Njoo, Unifuate
Julai 1–7. Matendo ya Mitume 1–5: ‘Nanyi Mtakuwa Mashahidi Wangu’


“Julai 1–7. Matendo ya Mitume 1–5: ‘Nanyi Mtakuwa Mashahidi Wangu’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano Jipya 2019 (2019)

“Julai 1–7. Matendo ya Mitume 1–5,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2019

Picha
siku ya Pentekoste

Siku ya Pentekoste, na Sidney King

Julai 1–7

Matendo ya Mitume 1–5

“Nanyi Mtakuwa Mashahidi Wangu”

Unapojifunza Matendo ya Mitume 1–5, Roho Mtakatifu anaweza kukupa mwongozo wa kiungu ili uzipate kweli ambazo zinahusika kwa ajili ya maisha yako. Andika kwa kifupi mistari inayokuvutia, na tafuta fursa za kuelezea kile unachojifunza.

Andika Misukumo Yako

Je, umewahi kujiuliza kuwa yawezekana Petro alikuwa akifikiria na kuhisi nini wakati yeye, na Mitume wengine, “walipokaza macho mbinguni” wakati Yesu akipaa kwa Baba Yake? (Matendo ya Mitume 1:10). Kanisa lililokuwa limeanzishwa na Mwana wa Mungu sasa lilikuwa likiongozwa na Yesu kupitia Petro, nabii wa Mungu. Jukumu la kuongoza juhudi za “kufundisha mataifa yote” sasa lilikuwa kwa Petro (Mathayo 28:19). Lakini kama alijiona kutokustahili au kuogopa, hatupati ushahidi wowote wa hilo katika kitabu cha Matendo ya Mitume. Kile tunachokiona ni mifano ya shuhuda za ujasiri na uongofu, miujiza ya uponyaji, maonyesho ya kiroho, na ukuaji mkubwa kwa Kanisa. Sasa, kwa kipawa cha Roho Mtakatifu, Petro hakuwa tena yule mvuvi asiye na elimu Yesu aliyemkuta katika fukwe za Bahari ya Galilaya. Wala hakuwa mtu aliyefadhaika ambaye wiki kadhaa kabla alikuwa akilia kwa uchungu kwa sababu alikana kwamba hakumjua Yesu wa Nazareti.

Katika kitabu cha Matendo ya Mitume, utasoma matamko yenye nguvu kuhusu Yesu Kristo na injili Yake. Utajionea pia ni kwa jinsi gani injili hiyo inaweza kuwabadilisha watu—ukiwemo wewe—kuwa wafuasi mashujaa ambao Mungu anajua wanaweza kuwa.

Picha
ikoni ya kujifunza binafsi

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Binafsi

Matendo ya Mitume 1:1–8, 15–26; 2:1–42; 4:1–13, 31–33

Yesu Kristo analiongoza Kanisa Lake kupitia Roho Mtakatifu.

Kitabu cha Matendo ya Mitume huelezea jitihada za Mitume kulijenga Kanisa la Yesu Kristo baada ya Kupaa kwa Mwokozi. Japokuwa Yesu Kristo hakuwepo tena duniani, Aliliongoza Kanisa kwa ufunuo kupitia Roho Mtakatifu. Fikiria jinsi Roho Mtakatifu alivyowaongoza viongozi wapya wa Kanisa la Kristo unapopitia tena dondoo zifuatazo: Matendo ya Mitume 1:1–8, 15–26; 2:1–42; 4:1–13, 31–33.

Je, ni zipi baadhi ya kazi, miito, au majukumu ambayo Bwana amekupatia wewe? Je, unajifunza nini kutokana na uzoefu wa Mitume hawa wa mwanzo kuhusu ni jinsi gani unaweza kumtegemea Roho Mtakatifu ili akuongoze?

Ona Kamusi ya Biblia, “Roho Mtakatifu.”

Matendo ya Mitume 2:1–18

Je, lengo la vipawa vya ndimi ni nini?

Vipawa vya ndimi wakati mwingine hujulikana kama kuzungumza katika lugha ambayo hakuna anayeielewa. Hata hivyo, Nabii Joseph Smith alirejea matukio katika Matendo ya Mitume 2 kufafanua kwamba kipawa hiki cha Roho “hutolewa kwa madhumuni ya kuhubiri [injili] miongoni mwa wale ambao lugha yao haieleweki; kama ilivyokuwa katika siku ya Pentekoste. … Mpango mkuu wa [kipawa cha] ndimi ni kuongea na wageni wanaoishi katika nchi” (Mafundisho ya Marais wa Kanisa: Joseph Smith [2008], 383–84). Sherehe ya Pentekoste, sikukuu kubwa ya mapumziko ya Kiyahudi, iliwaleta Wayahudi kutoka katika mataifa mengi kuja Yerusalemu. Kipawa cha ndimi kiliruhusu wageni hawa kuelewa maneno ya Mitume katika lugha mama zao.

Matendo ya Mitume 2:36–47; 3:13–21

Kanuni na ibada za kwanza za injili hunisaidia kuja kwa Kristo.

Je, umewahi kujisikia “kuchomwa moyoni [mwako],” kama wale Wayahudi katika siku ya Pentekoste? (Matendo ya Mitume 2:37). Labda ulifanya jambo unalojutia, au labda tu unataka kubadilisha maisha yako. Unapaswa kufanya nini unapokuwa na hisia hizi? Ushauri wa Petro kwa Wayahudi unapatikana katika Matendo ya Mitume 2:38. Gundua jinsi kanuni na ibada za kwanza za injili (ikijumuisha imani, toba, ubatizo, na kipawa cha Roho Mtakatifu—au kile ambacho wakati mwingine hujulikana kama mafundisho ya Kristo) yalivyowagusa waongofu hawa, kama ilivyoandikwa katika Matendo ya Mitume 2:37–47.

Yawezekana tayari umekwisha batizwa na kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu, je, ni kwa jinsi gani unaendelea kutumia mafundisho ya injili ya Kristo? Fikiria maneno haya kutoka kwa Mzee Dale G. Renlund: “Tunaweza kukamilishwa kwa kurudia rudia … kuifanyia kazi imani katika [Kristo], kutubu, kupokea sakramenti ili kufanya upya maagano na baraka za ubatizo, na kumpokea Roho Mtakatifu kama mwenza daima kwa kiwango kikubwa. Tunapofanya hivyo, tunakuwa zaidi kama Kristo na tunaweza kuvumilia hadi mwisho, na yote yanayoambatana na hayo” (“Watakatifu wa Siku za Mwisho Huendelea Kujaribu,” Ensign au Liahona, Mei 2015, 56).

Ona pia 2 Nefi 31; 3 Nefi 11:31–4127; Brian K. Ashton, “Injili ya Kristo,” Ensign au Liahona, Nov. 2016, 106–9.

Matendo ya Mitume 3:19–21

Je “nyakati za kuburudishwa” na “zamani za kufanywa upya vitu vyote” ni nini?

“Nyakati za kuburudishwa” humaanisha Milenia, wakati ambapo Yesu Kristo atarejea duniani. “Zamani za kufanywa upya vitu vyote” humaanisha Urejesho wa injili.

Matendo ya Mitume 3; 4:1–31; 5:12–42

Wafuasi wa Yesu Kristo hupewa nguvu kufanya miujiza katika jina Lake.

Mtu dhaifu alitumaini kupokea pesa kutoka kwa wale waliokuja hekaluni. Lakini watumishi wa Bwana walimpa kikubwa zaidi. Unaposoma Matendo ya Mitume 3; 4:1–31; na 5:12–42, fikiria jinsi gani muujiza uliofuata uliwagusa:

Mtu kiwete

Petro na Yohana

Washuhudiaji hekaluni

Kuhani mkuu na watu wa baraza

Watakatifu wengine

Ona pia filamu “Petro na Yohana Wanamponya Mtu Dhaifu Tangu Kuzaliwa,” “Petro Anahubiri na Anakamatwa” (LDS.org).

Picha
ikoni ya kujifunza kifamilia.

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kifamilia na Jioni ya Familia Nyumbani.

Unaposoma maandiko na familia yako, Roho anaweza kukusaidia kujua kanuni zipi zisisitizwe na kujadiliwa ili kukidhi mahitaji ya familia yako. Hapa kuna baadhi ya mapendekezo:

Matendo ya Mitume 2:37

Ni lini tumejisikia “kuchomwa mioyoni [mwetu]” wakati mtu alipokuwa akifundisha injili? Hisia hii inamaanisha nini? Kwa nini ni muhimu kusema, “Tutendeje?” tunapopata hisia kama hizi?

Matendo ya Mitume 3:1–8

Ni kwa jinsi gani mtu aliyekuwa hekaluni alibarikiwa tofauti na vile alivyokuwa akitegemea? Ni kwa jinsi gani tumeona baraka za Baba wa Mbinguni zikitujia katika njia tusizotegemea?

Picha
Petro anamponya mtu

Nilicho Nacho Ndicho Nikupacho, na Walter Rane

Matendo ya Mitume 3:12–26; 4:1–21; 5:12–42

Ni kitu gani kinakuvutia kuhusu uaminifu wa Petro na Yohana? Tunawezaje kuwa jasiri katika ushuhuda wetu juu ya Yesu Kristo?

Matendo ya Mitume 4:32–5:11

Familia yako inaweza kufurahia kuigiza tukio la Anania na Safira wakiwa na mavazi ya kawaida na sarafu kadhaa. Ni mafunzo gani tunapata kutoka kwenye hadithi hii? Kutegemea mahitaji ya familia yako, mnaweza kujadili uaminifu, kuwakubali viongozi wa kanisa, au wakfu.

Kwa mawazo zaidi juu ya kufundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii ndani ya Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Msingi.

Kuboresha Ufundishaji Wetu

Chagua mada. Acha wanafamilia kufanya zamu kuchagua mada kutoka Matendo ya Mitume 1–5 ili kujifunza pamoja.

Picha
Kupaa Kwa Yesu

Kupaa kwa Bwana, na William Henry Margetson

Chapisha