Njoo, Unifuate
Aprili 1–14. Mathayo16–17; Marko 9; Luka 9: ‘Wewe Ndiwe Kristo’


April 1–14. Mathayo 16–17; Marko 9; Luka 9: ‘Wewe Ndiwe Kristo’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano Jipya 2019 (2019)

April 1–14. Mathayo16–17; Marko 9; Luka 9,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2019

Kugeuka sura kwa Kristo

Kugeuka sura, na Carl Heinrich Bloch

Aprili 1–14.

Mathayo 16–17; Marko 9; Luka 9

“Wewe Ndiwe Kristo”

Kwa muda wa wiki mbili zijazo, tafakari ushuhuda wa Petro, unaopatikana katika Mathayo 16:15–17, na shuhuda za manabii na mitume ambazo utasikia wakati wa mkutano mkuu.

Andika Misukumo Yako

Je, si inashangaza kwamba Mafarisayo na Masadukayo walitaka kwamba Yesu awaonyeshe “ishara kutoka mbinguni”? Je, miujiza Yake mingi iliyojulikana vyema haikutosha? Je, vipi kuhusu mafundisho yake yenye nguvu au njia nyingi Alizotimiza unabii wa kale? Hitaji lao halikuchochewa na ukosefu wa ishara lakini kwa kutokuwa radhi “kutambua ishara” na kuzikubali. (Ona Mathayo 16:1–4.)

Petro, kama Mafarisayo na Masadukayo, alishuhudia miujiza ya Mwokozi na kusikia mafundisho Yake. Lakini ushuhuda wa hakika wa Petro, “Wewe Ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai,” haukuja kupitia milango ya fahamu za kimwili— “mwili na damu” yake. Ushuhuda wake ulifunuliwa kwake na “Baba yetu aliye mbinguni.” Ufunuo ni mwamba ambao juu yake Mwokozi alijenga Kanisa Lake wakati huo na sasa—ufunuo kutoka mbinguni kuja kwa watumishi Wake. Na huu ndio mwamba ambao juu yake tunaweza kujenga ufuasi wetu—ufunuo kwamba Yesu ndiye Kristo na kwamba watumishi Wake wanashikilia “funguo za ufalme.” Tunapokuwa tumejengwa juu ya msingi huu, “milango ya kuzimu haitatushinda [sisi].” Mathayo 16:15–19

Ikoni ya kujifunza binafsi

Mawazo ya Kujifunza Maandiko Binafsi

Mathayo 16:13–17; Luka 9:18–21

Ushuhuda wa Yesu Kristo huja kwa ufunuo.

Kama Yesu Kristo akiwauliza watu leo, “Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani?” majibu yao yatatofautiana na majibu yaliyotolewa na watu katika wakati Wake. Je, ni mitazamo ipi ya siku hizi kuhusu Yesu umeigundua? Je, wewe ungejibu nini kama Yesu angekuuliza “Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?” (Ona Mathayo 16:13–15.)

Tafakari ushuhuda wako wa Mwokozi na jinsi gani uliupokea. Je, unajifunza nini kutoka Mathayo 16:15–17 ambacho kinaweza kuuimarisha? Kama ungependa kujifunza zaidi kuhusu ushuhuda na ufunuo binafsi, yachunguze maandiko haya: Yohana 15:26; 1 Wakorintho 12:3; 2 Nefi 31:18; Alma 5:45–48; na Mafundisho na Maagano 8:2–3.

Mathayo 17:1–9; Marko 9:2–10; Luka 9:28–36

Je, ni kitu gani kilitokea katika Mlima wa Kugeuka Sura?

Yesu alipowachukua Petro, Yakobo, na Yohana kwenye “kilele cha mlima,” Aligeuka sura (au kuvikwa utukufu) mbele yao. Musa na Elia (Eliya) pia walitokea na kukabidhi funguo za ukuhani juu ya Mitume. Funguo hizi ziliwawezesha kuliongoza Kanisa la Kristo duniani baada ya Ufufuko Wake (ona Kamusi ya Biblia, “Kugeuka Sura, Mlima wa”). Funguo hizi pia zilirejeshwa katika siku yetu (ona M&M 110).

Mathayo16:13–19; 17:1–9

Je “funguo za ufalme wa mbinguni” ni nini?

“Funguo za ufalme wa mbinguni” ambazo Mwokozi aliahidi kumpa Petro ni funguo za ukuhani (Mathayo 16:19). “Funguo za ukuhani ni mamlaka ambayo Mungu amewapa viongozi wa ukuhani ili kuongoza, kudhibiti, na kutawala matumizi ya ukuhani Wake hapa duniani.” Matumizi ya mamlaka ya ukuhani hudhibitiwa na wale wanaoshikilia funguo zake (ona M&M 65:2; 81:2; 124:123). Wale wanaoshikilia funguo za ukuhani wana haki ya kuongoza na kulielekeza Kanisa ndani ya mamlaka yao” (Kitabu cha Muongozo 2: Usimamizi wa Kanisa [2010], 2.1.1).

sanamu ya Petro akipewa funguo

“Funguo za ufalme wa mbinguni” ni funguo za ukuhani.

Funguo za ukuhani zilizotolewa kwa Petro na Mitume wengine juu ya Mlima wa Kugeuka Sura zilirejeshwa katika siku yetu (ona M&M 110:11–16). Wale wanaoshikilia funguo za ukuhani hujumuisha Urais wa Kwanza na Akidi ya Mitume Kumi na Wawili na Viongozi wengine wakuu wenye mamlaka; marais wa mahekalu, misheni, vigingi, na wilaya; na maaskofu, marais wa matawi, na marais wa akidi.

Ona pia Neil L. Andersen, “Nguvu katika Ukuhani,” Ensign au Liahona, Nov. 2013, 92–95; True to the Faith, 126–27; “Funguo za Ukuhani: Urejesho wa Funguo za Ukuhani” (video, LDS.org).

Mathayo 17:14–21; Marko 9:14–29

Katika kutafuta imani kubwa, lazima kwanza nishikilie imani ambayo tayari ninayo.

Baba aliyetajwa katika Mathayo 17 na Marko 9 alikuwa na sababu za kuwa na shaka kwamba Yesu angeweza kumponya kijana wake. Aliwaomba wanafunzi wa Yesu kumponya kijana wake, na hawakuweza. Lakini Mwokozi alipomualika kuonyesha imani, hakuzingatia shaka yake. “Bwana, Ninaamini,” alisema, na kisha, katika kutambua kwamba imani yake haikuwa kamilifu, aliongeza “Nisaidie kutokuamini kwangu.”

Je, Roho alikufundisha nini uliposoma kuhusu muujiza huu? Je, ni kwa jinsi gani Baba wa Mbinguni amekusaidia kuzidisha imani yako? Je, unaweza kufanya nini ili kujenga juu ya imani ambayo tayari unayo? Pengine ungeweza kukusanya orodha ya maandiko, ujumbe wa mkutano, au uzoefu ambao umeimarisha imani yako.

Ona pia Jeffrey R. Holland, “Bwana, Naamini,” Ensign au Liahona, Mei 2013, 93–95.

ikoni ya kujifunza kwa familia.

Mawazo ya Kujifunza Maandiko Kwa Familia na Jioni ya Familia Nyumbani

Unaposoma maandiko na familia yako, Roho anaweza kukusaidia kujua kanuni zipi zisisitizwe na kujadiliwa ili kukidhi mahitaji ya familia yako. Haya ni baadhi ya mapendekezo:

Mathayo 16:13–19; 17:1–9

Kuwafundisha watoto kuhusu funguo za ukuhani, unaweza kusimulia hadithi ya Mzee Gary E. Stevenson kuhusu kufungiwa nje ya gari lake (ona “Ziko Wapi Funguo na Mamlaka ya Ukuhani?” Ensign au Liahona, Mei 2016, 29–32). Unaweza kuwaacha watoto wako watumie funguo kufungua nyumba, gari, au vifufi vingine. Fikiria kuonyesha picha ya Rais wa Kanisa na kushuhudia kwamba anashikilia funguo zote za ukuhani, kama ilivyokuwa kwa Petro.

Mathayo 17:20

Manabii wenye imani katika Yesu Kristo wamehamisha milima (ona Yakobo 4:6; Musa 7:13). Ushuhuda ufuatao kutoka kwa Askofu Richard C. Edgley unaweza kufanya mstari huu uwe husika kwa familia yako: “Sijawahi kushuhudia kuhamishwa kwa mlima halisi. Lakini kwa sababu ya imani, Nimeona mlima wa shaka na kukata tamaa ukihamishwa na kubadilishwa na tumaini na msimamo wa kutegemea mazuri. Kwa sababu ya imani, mimi binafsi nimeshuhudia mlima wa dhambi ukibadilishwa na toba na msamaha. Na kwa sababu ya imani, mimi binafsi nimeshuhudia mlima wa maumivu ukibadilishwa na amani, tumaini, na shukrani. Ndiyo, Nimeona milima ikihamishwa” (“Imani—Chaguo Ni Lako,” Ensign au Liahona, Nov. 2010, 33). Je, ni baadhi ya milima ipi katika maisha yetu ambayo inahitaji kuhamishwa? Je, ni kwa jinsi gani tunaweza kuonyesha imani katika nguvu za Mungu za kutusaidia sisi kuhamisha milima hii?

Luka 9:61–62

Je, inamaanisha nini kuangalia nyuma baada ya kuweka mkono kwenye jembe? Je, kwa nini mtazamo huu hutufanya sisi tusifae kwenye ufalme wa Mungu?

Kwa mawazo zaidi juu ya kufundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii ndani ya Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Msingi.

Kuboresha Ufundishaji Wetu

Kusanyika pamoja mara kwa mara. Rais Henry B. Eyring alifundisha: “Kamwe usipoteze nafasi ya kuwakusanya watoto pamoja ili kujifunza mafundisho ya injili ya Yesu Kristo. Nyakati kama hizo ni chache sana ikilinganishwa na juhudi za adui” (“Nguvu ya Kufundisha Injili,” Ensign, Mei 1999, 74).

mtu mwenye kijana mgonjwa mbele ya Yesu

Bwana, Nimemleta kwako Mwana Wangu, na Walter Rane