Kujeruhiwa
Katika kalibu ya majaribu ya duniani, kwa subira songa mbele, na nguvu ya Mwokozi ya uponyaji itakuletea nuru, uelewa, amani, na tumaini.
Mnamo Machi 22, 2016 muda mfupi kabla ya saa mbili za asubuhi, mabomu mawili ya kigaidi yalilipuka katika Uwanja wa Ndege wa Brussels. Mzee Richard Norby, Mzee Mason Wells, na Mzee Joseph Empey walikuwa wamempeleka Dada Fanny Clain kwenye uwanja wa ndege kwa ajili ya safari yake ya kuelekea katika misheni yake kule Cleveland, Ohio. Watu thelathini na wawili walipoteza maisha yao, na wamisionari wote walijeruhiwa.
Aliyejeruhiwa vibaya zaidi alikuwa Mzee Richard Norby, miaka 66, akihudumu na mkewe, Dada Pam Norby.
Mzee Norby aliakisi kuhusu tukio hilo:
“Mara moja, nilifahamu kilichokuwa kimetendeka.
“Nilijaribu kukimbilia usalama, lakini punde tu nikaanguka chini. … Niliweza kuona kwamba mguu wangu wa kushoto ulikuwa umejeruhiwa vibaya sana. [niligundua] masizi, meusi, mfano wa utando wa buibui, yakining’inia kutoka kwenye mikono yote miwili. Niliyavuta taratibu, lakini nikagundua hayakuwa masizi bali ngozi yangu ambayo ilikuwa imeungua. Shati langu jeupe lilikuwa likigeuka kuwa rangi nyekundu kutokana na jeraha mgongoni mwangu.
“Fahamu ya kile kilichokuwa kimetokea ilipokuwa ikijaa akilini mwangu, [nilipata] wazo hili lenye nguvu sana: … Mwokozi alifahamu mahali ambapo nilikuwa, kile kilichokuwa kimetokea, na [kile] nilichokuwa nikipitia wakati huo.”1
Kulikuwa na wakati mgumu katika siku za usoni kwa Richard Norby na mkewe, Pam. Alikuwa katika hali ya kutojitambua, ikifuatiwa na upasuaji, maambukizo, na wasi wasi mkubwa.
Richard Norby aliishi, lakini maisha yake hayangekuwa jinsi yalivyokuwa hapo mwanzo. Miaka miwili na nusu baadaye, majeraha yake yangali yanapona; gango linafunika sehemu ya mguu wake aliyoipoteza; kila hatua ni tofauti kuliko wakati kabla ya tukio lile katika Uwanja wa Ndege wa Brussels.
Kwa nini hili liwapate Richard na Pam Norby?2 Walikuwa wametii maagano yao, walikuwa wamehudumu misheni awali kule Ivory Coast, na kulea familia ya kupendeza. Ingeeleweka kama mtu angesema, “Siyo haki! Kamwe si haki! Walikuwa wakitoa maisha yao kwa ajili ya injili ya Yesu Kristo; hili lingewezaje kufanyika?”
Haya ni maisha ya muda
Ingawaje maelezo ya kina yatatofautiana, mikasa, majaribu yasiyotarajiwa, ya kimwili na ya kiroho, huja kwa kila mmoja wetu kwa sababu, haya ni maisha ya muda.
Nilipofikiria asubuhi ya leo kuhusu wasemaji katika kikao hiki tu cha mkutano, iliniingia mawazoni kwamba wawili wamepoteza watoto na watatu wamepoteza wajukuu ambao walirudi kighafla nyumbani kwao mbinguni. Hakuna aliyenusurika ugonjwa na huzuni, na kama ilivyozungumzwa, wiki hii malaika wa hapa duniani ambaye wote tunampenda, Dada Barbara Ballard, alitembea polepole kuvuka pazia. Rais Ballard, hatutasahau kamwe ushuhuda wako asubuhi hii.
Tunatafuta furaha. Tunatamani amani. Tunatumainia upendo. Na Bwana anatunyunyizia baraka tele za ajabu. Lakini zikiwa zimechanganyika pamoja na ile shangwe na furaha, kitu kimoja ni hakika: kutakuwa na nyakati, saa, siku, wakati mwingine miaka ambapo nafsi yako itajeruhiwa.
Maandiko yanafundisha kwamba tutaonja machungu na matamu3 na kwamba kutakuwa na “upinzani katika vitu vyote.”4 Yesu alisema, “[Baba yenu] huwaangazia jua lake waovu na wema, na huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.”5
Majeraha ya nafsi sio ya kipekee kwa matajiri au maskini, kwa utamaduni mmoja, taifa moja, au kizazi kimoja. Yanawajia wote na ni sehemu ya mafunzo tunayopata kutokana na maisha haya ya muda.
Wema Hawajakingwa
Ujumbe wangu leo hii ni hasa kwa wale wanaotii amri za Mungu, wanaoheshimu ahadi zao kwa Mungu, na, kama kina Norby na wanaume wengine wengi, wanawake, na watoto katika mkusanyiko huu ulimwengu kote, wanakabiliwa na majaribu na changamoto ambazo hazitarajiwi na ni za uchungu.
Majeraha yetu yanaweza kutokana na majanga ya kiasili au ajali isiyoepukika. Yanaweza kutokana na mume au mke asiyekuwa mwaminifu, yakipindua maisha juu chini kwa mwenza muadilifu na watoto. Majeraha yanaweza kuja kutokana na giza na majonzi ya huzuni, kutokana na ugonjwa usiotarajiwa, kutokana na mateso au kufariki kusikotarajiwa kwa mtu tunayempenda, huzuni kutokana na mwanafamilia kuasi imani yake, kutokana na upweke wakati mazingira hayaleti mwenza wa milele, au kutokana na mamia ya majaribu mengine ya kuvunja moyo, machungu na ya “[kusikitisha] ambayo macho hayawezi kuona.”6
Kila mmoja wetu anaelewa kwamba matatizo ni sehemu ya maisha, lakini yanapotujia kibinafsi, yanaweza kutushtusha. Bila kujulishwa kabla, ni lazima tujitayarishe. Mtume Petro alisema, “Msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho.”7 Pamoja na rangi ang’avu za furaha na shangwe, nyuzi za majaribu na mikasa zenye rangi iliyokoza zimefumwa kwa kina katika kitambaa cha mpango wa Baba yetu. Shida hizi, ingawaje ni ngumu, mara nyingi huwa mwalimu wetu mkuu.8
Kwa kuelezea hadithi ya kimiujiza ya vijana 2060 wa jeshi la Helamani, tunapenda andiko hili: “Kulingana na wema wa Mungu, na kwa mshangao wetu, na pia shangwe ya jeshi lote, hakukuwa na nafsi moja miongoni mwao ambaye aliangamia.”
Lakini sentensi inaendelea: “Na wala hakukuwa na mmoja miongoni mwao ambaye hakupata majeraha mengi.”9 Kila mmoja wa wale 2,060 alipata majeraha mengi, na kila mmoja wetu atajeruhiwa katika vita vya maisha, iwe kimwili, kiroho, au vyote viwili.
Yesu Kristo ni Msamaria Wetu Mwema.
Usikate tamaa—majeraha ya nafsi yako yawe makali kiasi gani, bila kujali chanzo chake, vyovyote au wakati wowote yanapotokea, na hata hivyo muda mfupi au muda mrefu yanapoendelea kuwepo, haujakusudiwa kuangamia kiroho. Unatarajiwa kunusurika kiroho na kushamiri katika imani na tumaini lako katika Mungu.
Mungu hakuumba roho zetu ziwe zenye kutomtegemea Yeye. Bwana na Mwokozi wetu, Yesu Kristo, kupitia zawadi yake ya Upatanisho isiyo na kifani, siyo tu anatuokoa kutokana na kifo na kutupatia, kupitia toba, msamaha wa dhambi zetu, lakini pia yuko tayari kutuokoa kutoka kwenye huzuni na uchungu wa nafsi zetu zilizo jeruhiwa.10
Mwokozi ni Msamaria wetu Mwema,11 aliyetumwa “kuwaganga waliovunjika moyo.”12 Yeye anatukaribia wakati wengine wanapopita kando yetu. Akiwa na huruma Anapaka vidonda vyetu mafuta ya uponyaji na kuviganga. Anatubeba. Anatujali. Anatuita, “Njooni kwangu … na nitawaponya.”13
“Na [Yesu] … [atateseka] maumivu na masumbuko na majaribio ya kila aina; … kwamba … yeye [abebe] maumivu na magonjwa ya watu wake … [Akijichukulia juu Yake] unyonge wetu, [akiwa] amejawa na rehema”14
Njooni, enyi wenye huzuni, popote mlipo;
Njooni kwenye kiti cha rehema, na mpige magoti kwa unyenyekevu.
Hapa leteni mioyo yenu iliyojeruhiwa; hapa semeni maumivu yenu.
Dunia haina huzuni isiyoweza kuponywa na mbingu.15
Wakati wa mateso makali, Bwana alimwmbia Nabii Joseph, “Mambo haya yote yatakupa wewe uzoefu, na yatakuwa kwa faida yako.”16 Ni kwa jinsi gani majeraha yaweza kuwa kwa faida yetu? Katika kalibu ya majaribu ya duniani, songa mbele kwa subira na nguvu ya Mwokozi ya uponyaji itakuletea nuru, uelewa, amani, na tumaini.17
Usikate Tamaa Kamwe
Sali kwa moyo wako wote. Imarisha imani yako katika Yesu Kristo, katika uhalisia Wake, katika neema Yake. Shikilia maneno Yake: “Neema yangu yakutosha: maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu.”17
Kumbuka, toba ni tiba ya kiroho yenye nguvu.19 Kuweni waaminifu kwa amri na wastahiki wa Msaidizi, mkikumbuka kwamba Mwokozi aliahidi, “Sitawaacha ninyi yatima. Naja kwenu.”20
Amani ya hekaluni ni mafuta yenye kutuliza nafsi iliyojeruhiwa. Rudi katika nyumba ya Bwana na moyo wako uliojeruhiwa pamoja na majina ya familia yako mara nyingi iwezekanavyo. Hekalu huonyesha muda wetu mfupi katika maisha haya ya muda kwenye skrini kubwa ya milele.21
Tazama nyuma, ukikumbuka kwamba ulithibitisha ustahili wako katika hali yako ya kabla ya kuzaliwa. Wewe ni mtoto hodari wa Mungu, na kwa usaidizi Wake, unaweza kuwa mshindi katika vita vya duniani hii iliyoanguka. Umefanya hivyo kabla, na unaweza kufanya hivyo tena.
Tazama mbele. Shida na huzuni zako ni za kweli kabisa, lakini hazitadumu milele.22 Usiku wako wa kiza utapita, kwa sababu “Mwana … [alifufuka] na uponyaji kwenye mbawa zake.”23
Kina Norby waliniambia, “Masikitiko huja kwa wakati fulani lakini hayaruhusiwi kudumu.”24 Mtume Paulo alisema, “Twadhikika … bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa; twaudhiwa, bali hatuachwi; twatupwa chini, bali hatuangamizwi.”25 Waweza kuwa umechoka, lakini kamwe usikate tamaa.26
Hata na majeraha yako yenye uchungu, kisilika utawaendea wengine, ukiamini katika ahadi ya Mwokozi: “Mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona.”27 Waliojeruhiwa wanaouguza majeraha ya wengine ni malaika wa Mungu duniani.
Baada ya muda mfupi, tutamsikiliza nabii wetu mpendwa, Rais Russell M. Nelson, mtu aliye na imani thabiti katika Yesu Kristo, mtu mwenye tumaini na amani, anayependwa na Mungu lakini hajakingwa kutokana na majeraha ya nafsi.
Mwaka 1995 binti yake Emily, akiwa mjamzito, alibainika kuwa na saratani. Kulikuwa na siku za matumaini na furaha wakati mtoto wake mwenye afya alipozaliwa. Lakini saratani ilirudi, na Emily wao mpendwa angeyaaga maisha haya wiki mbili tu baada ya miaka yake 37 ya kuzaliwa, akimwacha mumewe mpendwa na watoto watano wadogo.
Katika mkutano mkuu, muda mfupi baada ya kifo chake, Rais Nelson alikiri: “Machozi yangu ya huzuni yametiririka pamoja na matamanio yangu kwamba ningeweza kufanya zaidi kwa ajili ya binti yetu. … Kama ningelikuwa na uwezo wa kufufua, ningelishawishika kumrudishia uhai. … [Lakini] Yesu Kristo anazo funguo hizo na atazitumia kwa ajili ya Emily … na kwa watu wote kwa wakati Wake Bwana.”28
Mwezi uliopita, akiwatembelea Watakatifu kule Puerto Rico na akikumbuka Kimbunga haribifu cha mwaka jana, Rais Nelson alizungumza kwa upendo na huruma:
“[Hii] ni sehemu ya maisha. Ni sababu ya sisi kuwa hapa. Tuko hapa kuwa na mwili na kujaribiwa na kupimwa. Baadhi ya majaribu hayo ni ya kimwili; baadhi ni ya kiroho, na majaribu yenu hapa yamekuwa yote ya kimwili na kiroho.”29
“Hamjakata tamaa. Tunaona fahari [kubwa] juu yenu. Ninyi Watakatifu waaminifu mmepoteza vingi, lakini katika yote hayo, mmeweka imani yenu katika Bwana Yesu Kristo.”30
“Kwa kutii amri za Mungu, tunaweza kupata shangwe hata katikati ya hali zetu mbaya mno.”31
Machozi Yote Yatafutwa
Kaka zangu na dada zangu, ni ahadi yangu kwenu kwamba kuongeza imani yenu katika Bwana Yesu Kristo kutawaletea ongezeko la nguvu na tumaini kubwa. Kwenu, wenye haki, mponyaji wa nafsi zetu, katika wakati Wake na kwa njia Yake, ataponya majeraha yenu yote.32 Hakuna udhalimu, mateso, majaribu, huzuni, kuvunjika moyo, masumbuko, jeraha—yawe makubwa, yawe mapana, yawe machungu—yatakayotengwa kando na faraja, amani, na tumaini la kudumu la Yeye ambaye mikono Yake iliyonyooka na ambaye mikono Yake iliyo na makovu itatukaribisha tena katika uwepo Wake. Siku hiyo, Mtume Yohana anashuhudia, wenye haki “[wanaotoka] katika dhiki ile iliyo kuu”33 watasimama “wakiwa wamevikwa mavazi meupe … mbele ya kiti cha enzi cha Mungu.” Mwana-kondoo “atatanda hema miongoni [mwetu] … na Mungu atayafuta machozi yote katika macho [yenu].”34 Siku hii itakuja. Ninashuhudia hivyo katika jina la Yesu Kristo, amina.