2010–2019
Njoo, Usikie sauti ya Nabii
Oktoba 2018


Njoo, Usikie Sauti ya Nabii

Tunapoimarisha katika maisha yetu utamaduni wa kusikiliza na kutii sauti ya manabii wanaoishi, tutavuna baraka za milele.

Katika kumzungumzia Rais wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, Bwana alitangaza:

“Na tena, kazi ya Rais wa ofisi ya Ukuhani Mkuu ni kuliongoza kanisa lote, na kuwa kama Musa—

“… ndiyo, kuwa mwonaji, mfunuzi, mfasiri, na nabii, akiwa na vipawa vyote vya Mungu ambavyo huviweka juu ya kiongozi wa kanisa” (Mafundisho na Maagano 107:91–92; msisitizo umeongezwa).

Nimebarikiwa kushuhudia baadhi ya vipawa vya Mungu juu ya manabii Wake. Naweza kushiriki nanyi uzoefu mmoja mtakatifu? Kabla ya wito wangu wa sasa, nilisaidia katika utambuzi na kutoa mapendekezo ya maeneo ya baadaye ya hekalu. Baada ya Septemba 11, 2001, kuvuka kupitia mipaka ya Marekani kulikuwa kumedhibitiwa. Kama matokeo, ilichukua masaa mawili hadi matatu kwa waumini wengi wa Kanisa kuvuka kutoka Vancouver, Kanada, wakati wakienda Hekalu la Seattle Washington. Rais Gordon B. Hincley, Rais wa Kanisa wakati huo, alipendekeza kwamba hekalu huko Vancouver lingebariki waumini wa Kanisa. Ruhusa ya kutafuta eneo ilitolewa, na baada ya kupitia miliki kadhaa za Kanisa, maeneo mengine ambayo hayamilikiwi na Kanisa nayo pia yakachunguzwa.

Eneo zuri lenye maeneo ya kidini lililopakana na Barabara kuu ya Trans‑Canadian lilipatikana. Miliki ilikuwa ikifikika vizuri, ilikuwa imefunikwa na miti mizuri ya misonobari ya Kanada, na kufurahia mahali mashuhuri ambapo ingepafanya paonekane kwa maelfu waliopita na magari.

Tuliwasilisha eneo pamoja na picha na ramani kwenye kwenye mkutano wa Kamati wa kila mwezi wa Maeneo ya Hekalu. Rais Hinckley aliidhinisha kwamba tuliweke kwenye mkataba na kukamilisha utafiti muhimu. Mnamo Desemba ya mwaka huo, tulirudisha majibu kwenye kamati kwamba utafiti ulikuwa umekamilika, na tulitafuta idhini ya kuendelea na manunuzi. Baada ya kusikiliza ripoti yetu, Rais Hinckley alisema, “Nahisi ninapaswa kuliona eneo hili.”

Baadaye mwezi huo, siku mbili baada ya Krismasi, tuliondoka kwenda Vancouver pamoja na Rais Hinckley; Rais Thomas S. Monson; na Bill Williams, msanifu majengo ya hekalu. Tulipokelewa na Paul Christensen, rais wa kigingi wa eneo lile, ambaye alitusafirisha kwenda kwenye eneo. Kulikuwa na majimaji kidogo na ukungu siku hiyo, lakini Rais Hinckley aliruka nje ya gari na kuanza kutembea kote katika eneo.

Baada ya kutumia muda katika eneo, nilimuuliza Rais Hinckley kama angependa kuona baadhi ya maeneo mengine ambayo yalikuwa yamefikiriwa. Alisema, Ndiyo, angependa hilo. Unaona, kwa kuangalia maeneo mengine, tuliweza kufanya ulinganishi wa ubora wake.

Tulifanya mzunguko wa mzingo kuzunguka Vancouver, tukiangalia miliki zingine, hatimaye tulirejea kwenye sehemu ya kwanza. Rais Hinckley alisema, “Hii ni sehemu ya kupendeza.” Kisha akauliza, “Tunaweza kwenda kwenye nyumba ya ibada ya kanisa kama robo maili (0.4 km) toka hapa?”

“Hakika, Rais,” tulijibu.

Tulirudi ndani ya magari na kwenda kwenye nyumba ya ibada ya karibu. Tulipofika kwenye kanisa, Rais Hinckley alisema, “Pinda kushoto hapa.” Tulipinda na kufuata mtaa kama tulivyoelekezwa. Mtaa ulianza kuonekana kwa mbali kidogo.

Pale tu gari ilipofikia kilele cha muonekano, Rais Hinckley alisema, “Simamisha gari, simamisha gari.” Kisha akaonyesha kwa kidole upande wa kulia sehemu ya chini na kusema, “Vipi kuhusu miliki hii? Hapa ndipo hekalu litakuwa. Hapa ndipo Bwana anataka hekalu. Je, mnaweza kupapata?” Je, mnaweza kupapata?”

Tulikuwa hatukuangalia miliki hii. Ilikuwa nyuma sana na mbali kutoka barabara kuu, na ilikuwa haijaorodheshwa kuuzwa. Tulipojibu hatujui, Rais Hinckley alionyesha kwa kidole miliki na kusema tena, “Hapa ndipo hekalu litakuwa.” Tulikaa kwa dakika chache kisha kwenda uwanja wa ndege ili kurudi nyumbani.

Siku iliyofuata, mimi na Kaka Williams tuliitwa kwenye ofisi ya Rais Hinckley. Alikuwa amechora kila kitu kwenye kipande cha karatasi: barabara, kanisa, pinda kushoto hapa, X ni alama ya mahali pa hekalu. Aliuliza kile tulichokipata. Tulimwambia hangeweza kuchagua miliki yenye ugumu sana. Ilikuwa ikimilikiwa na watu watatu: mmoja kutoka Kanada, mmoja kutoka India, na mmoja kutoka China! Na haikuwa na maeneo muhimu ya kidini.

“Vema, fanyeni yote muwezayo,” alisema.

Kisha miujiza ikatokea. Ndani ya miezi kadhaa tulipata umiliki, na baadaye jiji la Langley, British Columbia, lilitoa idhini ya kujenga hekalu.

Picha
Hekalu la Vancouver British Columbia

Katika kutafakari uzoefu huu, ninanyenyekezwa na utambuzi kwamba wakati mimi na Kaka Williams tulikuwa na elimu rasmi na miaka ya uzoefu katika miliki na ubunifu wa hekalu, Rais Hinckley hakuwa na mafunzo rasmi kama hayo; lakini alikuwa na kitu kikubwa zaidi: kipawa cha uonaji wa kinabii. Aliweza kuhisi pale hekalu la Mungu lingepaswa kusimama.

Bwana alipowaamuru Watakatifu wa mwanzo katika kipindi hiki cha maongozi ya Mungu kujenga hekalu, Yeye alitangaza:

“Bali acha nyumba ijengwe kwa jina langu kulingana na utaratibu ambao nitauonyesha kwao.

Na kama watu wangu hawatajenga kulingana na utaratibu ambao nitauonyesha … , sitaipokea kutoka mikononi mwao” (Mafundisho na Maagano 115:14–15).

Kama kwa Watakatifu wa mwanzo, ndivyo ilivyo kwetu leo: Bwana amefunua na anaendelea kufunua kwa Rais wa Kanisa mpangilio ambao ufalme wa Mungu unapaswa kuelekezwa katika siku yetu. Na, katika ngazi ya mtu binafsi, anatoa mwongozo wa jinsi kila mmoja wetu tunapaswa kuelekeza maisha yetu, ili kwamba mienendo yetu kadhalika ikubalike kwa Bwana.

Mnamo Aprili 2013 nilizungumza kuhusu juhudi zinazotumika katika matayarisho na kuimarisha msingi wa kila hekalu kuhakikisha kwamba litashinda dhoruba na majanga ambayo litapatwa nayo. Lakini msingi ni mwanzo tu. Hekalu linatengenezwa kwa matofali mengi ya kujengea, yakikazwa pamoja kulingana na mpangilio uliobuniwa kabla. Kama maisha yetu yanakuwa mahekalu kila mmoja wetu anajitahidi kujenga kama ilivyofundishwa na Bwana (ona 1 Wakorintho 3:16–17), tungejiuliza wenyewe, “Ni matofali gani ya kujengea tunapaswa kuyaweka ili kuyafanya maisha yetu ya kupendeza, matukufu, na kinzani kwa dhoruba za ulimwengu?”

Tunaweza kupata jibu la swali hili katika Kitabu cha Mormoni. Kuhusu Kitabu cha Mormoni, Nabii Joseph Smith alisema: “Niliwaambia ndugu kwamba Kitabu cha Mormoni ndicho kitabu sahihi duniani, na ndicho jiwe la katikati la tao la dini yetu, na kuwa mwanadamu angemkaribia Mungu zaidi kwa kufuata mafunzo yake, zaidi ya kitabu kingine” (dibaji ya Kitabu cha Mormoni). Katika dibaji ya Kitabu cha Mormoni, tunafundishwa kuwa “wale ambao wanapata ushuhuda huu mtakatifu kutokana na Roho Mtakatifu kwamba Kitabu cha Mormoni ni neno la Mungu watajua pia kutokana na huo uwezo kwamba Yesu Kristo ndiye Mwokozi wa ulimwengu, na kwamba Joseph Smith ndiye mfunuzi na nabii wake wa Urejesho, na kwamba Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ndilo ufalme wa Bwana ambao umejengewa mara nyingine hapa ulimwenguni.”

Haya kisha ni baadhi ya matofali muhimu ya kujengea ya imani na ushuhuda wetu binafsi:

  1. Yesu Kristo ni Mwokozi wa ulimwengu.

  2. Kitabu cha Mormoni ni neno la Mungu.

  3. Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni ufalme wa Mungu duniani.

  4. Joseph Smith ni nabii, na tuna manabii wanaoishi duniani leo.

Katika miezi ya karibuni, nimesikiliza kila hotuba ya mkutano mkuu ambayo Rais Nelson ametoa tangu alipoitwa mwanzo kama Mtume. Zoezi hili limebadilisha maisha yangu. Nilipojifunza na kutafakari miaka 34 ya mkusanyiko wa hekima ya Rais Nelson, dhamira za uwazi na uthabiti zimedhihirika kutokana na mafundisho yake. Kila moja ya dhamira hizi zinahusiana na matofali hayo ya kujengea yaliyotajwa punde au ni tofali lingine la msingi kwa mahekalu yetu binafsi. Yanajumuisha imani katika Bwana Yesu Kristo; toba; ubatizo kwa ondoleo la dhambi; kipawa cha Roho Mtakatifu; ukombozi wa wafu na kazi ya hekalu; kuifanya takatifu siku ya Sabato; anza na mwisho akilini; baki kwenye njia ya agano. Rais Nelson ameyazungumzia yote kwa upendo na bidii.

Jiwe kuu la pembeni na tofali la kujengea la Kanisa na la maisha yetu ni Yesu Kristo. Hili ni Kanisa Lake. Rais Nelson ni nabii Wake. Mafundisho ya Rais Nelson yanashuhudia na kufunua kwa faida yetu maisha na sifa ya Yesu Kristo. Anazungumza kwa upendo na kwa kujua juu ya uhalisia wa Mwokozi na huduma Yake. Yeye pia ametoa ushuhuda wa kila mara na wa dhati juu ya wito mtakatifu wa manabii wanaoishi—Marais wa Kanisa—ambao chini yao ametumikia.

Sasa, leo, ni fursa yetu kumuunga mkono yeye kama nabii wa Bwana anayeishi duniani. Tumezoea kuwaunga mkono viongozi wa Kanisa kupitia mpangilio mtakatifu wa kuinua mikono yetu juu kuonyesha ukubali na usaidizi wetu. Tumefanya hili dakika chache tu zilizopita. Lakini kuunga mkono kwa kweli kunaenda vema zaidi ya ishara hii ya nje. Kama ilivyokumbushwa katika M&M 107:22, Urais wa Kwanza unapaswa “kuungwa mkono kwa kuaminiwa, imani, na sala ya kanisa.” Tunakuja kwa ukamilifu na kwa uhakika kumuunga mkono nabii anayeishi pale tunapojenga mpangilio wa kuamini katika maneno yake, kuwa na imani ya kuyafanyia kazi, na kisha kuomba kwa ajili ya baraka endelevu za Bwana juu yake.

Ninapomfikiria Rais Russell M. Nelson, ninapata faraja katika maneno ya Mwokozi aliposema, “Na kama watu wangu wataisikiliza sauti yangu, na sauti ya watumishi wangu ambao nimewateua kuwaongoza watu wangu, tazama, amini ninawaambia, wao hawataondoshwa kutoka mahali pao” (Mafundisho na Maagano 124:45).

Kuwasikiliza na kuwatii manabii wanaoishi kutakuwa na matokeo makubwa, hata ya athari za kubadili maisha katika maisha yetu. Tunaimarishwa. Tunahikishiwa zaidi na kuwa na imani katika Bwana. Tunasikia neno la Bwana. Tunahisi upendo wa Mungu. Tutajua jinsi ya kusimamia maisha yetu kwa lengo.

Ninampenda na kumuunga mkono Rais Russell M. Nelson pamoja na wengine ambao wameitwa kama manabii, waonaji, na wafunuzi. Ninashuhudia kwamba ana vipawa Bwana alivyoweka juu ya kichwa chake, na ninatoa ushahidi kwamba tunapoimarisha katika maisha yetu utamaduni wa kusikiliza na kutii sauti ya manabii wanaoishi, maisha yetu yatajengwa kulingana na mpangilio mtakatifu wa Bwana kwa ajili yetu, na tutavuna baraka za milele. Mwaliko umetolewa kwa wote. Njoo, usikie sauti ya nabii; ndio, njoo kwa Kristo na uishi. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.

Chapisha