2010–2019
Ukweli na Mpango
Oktoba 2018


15:49

Ukweli na Mpango

Wakati tunapotafuta ukweli kuhusu dini, tunapaswa kutumia mbinu za kiroho zinazofaa kwa ajili ya uchunguzi huo.

Ufunuo wa kisasa unafafanua ukweli kama “maarifa ya mambo kama yalivyo, na kama yalivyokuwa, na kama yatakavyokuwa” (Mafundisho na Maagano 93:24). Huu ni ufafanuzi kamili wa mpango wa wokovu na “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu.”

Tunaishi katika kipindi cha taarifa nyingi na zilizoenezwa. Lakini siyo taarifa zote ni za kweli. Tunahitaji kuwa waangalifu wakati tunapotafuta ukweli na kuchagua vyanzo kwa ajili ya uchunguzi huo. Hatufai kuzingatia umaarufu au mamlaka ya kidunia kama vyanzo vya ukweli vya kuaminika. Tunapaswa kuwa waangalifu kuhusu kutegemea taarifa au ushauri usio stadi unaotolewa na nyota wa burudani, wanariadha mashuhuri, au vyanzo vya mtandaoni visivyojulikana. Ustadi katika taaluma moja haifai kuchukuliwa kama ustadi kuhusu ukweli katika masomo mengine.

Pia tunapaswa kuchukua tahadhari kuhusu kuzingatia motisha ya mwenye kutoa taarifa. Hii ndiyo sababu maandiko yanatuonya dhidi ya ukuhani wa uongo (ona 2 Nefi 26:29). Kama chanzo hakina jina au hakijulikani, taarifa hiyo pia inaweza kuwa yenye shaka.

Uamuzi wetu wa kibinafsi unapaswa kuwa na msingi kwenye taarifa zenye vyanzo vilivyothibitishwa juu ya somo hilo na huru kutokana na motisha za kibinafsi.

I.

Wakati tunapotafuta ukweli kuhusu dini, tunapaswa kutumia mbinu za kiroho zinazofaa kwa ajili ya uchunguzi huo: ushahidi wa Roho Mtakatifu, na kujifunza maandiko na maneno ya manabii wa sasa. Mimi daima huhuzunika ninaposikia mtu anayepoteza imani ya kidini kwa sababu ya mafunzo ya kidunia. Wale ambao kwa wakati mmoja waliwahi kupata ono wanaweza kuteseka kutokana na upofu wa kiroho wa kujiletea. Kama alivyosema Rais Henry B. Eyring, “Shida yao haipatikani katika kile wanadhani wanakiona; inapatikana katika kile wasichoweza bado kukiona.”1

Mbinu za kisayansi zinatuongoza kufikia kile tunachoita ukweli wa kisayansi. Lakini “ukweli wa kisayansi” si kila sehemu ya maisha. Wale wasiojifunza “kwa kusoma na pia kwa imani” (Mafundisho na Maagano 88:118) wanaweka mipaka kwa uelewa wao wa ukweli na kile wanachoweza kuthibitisha kupitia mbinu za kisayansi. Hilo linaweka mipaka bandia katika kutafuta ukweli.

Rais James E. Faust alisema: “Wale ambao [wamebatizwa] wanahatarisha nafsi zao za milele kwa kutafuta bila uangalifu vyanzo vya mafunzo ya kidunia. Tunaamini ya kwamba Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho lina utimilifu wa injili ya Kristo, injili ambayo ni kiini cha ukweli na kuelimika kwa milele.”2

Tunapata shangwe ya kweli na inayodumu kwa kuja kujua na kutenda kulingana na ukweli kuhusu sisi ni kina nani, maana ya maisha ya kufa, na tunakokwenda wakati tutakapokufa . Kweli hizo hatuwezi kujifunza kupitia mbinu za kisayansi au kidunia.

II.

Sasa nitazungumzia kweli za injili zilizorejeshwa ambazo ni mafundisho ya msingi ya Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Tafadhali zingatia kweli hizi kwa makini. Zinaelezea mengi kuhusu mafundisho na desturi zetu, pengine ikijumuisha baadhi ambazo bado hazijaeleweka.

Kuna Mungu, ambaye ni Baba mpendwa wa roho za wale wote ambao wamewahi kuishi au watakaoishi.

Jinsia ni ya milele. Kabla hatujazaliwa duniani, tuliishi kama roho za kiume na za kike katika uwepo wa Mungu.

Tumetoka tu kuisikiliza Kwaya ya Tabernacle kule Temple Square ikiimba “I Will Follow God’s Plan.”3 Huu ndio mpango Mungu alianzisha ili watoto Wake wote wa kiroho wangeweza kuendelea milele. Mpango huu ni muhimu kwa kila mmoja wetu.

Chini ya mpango huo, Mungu aliumba dunia hii kama mahali ambapo watoto wa kiroho wapendwa wangeweza kuzaliwa katika maisha ya muda kupokea mwili na kupata nafasi ya kuweza kuendelea milele kwa kufanya chaguzi za haki.

Ili kuwa za maana, chaguzi ilibidi zifanywe kati ya nguvu zinazoshindana za wema na uovu. Ilikuwa ni lazima kuwe na upinzani, hata hivyo adui, aliyetupwa nje kwa sababu ya uasi, aliruhusiwa kuwajaribu watoto wa Mungu watende kinyume na mpango wa Mungu.

Lengo la mpango wa Mungu lilikuwa kuwapa watoto Wake nafasi ya kuchagua maisha ya milele. Hili lingewezekana tu kupitia uzoefu wa maisha na, baada ya kifo, kukua baada ya maisha ya muda katika ulimwengu wa roho.

Katika maisha ya muda, sote tungechafuliwa na dhambi wakati tungeshindwa na majaribu maovu ya adui, na hatimaye tungekufa. Tulikubali changamoto hizo kwa kutegemea hakikisho kwamba Mungu Baba yetu angetoa Mwokozi, Mwanawe wa Pekee, ambaye angetuokoa kupitia ufufuo wa wanadamu wote katika maisha yenye mwili baada ya kifo. Mwokozi pia angetoa upatanisho ili kulipa gharama kwa ajili ya kila mmoja kusafishwa dhambi kwa masharti Aliyotoa. Masharti hayo yalijumuisha imani katika Kristo, toba, ubatizo, kipawa cha Roho Mtakatifu, na ibada zinginezo zinazotekelezwa na kupitia mamlaka ya ukuhani.

Mpango mkuu wa Mungu wa furaha unatoa usawa kamili kati ya haki ya milele na rehema tunayoweza kupata kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo. Pia inatuwezesha kubadilishwa kuwa viumbe vipya katika Kristo.

Mungu apendaye anafikia kila mmoja wetu. Tunajua ya kwamba kupitia upendo Wake na kwa sababu ya Upatanisho wa Mwanawe wa Pekee, wanadamu wote wanaweza kuokolewa, kwa kutii sheria na ibada za Injili [Yake]”(Makala Imani 1:3; mkazo umeongezwa).

Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho linajulikana vyema kama Kanisa linaloweka familia kama kiini chake. Lakini kile ambacho hakijaeleweka vyema ni kwamba kuweka familia kama kiini kunalenga zaidi ya uhusiano wa muda. Mahusiano ya milele ni ya kimsingi katika teolojia yetu. Familia imetakaswa na Mungu.”4 Chini ya mpango mkuu wa Muumbaji wetu mpendwa, misheni ya Kanisa Lake la urejesho ni kuwasaidia watoto wa Mungu kuhitimu baraka takatifu ya kuinuliwa katika ufalme wa selestia, ambayo inaweza kupatikana tu kupitia ndoa ya milele baina ya mwanaume na mwanamke (ona Mafundisho na Maagano 131:1–3). Tunathibitisha mafunzo ya Mwokozi kwamba, “jinsia ni hulka muhimu ya utambuzi wa maisha kabla ya maisha ya dunia, na maisha ya dunia ya mtu na utambulisho na dhamira” na kwamba “ndoa kati ya mwanaume na mwanamke ni muhimu kwa mpango Wake wa milele.”5

Hatimaye, upendo wa Mungu ni mkuu kiasi cha kwamba, isipokuwa kwa wachache ambao kimakusudi wanakuwa wana wa wapotevu, Ametayarisha takdiri ya utukufu kwa ajili ya watoto Wake wote. “Watoto Wake wote” ikijumuisha wale waliokufa. Tunafanya ibada wao kwa niaba yao katika mahekalu yetu. Lengo la Kanisa la Yesu Kristo ni kuwawezesha Watoto Wake kwa ajili ya kiwango cha juu zaidi cha utukufu, ambacho ni kuinuliwa au maisha ya milele. Kwa wale ambao hawana nia au hawahitimu hiyo, Mungu Ametayarisha ufalme mwingine ingawaje mdogo.

Yeyote ambaye anaelewa kweli hizi za milele anaweza kuelewa ni kwa nini sisi waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho hufikiria jinsi tufanyavyo na kutenda jinsi tutendavyo.

III.

Sasa nitazitaja baadhi ya matumizi ya kweli hizi za milele, ambazo zinaweza tu kueleweka katika nuru ya mpango wa Mungu.

Kwanza, tunaheshimu wakala wa mtu binafsi. Wengi wanafahamu kuhusu juhudi kubwa za Kanisa la urejesho kusaidia kuwepo kwa uhuru wa kidini Marekani na kote duniani. Juhudi hizi haziendelezi tu maslahi yetu lakini, kulingana na mpango Wake, zinatafuta kuwasaidia watoto wote wa Mungu kufurahia uhuru wa kuchagua.

Pili, sisi ni watu wa umisionari. Wakati mwingine huwa tunaulizwa ni kwa nini tunawatuma wamisionari katika mataifa mengi, hata miongoni mwa mataifa ya kikristo. Tunapokea swali sawa na hilo kuhusu kwa nini tunapeana mamilioni ya dola ya msaada wa kibinadamu kwa watu ambao si waumini wa Kanisa letu na ni kwa nini hatuunganishi msaada huu na juhudi zetu za kimisionari. Tunafanya haya kwa sababu tunawachukulia wanadamu wote ni watoto wa Mungu—kaka zetu na dada zetu—na tunataka kushiriki wingi wetu wa kiroho na mali na kila mmoja.

Tatu, maisha ya muda ni matakatifu kwetu. Kujitolea kwetu kwa mpango wa Mungu kunahitaji sisi kupinga utoaji mimba na eutanasia.

Nne, wengine wanafadhaishwa na baadhi ya misimamo ya Kanisa juu ya ndoa na watoto. Ufahamu wetu kuhusu mpango wa Mungu wa wokovu uliofunuliwa unatuhitaji kupinga zaidi mashinikizo ya kijamii na kisheria ya kisasa kujitenga na ndoa za kimila au mabadiliko yanayochanganya au yanayobadili jinsia au yanayosawazisha tofauti kati ya wanaume na wanawake. Tunajua ya kwamba mahusiano, utambulisho, na majukumu ya wanaume na wanawake ni muhimu katika kutimiza mpango mkuu wa Mungu.

Tano, pia tuna mtazamo wa kipekee kuhusu watoto. Tunafikiria uzazi na kuwatunza watoto kama sehemu ya mpango wa Mungu na kazi ya shangwe na takatifu ya wale waliopewa fursa ya kushiriki. Katika mtazamo wetu, tunaamini kwamba hazina kubwa hapa duniani na mbinguni ni watoto wetu na vizazi vyetu. Kwa hivyo, ni lazima tufundishe na kupingana kwa ajili ya kanuni na desturi ambazo zinaleta hali bora kwa ukuaji na furaha ya watoto—watoto wote.

Mwisho, sisi ni watoto wapendwa wa Baba wa Mbinguni, ambaye ametufundisha kuwa uwanaume na uwanamke, ndoa kati ya mwanaume na mwanamke, na ulezi na kuwatunza watoto vyote ni muhimu kwa mpango Wake mkuu wa furaha. Misimamo yetu juu ya mambo haya muhimu mara kwa mara huchochea upinzani kwa Kanisa. Tunafikiria hio haiepukiki. Upinzani ni sehemu ya mpango huo, na upinzani mkali zaidi wa Shetani unaelekezwa kwa kile kilicho muhimu zaidi katika mpango wa Mungu. Anatafuta kuharibu kazi ya Mungu. Mbinu zake kuu ni kumwaibisha Mwokozi na mamlaka yake takatifu, kufuta athari za Upatanisho wa Yesu Kristo, kuzuia toba, kutoa ufunuo wa uongo, na kukanusha uwajibikaji wa kibinafsi. Pia anatafuta kuchanganya jinsia, kupotosha ndoa, na kukatisha tamaa ya kuwa na watoto—hasa kwa wazazi ambao watawalea watoto katika ukweli.

IV.

Kazi ya Bwana inasonga mbele licha ya upinzani uliopangwa na wa kila mara ambao unatukabili tunapojitahidi kutenda mafundisho ya Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Kwa wale wanaotatizika chini ya upinzani huo, ninatoa mapendekezo haya.

Kumbuka kanuni ya toba inawezekana kwa kupitia uwezo wa nguvu za Upatanisho wa Yesu Kristo. Kama Mzee Neal A. Maxwell alivyosihi, usikuwe miongoni mwa “wale ambao wangependa kubadilisha Kanisa badala ya kujibali wao wenyewe.”6

Jinsi Mzee Jeffrey R. Holland alisihi:

“Shikilia imara kwa kile unachojua tayari na simama kwa uthabiti mpaka uelewa wa ziada uje.

Katika Kanisa hili, kile tunachofahamu daima kitashinda kile ambacho hatukifahamu.7

Kuwa na imani katika Bwana Yesu Kristo, ambayo ni kanuni ya kwanza ya injili.

Tatu, tafuta usaidizi. Viongozi wetu wa Kanisa wanakupenda na hutafuta maongozi ya kiroho ili kukusaidia. Tunatoa nyenzo nyingi kama zile utakazopata kuptia LDS.org na misaada kwa ajili ya kujifunza injli nyumbani. Sisi pia, tuna kaka na dada wa kuhudumu walioitwa kutoa msaada wa upendo.

Baba yetu mpendwa wa Mbinguni anawataka watoto Wake wawe na shangwe hilo ndilo lengo la uumbwaji wetu. Takdiri hiyo ya shangwe ni maisha ya milele, ambayo tunaweza kuipokea kwa kusonga mbele katika kile nabii wetu, Rais Russell M. Nelson, mara nyingi huita “njia ya agano.” Hiki ndicho kile alichokisema katika ujumbe wake wa kwanza kama Rais wa Kanisa: “Baki katika njia ya agano. Kujitolea kwako kumfuata Mwokozi kupitia kufanya maagano Naye na Kisha kuyaishika maagano hayo kutafungua mlango kwa kila baraka ya kiroho na fadhila unaopatikana kwa wanaume, wanawake, na watoto kila mahali.”8

Ninashuhudia kwa dhati kwamba vitu ambavyo nimesema ni vya kweli, na vinawezekana kupitia mafundisho na Upatanisho wa Yesu Kristo, ambaye anafanya kila kitu kuwezekana chini ya mpango mkuu wa Mungu, Baba yetu wa Milele. Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Henry B. Eyring, To Draw Closer to God: A Collection of Discourses (1997), 143.

  2. James E. Faust, “The Abundant Life,” Ensign, Nov. 1985, 9.

  3. “I Will Follow God’s Plan,” Children’s Songbook, 164–65.

  4. Familia: Tangazo kwa Ulimwengu,” Liahona, Mei 2017, 145.

  5. The Family: A Proclamation to the World,” 145.

  6. Neal A. Maxwell, If Thou Endure It Well (1996), 101.

  7. Jeffrey R. Holland, “Lord, I Believe,” Liahona, May 2013, 94; emphasis in original.

  8. Russell M. Nelson, “As We Go Forward Together,” Liahona, Apr. 2018, 7.