Njoo, Unifuate
Julai 8–14. Matendo ya Mitume 6–9: ‘Ni Nini Unataka Nifanye?’


“Julai 8–14. Matendo ya Mitume 6–9: ‘Ni Nini Unataka Nifanye?’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano Jipya 2019 (2019)

“Julai 8–14. Matendo ya Mitume 6–9,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2019

Picha
Paulo katika barabara ya kwenda Dameski

Na Tuishi Hivyo, na Sam Lawlor

Julai 8–14

Matendo ya Mitume 6-9

“Ni Nini Unataka Nifanye?”

Anza kwa kusoma Matendo ya Mitume 6–9. Mapendekezo katika muhtasari huu yanaweza kukusaidia kutambua baadhi ya kanuni muhimu katika sura hizi, japokuwa unaweza kupata zingine katika kujifunza kwako mwenyewe.

Andika Misukumo Yako

Kama mtu yeyote alionekana kama mtu asiyewezekana kwa uongofu, yawezekana alikuwa Sauli—mfarisayo ambaye alikuwa na sifa ya kuwatesa Wakristo. Hivyo Bwana alipomwambia mfuasi aliyeitwa Anania kumtafuta Sauli na kumpa baraka, Anania alikuwa na kusita kunakoeleweka. “Bwana,” alisema, “Nimesikia habari za mtu huyu kwa watu wengi, mabaya mengi aliyowatenda watakatifu wako” (Matendo ya Mitume 9:13). Lakini Bwana aliujua moyo wa Sauli na uwezo wake, na Alikuwa na wito akilini kwa ajili ya Sauli: “Huyu ni chombo kiteule kwangu, kulichukua Jina langu mbele ya Mataifa, na wafalme, na wana wa Israeli” (Matendo ya Mitume 9:15). Hivyo Anania alitii, na alipompata huyu mtesaji wa zamani, alimuita “Ndugu Sauli” (Matendo ya Mitume 9:17). Kama Sauli aliweza kubadilika kabisa na Anania kuweza kumkaribisha kwa uhuru, je, tunapaswa kumfikiria mtu yeyote kama asiyewezekana kubadilika—ikiwemo sisi wenyewe?

Picha
ikoni ya kujifunza binafsi

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Binafsi

Matendo ya Mitume 6–8

Moyo wangu unahitaji kuwa “mnyofu mbele za Mungu.”

Kukua kwa kanisa kulimaanisha kukua kwa hitaji la wafuasi kutumikia katika ufalme. Kulingana na Matendo ya Mitume 6:1–15, ni sifa zipi Mitume Kumi na Wawili waliangalia kwa wale ambao wangetumikia pamoja nao? Unaposoma Matendo ya Mitume 6–8, gundua jinsi sifa hizi, na zingine, zilidhihirishwa katika watu kama Stefano na Filipo. Nini kilipungua kwa Simoni, na nini tunaweza kujifunza kutoka kwake kuhusu kuwa radhi kubadilika?

Je, kuna chochote unahisi kushawishika kukibadilisha ili kuhakikisha kwamba moyo wako ni “mnyofu mbele za mungu”? (Matendo ya Mitume 8:21–22). Ni kwa jinsi gani kufanya badiliko hili kutakubariki unapomtumikia Mungu?

Matendo ya Mitume 6–7

Kumpinga Roho Mtakatifu kunaweza kusababisha kumkataa Mwokozi na manabii Wake.

Viongozi wa Kiyahudi, japo walikabidhiwa jukumu la kuwaandaa watu kwa ujio wa Masiya, walimkataa Yesu Kristo na kudai Kusulubiwa Kwake kwa sababu ya kiburi chao na kutafuta madaraka. Ni kwa jinsi gani hili lilitokea? Stefano aliwatangazia, “Siku zote mnampinga Roho Mtakatifu” (Matendo ya Mitume 7:51). Unafikiri inamaanisha nini kumpinga Roho Mtakatifu? Ni kwa nini kumpinga Roho Mtakatifu husababisha kumkataa Mwokozi na manabii Wake?

Unaposoma Matendo ya Mitume 6–7, tafuta ujumbe mwingine ambao Stefano aliwafundisha Wayahudi. Alikuwa akionya dhidi ya mitazamo ipi? Je, unagundua mitazamo yoyote kama hiyo ndani yako? Je, ni maneno gani ya Stefano hukufundisha kuhusu matokeo ya kumpinga Roho Mtakatifu? Ni kwa jinsi gani unaweza kuwa mwepesi kuhisi na kuitikia ushawishi wa Roho Mtakatifu katika maisha yako?

Ona pia filamu “Kifo cha Kishahidi cha Stefano” (LDS.org).

Matendo ya Mitume 7:54–60

Tofauti na Stefano, nani mwingine alikufa kifo cha kishahidi kwa ajili ya ushuhuda wao juu ya Yesu Kristo?

Stefano ni Mkristo wa kwanza anayejulikana kufa kifo cha kishahidi (mtu anayeuwawa kwa sababu ya imani yake) baada ya Ufufuko wa Yesu. Watakatifu wengine wengi katika historia waliuawa pia kwa sababu hawangeikana imani yao katika Yesu Kristo. Baadhi ya hawa wametajwa katika 2 Mambo ya Nyakati 24:20–21; Marko 6:17–29; Matendo ya Mitume 12:1–2; Ufunuo 6:9–11; Mosia 17:20; Alma 14:8–11; Helamani 13:24–26; Mafundisho na Maagano 109:47–49; 135:1–7; na Ibrahimu 1:11. Inawezekana kwamba baada ya Ufufuo wa Mwokozi, Mitume wote isipokuwa Yohana walikufa kama mashahidi.

Matendo ya Mitume 8:26–39

Roho Mtakatifu atanisaidia kuwaongoza wengine kwa Yesu Kristo.

Je, unajifunza nini kuhusu kushiriki na wengine injili kutokana na tukio katika Matendo ya Mitume 8:26–39? Ni kwa jinsi gani Roho Mtakatifu alimsaidia Filipo? Ni kwa jinsi gani kushiriki injili na wengine ni kama kuwa kiongozi? (Ona Matendo ya Mitume 8:31).

Matendo ya Mitume 9:1–31

Ninapojiweka chini ya mapenzi ya Bwana, ninaweza kuwa chombo katika mikono Yake.

Uongofu wa Sauli unaonekana wa ghafla sana; alikwenda “moja kwa moja” kutoka kwenye kuwafunga Wakristo mpaka kwenye kumhubiri Kristo katika masinagogi (Matendo ya Mitume 9:20). Unaposoma hadithi yake, tafakari ni kwa nini alikuwa radhi kubadilika. (Kusoma maelezo ya Sauli mwenyewe juu ya uongofu wake, ona Matendo ya Mitume 22:1–16 na 26:9–18. Kumbuka kuwa katika wakati wa matukio haya, jina la Sauli lilikuwa limebadilishwa kuwa Paulo.)

Wakati ni kweli kwamba uzoefu wa Sauli siyo wa kawaida—kwa watu wengi, uongofu ni mchakato mrefu zaidi—je, kuna chochote unachoweza kujifunza kutoka kwa Sauli kuhusu uongofu? Je, unajifunza nini kutokana na jinsi Anania na wafuasi wengine walivyopokea uongofu wa Sauli? Je, utafanya nini ili kutumia mafundisho haya maishani mwako? Unaweza kuanza kwa kuuliza katika maombi, kama Sauli alivyofanya, “Ni Nini Unataka Nifanye?” Au unaweza kuandika swali hili kama kichwa cha habari katika shajara yako na kuandika mawazo yanayokujia baada ya muda.

Ona pia Dieter F. Uchtdorf, “Kusubiri katika Barabara ya Dameski,” Ensign au Liahona, Mei 2011, 70–77; “Barabara ya kwenda Dameski” (filamu, LDS.org).

Picha
ikoni ya kujifunza kifamilia.

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kifamilia na Jioni ya Familia Nyumbani.

Unaposoma maandiko na familia yako, Roho anaweza kukusaidia kujua kanuni zipi zisisitizwe na kujadiliwa ili kukidhi mahitaji ya familia yako. Hapa kuna baadhi ya mapendekezo:

Matendo ya Mitume 6:8–7:60

Linganisha matukio ya Stefano katika Matendo ya Mitume 6:8 na Matendo ya Mitume 7:51–60 na matukio ya Mwokozi katika Luka 23:1–46. Ni kwa jinsi gani Stefano alifuata mfano wa Mwokozi?

Matendo ya Mitume 7:51–60

Ni kwa jinsi gani Roho Mtakatifu alimbariki Stefano alipokuwa akiteswa? Ni lini tumepokea nguvu kutoka kwa Roho Mtakatifu wakati wa nyakati ngumu?

Matendo ya Mitume 9:5

Je, familia yako inajua “kujisumbua bure? humaanisha nini? Mchomo ilikuwa ni mkuki wenye ncha kali uliotumika kuendesha wanyama. Kwa kawaida wanyama wangepiga teke kwa nyuma walipochomwa, tendo ambalo lingefanya mkuki kuzama zaidi kwenye mwili wa mnyama. Ni kwa njia zipi analojia hii inaweza kutumika kwetu?

Picha
Petro akimfufua Tabitha kutoka wafu

Tabitha Ondoka, na Sandy Freckleton Gagon

Matendo ya Mitume 9:32–43

Fikiria kuwaalika wanafamilia wako kuchora picha za hadithi katika Matendo ya Mitume 9:32–43. Je, wanajifunza nini kuhusu ufuasi wa kweli kutoka kwa Ainea, Tabitha, na wajane wa Yafa? Ni kwa jinsi gani mtu ambaye “amejaa matendo mema” huwasaidia wengine kuamini katika Bwana? (ona Matendo ya Mitume 9:36, 42; “Sura ya 60: Petro anamrudishia Tabitha Uzima,” Hadithi za Agano Jipya, 156–57, au filamu inayohusiana katika LDS.org).

Kwa mawazo zaidi juu ya kufundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii ndani ya Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Msingi.

Kuboresha Kujifunza Binafsi

Linganisha Maandiko na Maisha Yako. Unaposoma, fikiria ni kwa jinsi gani hadithi na mafundisho katika maandiko yanahusika katika maisha yako. Kwa mfano, ni lini umehisi “kujaa Roho Mtakatifu” katika nyakati za jaribu au mateso? (Matendo ya Mitume 7:55)

Picha
Stefano akipigwa mawe

Namuona Mwana wa Mtu Amesimama Mkono wa Kuume wa Mungu, na Walter Rane

Chapisha