Wataka Kuwa Mzima?
Kwa sababu ya Upatanisho wa Yesu Kristo, kama tutachagua kutubu na kuigeuza mioyo yetu yote kwa Mwokozi, Atatuponya kiroho.
Miezi michache kwenye misheni yake, kijana wetu wa mwisho na mmisionari mwenzake walikuwa wanamaliza kusoma wakati kijana wetu alipohisi maumivu kiasi ya kichwa. Alihisi tofauti sana; kwanza hakuweza kuudhibiti mkono wake wa kushoto, kisha ulimi wake ukafa ganzi. Upande wa kushoto wa uso wake ulianza kuinama. Alipata tabu kuzungumza. Alijua kitu fulani kilikuwa hakiko sawa. Kile ambacho hakujua ni kwamba alikuwa katikati ya kiharusi kikubwa katika maeneo matatu ya ubongo wake. Woga ukaanza kuingia alipoanza kupooza kwa sehemu. Jinsi gani kwa haraka mgonjwa wa kiharusi anaweza kupokea uangalizi kunaweza kuwa na matokeo mazuri katika uponaji wake. Mmisionari mwenzake mwaminifu alifanya uamuzi wa haraka. Baada ya kupiga 911 alimpa baraka. Kimiujiza, gari la wagonjwa lilikuwa umbali wa mwendo wa dakika tano tu.
Baada ya kijana wetu kukimbizwa hospitali, madakatari haraka walichunguza hali ilivyo na waliamua kutoa dawa kwa kijana wetu ambayo ingeweza kugeuza athari ya kupooza kutokana na kiharusi baada ya muda.1 Hata hivyo, kama kijana wetu hangekuwa na kiharusi, dawa ingeweza kuwa na madhara makubwa, kama vile kuvuja kwa damu kwenye ubongo. Kijana wetu alipaswa kuchagua. Alichagua kukubali tiba. Wakati kupona kamili kulihitaji upasuaji zaidi na miezi mingi, kijana wetu hatimaye alirudi na alimaliza misheni yake baada ya athari za kiharusi chake kupona kwa uthabiti.
Baba yetu wa Mbinguni ni mwenye uwezo wote na anajua yote. Anajua masumbuko yetu ya kimwili. Yeye anafahamu maumivu yetu ya kimwili kutokana na kuumwa, ugonjwa, uzee, ajali, au ulemavu wa kuzaliwa. Yeye anafahamu juu ya masumbuko ya kihisia yanayohusiana na wasiwasi, upweke, mfadhaiko, au ugonjwa wa akili. Yeye anamjua kila mtu aliyeteseka na uonevu au ambaye amenyanyaswa. Yeye anajua mapungufu yetu na hulka na majaribu tunayosumbuka nayo.
Wakati wa maisha haya ya muda tunajaribiwa ili kuona kama tutachagua mema dhidi ya mabaya. Kwa wale wanao tii amri zake, wataishi pamoja Naye “katika hali ya furaha ambayo kamwe-haina mwisho.”2 Kutusaidia katika uendeleaji wetu kuwa kama Yeye, Baba wa Mbinguni amempa uwezo na maarifa yote Mwanae, Yesu Kristo. Hakuna ugonjwa wowote wa kimwili, kihisia, au kiroho ambao Kristo haweza kuuponya.3
Wakati wa huduma ya Mwokozi hapa duniani, maandiko yanasimulia matukio mengi ya kimiujiza ambapo Yesu Kristo alitumia nguvu zake takatifu kuwaponya wale ambao waliteseka kimwili.
Injili ya Yohana inasimulia hadithi ya mtu fulani ambaye alivumilia ugonjwa wa kudhoofisha kwa miaka 38.
“Yesu alipomwona huyu amelala, naye akijua ya kuwa amekuwa hali hiyo siku nyingi, alimwambia, Wataka kuwa mzima?”
Yule mtu dhaifu akajibu kwamba hapakuwa na yoyote karibu kumsaidia alipohitaji zaidi msaada huo.
“Yesu akamwambia, “Simama, jitwike godoro lako, uende.
“Mara yule mtu akawa mzima, akajitwika godoro lake, akaenda.”4
Tafadhali zingatia ulinganifu wa muda ambao mtu huyu aliteseka peke yake—miaka 38—na jinsi kwa haraka uponyaji ulivyokuja mara tu Mwokozi alipohusika. Uponyaji ulikuwa “mara moja.”
Katika mfano mwingine, mwanamke mwenye kutokwa damu kwa miaka 12, ambaye “aliyekuwa amegharimiwa mali zake zote kwa kuwapa waganga, … alikwenda nyuma ya Yesu, akaugusa upindo wa vazi lake: na mara hiyo kutoka damu kwake [kulikoma]. …
“Yesu akasema, Mtu alinigusa: maana naona ya kuwa nguvu zimenitoka.
“Yule mwanamke, alipoona ya kwamba hawezi kusitirika … akamweleza mbele ya watu wote … jinsi alivyoponywa mara.”5
Kupitia huduma Yake, Kristo alifundisha kwamba Alikuwa na uwezo juu ya mwili. Hatuwezi kudhibiti mpangilio wa muda wa lini uponyaji wa Kristo wa maradhi ya mwili utatokea. Uponyaji hutokea kulingana na mapenzi na hekima Yake. Katika maandiko, baadhi waliteseka kwa miongo mingi; wengine, maisha yao yote duniani. Udhaifu wa kidunia unaweza kututakasa na kuongeza utegemezi wetu kwa Mungu. Lakini wakati tunapo mruhusu Kristo kuhusika, mara zote atatuimarisha kiroho ili tuwe na uwezo mkubwa wa kuvumilia mizigo yetu.
Hatimaye, tunajua kwamba kila maradhi ya kimwili, ugonjwa, au mapungufu yataponywa katika Ufufuko. Hiyo ni zawadi kwa wanadamu wote kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo.6
Yesu Kristo anaweza kuponya zaidi ya hata miili yetu. Anaweza kuponya roho zetu pia. Katika maandiko tunajifunza jinsi Kristo alivyowasaidia wale ambao roho zao zilikuwa dhaifu na kuwafanya wazima,7 Tunapo tafakari uzoefu huu, mategemeo yetu na imani katika uwezo wa Mwokozi kubariki maisha yetu huongezeka. Yesu Kristo anaweza kubadilisha mioyo yetu, kutuponya dhidi ya matokeo ya uonevu au manyanyaso tunayoweza kuyapitia, na kuimarisha uwezo wetu wa kubeba hasara na maumivu ya moyo, akituletea amani ya kutusaidia kuvumilia majaribu ya maisha yetu, akituponya kihisia.
Kristo pia anaweza kutuponya pale tunapotenda dhambi. Tunatenda dhambi pale kwa kujua tunapovunja moja ya sheria za Mungu.8 Tunapotenda dhambi, nafsi yetu huwa chafu. Na hakuna kitu kichafu kinachoweza kuishi katika uwepo wa Mungu.9 “Kuwa msafi kutoka kwenye dhambi ni kuponywa kiroho.”10
Mungu Baba anajua tutatenda dhambi, lakini Ameandaa njia kwa ajili yetu ya kukombolewa. Mzee Lynn G. Robbins alifundisha: Toba sio mpango wa [Mungu] wa akiba katika tukio tunaloweza kushindwa. Toba ni mpango Wake, akijua kwamba tutashindwa.”11 Tunapotenda dhambi, tunakuwa na fursa ya kuchagua mema au maovu. Tunachagua mema wakati tunapotubu baada ya kufanya dhambi. Kupitia Yesu Kristo na dhabihu Yake ya Upatanisho, tunaweza kukombolewa kutoka kwenye dhambi zetu na kurudishwa kwenye uwepo wa Mungu Baba kama tukitubu. Uponywaji wa kiroho sio wa upande mmoja—unahitaji uwezo wa ukombozi wa Mwokozi na toba ya kweli kwa upande wa mwenye dhambi. Kwa wale wanaochagua kutotubu, wanakataa uponyaji Kristo anaotoa. Kwao, nikama vile hakuna ukombozi uliofanywa.12
Nilipo shauriana na wengine waliotafuta kutubu, Nilishangazwa kwamba watu waliokuwa wakiishi katika dhambi walikuwa na wakati mgumu kafanya maamuzi yaliyo sahihi. Roho Mtakatifu angewaacha, na mara nyingi walihangaika kufanya maamuzi ambayo yangewaleta karibu zaidi na Mungu. Wangehangaika kwa miezi au hata miaka, wakiona aibu au kuogopa juu ya matokeo ya dhambi zao. Mara nyingi walihisi kwamba wasingeweza kubadilika au kusamehewa. Mara nyingi niliwasikia wakishiriki hofu yao kwamba kama wapendwa wao wangejua kile walichofanya,wangeacha kuwapenda au kuwatenga. Wakati walipofuata mwelekeo huu wa kufikiri, waliamua kunyamaza tu na kuchelewesha toba yao. Walihisi kimakosa kwamba ilikuwa vyema kutotubu sasa ili kwamba wasiendelee kuwaumiza zaidi wale walio wapenda. Katika mawazo yao ilikuwa ni bora zaidi kuteseka baada ya maisha haya kuliko kupitia njia ya toba sasa. Akina kaka na akina dada, kamwe si wazo zuri kucheleweasha toba yako. Adui mara nyingi hutumia woga kutuzuia kutenda mara moja juu ya imani yetu katika Yesu Kristo.
Wakati wapendwa wetu wanapokabiliwa na ukweli kuhusu tabia ya dhambi, wakati wanaweza kuhisi kuumizwa sana, mara nyingi wanataka kumsaidia mwenye kutubu kwa dhati kubadilika na kupatana na Mungu. Kwa kweli, uponyaji wa kiroho unaharakishwa wakati mwenye dhambi anaungama na kuzungukwa na wale wanaowapenda na kuwasaidia kuacha dhambi zao. Tafadhali kumbuka kwamba Yesu Kristo ni mwenye nguvu pia katika jinsi anavyowaponya wahanga wasio na hatia ya dhambi ambao Humgeukia.13
Rais Boyd K. Packer alisema: “Roho zetu huaribika tunapotenda makosa na dhambi. Lakini tofauti na miili yetu, wakati mchakato wa toba unapokamilika, hakuna makovu yanayobaki kwa sababu ya Upatanisho wa Yesu Kristo. Ahadi ni: ‘Tazama, yule ambaye ametubu dhambi zake, huyu anasamehewa, na Mimi, Bwana, sizikumbuki tena’ [Mafundisho na Maagano 58:42].”14
Tunapotubu kwa “kwa lengo kuu la moyo,” “15 “mara moja mpango mkuu wa ukombozi utafanya kazi” katika maisha yetu.16 Mwokozi atatuponya.
Mmisionari mwenza na madaktari bingwa waliomsaidia kijana wetu aliyeteseka kwa kiharusi katika eneo la misheni walifanya haraka. Kijana wetu alichagua kupokea dawa ya kutibu kiharusi. Athari za kupooza za kiharusi chake ambazo zingemfuata katika muda wote uliobaki wa maisha yake ya hapa dunuani zilitibiwa. Vivyo hivyo, haraka tunapotubu na kuleta Upatanisho wa Yesu Kristo kwenye maisha yetu, ndipo mapema tunavyoweza kuponywa kutokana na madhara ya dhambi.
Rais Russell M. Nelson alitoa mwaliko huu: “Kama umetoka nje ya njia, … ninakualika … tafadhali rudi. Bila kujali wasiwasi wako wowote, changamoto zako zozote, kuna nafasi yako katika hili, Kanisa la Bwana. Wewe na vizazi ambavyo bado havijazaliwa vitabarikiwa kwa matendo yako ya sasa ya kurudi kwenye njia ya agano.”17
Uponaji wetu wa kiroho unatuhitaji sisi kujitoa wenyewe kwenye hali ambayo Mwokozi wetu ametueleza. Hatutakiwi kuchelewa! Lazima tufanye leo! Fanya sasa ili kwamba kupooza kiroho kusizuie maendeleo yako ya milele. Wakati nikiwa nazungumza, kama umehisi haja ya kuomba msamaha kwa mtu fulani uliyemkosea, ninakualika kufanya hivyo. Waambie kile ulichokifanya. Omba msamaha. Kama umefanya dhambi ambayo inaathiri ustahili wako wa hekaluni, ninakualika kushauriana na askofu wako—leo. Usichelewe.
Akina kaka na dada zangu, Mungu ni Baba yetu anayetupenda wa Mbinguni. Ametoa uwezo wote na maarifa kwa Mwanae Mpendwa, Yesu Kristo. Kwa sababu Yake, wanadamu wote siku moja wataponywa kila maradhi ya mwili milele. Kwa sababu ya Upatanisho wa Yesu Kristo, kama tutachagua kutubu na kuigeuza mioyo yetu yote kwa Mwokozi, Atatuponya kiroho. Uponyaji huo unaweza kuanza mara moja. Uchaguzi ni wetu. “Je Tunataka kuwa wazima?
Ninashuhudia kuwa Yesu Kristo alilipa gharama ili kwamba tuweze kuwa wazima. Lakini lazima tuchague kuchukua dawa ya uponyaji anayotoa. Ichukue sasa. Usichelewe. Katika jina la Yesu Kristo, amina.