“Novemba 30–Desemba 6. Moroni 1–6: ‘Kuwaweka Kwa Njia Nzuri,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Kitabu cha Mormoni 2020 (2020)
“Novemba 30–Desemba 6. Moroni 1–6,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2020
Novemba 30–Desemba 6
Moroni 1–6
“Kuwaweka kwa Njia Nzuri”
Moroni aliandika kile alichotumaini kingekua “chenye thamani … katika siku zijazo” (Moroni 1:4). Unagundua nini katika Moroni 1–6 ambacho ni cha thamani kwako? Andika kile unachogundua, na fikiria kushiriki na mtu ambaye anaweza kuona manufaa yake.
Andika Misukumo Yako
Baada ya kumaliza kumbukumbu ya baba yake juu ya Wanefi na ufupisho wa kumbukumbu ya Wayaredi, Moroni alifikiria kwamba hii kazi ya kuweka kumbukumbu ilikuwa imekamilika (ona Moroni 1:1). Kulikuwa na nini cha ziada cha kusema kuhusu mataifa mawili yaliyokuwa yameangamizwa kabisa? Lakini Moroni alikuwa ameona siku zetu (ona Mormoni 8:35), na alitiwa msukumo “kuandika vitu vichache zaidi, kwamba vingekuwa vya manufaa … katika siku zijazo” (Moroni 1:4). Alijua kwamba ukengeufu uliotapakaa ulikuwa unakaribia, na kuleta machafuko kuhusu ibada za ukuhani na dini kwa ujumla. Hii yaweza kuwa sababu ya yeye kutoa maelezo bayana kuhusu sakramenti, ubatizo, kutunukia kipawa cha Roho Mtakatifu, na baraka za kukusanyika pamoja na waumini wenzetu “kuwaweka [kila mmoja] katika njia nzuri, … wakitegemea tu katika nguvu ya wokovu ya Kristo, ambaye alikuwa mwanzilishi na mtimizaji wa imani [yetu]” (Moroni 6:4). Umaizi wa thamani kama huu unatupatia sababu ya kuwa na shukrani kwamba Bwana alilinda uhai wa Moroni ili aweze “kuandika vitu zaidi” (Moroni 1:4).
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kibinafsi
Wanafunzi wa Yesu Kristo wanabakia kuwa waaminifu licha ya upinzani.
Kwa baadhi ya watu, ni rahisi kuwa mwaminifu katika nyakati za utulivu na starehe. Lakini kama wanafunzi wa Yesu Kristo, lazima tuwe waaminifu hata wakati tunakumbana na majaribu na upinzani. Unaposoma Moroni 1, ni nini kinachokutia msukumo kuhusu uaminifu wa Moroni kwa Bwana na wito wake? Ni kwa jinsi gani unaweza kufuata mfano wake?
Ibada za ukuhani lazima zisimamiwe kulingana na Bwana anavyoagiza.
Wakati wa huduma yake duniani, Mwokozi alipokea na kusimamia ibada takatifu, kama vile ubatizo (ona Mathayo 3:13–17; Tafsiri ya Joseph Smith, Yohana 4:1–3 [katika kiambatisho cha Biblia]), kutawazwa kwa ukuhani (ona Marko 3:13–19), na sakramenti (ona Mathayo 26:26–28). Hata hivyo, kwa sababu ya Ukengeufu Mkuu, watu wengi leo hii wamechanganyikiwa kuhusu jinsi gani ibada zinapaswa kutekelezwa—na hata ikiwa zinahitajika. Katika Moroni 2–6, Moroni alitoa maelezo muhimu kuhusu ibada fulani za ukuhani ambazo zinaweza kusaidia kuondoa kwa kiasi fulani kuchanganyikiwa huko. Ni misukumo gani inakuja unapojifunza kuhusu ibada zinazopatikana katika sura hizi? Yafuatayo ni baadhi ya maswali unayoweza kuuliza ili yaweze kukusaidia kujifunza:
-
Uthibitisho (Moroni 2; 6:4).Ni nini maagizo ya Mwokozi katika Moroni 2:2 yanakufundisha kuhusu ibada ya uthibitisho? Unafikiri ni nini maana ya “kuhemshwa na kusafishwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu”? (Moroni 6:4).
-
Kutawazwa kwa ukuhani (Moroni 3).Ni nini unachopata katika sura hii ambacho kinaweza kumsaidia mtu kujitayarisha kutawazwa kwenye ukuhani? Je, unapata nini ambacho kinaweza kumsaidia mtu kufanya utawazo?
-
Sakramenti (Moroni 4–5; 6:6).Angalia ahadi katika sala za sakramenti (ona Moroni 4:3; 5:2), na tafakari kile ambacho unakifanya ili kutunza ahadi zako. Unaweza kufanya nini ili kualika ushawishi wa Roho kwa nguvu zaidi unaposhiriki sakramenti?
-
Ubatizo (Moroni 6:1–3).Unaweza kufanya nini ili kuendelea kuwa mstahiki wa vigezo vinavyotolewa kwa ajili ya ubatizo katika aya hizi, hata baada ya kubatizwa kwako? Aya hizi zinapendekeza nini kwako kuhusu maana ya kuwa mshiriki wa Kanisa la Yesu Kristo?
Kulingana na kile ulichojifunza, utabadili kwa namna gani jinsi unavyofikiri kuhusu, kushiriki katika, au kuwatayarisha wengine kwa ajili ya ibada hizi? Kwa nini ni muhimu kwamba ibada hizi “[zisimamiwe … kulingana na amri za Kristo”? (Moroni 4:1).
Ona pia “Ibada,” Mada za Injili, topics.ChurchofJesusChrist.org.
Wafuasi wa Yesu Kristo hujali ustawi wa nafsi za wengine.
Wakati ni kweli kwamba sisi sote “tunatimiza wokovu [wetu] wenyewe” (Mormoni 9:27), Moroni pia alifundisha kwamba “[kukutana] pamoja mara kwa mara” pamoja na waumini wenzetu kunaweza kusaidia kutuweka “katika njia sahihi ” (Moroni 6:4–5). Unaposoma Moroni 6:4–9, tafakari baraka ambazo zinakuja kutokana na “kuhesabiwa miongoni mwa watu wa kanisa la Kristo” (Moroni 6:4). Ni kwa jinsi gani ungeweza kusaidia kufanya uzoefu ambao wewe na wengine mmekwisha kuwa nao kanisani kuwa zaidi kama ule Moroni alioelezea, iwe wewe ni kiongozi au mshiriki?
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kifamilia na Jioni ya Familia Nyumbani
Unaposoma maandiko na familia yako, Roho anaweza kukusaidia kujua kanuni zipi zisisitizwe na kujadiliwa ili kukidhi mahitaji ya familia yako. Haya ni baadhi ya mawazo.
Moroni 1; Moroni 6:3
Inamaanisha nini “kumkana Kristo?” (Moroni 1:2–3). Je, tunawezaje kuonyesha “dhamira yetu ya kumtumikia hadi mwisho”? (Moroni 6:3). Shiriki mifano ya watu unaowajua walio na dhamira hii ya kumtumikia Yeye.
Moroni 4:3; Moroni 5:2
Kusoma sala za sakramenti kama famiilia kunaweza kuleta mjadala kuhusu kuchukulia sakramenti kwa heshima kuu zaidi. Pengine wanafamilia wanaweza kujadili virai kutoka kwenye sala hizi ambavyo ni vyenye maana kwao. Pia wanaweza kuandika mawazo yao kuhusu virai hivi au kuchora picha inayowasaidia kufikiria juu ya Mwokozi. Wanaweza kuleta kile walichoandika au kuchora katika mkutano wa sakramenti ili kuwasaidia kufokasi mawazo yao Kwake. Iambie familia yako jinsi unavyohisi kuhusu sakramenti na dhabihu ya Mwokozi.
Moroni 6:1–4
Inamaanisha nini kuwa na “moyo uliovunjika na roho iliyopondeka”? (Moroni 6:2). Ni kwa jinsi gani hii hutusaidia kujitayarisha kwa ajili ya ubatizo? Ni kwa namna gani inaweza kutusaidia baada ya sisi kubatizwa?
Moroni 6:4–9
Kulingana na aya hizi, ni nini baadhi ya baraka zinazokuja kutokana na kuwa “waliohesabiwa miongoni mwa watu wa kanisa la Kristo”? (Moroni 6:4). Kwa nini tunahitaji Kanisa?
Moroni 6:8
Nini aya hii inatufundisha kuhusu toba? Inamaanisha nini kutafuta msamaha kwa “kusudi la kweli”? (Moroni 6:8). Fikirieni kuimba wimbo kuhusu msamaha, kama vile “Help Me, Dear Father” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 99).
Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kufundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi.