Chapisha