Jukumu la Kitabu cha Mormoni katika Uongofu
Tunaikusanya Israeli kwa mara ya mwisho na tunafanya hivyo kwa Kitabu cha Mormoni, moja kati ya zana zenye nguvu za uongofu.
Watu wengi leo hii wanashangaa kuhusu uhalisia wa Mungu na uhusiano wetu Kwake. Wengi wanajua kidogo au hawajui kabisa kuhusu mpango Wake mkuu wa furaha. Zaidi ya miaka 30 iliyopita, Rais Ezra Taft Benson aliona kwamba “Sehemu kubwa ya … ulimwengu leo hii hukataa uungu wa Mwokozi. Wanatilia shaka kuzaliwa Kwake kwa kimiujiza, maisha Yake ya ukamilifu, na uhalisia wa ufufuko Wake mtukufu.”1
Katika siku yetu, maswali yanalenga si tu kwa Mwokozi wetu bali pia kwa Kanisa Lake—Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho—ambalo alillirejesha kupitia Nabii Joseph Smith. Maswali haya mara nyingi hulenga historia, mafundisho, au mifumo ya Kanisa la Mwokozi.
Kitabu cha Mormoni hutusaidia kukua katika Ushuhuda.
Kutoka katika Hubiri Injili Yangu, tunasoma: “Kumbuka kwamba uelewa wetu [wa Baba wa Mbinguni na mpango Wake wa furaha] huja kutoka kwa manabii wa sasa—Joseph smith na waliomfuatia—ambao wanapokea ufunuo moja kwa moja kutoka kwa Mungu. Hivyo swali la kwanza ambalo mtu anatakiwa kujibu ni kama Joseph Smith alikuwa nabii, na mtu huyo anaweza kujibu swali hili kwa kusoma na kusali kuhusu Kitabu cha Mormoni.”2
Ushuhuda wangu wa wito mtakatifu wa Nabii Joseph Smith umeimarishwa kwa kusoma kwa sala Kitabu cha Mormoni: Ushuhuda mwingine wa Yesu Kristo. Nimefuata mwaliko wa Moroni wa “kumuuliza Mungu, Baba wa Milele, katika jina la Kristo” kujua ukweli wa Kitabu cha Mormoni.3 Ninashuhudia kwamba ninajua ni cha kweli. Uelewa huo umekuja kwangu, kama unavyoweza kuja kwako, “kwa nguvu za Roho Mtakatifu.”4
Dibaji ya Kitabu cha Mormoni inasema: “Wale ambao wanapata ushuhuda huu mtakatifu kutokana na Roho Mtakatifu watajua pia kutokana na huo uwezo kwamba Yesu Kristo ndiye Mwokozi wa ulimwengu, na kwamba Joseph Smith ndiye mfunuzi na nabii wake katika siku hizi za baadaye, na kwamba Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ndilo falme la Bwana ambalo limejengewa mara ingine hapa ulimwenguni kwa matayarisho ya ujio wa pili kwa Masiya.”5
Kama mmisionari kijana huko Chile, nilijifunza somo zuri la kubadili maisha kuhusu nguvu ya kuongoa ya Kitabu cha Mormoni. Bwana Gonzales alitumikia katika nafasi ya kuheshimika katika kanisa lake kwa miaka mingi. Alikuwa na mafunzo ya kina ya kidini ikijumuisha shahada katika elimu ya dini. Alikuwa akijivunia sana weledi wake katika biblia. Ilikuwa wazi kwetu kwamba alikuwa mbobezi katika dini.
Alikuwa akiwajua vizuri wamisionari wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho walipokuwa wakifanya kazi yao katika mji alikozaliwa huko Lima, Peru. Mara zote alitaka kukutana nao ili awafundishe kuhusu Biblia.
Siku moja, kama zawadi kutoka mbinguni, ndivyo alivyofikiria, wamisionari wawili walimsimamisha mtaani na kuuuliza kama wangeweza kumtembelea kwake na kushiriki maandiko pamoja naye. Hii ilikuwa ni kutimia kwa ndoto yake! Sala zake zimejibiwa. Hatimaye, angeweza kuwaongoza kwenye usahihi wavulana hawa waliopotea. Aliwaambia kuwa angefurahi sana kuwa nao nyumbani kwake kujadiliana maandiko.
Alisubiri sana kwa shauku kukutana nao. Alikuwa tayari kutumia Biblia kukanusha imani yao. Alikuwa na ujasiri kwamba Biblia ingeweza kwa wazi na usahihi kuonyesha makosa katika njia zao. Usiku uliochaguliwa ulifika, na wamisionari waligonga mlangoni kwake. Alikuwa mkarimu sana. Muda wake hatimaye ulikuwa umefika.
Alifungua mlango na kuwakaribisha wamisionari nyumbani kwake. Mmoja wa wamisionari alimpa nakala ya kitabu cha bluu na kutoa ushuhuda wa dhati kwamba alijua kitabu kina neno la Mungu. Mmisionari wa pili aliongezea ushuhuda wake wenye nguvu juu ya kitabu, akishuhudia kwamba kilitafsiriwa na nabii wa siku za mwisho wa Mungu, aliyeitwa Joseph Smith, na kwamba kinafundisha kuhusu Kristo. Wamisionari waliomba udhuru na wakaondoka nyumbani kwake.
Bwana Gonzales alikatishwa tamaa sana. Lakini alifungua kitabu, na kuanza kupitia kurasa zake. Alisoma ukurasa wa kwanza. Alisoma ukurasa baada ya ukurasa baada ya ukurasa na hakuacha mpaka kesho yake mchana. Alisoma kitabu chote na alijua kilikuwa cha kweli. Alijua nini alitakiwa kufanya. Aliwaita wamisionari, akapokea mafundisho, na kuacha maisha aliyokuwa akiyajua na kuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.
Mtu huyo mzuri alikuwa mwalimu wangu wa maaandizi ya umisionari huko Provo, Utah. Hadithi ya uongofu ya bwana Gonzales na nguvu ya Kitabu cha Mormoni vilisababisha ushawishi mkuu kwangu.
Nilipofika Chile, rais wangu wa misioni, Rais Royden J. Glade, alitualika kusoma ushuhuda wa Nabii Joseph Smith ulioandikwa kwenye Historia ya—Joseph Smith kila wiki. Alitufundisha kuwa ushuhuda wa Ono la Kwanza ungekuwa na uhusiano wa moja kwa moja na ushuhuda wetu wa injili na ushuhuda wetu wa Kitabu cha Mormoni.
Nilichukulia mwaliko wake kwa makini. Nimesoma matukio ya Ono la Kwanza; nimesoma Kitabu cha Mormoni. Nimesali kama ilivyoelekezwa na Moroni na kumuuliza “Mungu, Baba wa Milele, katika jina la Kristo”6 kama Kitabu cha Mormoni ni cha Kweli. Ninashuhudia leo kwamba ninajua Kitabu cha Mormoni, kama Nabii Joseph Smith alivyosema, ndicho “kitabu sahihi duniani, na ndicho jiwe la katikati la leo la dini yetu, na kuwa mwanadamu [ata]mkaribia Mungu zaidi kwa kufuata mafunzo yake, zaidi ya kitabu kingine”7 Nabii Joseph pia alitangaza: “Toa kitabu cha Mormoni na ufunuo, je dini yetu iko wapi? Hatuna chochote.”8
Uongofu Binafsi
Kadiri tunavyoelewa sisi ni nani na dhumuni la Kitabu cha Mormoni, uongofu wetu hukua kwa kina na kuwa dhahiri zaidi. Tunaimarishwa katika kujitoa kwetu kushika maagano tuliyoweka na Mungu.
Kanuni kuu ya Kitabu cha Mormoni ni kuikusanya Israeli iliyotawanyika. Kukusanywa huku huwapatia watoto wote wa Mungu fursa ya kuingia katika njia ya agano na, kwa kuyaheshimu maagano hayo, kurudi tena kwenye uwepo wa Baba. Wakati tunapofundisha toba na kubatiza waongofu, tunaikusanya Israeli iliyotawanyika.
Kitabu cha Mormoni kina marejeo 108 kuhusu nyumba ya Israeli. Mwanzoni mwa Kitabu cha Mormoni , Nefi alifundisha “Kwani lengo langu kamili ni kuwashawishi watu waje kwa Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo ili waokolewe.”9 Mungu wa Ibrahim, Isaka, na Yakobo ni Yesu Kristo, Mungu wa Agano a Kale. Tuanaokolewa pale tunapokuja kwa Kristo kupitia kuishi injili Yake.
Baadaye Nefi aliandika:
“Ndio, baba yangu hata alizungumza mengi kuhusu Wayunani, na pia kuhusu nyumba ya Israeli, kwamba watalinganishwa na mzeituni, ambao matawi yake yatakatwa na kutawanywa kote kote usoni mwa dunia. …
“Na baada ya nyumba ya Israeli kutawanyika watakusanyika tena pamoja; au, kwa usemi mwingine, baada ya Wayunani kupokea utimilifu wa Injili, matawi ya asili ya mzeituni, au masazo ya nyumba ya Israeli, yatapandikizwa, au kumfahamu Masiya wa ukweli, Bwana wao na Mkombozi wao.”10
Vivyo hivyo, mwishoni mwa Kitabu cha Mormoni, nabii Moroni anatukumbusha kuhusu maagano yetu, akisema, “Kwamba hutachanganywa tena, kwamba agano la Baba wa milele ambalo amefanya kwako, Ee nyumba ya Israeli, liwezekane kutimizwa.”11
Maagano ya Baba wa Milele
Je yapi ni “maagano ya Baba wa Milele” ambayo Moroni anayazungumzia? Tunasoma kutoka kitabu cha Ibrahimu:
“Jina langu ni Yehova, nami ninajua mwisho kutoka mwanzo; kwa hiyo mkono wangu utakuwa juu yako.
“Nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, nami nitakubariki kupita kipimo, na kulifanya jina lako kuwa kubwa miongoni mwa mataifa yote, nawe utakuwa baraka kwa uzao wako baada yako, ili katika mikono yao wataichukua huduma hii na Ukuhani kwa mataifa yote,”12
Rais Russell M. Nelson alifundisha katika matangazo ya ulimwenguni kote ya hivi karibuni kwamba “Hakika hizi ni siku za mwisho, na Bwana anaharakisha kazi Yake ya kuikusanya Israeli. Kukusanywa huko ni kitu muhimu sana kinachofanyika duniani hivi leo. Hakulinganishwi na chochote katika ukubwa, hakulinganishwi na chochote katika umuhimu, hakulinganishwi na chochote katika utukufu. Na kama utachagua, kama unataka, unaweza kuwa sehemu kubwa ya hilo. Unaweza kuwa sehemu kubwa ya kitu kikubwa, kitu kikuu, kitu kitukufu!
“Tunapozungumza kuhusu kukusanywa, kiurahisi tunasema kanuni hii ya kweli: Kila mmoja wa watoto wa Baba wa Mbinguni, katika pande zote za pazia, anastahili kusikia ujumbe wa injili ya urejesho ya Yesu Kristo. Wanajiamulia wao wenyewe kama wanataka kujua zaidi.”13
Hicho ndicho ambacho tunakifanya kama waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za mwisho: tunatafuta kuuleta ulimwengu katika uelewa wa—na uongofu katika—injili ya Yesu Kristo. Sisi ni “wakusanyaji wa siku za mwisho.”14 Kazi yetu i dhahiri. Akina kaka na akina dada, acha tujulikane kama wale waliochukua ahadi ya Moroni katika mioyo yetu, waliosali na kupokea jibu kujua kwamba Kitabu cha Mormoni ni cha kweli, na kisha kushiriki uelewa huo na wengine kupitia maneno, na muhimu zaidi, katika matendo.
Jukumu la Kitabu cha Mormoni katika Uongofu
Kitabu cha Mormoni kinacho utimilifu wa injili ya Yesu Kristo.15 Kinatuongoza kwenye agano la Baba, ambalo kama litatunzwa litatuhakikishia zawadi Yake kuu—uzima wa milele.16 Kitabu cha Mormoni ni jiwe la katikati la tao katika uongofu wa watoto wote wa Baba wa Mbinguni wana na mbinti.
Nikimnukuu tena Rais Nelson: “Unaposoma … kila siku kutoka kwenye Kitabu cha Mormoni, utajifunza mafundisho ya kukusanya, kweli kuhusu Yesu Kristo, Upatanisho Wake, na utimilifu wa injili Yake ambao haupo kwenye Biblia. Kitabu cha Mormoni ni kitovu katika kukusanya Israeli. Kwa kweli, kama kusingekuwa na Kitabu cha Mormoni, mkusanyiko ulioahidiwa wa Israeli haungetokea.”17
Acha nihitimishe kwa maneno ya Mwokozi wakati alipowafundisha Wanefi juu ya baraka zilizoahidiwa: “Nyinyi ni watoto wa manabii; na nyinyi ni wa nyumba ya Israeli; na ni wa agano ambalo Baba alifanya na babu zenu, akisema kwa Ibrahimu: Na kupitia uzao wako, makabila yote ya dunia yatabarikiwa.”18
Ninashuhudia kwamba sisi ni wana na mabinti za Mungu, uzao wa Ibrahaimu, nyumba ya Israeli. Tunaikusanya Israeli kwa mara ya mwisho na tunafanya hivyo kwa Kitabu cha Mormoni—kitabu ambacho, kikiunganishwa na Roho wa Bwana ni zana yenye nguvu katika uongofu. Tunaongozwa na nabii wa Mungu, Rais Russell M. Nelson, ambaye anaongoza ukusanyaji wa Israeli katika siku yetu. Kitabu cha Mormoni ni cha kweli. Kimebadilisha maisha yangu. Ninakuahidi, kama vile Moroni na manabii wengi katika nyakati zilizopita, kwamba kinaweza kuyabadili maisha yako.19 Katika jina la Yesu Kristo, amina.