Mafundisho na Maagano 2021
Septemba 6–12. Mafundisho na Maagano 98–101: “Tulieni na Mjue Kuwa Mimi ni Mungu”


“Septemba 6–12. Mafundisho na Maagano 98–101: ‘Tulieni na Mjue Kuwa Mimi ni Mungu,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Mafundisho na Maagano 2021 (2020)

“Septemba 6–12. Mafundisho na Maagano 98–101,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2021

Picha
Watakatifu wakikimbia kutoka kwa kundi la wavamizi

C.C.A. Christensen (1831–19120, Watakatifu wakifukuzwa kutoka Jackson County Missouri, c. 1878, tempera on muslin, 77 ¼ × 113 inches. Makumbusho ya Sanaa ya Chuo Kikuu cha Brigham Young, zawadi ya wajukuu wa C.C.A. Christensen, 1970.

Septemba 6–12

Mafundisho na Maagano 98–101

“Tulieni na Mjue Kuwa Mimi ni Mungu”

Unaposoma Mafundisho na Maagano 98–101, sikiliza mawazo na misukumo ambayo inakuja. Ni kwa jinsi gani kuyafanyia kazi kunakusaidia kuwa mtu ambaye Mungu anataka uwe?

Andika Misukumo Yako

Kwa Watakatifu mnamo miaka ya 1830, Independence, Missouri, kiuhalisia ilikuwa nchi ya ahadi. Palikuwa “mahali pa katikati” ya Sayuni (ona Mafundisho na Maagano 57:3)—jiji la Mungu duniani—ambalo walikuwa wakitoa dhabihu kubwa mno kulijenga. Kwao, kukusanyika kwa Watakatifu pale kulikuwa utangulizi wa furaha na tukufu kwa Ujio wa Pili. Lakini majirani zao sehemu ile waliona mambo kitofauti. Walichukulia swala kwa madai kwamba Mungu ametoa nchi kwa Watakatifu, na walikuwa hawana raha kwa matokeo ya kisiasa, kiuchumi, na kijamii ya watu wengi mno kutoka dini zisizofahamika zikiingia katika eneo kwa haraka mno. Mara dukuduku likageuka kuwa vitisho, na vitisho vikageuka kuwa mateso na vurugu. Mnamo Julai 1833, ofisi ya uchapishaji ya Kanisa iliharibiwa, na mnamo Novemba Watakatifu walilazimishwa kuacha nyumba zao zilizokuwa huko Jackson County, Missouri.

Joseph Smith alikuwa mbali zaidi ya maili 800 huko Kirtland, na habari hizi zilichukuwa wiki nyingi kumfikia. Lakini Mungu alijua nini kilichokuwa kinatokea, na alifunua kwa Nabii Wake kanuni za amani na za kutia moyo ambazo zingewafariji Watakatifu—kanuni ambazo pia zinaweza kutusaidia wakati tunapokumbana na mateso, wakati matamanio yetu ya haki hayatimizwi, au wakati tunahitaji kukumbushwa kwamba mateso yetu ya kila siku hatimaye, kwa vyovyote vile, “yatafanya kazi kwa pamoja kwa faida [yetu]” (Mafundisho na Maagano 98:3).

Ona Watakatifu, 1:171–93; “Subirirni Neno la Bwana,” Ufunuo katika Muktadha, 196–201.

Picha
ikoni ya kujifunza binafsi

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Binafsi Maandiko

Mafundisho na Maagano 98:1–3, 11–14; 101:1–16

Majaribu yangu yanaweza kufanya kazi pamoja kwa faida yangu.

Baadhi ya mateso yetu maishani yanasababishwa na chaguzi zetu wenyewe. Mengine yanasababishwa na chaguzi za wengine. Na wakati mwingine hakuna wa kumlaumu—mambo mabaya hutokea tu. Bila kujali sababu, shida zinaweza kusaidia kutimiza azma takatifu. Unaposoma kile Mungu alichosema kuhusu shida za Watakatifu katika Mafundisho na Maagano 98:1–3, 11–14 na 101:1–16, unapata nini ambacho kinaweza kukusaidia kwenye majaribu yako? Ni kwa jinsi gani mistari hii inaathiri jinsi unavyoona changamoto unazokumbana nazo? Tafakari jinsi majaribu yako yalivyofanya kazi pamoja kwa faida yako na kufanikisha azma za Mungu katika maisha yako.

Ona pia 2 Nefi 2:2; Mafundisho na Maagano 90:24.

Mafundisho na Maagano 98:23–48

Bwana ananitaka kutafuta amani katika njia Yake.

Wakati si kila kitu katika Mafundisho na Maagano 98:23–48 kitatumika kwenye mwingiliano wako binafsi na wengine, je, ni kanuni zipi unazozipata ambazo zinaweza kukuongoza wakati wengine wanapokukosea? Inaweza kuwa yenye msaada kuwekea alama maneno au virai vinayoeleza jinsi Bwana alivyotaka Watakatifu kushughulikia migogoro huko Missouri.

Ona pia Jeffrey R. Holland, “Huduma ya Maridhiano,” Ensign au Liahona, Nov. 2018, 77–79.

Picha
Yesu Kristo

Maelezo kutoka Kristo na Kijana Tajiri Mtawala, na Heinrich Hofmann

Mafundisho na Maagano 100

Bwana anawajali wale wanaomtumikia.

Wiki chache tu baada ya Joseph kujua kuhusu mateso huko Missouri, mwongofu mpya alimwomba kusafiri kwenda Canada kushiriki injili pamoja na wanawe. Joseph alikubali, ingawa alikuwa na mashaka kuhusu kuiacha familia yake, hususani kwa sababu ya mateso na vitisho kwa familia yake pamoja na Kanisa. Wakiwa njiani kwenda Canada, Joseph na mwenzake, Sidney Rigdon, walisali kwa ajili ya faraja, na Sehemu ya 100 ilikuwa jibu la Bwana kwao. Unapata nini katika jibu la Bwana ambalo liliweza kuwapa hakikisho na kuwasaidia?

Yawezekana umewahi pia kuwa na uzoefu ambao ulikuhitaji wewe kuweka usawa kati ya dukuduku kwa ajili ya majukumu ya Kanisa na dukuduku kwa ajili ya familia yako. Ni kwa jinsi gani maneno ya Bwana katika sehemu ya 100 yanakusaidia katika hali kama hizo?

Ona pia “Misheni ya kwenda Canada,” Ufunuo katika Muktadha, 202–7.

Mafundisho na Maagano 101:43–65

Kufuata ushauri wa Mungu kunasaidia kuniweka salama.

Fumbo katika Mafundisho na Maagano 101:43–62 lilitolewa kuelezea kwa nini Bwana aliruhusu Watakatifu kufukuzwa nje ya Sayuni. Unaposoma mistari hii, je, unaona mifanano yoyote kati yako mwenyewe na watumishi katika fumbo? Unaweza kujiuliza mwenyewe: Je, nimewahi kuonyesha wasiwasi juu ya amri za Mungu? Ni kwa jinsi gani ukosefu wa imani au msimamo vinaweza kumruhusu “adui” kuwa na athari katika maisha yangu? Ni kwa jinsi gani ninaweza kumwonyesha Mungu kwamba nipo “tayari kuongozwa katika njia ya haki na iliyo sahihi kwa wokovu [wangu]”? (Ona mistari 63–65).

Picha
ikoni ya kujifunza kifamilia

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kifamilia na Jioni ya Nyumbani

Mafundisho na Maagano 98:16, 39–40.Kitu gani katika mistari hii kinaweza kutusaidia kuwa na amani zaidi katika familia yetu? Mngeweza kuimba wimbo kuhusu amani au msamaha, kama vile “Truth Reflects upon Our Senses” (Nyimbo za Kanisa, na. 273). Watoto wadogo wanaweza kupenda kuigiza kusameheana wao kwa wao.

Mafundisho na Maagano 99.Wakati John Murdock alipoitwa kuacha nyumba yake “ili kutangaza injili isiyo na mwisho” (mstari wa 1), alikuwa ndio kwanza amerudi kutoka kwenye misheni ngumu, iliyomchukua mwaka mmoja huko Missouri (ona “Misheni ya John Murdock kwenda Missouri,” Ufunuo katika Muktadha, 87–89). Tunapata nini katika sehemu ya 99 ambacho kiliweza kuwa cha msaada au cha kutia moyo kwa Kaka Murdock? Je, ni ujumbe upi Bwana anao kwa ajili yetu katika ufunuo huu?

Mafundisho na Maagano 100:16; 101:3–5, 18.Baada ya kusoma mistari hii, mnaweza kujadiliana jinsi ambavyo wahunzi lazima wapashe chuma kwa moto mkali kuondoa uchafu na kisha kukipa umbo kwa kukipiga na nyundo tena na tena (ona video “The Refiner’s Fire” kwenye ChurchofJesusChrist.org). Mnaweza pia kujifunza kuhusu jinsi vitu vingine vinavyosafishwa, kama vile maji au chumvi. Labda mngeweza kusafisha au kuosha kitu fulani kama familia. Kwa nini tunataka kuwa wasafi? Ni nini mifano hii hutufundisha kuhusu jinsi majaribu yetu yanavyoweza kutusaidia kuwa “watu safi”?

Mafundisho na Maagano 101:22–36.Ni kwa jinsi gani mistari hii iliweza kuwasaidia Watakatifu waliokuwa wanakabiliana na mateso? Ni kwa jinsi gani inaweza kuwasaidia watu wanaohisi hofu kuhusu hali za ulimwengu leo?

Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Msingi.

Wimbo uliopendekezwa: “Help Me, Dear Father,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 99.

Kuboresha Kujifunza Binafsi

Tafuta kanuni. Mzee Richard G. Scott alifundisha: “unapotafuta elimu ya kiroho, tafuta kanuni. … Kanuni ni mchanganyiko wa kweli, zilizofungashwa kwa matumizi ya hali mbali mbali” (“Acquiring Spiritual Knowledge,” Ensign, Nov. 1993, 86).

Picha
kundi la wavamizi likiwatesa Watakatifu

Missouri Inaungua, na Glen S. Hopkinson

Chapisha