Inueni Vichwa Vyenu na Mfurahi.
Tunapokumbana na mambo magumu katika njia za Bwana, naomba tuinue vichwa vyetu na kufurahi.
Mnamo mwaka 1981, baba yangu, marafiki wawili wa karibu, nami tulikwenda kwa ziara ya jusura huko Alaska. Tulitakiwa tufike kwenye ufukwe wa ziwa lililotengwa na kupanda kwenye maeneo mazuri ya juu. Ili kupunguza mzigo ambao tulipaswa kubeba binafsi, tulifunga vitu vyetu kwenye maboksi, tukifunika kwa sponji, tukafunga tepe za rangi, na tukayatupa nje dirishani mwa ndege ya vichakani kwenye sehemu tuliyokusudia kufika.
Baada ya kuwasili, tulitafuta na kutafuta, lakini kwa msikitiko wetu, hatukuweza kuona boksi hata moja. Hatimaye tulilipata moja. Lilikuwa na stove ndogo ya gesi, turubai, peremende, na vifurushi kadhaa vya kutengenezea hambaga—lakini hakuna hambaga yenyewe. Hatukuwa na njia ya kuwasiliana na upande mwingine na ratiba ya kuja kuchukuliwa ilikuwa wiki moja ijayo.
Nilijifunza masomo mawili muhimu kutoka kwa huu uzoefu: Kwanza, usitupe chakula nje ya dirisha Pili, wakati mwingine tunahitaji kukumbana na mambo magumu.
Mara kwa mara, tendo letu la kwanza kwa vitu vigumu ni “Kwa nini mimi?” Kuuliza kwa nini, hata hivyo, hakuondoi vitu vigumu kamwe. Bwana anahitaji kwamba sisi tushinde changamoto, na ameonyesha “mambo haya yote yatatupa [sisi] uzoefu, na yatakuwa kwa faida [yetu].”1
Wakati mwingine Bwana anatutaka sisi tufanye mambo magumu, na wakati mwingine changamoto zetu zinaletwa na uhuru wetu wa kujiamulia au watu wengine. Nefi alikumbana na hali hizi zote mbili. Wakati Lehi alipowaalika wana wake kurudi kwenda kuchukua mabamba toka kwa Labani, alisema, “Tazama kaka zako wananung’unika, wakisema kuwa ni kitu kigumu ninachokihitaji kutoka kwao; lakini, tazama mimi sijahitaji hilo kwao, lakini ni amri ya Bwana.”2 Katika tukio jingine, kaka zake Nefi walitumia uhuru wao wa kujiamulia ili kukwamisha wake: “Walinikamata, kwani tazama, walikuwa na hasira nyingi, na wakanifunga kwa kamba, kwani walitaka kunitoa uhai wangu, kwamba wangeniacha nyikani niliwe na wanyama wa mwituni.”3
Joseph Smith alikumbana na mambo magumu katika Jela ya Liberty. Bila ya msaada iliyoonekana na katika kukata tamaa, Joseph alilia kwa sauti,“Ee Mungu, uko wapi?”4 Bila shaka baadhi yetu wamehisi kama Joseph.
Kila mtu anakumbana na mambo magumu: kifo cha umpendaye, talaka, mtoto aliyepotoka, magonjwa, majaribu ya imani, kupoteza kazi, au matatizo mengine magumu.
Nilibadilishwa daima kwa kusikia maneno haya kutoka kwa Mzee Neal A. Maxwell wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, aliyonena akisumbuliwa na ugonjwa wa damu (leukemia). Alisema, “Nilikuwa natafakari kwa kina maneno haya ya kufundisha na ya ahadi yaliyotoka kwenye fikra zangu: ‘Nimewapa ugonjwa wa damu ili muweze kuwafundisha watu wangu kwa uhalisia.’” Kisha akaendelea kuelezea jinsi uzoefu huu ulivyomfundisha “taswira kuhusu ukweli halisia juu ya umilele. … Mtazamo wa aina hii wa umilele unaweza kutusaidia kusafiri kwa yadi 100 zijazo, ambapo inaweza kuwa vigumu sana.”5
Ili kutusaidia sisi kusafiri na kuzishinda nyakati zetu ngumu kwa mtazamo huu wa milele, naomba nishauri vitu viwili. Lazima tuyakabili mambo magumu, kwanza, kwa kuwasamehe wengine, pili, kwa kujitoa wenyewe kwa Baba yetu wa Mbinguni.
Kuwasamehe wale ambao walitusababishia mambo magumu na kujiridhia “[sisi]wenyewe kwa mapenzi ya Mungu”6 inaweza kuwa vigumu sana. Inaweza kuumiza zaidi wakati mambo yetu magumu yanasababishwa na mwanafamilia, rafiki wa karibu, au hata sisi wenyewe.
Nikiwa askofu kijana, nilijifunza kusamehe wakati rais wangu wa kigingi, Bruce M. Cook, aliposhiriki hadithi ifuatayo. Yeye alielezea:
“Wakati wa kipindi cha mwisho cha miaka ya 1970, baadhi ya marafiki pamoja nami tulianzisha biashara. Ijapokuwa hatukufanya jambo kinyume na sheria, baadhi ya maamuzi mabaya, yakijumuishwa na changamoto za kiuchumi za wakati huo, zilipelekea kushindwa kwetu.
“Baadhi ya wawekezaji walifungua kesi ili kufidiwa hasara zao. Wakilini wao alitokea kuwa ni mshauri katika uaskofu wa familia yangu. Ilikuwa ni vigumu kumkubali mtu aliyeonekana anataka kuniangamiza. Nilianzisha chuki ya waziwazi dhidi yake na kumfikiria kama adui yangu. Baada ya miaka mitano ya mapigano ya kisheria, tulipoteza kila kitu tulichomiliki, yakiwemo makazi yetu.
“Mnamo mwaka 2002, mke wangu na mimi tulijifunza kwamba urais wa kigingi ambao mimi nilikuwa ninahudumu kama mshauri ulikuwa unaundwa upya. Tulipokuwa tukisafiri kwenye mapumziko mafupi kabla ya kuachiliwa aliniuliza ni nani ningewachagua kuwa washauri wangu iwapo nitaitwa kuwa rais wa kigingi. Sikutaka kuzungumzia juu ya jambo hili, lakini alisisitiza. Hatimaye, jina moja likaja kwenye mawazo yangu. Kisha akalitaja jina la wakili ambaye tulimfikiria amekuwa chanzo cha matatizo yetu kwa miaka 20 ya nyuma. Alipokuwa anaongea, Roho alishuhudia kwamba alitakiwa kuwa yule mshauri mwingine. Ningeweza kumsamehe mtu huyu?
“Wakati Mzee David E. Sorensen aliponipa wito wa kuhudumu kama rais wa kigingi, alinipa saa moja ya kuchagua washauri. Kwa machozi, nilionyesha kwamba Bwana tayari alikuwa ametoa ufunuo. Nilipolisema jina la mtu niliyemfikiria kuwa adui yangu, hasira, uhasama na chuki niliyohifadhi vikapotea. Katika wakati ule, nilijifunza amani itokanayo na kusamehe kupitia Upatanisho wa Kristo.
Kwa maneno mengine, rais wangu wa kigingi “alimsamehe waziwazi” kama Nefi wa kale.7 Nilimjua Rais Cook na mshauri wake kama viongozi wa ukuhani wenye haki ambao walipendana. Niliamua kuwa kama wao.
Miaka kadhaa kabla, wakati wa safari yetu ya hatari huko Alaska, mara moja nikajifunza kwamba kulaumu wengine kwa ajili ya hali zetu—rubani akirusha kile chakula nje kwa mwanga uliokuwa unafifia—haikuwa ndio suluhisho. Hata hivyo, tukiwa tunakabiliwa na kuchoka kimwili, kukosa chakula, maradhi, na kulala chini wakati wa dhoruba kali tukiwa na turubai la kujifunika, nilijifunza kwamba, “kwa Mungu hakuna lisilowezekana.”8
Vijana, Mungu anahitaji mambo magumu kutoka kwenu. Msichana mmoja wa miaka 14 alishiriki kwenye mashindano wa mpira wa kikapu. Aliota akicheza mpira wa kikapu akiwa shule ya upili kama ilivyokuwa kwa dada yake. Kisha akagundua kwamba wazazi wake walikuwa wameitwa kuhudumu misheni huko Guatamala.
Apowasili, aligundua kwamba baadhi ya madarasa yake yatakuwa ya Kihispania, lugha ambayo hajawahi kuiongea. Hapakua na timu yoyote ya michezo ya wasichana katika shule yake. Aliishi kwenye ghorofa ya 14 kwenye jengo lenye ulinzi mkali. Na juu ya yote, hakutakiwa kwenda nje peke yake kwa sababu za kiusalama.
Wazazi wake walisikia kilio chake kila usiku kwa miezi. Hali hii ilivunja mioyo yao! Hatimaye waliamua wamrudishe nyumbani kwa bibi yake akasome shule ya upili.
Wakati mke wangu alipoingia chumbani kwa binti yetu kumwambia uamuzi wetu, alimuona binti yetu amepiga magoti akisali pamoja na Kitabu cha Mormoni kikiwa kipo kitandani kimefunguliwa. Roho alimnong’oneza mke wangu, “Atakuwa Sawa,” na mke wangu aliondoka chumbani kimya kimya.
Hatukuwahi tena kumsikia akilia wakati wa kulala. Kwa ushupavu na msaada wa Bwana, miaka ile mitatu alikabiliana na ujasiri.
Mwishoni mwa misheni yetu, nilimwuliza binti yangu kama atakwenda kuhudumu misheni. Jibu lake lilikuwa “Hapana, Baba, tayari nimeshahudumu.”
Nilikuwa sawa na hilo! Lakini miezi sita baadaye, Roho aliniamsha usiku kwa tafakari hii: “Nimemwita binti yako kuhudumu misheni.”
Jibu langu lilikuwa “Baba wa Mbinguni, amejitolea sana.” Mara moja nilisahihishwa na Roho na nikapata kuelewa kwamba huduma yake ilihitajika na Bwana.
Baadaye nikaenda kupata chakula cha mchana na binti yangu. Kutoka upande mwingine wa meza, nikasema, “Ganzie, unajua kwa nini tupo hapa?”
Alisema “Ndiyo, Baba. Unajua nahitaji kuhudumu misheni. Sitaki kwenda, lakini ninakwenda.”
Kwa sababu alijitoa kwa Baba wa Mbinguni, alimtumikia kwa moyo wake wote, uwezo, akili na nguvu. Amemfundisha baba yake jinsi ya kufanya jambo gumu.
Katika ibada ya vijana duniani kote Rais Russell M. Nelson, alihitaji mambo magumu kutoka kwa vijana. Rais Nelson alisema: “Mwaliko wangu wa tano ni kwa ajili yenu kusimama; kuwa tofauti na ulimwengu. … Bwana anahitaji ninyi kuonekana kama, kusikika kama, kutenda kama, na kuvaa kama wafuasi wa kweli wa Yesu Kristo.”9 Hilo linaweza kuwa jambo gumu, hata hivyo najua mnaweza kufanya—kwa shangwe.
Kumbukeni kwamba “wanadamu wapo, ili wapate shangwe.”10 Kwa yale yote aliyokumbana nayo Lehi, bado alipata furaha. Kumbuka wakati Alma “alipozidiwa na huzuni”11 kwa sababu ya watu wa Amoniha? Malaika alimwambia “Heri wewe, Alma; kwa hivyo, inua kichwa chako na ufurahi … Kwani umekuwa mwaminifu katika kutii amri za Mungu.”12 Alma amejifunza ukweli mkubwa: tunaweza kufurahi kila mara tunapotii amri. Kumbuka kwamba wakati wa vita na changamoto zilizojitokeza wakati wa Kapteni Moroni, “hakujakuwa wakati wa furaha miongoni mwa watu Nefi.”13 Tunaweza na tunatakiwa kupata furaha tunapokumbana na mambo magumu.
Mwokozi alikumbana na mambo magumu: “Ulimwengu … utamhukumu kuwa jambo la dharau; kwa hivyo wanampiga kwa mijeledi, na anavumilia; na wanamchapa, na anavumilia. Ndio, na wanamtemea mate, na anavumilia, kwa sababu ya upendo wake mkarimu na subira yake kwa watoto wa watu”14.
Kwa sababu ya upendo wa wema, Yesu Kristo alisumbuka katika Upatanisho. Kwa matokeo, Anasema kwa kila mmoja wetu, “Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.”15 Kwa sababu ya Kristo, nasi pia tunaweza kuushinda ulimwengu.
Tunapokumbana na mambo magumu katika njia za Bwana, naomba tuinue vichwa vyetu na kufurahi. Kwa fursa hii tukufu ya kushuhudia kwa ulimwengu, ninatangaza kwamba Mwokozi wetu anaishi na analiongoza Kanisa Lake. Katika jina la Yesu Kristo, amina.