“Februari 27–Machi 5. Mathayo 8; Marko 2–4; Luka 7: ‘Imani Yako Imekuponya’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano Jipya 2023 (2022)
“Februari 27–Machi 5. Mathayo 8; Marko 2–4; Luka 7,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano Jipya 2023
Februari 27–Machi 5
Mathayo 8; Marko 2–4; Luka 7
“Imani Yako Imekuponya”
Kuwa makini usiharakishe kujifunza maandiko kwako. Tenga muda wa kutafakari kwa maombi, hata ikiwa huna muda wa kusoma kila mstari. Nyakati kama hizi za kutafakari mara nyingi hutuongoza kwenye ufunuo binafsi.
Andika Misukumo Yako
Moja ya jumbe zilizo wazi katika Agano Jipya ni kwamba Yesu Kristo ni mponyaji. Hadithi za Mwokozi akiponya wagonjwa na walioteseka ni nyingi—kutoka mwanamke mwenye homa hadi mwana wa mjane ambaye alikuwa amefariki. Kwa nini kusisitiza juu uponyaji wa kimwili? Je, ni ujumbe gani unaweza kuwa pale kwa ajili yetu katika miujiza hii? Hakika ujumbe mmoja wa wazi ni kwamba Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu, mwenye nguvu juu ya mambo yote, ikijumuisha maumivu yetu ya kimwili na mapungufu yetu. Lakini maana nyingine inapatikana katika maneno Yake kwa waandishi wenye kushuku: “Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi” (Marko 2:10). Kwa hiyo unaposoma kuhusu mtu kipofu au mkoma kuponywa, unaweza kufikiria uponyaji—wote wa kiroho na kimwili—unaoweza kupokea kutoka kwa Mwokozi na kumsikia akikuambia, “Imani Yako Imekuponya” (Marko 7:50).
Mawazo kwa Ajili ya Kujifunza Binafsi Maandiko
Mwokozi anaweza kuponya udhaifu na magonjwa.
Sura hizi chache zimeandikwa mifano mingi ya uponyaji wa kimiujiza uliofanywa na Mwokozi. Unapojifunza uponyaji huu, tafuta ujumbe unaoweza kuwa kwa ajili yako. Unaweza kujiuliza mwenyewe: Je, mistari hii hufundisha nini kuhusu imani katika Yesu Kristo? Je, hadithi hii hufundisha nini kumhusu Mwokozi? Je, Mungu anataka nijifunze nini kutokana na muujiza huu? Hapa kuna baadhi ya mifano, lakini iko mingine mingi zaidi:
-
Mwenye ukoma (Mathayo 8:1–4)
-
Mtumishi wa akida (Mathayo 8:5–13; Luka 7:1–10)
-
Mama mkwe wa Petro (Mathayo 8:14–15)
-
Mtu mwenye kupooza (Marko 2:1–12)
-
Mtu mwenye mkono uliopooza (Marko 3:1–5)
-
Mwana wa mjane wa Naini (Luka 7:11–16)
Ona pia David A. Bednar, “Kuyakubali Mapenzi na Wakati wa Bwana,” Liahona, Agos. 2016, 17–23; Neil L. Andersen, “Waliojeruhiwa,” Liahona, Nov. 2018, 83–86.
Yesu Kristo hakuja kuwahukumu wenye dhambi bali kuwaponya.
Unaposoma katika mistari hii kuhusu miingiliano ya Yesu na waandishi na Mafarisayo, ungeweza kufikiria ikiwa unajiona mwenyewe katika maelezo haya. Kwa mfano, mawazo na matendo yako yamekuwa kama yale ya Simoni Mfarisayo? Ni kwa jinsi gani unaweza kuelezea tofauti baina ya Yesu alivyowaona wenye dhambi na jinsi Mafarisayo kama Simoni walivyowaona? Fikiria jinsi ambavyo wale wanaolemewa na dhambi wanaweza kuhisi wanapokuwa pamoja na Mwokozi? Je! wanahisi vipi wanapokuwa nawe?
Ungeweza pia kutafakari jinsi wewe ulivyo kama yule mwanamke aliyeelezewa katika Luka 7:36–50. Je, ni lini umeuona upole na huruma ambayo Mwokozi alimuonyesha? Je, unajifunza nini kutokana na mfano wake wa imani, upendo na unyenyekevu?
Ona pia Yohana 3:17; Luka 9:51–56; Dieter F. Uchtdorf, “Kipawa cha Neema,” Liahona, Mei 2015, 107–10.
Mathayo 8:18–22; Marko 3:31–35
Kuwa wafuasi wa Yesu Kristo inamaanisha kwamba ninamweka Yeye kwanza katika maisha yangu.
Katika mistari hii, Yesu alifundisha kwamba kuwa wafuasi Wake kunatuhitaji sisi kumweka Yeye kwanza katika maisha yetu, hata kama hiyo mara nyingine humaanisha tunapaswa kuacha mambo mengine ambayo tunayathamini. Unapojifunza vifungu hivi, tafakari juu ya ufuasi wako wewe mwenyewe. Je, kwa nini ni lazima wafuasi wawe tayari kumweka Mwokozi kwanza? Je, ungehitajika kuacha nini ili kumweka Yesu kwanza? (Ona pia Luka 9:57–62.)
Mathayo 8:23–27; Marko 4:35–41
Yesu Kristo ana uwezo wa kuleta amani katikati ya dhoruba za maisha.
Je, umewahi kuhisi jinsi wanafunzi wa Yesu walivyohisi kwenye dhoruba baharini—kuangalia mawimbi ya maji yakikijaza chombo na kuuliza, “Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia?”
Katika Marko 4:35–41, unapata maswali manne. Orodhesha kila moja, na tafakari linakufundisha nini kuhusu kukabiliana na changamoto za maisha ukiwa na imani katika Yesu Kristo. Je, ni kwa jinsi gani Mwokozi huleta amani katika dhoruba za maisha yako?
Ona pia Lisa L. Harkness, “Amani, Tulia,” Liahona, Nov. 2020, 80–82.
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko kama Familia na Jioni ya Nyumbani
-
Mathayo 8; Marko 2–4; Luka 7.Fikiria kutengeneza orodha ya miujiza aliyoelezewa katika sura hizi. Jaribu kutafuta picha au michoro ya baadhi ya miujiza hiyo. (ona Kitabu cha Sanaa ya Injili au ChurchofJesusChrist.org). Kila mwanafamilia anaweza kutumia picha ili kuelezea kuhusu mojawapo ya miujiza na kushiriki kile walichojifunza kutokana na miujiza hiyo. Unaweza kuelezea baadhi ya mifano ya miujiza ambayo umeiona au kusoma kuhusu miujiza hiyo katika siku zetu.
Ona pia video “Widow of Nain” na “Calming the Tempest” (ChurchofJesusChrist.org).
2:222:17 -
Mathayo 8:5–13; Luka 7:1–10.Je, ni nini katika imani ya akida ambacho kilimvutia Yesu? Je, tunawezaje kuonyesha imani kama hiyo katika Yesu Kristo?
-
Marko 2:1–12. “Sura ya 23: Mtu Ambaye Hakuweza Kutembea” (katika Hadithi za Agano Jipya, 57–58, au video inayofanana nayo kwenye ChurchofJesusChrist.org) ingeweza kusaidia familia yako kujadili Marko 2:1–12. (Ona pia video “Jesus Forgives Sins na Heals a Man Stricken with Palsy” kwenye ChurchofJesusChrist.org.) Ni kwa jinsi gani tunaweza kuwa kama marafiki wa mtu ambaye hakuweza kutembea? Je, ni nani amekuwa aina ya rafiki kama huyu kwetu?
NaN:NaN2:57 -
Marko 4:35–41.Maelezo haya yangeweza kuwasaidia wanafamilia wanapohisi kuogopa? Pengine wangeweza kusoma mstari wa 39 na kushiriki uzoefu wao wakati Mwokozi alipowasaidia kuhisi amani.
Watoto wangeweza kufurahia kujifanya wako kwenye mashua katika bahari iliyo na dhoruba wakati mtu anasoma Marko 4:35–38. Kisha, wakati mtu anaposoma mstari wa 39, wangeweza kujifanya wako katika mashua katika bahari iliyotulia. Mnaweza pia kuimba pamoja wimbo kuhusu kupata amani katika Mwokozi kama vile “Master, the Tempest Is Raging” (Nyimbo za Kanisa, na. 105). Ni virai gani katika wimbo huu vimekufundisha kuhusu amani anayotoa Yesu?
Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi.
Wimbo uliopendekezwa “Master, the Tempest Is Raging,” Nyimbo za Kanisa, na. 105.