Wazazi na Watoto
Mpango mkuu wa furaha wa Baba yetu wa Mbinguni unakuambia wewe ni nani na lengo la maisha yako ni nini.
Dada zangu wapendwa, jinsi gani inapendeza kuwa na kikao hiki kipya cha mkutano mkuu wa wanawake wa Kanisa wa miaka minane na zaidi. Tumesikia jumbe zenye mwongozo kutoka kwa akina dada viongozi na kutoka kwa Rais Henry B. Eyring. Rais Eyring pamoja nami tunapenda kufanya kazi chini ya uelekezi wa Rais Russell M. Nelson, na tunatazamia hotuba yake ya kinabii.
I.
Watoto ni zawadi yetu ya thamani kubwa kutoka kwa Mungu—ongezeko letu la milele. Lakini bado, tunaishi katika kipindi ambacho wanawake wengi wanatamani kutokuwa sehemu ya uzazi na ulezi wa watoto. Vijana wengi wadogo huchelewesha ndoa mpaka mahitaji ya kidunia yatoshelezwe. Wastani wa umri wa ndoa za WSM umeongezeka kwa zaidi ya miaka miwili, na idadi ya uzazi kwa waumini wa Kanisa inashuka. Marekani na baadhi ya mataifa mengine yanakabiliwa na wakati ujao wa watoto wachache mno wanaopevuka kwenye utu uzima kusaidia idadi kubwa ya watu wazima wanaostaafu.1 Zaidi ya asilimia 40 ya uzazi katika Marekani ni kwa kina mama wasio katika ndoa. Watoto hao sio salama. Kila moja ya mitindo hii hukinzana na mpango mtakatifu wa wokovu wa Baba yetu.
II.
Wanawake Watakatifu wa Siku za Mwisho wanaelewa kwamba kuwa mama ni kipaumbele chao cha juu, furaha yao kuu. Rais gGordon B. Hinckley alisema: “Wanawake kwa sehemu kubwa huona mafanikio yao makubwa, furaha yao kuu katika nyumba na familia. Mungu ameweka ndani ya wanawake kitu kitakatifu ambacho kinajielezea chenyewe katika nguvu tulivu, katika utakaso, katika amani, katika wema, katika maadili, katika ukweli, katika upendo. Na sifa hizi zote zisizo kifani hupata ukweli wake na onyesho lake la kuridhisha katika umama.”
Aliendelea, “Kazi kubwa zaidi ambayo mwanamke yeyote atawahi kufanya itakuwa katika kulea na kufundisha na kuishi na kutia moyo na kuwalea watoto wake katika haki na kweli. Hakuna kitu kingine ambacho kitalingana na hilo, bila kujali kile anachofanya.”2
Akina mama, akina dada wapendwa, tunawapenda kwa vile mlivyo na kile mnachofanya kwetu sote.
Katika hotuba yake muhimu ya 2015 yenye kichwa cha habari “Ombi kwa Dada Zangu,” Rais Russell M. Nelson alisema:
“Ufalme wa Mungu si kamili na hauwezi kukamilika bila wanawake wanaofanya maagano matakatifu, na kuyashika, wanawake wanaoweza kusema kwa uwezo na mamlaka ya Mungu!
“Leo, … tunahitaji wanawake ambao wanajua jinsi ya kufanya vitu muhimu vitendeke kwa imani yao na ambao ni watetezi jasiri wa maadili na familia katika dunia iliyozagaa dhambi. Tunahitaji wanawake waliojitolea kulea watoto wa Mungu kwenye njia ya agano kuelekea kuinuliwa; wanawake ambao wanajua jinsi ya kupokea ufunuo binafsi, wanaoelewa uwezo na amani ya endaumenti ya hekaluni; wanawake wanaojua jinsi ya kuomba nguvu za mbinguni kulinda na kuimarisha watoto na familia; wanawake wanaofundisha bila woga.”3
Mafundisho haya yenye msukumo yote yamejikita kwenye “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu,” ambalo kwalo Kanisa hili la urejesho hudhihirisha mafundisho na utendaji ulio kiini cha mpango wa Muumba kabla ya Yeye kuumba dunia.
III.
Sasa ninazungumza na kundi chipukizi la hadhira hii. Dada zangu wapendwa chipukizi, kwa sababu ya ufahamu wenu wa injili ya urejesho ya Yesu Kristo, ninyi ni wa kipekee. Ufahamu wenu utawawezesha kustahimili na kushinda magumu ya ukuaji. Tangu umri mdogo, mmeshiriki katika miradi na mipango ambayo imekuza talanta zenu, kama vile kuandika, kuongea, na kupanga. Mmejifunza tabia za kuwajibika na jinsi ya kushinda majaribu ya kudanganya, ulaghai, au kutumia vileo au madawa.
Upekee wenu ulitambulika katika utafiti wa vijana na dini Marekani katika Chuo Kikuu. Makala ya Charlotte Observer ilikua na kichwa cha habari, “Vijana wa Kimormoni wanavumilia vyema: Utafiti unaonyesha wako juu ya wenzao kwenye kusimamia ubalehe.” Makala hii ilihitimisha kwamba “Wamormoni hufanya vizuri zaidi kwenye kuepuka tabia hatarishi, hufanya vizuri shuleni na kuwa na mtazamo chanya kuhusu siku zijazo. Mmoja wa watafiti katika utafiti huu, ambaye aliwahoji wengi wa vijana wetu, alisema, “kwenye karibu kila kundi tulilotazama, kulikuwa na mpangilio dhahiri: Wamormoni walikuwa wa kwanza.”4
Kwa nini mnavumilia vyema kwa magumu ya ukuaji? Wasichana, ni kwa sababu mnaelewa mpango mkuu wa furaha wa Baba yetu wa Mbinguni. Hii inakuambia ninyi ni kina nani na lengo la maisha yeni ni nini. Vijana wenye uelewa huo ni wa kwanza katika kutatua matatizo na wa kwanza katika kuchagua mema. Mnajua mnaweza kuwa na msaada wa Bwana katika kushinda magumu yote ya ukuaji.
Sababu nyingine kwa nini mko vizuri zaidi ni kwamba mnaelewa kwamba ninyi ni watoto wa Baba wa Mbinguni anayewapenda. Nina uhakika mnaufahamu wimbo wetu mkuu “Watoto Wapendwa, Mungu Yu Karibu Nanyi.” Hapa ni ubeti wa kwanza ambao wote tumeimba na kuamini:
Watoto wapendwa, Mungu yu karibu nanyi,
Akiwalinda mchana na usiku,
Na hufurahia kuwamiliki na kuwabariki,
Kama mtajitahidi kutenda mema.5
Kuna mafunzo mawili katika ubeti huo: Kwanza, Baba yetu wa Mbinguni yu karibu nasi na hutulinda mchana na usiku. Fikiria hilo! Mungu anatupenda, Yeye yu karibu nasi, na Yeye hutulinda. Pili, Yeye hufurahia kutubariki “tunapojitahidi kutenda mema.” Faraja iliyoje katikati ya wasiwasi na matatizo!
Ndiyo, wasichana, mmebarikiwa na ninyi ni wazuri, lakini ninyi ni kama watoto wote wa Baba wa Mbinguni katika hitaji lenu la “kujitahidi kutenda mema.”
Hapa ninaweza kuwapa ushauri katika mambo mengi tofauti, lakini nimechagua kuongelea mawili tu.
Ushauri wangu wa kwanza unahusu simu za mkononi. Uchunguzi wa karibuni wa kitaifa umegundua kwamba zaidi ya nusu ya vijana wa Marekani walisema walitumia muda mwingi zaidi kwenye simu zao za mkononi. Zaidi ya asilimia 40 walisema walihisi wasiwasi pale walipotenganishwa na simu zao za mkononi.6 Hili lilikuwa kawaida zaidi kwa wasichana kuliko wavulana. Dada zangu chipukizi—na wanawake wakubwa pia—itabariki maisha yenu kama mtapunguza matumizi na utegemezi wenu kwenye simu za mkononi.
Ushauri wangu wa pili ni muhimu zaidi. Kuweni wakarimu kwa wengine. Ukarimu ni kitu wengi wa vijana wetu tayari wanafanya. Baadhi ya makundi ya vijana katika jamii yameonyesha njia kwetu sote. Tumepata msukumo kwa matendo ya vijana ya ukarimu kwa wale wenye hitaji la upendo na msaada. Katika njia nyingi mnatoa msaada huo na kuonyesha upendo huo kwa kila mmoja wenu. Tunatamani sote tungefuata mfano wenu.
Wakati huo huo, tunajua kwamba adui hutushawishi sisi sote kutokuwa wakarimu, na bado kuna mifano mingi ya hili, hata kati ya watoto na vijana. Kutokuwa na ukarimu kunakoendelea kunajulikana kwa majina mengi, kama vile uonevu, kumpangia mtu njama, au kujiunga pamoja kuwakataa wengine. Mifano hii kwa kudhamiria huleta maumivu kwa wanafunzi wenza au marafiki. Dada zangu chipukizi, haimpendezi Bwana kama tu wadhalimu au wakatili kwa wengine.
Hapa kuna mfano. Ninamfahamu kijana mdogo, mkimbizi hapa Utah, aliyefanyiwa mzaha kwa kuwa tofauti, ikijumuisha wakati mwingine kuongea lugha yake ya asili. Aliteswa na genge la vijana matajiri mpaka akalipiza kisasi katika njia ambayo ilimfanya kufungwa jela kwa zaidi ya siku 70 wakati akifikiriwa kufukuzwa nchini. Sijui nini kilichochea kundi hili la vijana, wengi wao Watakatifu wa Siku za Mwisho kama ninyi, lakini naweza kuona athari ya ukatili wao, uzoefu wa huzuni na gharama kwa mmoja wa watoto wa Mungu. Matendo madogo ya kukosa ukarimu yanaweza kuwa na matokeo mabaya.
Niliposikia hadithi hiyo, niliilinganisha na kile nabii wetu, Rais Nelson, alikisema katika ibada ya karibuni wa ulimwengu kote wa vijana. Katika kuwaomba ninyi na vijana wengine wote kusaidia katika kukusanya Israeli, alisema: “Tokeza; kuwa tofauti na ulimwengu. Mimi na ninyi tunajua kwamba tunapaswa kuwa nuru ya ulimwengu. Kwa hivyo, Bwana anahitajimuonekane kama, mseme kama, mtende kama, na mvae kama mfuasi wa kweli wa Yesu Kristo.”7
Batalioni ya vijana Rais Nelson aliyowaalika mjiunge haitakuwa na ukatili kati mmoja kwa mwingine. Watafuata mafundisho ya Mwokozi kufikia na kuwa wenye upendo na kuwajali wengine, hata kugeuza shavu la pili wakati tunapohisi mtu fulani ametukosea.
Katika hotuba ya mkutano mkuu karibia kipindi wengi wenu milikuwa mmezaliwa, Rais Gordon B. Hinckley aliwasifu “wasichana wazuri ambao wanajitahidi kuishi injili.” Aliwaelezea, kama vile ninavyohisi kuwaelezea:
“Ni wakarimu kwa kila mmoja. Wanatafuta kuimarishana kila mmoja. Wao ni muamana kwa wazazi wao na katika nyumba wanazotoka. Wanakaribia uanamke na watabeba katika maisha yao yote mifano bora ambayo kwa sasa inawapa hamasa.”8
Kama mtumishi wa Bwana, ninasema kwenu wasichana, ulimwengu wetu unahitaji wema na upendo wenu. Kuweni wakarimu kwa kila mmoja wenu. Yesu alitufundisha kupendana na kuwatendea wengine kama vile tunavyotaka tutendewe. Tunapojitahidi kuwa wakarimu, tunasogea karibu na Yeye na ushawishi Wake wa upendo.
Dada zangu wapendwa, kama mnashiriki katika ukatili wowote au mambo ya upuuzi—kibinafsi au na kundi—amueni sasa kubadilika na wahimizeni wengine wabadilike. Huo ndiyo ushauri wangu, na ninautoa kwenu kama mtumishi wa Bwana Yesu Kristo kwa sababu Roho Wake amenisukuma kuzungumza nanyi kuhusu mada hii muhimu. Nashuhudia juu ya Yesu Kristo, Mwokozi wetu, ambaye ametufundisha kupendana kama Yeye alivyotupenda. Ninaomba kwamba tutafanya hivyo katika jina la Yesu Krist, amina.