2010–2019
Jaribu, Jaribu, Jaribu
Oktoba 2018


Jaribu, Jaribu, Jaribu

Mwokozi anaweka jina Lake katika mioyo yenu. Na mnahisi upendo msafi wa Kristo kwa wengine na kwenu.

Wapendwa akina kaka na dada zangu, nina furaha kwa fursa ya kuongea nanyi. Mkutano huu umekuwa wa kuinua na kuimarisha kwangu mimi. Muziki ulioimbwa na maneno yaliyonenwa yamebebwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu. Naomba kwamba ninachosema kikawafikie kupitia Roho yule yule.

Miaka mingi iliyopita, nilikuwa mshauri wa kwanza wa rais wa wilaya huko mashariki mwa Marekani. Zaidi ya mara moja, tukiwa tunaendesha gari kuelekea kwenye matawi yetu madogo, aliniambia, “Hal unapokutana na yeyote, watendee kana kwamba wako katika tatizo kubwa, na utakuwa sahihi karibu kila wakati.” Siyo tu alikuwa sahihi, bali nilijifunza kwa miaka mingi kwamba alikuwa chini sana katika makadirio yake. Leo, nataka kuwatia moyo katika matatizo mnayokumbana nayo.

Maisha yetu ya duniani yamepangwa na Mungu mpendwa kuwa jaribio na kuwa chanzo cha kukua kwa kila mmoja wetu. Unambuka maneno ya Mungu juu ya watoto Wake wakati wa Uumbaji wa ulimwengu: “Nasi tutawajaribu kwa njia hii, ili kuona kama wao watafanya mambo yote yale ambayo Bwana Mungu wao atawaamuru.”1

Tangu mwanzo, majaribio hayajawa rahisi. Tunakumbana na majaribu yatokanayo na kuwa na miili ya kufa. Sisi sote tunaishi katika ulimwengu ambao vita vya Ibilisi dhidi ya ukweli na dhidi ya furaha yetu inazidi kuwa kali zaidi. Ulimwengu na maisha yako yanaweza kuonekana kwako kuwa katika dhoruba iongezekayo.

Uhakikisho wangu ni huu: Mungu mpendwa aliyeruhusu haya majaribu kwako pia ameweka njia ya uhakika ya kuyapita. Baba wa Mbinguni aliupenda sana ulimwengu hata Akamtuma Mwana Wake wa Pekee kuja kutusaidia.2 Mwana Wake, Yesu Kristo, alitoa maisha Yake kwa ajili Yetu. Yesu Kristo alibeba kule Gethsemane na pale msalabani uzito wote wa dhambi zetu. Alipata huzuni zote, maumivu, na madhara ya dhambi zetu ili aweze kutufariji na kutuimarisha kupitia kila jaribu katika maisha.3

Unakumbuka kwamba Bwana aliwaambia watumishi Wake:

“Baba na Mimi tu wamoja. Mimi ni ndani ya Baba na Baba yu ndani yangu; na kadiri ninyi mlivyonipokea Mimi, ninyi mu ndani yangu nami ni ndani yenu,

“Kwa hivyo, Mimi nipo katikati yenu, na mimi ni mchungaji mwema, na jiwe la Israeli. Yule ajengaye juu ya mwamba huu hataanguka kamwe.”4

Nabii wetu, Rais Russell M. Nelson, naye pia ametupa uhakikisho kama huo. Zaidi, alielezea jinsi tunayoweza kujenga juu ya mwamba huo na kuliweka jina la Bwana juu ya mioyo yetu ili kutuongoza katika majaribu yetu.

Alisema: “Wewe ambaye huenda umevunjika moyo kwa muda mfupi, kumbuka, maisha hayakufanywa kuwa rahisi. Majaribu yanapaswa kubebwa na huzuni huvumiliwa njiani. Wakati unakumbuka kuwa ‘kwa Mungu hakuna kitu kisichowezekana’ (Luka 1:7), jua kwamba Yeye ni Baba yako. Wewe ni mwana au binti uliyeumbwa kwa mfano Wake, ukipewa haki kupitia ustahili wako kupata ufunuo wa kukusaidia kwenye jitihada zako za haki. Unaweza kujichukulia juu yako jina takatifu la Bwana. Unaweza kustahili kuongea katika jina takatifu la Mungu (ona M&M 1:20).”5

Maneno ya Rais Nelson yanatukumbusha juu ya ahadi zinazopatikana katika sala ya sakramenti, ahadi ambayo Baba wa Mbinguni anaitimiza tunapofanya kile tunachoahidi.

Sikiliza maneno hayo: “Ee, Mungu, Baba wa Milele, tunakuomba katika jina la Mwanao, Yesu Kristo, ubariki na utakase mkate huu kwa roho za wale wote watakaoula, ili waweze kuula kwa ukumbusho wa mwili wa Mwanao, na wakushuhudie, Ee Mungu, Baba wa Milele, kwamba wako radhi kujichukulia juu yao jina la Mwanao, na daima kumkumbuka, na kushika amri zake ambazo amewapa, ili daima Roho wake apate kuwa pamoja nao. Amina.”6

Kila wakati tunaposema neno amina wakati hiyo sala inapotolewa kwa niaba yetu, tunaahidi kwamba kwa kula mkate, tuko radhi kujichukulia juu yetu jina takatifu la Yesu Kristo, daima kumkumbuka Yeye, na kushika amri Zake. Kwa upande mwingine, tunaahidiwa kwamba tutakuwa na Roho Wake pamoja nasi. Kwa sababu ya ahadi hizi, Mwokozi ni mwamba ambao juu yake twaweza kusimama salama na bila woga katika kila dhoruba tunayo kumbana nayo.

Nilipotafakari maneno ya agano na baraka zitokanazo na ahadi, nimejiuliza ina maana gani kuwa radhi kujichukulia juu yetu jina la Yesu Kristo.

Rais Dallin H. Oaks anaelezea: “ni muhimu kwamba tunapo kula sakramenti hatushuhudii kwamba tunajichukulia juu yetu jina la Yesu Kristo. Tunashuhudia kwamba tuko radhi kufanya hivyo. (Ona M&M 20:77.) Ukweli kwamba tunashuhudia tu utayari wetu huonyesha kuwa kitu kingine lazima kitokee kabla ya kuchukua jina hilo takatifu juu yetu katika maana iliyo muhimu sana.”7

Sentensi kwamba tupo “radhi kujichukulia juu [yetu]” jina Lake kunatuambia kwamba wakati kwanza tulijichukulia jina Lake tulipo batizwa, kujichukulia jina Lake hakuishii wakati wa ubatizo. Lazima tufanye kazi wakati wote ili kujichukulia jina Lake katika maisha yetu yote, ikijumuisha wakati ule tunapofanya upya maagano katika meza ya sakramenti na kufanya maagano katika mahekalu matakatifu ya Bwana.

Hivyo maswali mawili muhimu kwa kila mmoja wetu yanakuwa “Nini yanipasa nifanye kujichukulia jina Lake juu yangu?” na “Je, nitajuaje ni wakati gani nasonga mbele?”

Kauli ya Rais Nelson inapendekeza jibu moja linalosaidia. Alisema kwamba tunaweza kujichukulia jina la Mwokozi juu yetu na kwamba tunaweza kuongea kwa niaba Yake. Tunapoongea kwa niaba Yake, tunamtumikia Yeye. “Kwani ni vipi mtu atamjua yule bwana ambaye hajamtumikia, na aliye mgeni kwake, na yuko mbali katika mawazo na nia za moyo wake?”8

Kuongea kwa niaba yake kunahitaji sala ya imani. Inahitaji sala ya dhati kwa Baba wa Mbinguni kujifunza maneno tunayoweza kuongea ili kumsaidia Mwokozi katika kazi Yake. Lazima tustahili ahadi yake: “Iwe kwa sauti yangu mwenyewe au kwa sauti ya watumishi wangu, yote ni sawa.”9

Tena, inachukua zaidi ya kuongea kwa ajili Yake ili kujichukulia jina Lake juu yetu. Kuna hisia katika mioyo yetu lazima tuwe nazo ili kustahili kama watumishi Wake.

Nabii Mormoni alielezea hisia ambazo zinatustahilisha na kutuwezesha kujichukulia jina Lake juu yetu. Hisia hizi ni pamoja na imani, tumaini, na upendo msafi wa Kristo.

Mormoni alielezea:

“Kwani ninaona kwamba mna imani katika Kristo kwa sababu ya uvumilivu wenu; kwani kama hamna imani ndani yake hamfai kuhesabiwa miongoni mwa watu wa kanisa lake.

“Na tena, ndugu zangu wapendwa, ninataka kuwazungumzia kuhusu tumaini. Inawezekanaje kwamba mtafikia imani, isipokuwa muwe na tumaini?

“Na ni kitu gani mtakachotumainia? Tazama nawaambia kwamba mtakuwa na tumaini kupitia upatanisho wa Kristo na uwezo wa kufufuka kwake, kuinuliwa kwa maisha ya milele, na hii kwa sababu ya imani yenu kwake kulingana na ile ahadi.

“Kwa hivyo, ikiwa mtu ana imani lazima ahitaji kuwa na tumaini; kwani bila imani hakuwezi kuwepo na tumaini lolote.

“Na tena, tazama ninawaambia kwamba hawezi kuwa na imani na tumaini, isipokuwa awe mnyenyekevu, na mpole katika moyo.

“Ikiwa hivyo, imani na tumaini lake ni bure, kwani hakuna yeyote anayekubaliwa mbele ya Mungu, isipokuwa yule aliye myenyekevu na mpole katika moyo; na mtu akiwa myenyekevu na mpole katika moyo, na kukiri kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwamba Yesu ni Kristo, lazima awe na hisani; kwani kama hana hisani yeye si kitu; kwa hivyo lazima awe na hisani.

Baada ya kuelezea hisani, Mormoni anaendelea kwa kusema:

“Lakini hisani ni upendo msafi wa Kristo, na inavumilia milele; na yeyote atakayepatikana nayo katika siku ya mwisho, itakuwa vyema kwake.

“Kwa hivyo, ndugu zangu wapendwa, ombeni kwa Baba kwa nguvu zote za moyo, kwamba mjazwe na upendo huu, ambao ametoa kwa wote ambao ni wafuasi wa kweli wa Mwana wake, Yesu Kristo; ili muwe wana wa Mungu; kwamba wakati atakapoonekana tutakuwa kama yeye, kwani tutamwona vile alivyo; ili tuwe na tumaini hili; ili tutakaswe hata vile alivyo mtakatifu. Amina.”10

Ushuhuda wangu ni kwamba Mwokozi anaweka jina Lake katika mioyo yenu. Kwa mlio wengi, imani yenu katika Yeye inaongezeka. Mnahisi tumaini zaidi na mtazamo chanya. Na mnahisi upendo msafi wa Kristo kwa wengine na kwenu.

Ninaona hilo kwa wamisionari wanaotumikia duniani kote. Ninaona hilo kwa waumini wanaozungumza na rafiki zao na wanafamilia kuhusu Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Wanaume, wanawake, vijana, na hata watoto wanahudumu kwa upendo kwa ajili ya Mwokozi na kwa ajili ya jirani zao.

Kwenye ripoti ya kwanza ya majanga ulimwenguni kote, waumini wanaandaa mipango ya kwenda kuokoa, wakati mwingine kuvuka bahari, bila ya kuombwa. Wakati mwingine inawawia vigumu kusubiri hadi eneo lililo haribiwa liwapokee.

Ninagundua kwamba baadhi yenu mnaosikiliza leo mnaweza kuhisi kwamba imani na tumaini lenu vinazidiwa na matatizo yenu. Na mnaweza kutamani kuhisi upendo.

akina kaka na akina dada, Bwana ana fursa karibu yenu kuhisi na kushiriki upendo Wake. Mnaweza kusali kwa ujasiri kwa Bwana ili awaongoze kumpenda mtu kwa ajili Yake. Anajibu sala za wanaojitolea wanyenyekevu kama ninyi. Mtahisi upendo wa Mungu kwenu na kwa mtu mnayemtumikia kwa ajili Yake. Unapowasaidia watoto wa Mungu katika matatizo yao, matatizo yako mwenyewe yataonekana mepesi. Imani yako na tumaini lako vitaimarishwa.

Mimi ni shahidi wa kweli hiyo. Katika kipindi cha maisha, mke wangu ameongea kwa ajili ya Bwana na alitumikia watu kwa ajili Yake. Kama nilivyosema hapo awali, mmoja wa maaskofu wetu aliwahi kuniambia: “Ninashangazwa. Kila wakati ninaposikia mtu katika kata ambaye yupo kwenye matatizo, nafanya haraka kumsaidia. Lakini wakati ninapo wasili, inaonekana kwamba mke wako tayari alishafika pale.” Hiyo imekuwa kweli katika sehemu zote tulizoishi kwa miaka 56.

Sasa anaweza kuongea maneno machache tu kwa siku. Anatembelewa na watu aliowapenda kwa ajili ya Bwana. Kila usiku na asubuhi ninaimba nyimbo pamoja naye na tunasali. Natakiwa kuwa sauti katika sala na katika nyimbo. Wakati mwingine naweza kumuona akitamka maneno ya nyimbo. Anapendelea nyimbo za watoto. wazo ambalo anaonekana kulipenda zaidi limefupishwa kwenye wimbo “Ninajaribu kuwa kama Yesu.”11

Siku moja, baada ya kuimba maneno ya kibwagizo: “Pendaneni kama Yesu anavyowapenda. Jaribu kuonyesha ukarimu katika yote unayofanya,” alisema kwa upole, lakini waziwazi , “Jaribu, Jaribu, Jaribu.” Ninafikiri kwamba atakuta, pale atakapomuona, kwamba Mwokozi wetu ameweka jina Lake katika moyo wake na kwamba amekuwa kama Yeye. Anambeba katika matatizo yake sasa, kama atakavyo kubeba wewe kwenye matatizo yako.

Ninatoa ushahidi wangu kwamba Mwokozi anakujua na kukupenda. Analijua jina lako kama unavyolijua Lake. Anayajua matatizo yako. Ameyapitia matatizo hayo. Kwa Upatanisho Wake, ameushinda ulimwengu. Kwa kuwa tayari kujichukulia jina Lake juu yako, utabeba mizigo ya wengine wengi. Na utaona wakati ukifika kwamba unamjua zaidi Mwokozi na kwamba unampenda zaidi. Jina Lake litakuwa katika moyo wako na kukaa katika kumbukumbu zako. Ni jina ambalo kwalo utaitwa. Ninashuhudia hivyo, kwa shukrani kwa ajili ya fadhili za upendo Wake kwangu, kwa wapendwa wangu, na kwenu, katika jina la Yesu Kristo, amina.

Chapisha