Njoo, Unifuate
Desemba 14–20. Moroni 10: “Mje kwa Kristo na Mkamilishwe Ndani Yake”


“Desemba 14–20. Mosia 10: ‘Mje kwa Kristo na Mkamilishwe Ndani Yake,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Kitabu cha Mormoni 2020 (2020)

“Desemba 14–20. Mosia 10,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2020

Picha
Kristo anawatokea Wanefi

Kwamba Mjue, na Gary L. Kapp

Desemba 14–20

Moroni 10

“Mje kwa Kristo, na Mkamilishwe Ndani Yake”

Unapomaliza kusoma Kitabu cha Mormoni, fikiria kutafuta ushahidi mpya kutoka kwa Roho Mtakatifu kwamba ni cha kweli. Unapofanya hivyo, andika misukumo unayopokea.

Andika Misukumo Yako

Kitabu cha Mormoni kinaanza na ahadi ya Nefi kutuonyesha ya kwamba “huruma nyororo ya Bwana iko juu ya wale ambao amewachagua, kwa sababu ya imani yao” (1 Nefi 1:20). Kitabu kinakamilika na ujumbe sawa na huo kutoka kwa Moroni alipokuwa akijitayarisha “kukifunga kwa kuweka muhuri” maandishi yale: alitualika “tukumbuke jinsi vile Bwana amekuwa na huruma” (Moroni 10:2–3). Hata kama tutafikiria tu kuhusu moja ya rehema nyingi zilizorekodiwa katika Kitabu cha Mormoni, hili linatupatia mambo mengi ya kufikiria. Ni mifano ipi inakujia kwenye akili yako? Unaweza tafakari njia ya rehema ambayo Mungu aliiongoza familia ya Nefi nyikani na alivyowavusha katika yale maji makuu, huruma nyororo Alizomuonyesha Enoshi wakati nafsi yake ilipata njaa ya msamaha, au rehema Aliyomuonyesha Alma, adui mkali wa Kanisa ambaye aligeuka na kuwa mmoja wa watetezi shupavu wa Kanisa. Au mawazo yako yanaweza kugeukia rehema ambayo Mwokozi aliyefufuka aliwaonyesha watu wakati alipowaponya wagonjwa wao na kuwabariki watoto wao wadogo. Pengine cha muhimu zaidi, yote haya yanaweza kukukumbusha “jinsi vile Bwana amekuwa na huruma” kwako, kwa maana mojawapo ya malengo makuu ya Kitabu cha Mormoni ni kualika kila mmoja wetu kupokea rehema ya Mungu—mwaliko unaodhihirishwa kwa urahisi katika ujumbe wa maneno ya buriani ya Moroni, “Ndio, mje kwa Kristo na mkamilishwe ndani yake” (Moroni 10:32).

Picha
ikoni ya kujifunza kibinafsi

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kibinafsi

Moroni 10:3–7

Naweza kujua ukweli kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.

Ahadi iliyoko katika Moroni 10:3–7 imebadilisha maisha ya mamilioni ya watu kote duniani. Je, ni kwa jinsi gani hili limekubadili? Kama unatafuta kupata au kuimarisha ushuhuda wako wa Kitabu cha Mormoni, mwaliko wa Moroni unakufaa wewe. Unaposoma Moroni 10:3–7, fikiria kusoma kwa uangalifu zaidi kuliko vile ambavyo umefanya awali. Unaweza kuchunguza kila kirai, ukijiuliza maswali kama haya: Hili lina maana gani? Ninawezaje kulifanya hili kwa njia bora? Ni uzoefu gani nimeupata kutokana na hili? Ni kwa jinsi gani Roho Mtakatifu amenionyesha ukweli wa Kitabu cha Mormoni?

Pia fikiria kuhusu mtu ambaye anahitaji kusikia ushuhuda wako wa Kitabu cha Mormoni. Utamsaidiaje mtu huyo kutafuta ushuhuda wake mwenyewe?

Moroni 10:8–25

“Msikatae karama za Mungu.”

Kuna njia nyingi mtu anaweza “[kukataa] … karama za Mungu” (Moroni 10:8). Baadhi ya watu wanakataa kuwa karama hizi zipo. Wengine wanaweza kukataa kuwa hawana karama za kiroho lakini wanazitambua kwa watu wengine. Na bado wengine wanazikataa karama zao kwa kuzipuuza au kushindwa kuzitunza.

Unaposoma Moroni 10:8–25, tafuta kweli ambazo zitakusaidia kugundua karama zako za kiroho na zitumie kwa uwezo mkubwa kujibariki wewe mwenyewe na wengine. Tafuta umaizi kuhusu karama ambazo Mungu amekupa au karama ambazo Anataka uzitafute. Kwa nini ni muhimu “kukumbuka kwamba kila karama nzuri hutoka kwa Kristo”? (Moroni 10:18).

Fikiria juu ya ushauri huu kutoka kwa Mzee John C. Pingree Jr.: “Hivyo basi, tunakujaje kutambua karama zetu? Tunaweza kurejelea baraka yetu ya baba mkuu, kuwauliza wale ambao wanatufahamu vizuri, na kibinafsi kutambua kile ambacho kawaida tunakifanya vizuri na kukifurahia. Muhimu zaidi, tunaweza kumuuliza Mungu (ona Yakobo 1:5; M&M 112:10). Anazifahamu karama zetu, kwa maana ni Yeye aliyetupa” (“Ninayo Kazi kwa Ajili Yako,” Ensign au Liahona, Nov. 2017, 33).

Ona Mwongozo wa Maandiko, “Karama za Roho,” scriptures.ChurchofJesusChrist.org.

Moroni 10:30–33

Ninaweza kukamilishwa kupitia neema ya Yesu Kristo.

Ushauri wa Moroni wa “Mje kwa Kristo” unajumuisha zaidi ya kujifunza au kufikiria tu juu Yake mara kwa mara au kujaribu kwa bidii kutii amri Zake, jinsi vitu hivi vilivyo muhimu. Badala yake, huu ni mwaliko wa kuja kwa Kristo katika fasili kamili iwezekanavyo—kuwa jinsi Alivyo. Unaposoma Moroni 10:30–33, weka akilini virai vinavyokusaidia kuelewa maana ya kuja kwa Kristo kikamilifu, kama vile “kushikilia juu ya kila karama nzuri,” “mjinyime ubaya wote ,” na, bila shaka, “ mkamilishwe ndani yake” (italiki imeongezwa).

Je, inawezekana vipi? Tafuta majibu katika Moroni 10:30–33. Roho anakwambia nini unachopaswa kufanya kikamilifu zaidi ili “uje kwa Kristo, na Ukamilishwe Ndani Yake” ?

Ona Omni 1:26; Mwongozo wa Maandiko, “Kamili,” scriptures.ChurchofJesusChrist.org.

Picha
ikoni ya kujifunza kifamilia

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kifamilia na Jioni ya Familia Nyumbani

Unaposoma maandiko na familia yako, Roho anaweza kukusaidia kujua kanuni zipi zisisitizwe na kujadiliwa ili kukidhi mahitaji ya familia yako. Haya ni baadhi ya mawazo.

Moroni 10

Someni sura hii pamoja, mkitafuta kila wakati Moroni alipotumia neno sihi. Orodhesha au weka alama ya kile ambacho Moroni anashauri—au anatutia moyo kwa nguvu—tufanye. Ni nini tunaweza kufanya kufuata ushauri wake?

Moroni 10:3

Tumejifunza nini kuhusu rehema ya Bwana tunaposoma Kitabu cha Mormoni mwaka huu? Ni jinsi gani Bwana amekuwa na rehema kwa familia yetu?

Moroni 10:3–5

Baada ya kusoma aya hizi, waweza ukawauliza wanafamilia washiriki jinsi walivyokuja kujua kwamba Kitabu cha Mormoni ni cha kweli. Fikirieni kuimba pamoja wimbo kuhusu kutafuta ukweli, kama vile “Search, Ponder, na Pray” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 109). Waweza pia kuwaalika wanafamilia kuandika shuhuda zao katika shajara ya familia.

Moroni 10:8–18

Kiasili Krismasi ni wakati wa kufikiria juu ya kupokea zawadi. Pengine wanafamilia wanaweza kufunga zawadi kwa ajili ya kila mmoja ambazo zinawakilisha “karama za Mungu” zilizotajwa katika Moroni 10:9–16. Zawadi hizi pia zaweza zikawakilisha karama zingine nzuri kutoka kwa Kristo ambazo wanaziona kwa kila mmoja wao.

Moroni 10:27–29, 34

Wanafamilia wanaweza kushiriki kile ambacho wangependa kumwambia Moroni wakati “watakapokutana na [yeye] mbele ya kiti cha enzi cha kupendeza cha Yehova mkuu.”

Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kufundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi.

Kuboresha Kujifunza Kibinafsi

Mtafute Yesu Kristo. Lengo la Kitabu cha Mormoni—na maandiko yote—ni kutoa ushuhuda juu ya Yesu Kristo. Unajifunza nini kuhusu Yesu Kristo katika Moroni 10? Je, unahisi kutiwa msukumo kufanya nini ili uje Kwake?

Picha
Moroni akizika bamba za dhahabu

Moroni Akizika Bamba za Dhahabu, na Jon McNaughton

Chapisha