“Machi 20–26. Mathayo 13; Luka 8; 13: ‘Mwenye Masikio na Asikie’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano Jipya 2023 (2022)
“Machi 20–26. Mathayo 13; Luka 8; 13,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2023
Machi 20–26
Mathayo 13; Luka 8; 13
“Mwenye Masikio na Asikie”
Unaposoma Mathayo 13 na Luka 8; 13, fikiria kuhusu jinsi utakavyojiandaa mwenyewe “kusikia” na kuthamini mafundisho ya Mwokozi katika mafumbo haya. Utafanya nini ili kutumia mafundisho haya maishani mwako?
Andika Misukumo Yako
Baadhi ya mafundisho ya kukumbukwa ya Mwokozi yalikuwa katika mfumo wa hadithi rahisi zilizoitwa mafumbo. Hizi zilikuwa ni zaidi ya hadithi fupi za kuvutia kuhusu vitu au matukio ya kawaida tu. Zilikuwa na kweli za maana sana kuhusu ufalme wa Mungu kwa ajili ya wale waliokuwa wamejiandaa kiroho. Mojawapo ya mafumbo ya kwanza yaliyoandikwa katika Agano Jipya—ni fumbo la mpanzi (ona Mathayo 13:3–23)—hutualika kujichunguza utayari wetu wa kupokea neno la Mungu. “Yeye apokeaye,” Yesu alitangaza, “atapewa, naye atazidishiwa tele” (Tafsiri ya Joseph Smith, Mathayo 13:10 [katika Mathayo 13:12, tanbihi a]). Kwa hiyo tunapojiandaa kujifunza mafumbo ya Mwokozi—au mafundisho Yake yoyote—sehemu nzuri ya kuanzia ni kujichunguza mioyoni mwetu na kuamua kama tunalipa neno la Mungu “udongo mzuri” (Mathayo 13:8) ambamo litakua, kuchanua, kustawi na kuzaa matunda ambayo yatatubariki sisi na familia zetu kwa wingi.
Mawazo kwa Ajili ya Kujifunza Binafsi Maandiko
Mathayo 13:3–23; Luka 8:4–15; 13:6–9
Moyo wangu lazima uuandaliwe ili kupokea neno la Mungu.
Je, ni kwa nini wakati mwingine mioyo yetu hupokea ukweli, hali wakati mwingine tunajaribiwa kuukataa? Kusoma fumbo la mpanzi kunaweza kutoa nafasi nzuri kufikiria kuhusu jinsi unavyopokea ukweli kutoka kwa Bwana. Inaweza kusaidia kwanza kulinganisha mstari wa 3–8 wa Mathayo 13 na tafsiri iliyotolewa katika mstari wa 18–23. Unaweza kufanya nini ili kulima“udongo mzuri” ndani yako? Ni kitu gani kinaweza kuwa baadhi ya “miiba” ambayo hukuzuia kusikia na kufuata kwa dhati neno la Mungu? Je, ni kwa jinsi gani unaweza kuishinda “miiba” hii?
Kujifunza kwako kwa fumbo hili kungeweza pia kushawishi jinsi unavyosoma fumbo katika Luka 13:6–9. Ni “tunda” gani ambalo Bwana anataka kutoka kwetu? Ni kwa jinsi gani tunarutubisha udongo wetu vizuri ili “uzae tunda”?
Ona pia Mosia 2:9; Alma 12:10–11; 32:28–43; Dallin H. Oaks, “Fumbo la Mpanzi,” Liahona, Mei 2015, 32–35.
Mathayo 13:24–35, 44–52; Luka 13:18–21
Mafumbo ya Yesu hunisaidia kuelewa ukuaji na hatima ya Kanisa Lake.
Nabii Joseph Smith alifundisha kwamba mafumbo katika Mathayo 13 huelezea ukuaji na hatima ya Kanisa katika siku za mwisho. Ungeweza kupitia tena maneno ya Nabii katika Teachings of Presidents of the Church: Joseph Smith (2007), 293–303, unapofikiria kile mafumbo yafuatayo yanachokufundisha kuhusu Kanisa la Bwana:
-
Ngano na magugu (13:24–30, 36–43)
-
Mbegu ya haradali (13:31–32)
-
Chachu (13:33)
-
Hazina iliyositirika na lulu ya thamani kuu (13:44–46)
-
Juya (13:47–50)
-
Mwenye nyumba (13:52)
Baada ya kutafakari mafumbo haya, unahisi kushawishika kufanya nini ili kushiriki zaidi katika kazi ya Kanisa la Kristo la siku za mwisho?
Ona pia Mwongozo wa Maandiko, “Ufalme wa Mungu au Ufalme wa Mbinguni,” “Fumbo,” scriptures.ChurchofJesusChrist.org.
Wema lazima wakue miongoni mwa waovu mpaka mwisho wa ulimwengu.
Njia moja ya kuchambua fumbo hili ni kuchora picha yake na kuiwekea alama za utambulisho kwa ufafanuzi katika Mathayo 13:36–43 na Mafundisho na Maagano 86:1–7. Gugu mwitu ni “jani lenye sumu, ambalo, mpaka litoe shuke, linafanana kwa muonekano na ngano” (Kamusi ya Biblia, “Magugu mwitu”). Ni kweli gani katika fumbo hili zinakushawishi kubaki mwaminifu licha ya uovu ulimwenguni?
Ni kwa njia zipi “wanawake shupavu” walimhudumia Mwokozi?
“Wafuasi wa kike walisafiri na Yesu na wale Kumi na Wawili, wakijifunza kutoka kwa [Yesu] kiroho na kumtumikia kimwili. … Katika nyongeza ya kupokea utumishi wa Yesu—habari njema ya injili Yake na baraka za nguvu Yake ya uponyaji—wanawake hawa walimtumikia Yeye, wakitoa vitu vyao na bidii zao” (Mabinti katika Ufalme Wangu [2017],4). Wanawake waliomfuata Mwokozi pia walitoa shuhuda zenye nguvu juu Yake (ona Linda K. Burton, “Wanawake Shupavu,” Liahona, Mei 2017, 12–15).
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko kama Familia na Jioni ya Nyumbani
-
Mathayo 13.Wanafamilia wako wanaposoma mafumbo ya Mwokozi, wanaweza kufurahia kufikiria mafumbo yao wenyewe ambayo hufundisha kweli zinazofanana kuhusu ufalme wa mbinguni (Kanisa), kwa kutumia vitu au hali ambazo zinafahamika kwao.
-
Mathayo 13:3–23; Luka 8:4–15.Baada ya kusoma fumbo la mpanzi pamoja, familia yako ingeweza kujadili maswali kama vile: “Ni nini kinaweza kuufanya “udongo” wetu (mioyo yetu) kuwa “mgumu” au “kulisonga” neno? Ni kwa jinsi gani tunaweza kuhakikisha udongo wetu ni mzuri na unazalisha?
Kama una watoto wadogo katika familia yako, itakuwa yenye kufurahisha kuwaalika wanafamilia kuigiza njia tofauti za kuiandaa mioyo yetu kusikia neno la Mungu wakati wanafamilia wengine wakibashiri kile wanachofanya.
-
Mathayo 13:13–16.Ni kwa jinsi gani unaweza kuwasaidia wanafamilia kuelewa umuhimu wa kupokea kwa hiari neno la Kristo? Ili kuonyesha “masikio [ambayo] hayasikii vyema,” unaweza kufunga masikio ya mwanafamilia wakati ukisoma kimya kimya Mathayo 13:13–16. Ni kwa kiasi gani mwanafamilia huyo ameelewa kutoka katika mistari hii? Ni njia zipi ambazo kwazo tunafungua macho, masikio, na mioyo yetu kwa ajili ya neno la Mungu?
-
Mathayo 13:44–46.Watu hawa wawili katika mafumbo haya wana mambo gani yanayofanana? Je, kuna mambo ya ziada tunayopaswa kuwa tunafanya kama watu binafsi na kama familia ili kuweka ufalme wa Mungu kwanza katika maisha yetu?
-
Luka 13:11–17.Je, wanafamilia wamepata uzoefu ambao uliwasababisha kuhisi kwamba hawangeweza “kujiinua [wenyewe]”? Je, tunamjua mtu yeyote ambaye anahisi hivi? Tunawezaje kumsaidia? Ni jinsi gani Mwokozi “anatufungua” kutokana na udhaifu wetu?
Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi.
Wimbo uliopendekezwa“We Are Sowing,” Nyimbo za Kanisa, na. 216.