Njoo, Unifuate
Julai 22–28. Matendo ya Mitume 16–21: ‘Bwana Alituita Kuihubiri Injili’


“Julai 22–28. Matendo ya Mitume 16–21: ‘Bwana Alituita Kuihubiri Injili’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano Jipya 2019 (2019)

“Julai 22–28. Matendo ya Mitume 16–21,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2019

Picha
Paulo juu ya Kilima Maazi

Julai 22–28.

Matendo ya Mitume 16–21

“Bwana Alituita Kuihubiri Injili”

Unaposoma kuhusu jihudi za Paulo kuhubiri injili, Roho anaweza kukuvuvia kwa mawazo au hisia. Andika misukumo hiyo, na weka mipango ya kuifanyia kazi.

Andika Misukumo Yako

Kati ya maneno ya mwisho ya Bwana kwa Mitume Wake ilikuwa ni amri, “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu: na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi” (Mathayo 28:19–20). Hali Mitume hawakuweza kufika katika mataifa yote , Matendo ya Mitume 16–21 huonyesha kwamba Paulo na wenzake walifanya maendeleo yasiyo kifani katika kulikuza Kanisa. Walifundisha, walibatiza, na kutunuku kipawa cha Roho Mtakatifu. Walifanya miujiza, hata kumfufua mtu kutoka wafu, na kutabiri Ukengeufu Mkuu (Matendo ya Mitume 20:7–12; 20:28–31). Na kazi waliyoanzisha inaendelea kwa Mitume wanaoishi leo, sambamba na wafuasi wanaojitoa kama wewe, ambao husaidia kutimiza wajibu wa Mwokozi katika njia ambazo Paulo hakuweza kufikiria. Pengine unawajua watu ambao hawamjui Baba yao wa Mbinguni au injili Yake. Pengine umehisi kwamba “roho yako ilichochewa sana ndani [yako]” kushiriki na wengine kile unachojua kumhusu Yeye (Matendo ya Mitume 17:16). Kama ukifuata mfano wa Paulo wa unyenyekevu na ujasiri katika kushiriki injili, unaweza kumpata mtu “ambaye moyo wake [umefunguliwa] na Bwana” (Matendo ya Mitume 16:14).

Picha
ikoni ya kujifunza binafsi

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Binafsi

Matendo ya Mitume 16–21

Roho ataniongoza katika jitihada zangu za kushiriki na wengine injili.

Kila mmoja anahitaji injili ya Yesu Kristo, lakini baadhi ya watu wako tayari zaidi kuipokea kuliko wengine. Hii ni sababu moja ambapo tunamuhitaji Roho Mtakatifu wakati tunaposhiriki na wengine injili—ili atuongoze kwa wale ambao wako tayari. Unaposoma Matendo ya Mitume 16–21, gundua nyakati ambapo Roho aliwaongoza Paulo na wenzake. Ni baraka zipi zilikuja kwa sababu walimfuata Roho? Je, ni lini wewe umehisi Roho akikushawishi katika jitihada zako za kushiriki na wengine injili?

Ona pia Alma 7:17–20; Dallin H. Oaks, “Kushiriki Injili ya Urejesho,” Ensign au Liahona, Nov. 2016, 57–60; Hubiri Injili Yangu, 92–93.

Matendo ya Mitume 16–21

Ninaweza kutangaza injili katika hali zozote.

Kuwekwa gerezani kwa kuhubiri injili yaweza kuonekana kama sababu ya kueleweka kuacha kuhubiri. Lakini kwa Paulo na Sila, ilikuwa ni fursa ya kumuongoa mlinzi wa gereza (ona Matendo ya Mitume 16:16–34). Kote katika Matendo ya Mitume 16–21, tafuta mifano mingine ya utayari wa Paulo kutoa ushahidi wake kwa kila mtu. Kwa nini unadhani alikuwa mkakamavu na jasiri? Je, unajifunza nini kutoka katika mfano wa Paulo?

Kuna ujumbe mwingi zaidi kuhusu kushiriki na wengine injili katika sura 16–21. Ukiangalia kwa makini, unaweza kupata baadhi ambao unahusika hasa kwako. Jaribu kusoma sura hizi ukiwa na lengo hili akilini. Je, unapata nini?

Matendo ya Mitume 17:16–34

“Sisi ni uzao wa Mungu.”

Katika Athene, Paulo alikuta watu wa mawazo tofauti na mitazamo ya kidini. Wao daima walitafuta “kusikia elimu mpya,” na kile Paulo alichotaka kuwapa kilikuwa hasa kipya kwao (ona Matendo ya Mitume 17:19–21). Waliabudu miungu mingi, akiwemo mmoja waliyemuita “Mungu asiyejulikana” (Matendo ya Mitume 17:23), lakini waliamini kwamba miungu ilikuwa ni uwezo au nguvu , siyo viumbe, walio hai, na kwa uhakika siyo Baba yetu. Soma kile ambacho Paulo alisema ili kuwasaidia kumjua Mungu, na andika sifa za Mungu unazopata. Inamaanisha nini kwako kuwa “uzao wa Mungu”? (Matendo ya Mitume 17:29). Kwa maoni yako, ni kwa jinsi gani kuwa mwana wa Mungu kunatofautiana na kuwa mmoja wa viumbe Wake tu? Kama ulikuwa umesimama kando ya Paulo wakati alipokuwa akishuhudia, ni nini ungewaambia Wagiriki wa zamani kuhusu Baba yetu wa Mbinguni? Je, unamjua mtu anayeweza kunufaika kutokana na kusikiliza ushuhuda wako?

Picha
Yesu akiwa amembeba mvulana mdogo

Thamani ya Nafsi, na Liz Lemon Swindle

Ona pia Warumi 8:16; 1 Yohana 5:2; “Sisi ni Uzao wa Mungu” (filamu, LDS.org).

Picha
ikoni ya kujifunza kifamilia.

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kifamilia na Jioni ya Familia Nyumbani.

Unaposoma maandiko na familia yako, Roho anaweza kukusaidia kujua kanuni zipi zisisitizwe na kujadiliwa ili kukidhi mahitaji ya familia yako. Hapa kuna baadhi ya mapendekezo:

Matendo ya Mitume 16–21

Ili kuisaidia familia yako kupata taswira ya kile kinachotokea katika sura hizi, inaweza kuwa ya kufurahisha, mnaposoma pamoja, kuwekea alama miji ambayo Paulo alitembelea katika ramani (ona ramani mwisho wa muhtasari huu).

Matendo ya Mitume 17:11; 18:24–28

Ni kwa jinsi gani tunaweza kuwa zaidi kama Watakatifu katika maandiko haya? Ni kwa jinsi gani kujifunza maandiko kila siku hutufanya kuwa “waungwana” zaidi? (Matendo ya Mitume 17:11). Je, tunaweza kufanya nini ili kuwa “hodari katika maandiko”? (Matendo ya Mitume 18:24)

Matendo ya Mitume 19:1–7

Mafundisho haya kutoka kwa Nabii Joseph Smith yanaweza kuisaidia familia yako kujadili Matendo ya Mitume 19:1–7: “Ubatizo kwa maji ni bali nusu tu ya ubatizo, na hauna faida yoyote bila ya nusu ya upande mwingine—ambayo ni, ubatizo kwa Roho Mtakatifu. … ‘Kuzaliwa kwa maji na kwa Roho’ ilimaanisha kuwa kuzamishwa majini kwa ondoleo la dhambi na kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu baada ya hapo. Hiki kilitolewa kwa kuwekewa mikono na mtu mwenye mamlaka aliyopewa na Mungu” (Mafundisho ya Manabii wa Kanisa: Joseph Smith, 95). Ni baraka zipi tumepata kutokana na kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu?

Matendo ya Mitume 7:13–20

Je, ni kitu gani kiliwapa mwongozo wa kiungu watu katika mistari hii kuchoma vitabu vyao vyenye thamani ya “vipande hamsini elfu vya fedha”? (Matendo ya Mitume 7:19). Je, kuna mali za dunia au shughuli ambazo tunahitaji kuviacha ili kupokea baraka za mbinguni?

Matendo ya Mitume 20:32–35

Je, ni wakati gani familia yako ilipata uzoefu wa fundisho la Kristo kwamba “ni heri kutoa kuliko kupokea”? (Matendo ya Mitume 20:35). Je, kuna mtu anayeweza kunufaika kutokana na huduma, muda, au karama ambayo familia yako inaweza kutoa? Kama familia, jadilini baadhi ya mawazo na muweke mipango ya kumtumikia mtu. Tunajisikiaje tunapowatumikia wengine? Kwa nini ni heri kutoa kuliko kupokea?

Kwa mawazo zaidi juu ya kufundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii ndani ya Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Msingi.

Kuboresha Kujifunza Binafsi

Andika misukumo. Wakati misukumo au utambuzi unapokuja, uaandike. Kwa mfano, unaweza kuandika mawazo yako pembeni mwa maandiko yako, kwenye app. ya Maktaba ya Injili, au katika shajara ya kujifunza. “Wakati unapoandika misukumo ya kiroho, unamuonyesha Bwana kwamba unathamini kuongozwa Naye, na atakubariki zaidi kwa ufunuo wa kila mara” (Kufundisha katika Njia ya Mwokozi, 12; ona pia 30).

Picha
ramani ya safari za kimisionari za Paulo

Safari za umisionari za Mtume Paulo.

Chapisha