Njoo, Unifuate
Machi 4–10. Mathayo 8–9; Marko 2–5: ‘Imani Yako Imekuponya’


“Machi 4–10. Mathayo 8–9; Marko 2–5: ‘Imani Yako Imekuponya’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano Jipya 2019 (2019)

“Machi 4–10. Mathayo 8–9; Marko 2–5,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2019

Picha
Yesu Anamponya Mtu kiwete

Uponyaji kwenye Mbawa Zake, na John McNaughton

Machi 4–10.

Mathayo 8–9; Marko 2–5

“Imani Yako Imekuponya”

Unaposoma Mathayo 8–9 na Marko 2–5, itikia misukumo unayopokea kutoka kwa Roho Mtakatifu. Fikiria kuandika chini ushawishi unaopokea na mambo unayoweza kufanya ili kufanyia kazi ushawishi huo.

Andika Misukumo Yako

Ni vigumu kusoma Agano Jipya bila kuvutiwa na matukio mengi ya Mwokozi akiponya wagonjwa na walioteseka—kila mmoja kuanzia mwanamke mwenye homa hadi kwa binti aliyekuwa ametangazwa kuwa amekufa. Je, ni ujumbe gani unaweza kuwa pale kwa ajili yetu katika miujiza hii ya uponyaji wa kimwili? Hakika ujumbe mmoja wa wazi ni kwamba Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu, mwenye nguvu juu ya mambo yote, ikijumuisha maumivu yetu ya kimwili na kutokukamilika kwetu. Lakini maana nyingine inapatikana katika maneno Yake kwa waandishi wenye kushuku: “Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi” (Marko 2:10). Kwa hiyo unaposoma kuhusu mtu kipofu au mkoma kuponywa, unaweza kufikiria uponyaji—wote kiroho na kimwili—unaoweza kupokea kutoka kwa Mwokozi na kumsikia akikuambia, “Imani Yako Imekuponya” (Marko 5:34).

Picha
ikoni ya kujifunza binafsi

Mawazo ya Kujifunza Maandiko Binafsi

Mathayo 8–9; Marko 25

Mwokozi anaweza kuponya udhaifu na magonjwa.

Sura hizi chache zimeandikwa mifano mingi ya uponyaji wa kimiujiza uliofanywa na Mwokozi. Unapojifunza uponyaji huu, tafuta ujumbe unaowezekana kuwa ni wa kwako. Unaweza kujiuliza mwenyewe: Je, mistari hii hufundisha nini kuhusu imani? Je, hadithi hii hufundisha nini kuhusu Mwokozi? Je, Mungu anataka nijifunze nini kutokana na muujiza huu?

Ona pia Dallin H. Oaks, “Kuponya Wagonjwa,” Ensign au Liahona, Mei 2010, 47–50.

Picha
Yesu anamponya mgonjwa

Yesu Anamponya Mgonjwa, na Joseph Brickey, baada ya Heinrich Hofmann

Mathayo 8:5–13; Marko 5:24–34

Ninaweza kutafuta msaada wa Mungu hata kama ninajiona kutostahili.

Akida, Myunani, alijiona kutostahili kuwa na Mwokozi nyumbani kwake. Mwanamke mwenye tatizo la kutokwa damu alifikiriwa mchafu na alitengwa na jamii ya Kiyahudi. Bado Mwokozi aliwabariki wote. Je, unajifunza nini kutokana na matukio haya mawili kuhusu kutafuta msaada kutoka kwa Bwana?

Mathayo 8:18–22; Marko 3:31–35

Kuwa mfuasi wa Yesu Kristo inamaanisha kwamba ninamweka Yeye kwanza katika maisha yangu.

Katika mistari hii, Yesu alifundisha kwamba kuwa wafuasi Wake kunatuhitaji sisi kumweka Yeye kwanza katika maisha yetu, hata kama hiyo mara nyingine humaanisha tunapaswa kuacha mambo mengine ambayo tunayathamini. Unapojifunza dondoo hizi, tafakari ufuasi wako wewe mwenyewe. Je, ni kwa nini ni lazima wafuasi wawe tayari kumweka Mwokozi kwanza? Je, ni kipi ungehitajika kukiacha ili kumweka Yesu kwanza? (Ona pia Luka 9:57–62.)

Mathayo 8:23–27; Marko 4:35–41

Yesu Kristo ana uwezo wa kuleta amani katikati ya dhoruba za maisha.

Je, umewahi kujisikia jinsi wanafunzi wa Yesu walivyokuwa kwenye dhoruba baharini—kuangalia mawimbi ya maji yakikijaza chombo na kuuliza, “Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia?”

Katika Marko 4:35–41, unapata maswali manne. Orodhesha kila moja, na tafakari linakufundisha nini kuhusu kukabiliana na changamoto za maisha ukiwa na imani katika Yesu Kristo. Je, ni kwa jinsi gani Mwokozi huleta amani katika dhoruba za maisha yako?

Mathayo 9:1–13; Marko 2:15–17

Ninaweza kutetea imani zangu kwa kufundisha kanuni za kweli.

Wakati mwingine ni vigumu kujua tujibu nini wakati watu wanapokosoa imani na desturi za dini yetu. Unaposoma Mathayo 9:1–13 na Marko 2:15–17, tafuta ukosoaji wa washitaki na majibu ya Mwokozi. Fikiria kuwekea alama ukosoaji na majibu katika rangi tofauti au kuyaandika chini. Je, unaona nini kuhusu jinsi Mwokozi alivyofundisha? Je, kufuata mfano Wake kungekusaidiaje kama ungepaswa kutetea kanuni ya injili au desturi ya Kanisa?

Ona pia video ya “Everyday Example: When Beliefs Are Questioned:” (LDS.org).

Mathayo 9:1–8

Kwa sababu ya toba, ninaweza kujipa moyo mkuu.

Wakati mtu aliyepooza alipoletwa kwa Mwokozi, ilikuwa wazi kwa umati kwamba alihitaji kuponywa kimwili. Lakini Yesu alishughulikia hitaji kuu la mtu yule kwanza—msamaha wa dhambi zake. Hata kama mtu yule asingeliponywa kimwili, bado angeweza kufuata ushauri wa Yesu wa ku “jipa moyo mkuu” (Mathayo 9:2). Je, ni wakati gani umehisi shangwe kwa sababu umesamehewa? (Ona pia Alma 36:18–24.)

Picha
ikoni ya kujifunza kwa familia.

Mawazo ya Kujifunza Maandiko Kwa Familia na Jioni ya Familia Nyumbani

Unapoendelea kujifunza kuhusu huduma ya Mwokozi na familia yako, Roho anaweza kukusaidia kujua kanuni zipi zisisitizwe na kujadiliwa ili kukidhi mahitaji ya familia yako. Haya ni baadhi ya mapendekezo:

Mathayo 8–9; Marko 25

Fikiria kutengeneza orodha ya miujiza iliyoelezwa katika sura hizi na kutafuta picha za baadhi ya miujiza hiyo. (ona Kitabu cha Sanaa ya Injili au LDS.org). Unaweza kumuuliza kila mwanafamilia kuelezea kuhusu mojawapo ya miujiza (kwa kutumia picha kama ipo) na kuelezea walichojifunza. Unaweza kuelezea baadhi ya mifano ya miujiza ambayo umeshuhudia au kusoma katika historia ya kanisa katika siku hizi za mwisho.

Mathayo 9:10–13

Je, tunajifunza nini kutokana na jinsi Mwokozi alivyowachukulia watoza ushuru na wenye dhambi, ambao walitengwa na wengine? Je, ni kwa jinsi gani tunaweza kufuata mfano Wake tunapotangamana na watu wengine?

Mathayo 9:36–38

Je, ni kwa jinsi gani unaweza kuwasaidia watu wa familia yako kuelewa ombi la Mwokozi la wafanyakazi zaidi ili kusaidia kufundisha injili? Ungeweza kufanya kitu rahisi kama kufanya kazi pamoja katika jukumu ambalo lingechukua muda mrefu kwa mtu mmoja, kama vile kusafisha jiko baada ya chakula cha jioni. Je, tunaweza kufanya nini katika kushiriki na wengine ujumbe wa injili?

Marko 4:35–41

Maelezo haya yangeweza kuwasaidia wanafamilia wanapohisi kuogopa? Pengine wangeweza kusoma mstari 39 na kuelezea uzoefu wao wakati Mwokozi alipowasaidia kuhisi amani wakati wa nyakati za misukosuko au hofu.

Kwa mawazo zaidi juu ya kufundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii ndani ya Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Msingi.

Kuboresha Ufundishaji Wetu

Kuwa mwenye kupatikana na kufikika. Baadhi ya nyakati bora zaidi za kufundisha huanza kama maswali au wasiwasi katika mioyo ya wanafamilia. Acha wanafamilia wajue kupitia maneno na matendo yako kwamba una shauku ya kuwasikiliza (ona Kufundisha katika Njia ya Mwokozi, 16).

Picha
mtu kitandani akishushwa kwa Yesu kupitia juu ya paa

Kristo na mtu mwenye kupooza, na J. Kirk Richards

Chapisha