Imara na Thabiti kwenye Imani ya Kristo
Kuvumilia kuwa imara na thabiti kwenye imani ya Kristo kunahitaji kwamba injili ya Yesu Kristo iweze kupenya moyo na nafsi ya mtu.
Katika historia ya Agano la Kale, tunasoma kuhusu vipindi mfululizo wakati wana wa Israeli waliheshimu agano lao na Yehova na kumwabudu na yakati zingine ambapo walipuuza agano hilo na kuabudu sanamu au Baalimu.1
Utawala wa Ahabu ulikuwa mojawapo ya kipindi cha kupotoka katika ufalme wa Israeli wa Kaskazini. Nabii Eliya kwa wakati mwingine alimwambia Mfalme Ahabu kukusanya wana wa Israeli pamoja na manabii au makuhani wa Baali kwenye Mlima wa Karmeli Watu walipokuwa wamekusanyika, Eliya akanena “Mtasita-sita katikati ya mawazo mawili hata lini? [Kwa maana nyingine, “Mtaamua lini kabisa?”] Bwana akiwa ndiye Mungu, mfuateni; bali ikiwa Baali ni Mungu, haya! Mfuateni yeye. Wale watu hawakumjibu neno.2 Kwa hivyo Eliya akamuru kuwa yeye na manabii wa Baali wamkatekate yule ndume mchanga na kumweka juu ya kuni katika madhabu yao ila “wasitie moto ndani.”3 Kisha, “ombeni kwa jina la miungu yenu, nami nitaomba kwa jina la Bwana; na Mungu yule ajibuye kwa moto, na awe ndiye Mungu. Watu wote wakajibu wakasema, Maneno haya ni mazuri.4
Mtakumbuka kwamba makuhani wa Baali walifanya makelele kwa mungu wao asiyekuwepo kwa masaa ili atume moto chini, lakini “hapakuwa na sauti, wala aliyejibu wala aliyeangalia.5 Ilipofika zamu ya Eliya, alirekebisha madhabahu ya Bwana yaliyokuwa yamevunjika, akaweka kuni, na dhabihu juu yake, kisha akaamuru maji yamwagiliwe humo, si mara moja, wala mara mbili, lakini mara tatu. Hapakuwa na tashwishi kuwa si yeye wala nguvu zingine zozote za kibinadamu zingeweza kuwasha moto.
“Ikawa, wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, Eliya nabii akakaribia, akasema, Ee Bwana, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, na ijulikane leo ya kuwa wewe ndiwe Mungu katika Israeli, na ya kuwa mimi ni mtumishi wako, na ya kuwa nimefanya mambo haya yote kwa neno lako. …
Ndipo moto wa Bwana ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, na mavumbi, ukayaramba yale maji yaliyokuwamo katika mfereji.
Na watu wote walipoona, wakaanguka kifudifudi; wakasema, Bwana ndiye Mungu, Bwana ndiye Mungu.6
Hivi leo Eliya angesema:
-
Iwe Mungu, Baba yetu wa Mbinguni anaishi au haishi, lakini kama Anaishi, mwabuduni Yeye.
-
Ama, Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu, Mkombozi aliyefufuka wa Wanadamu, au siye, lakini kama ndiye, Mfuateni.
-
Ama, Kitabu cha Mormoni ni neno la Mungu au siyo, lakini kikiwa, basi, “mkaribie Mungu zaidi kwa kufuata mafunzo yake.”7
-
Ama, Joseph Smith aliwaona na kuzungumza na Baba na Mwana siku hiyo ya msimu wa kuchipua ya 1820 au hakufanya hivyo, lakini kama alifanya, basi fuata joho la kinabii pamoja na funguo za kufungisha ambazo mimi Eliya nilimtunukia.
Kwenye mkutano mkuu wa hivi majuzi zaidi Rais Russell M. Nelson alitangaza: Hupaswi kuona shani kuhusu kilicho kweli [Ona Moroni 10:5]. Hupaswi kuwa na shani nani unaweza kumwamini kiusalama. Kupitia kwa ufunuo binafsi, unaweza kupokea ushahidi wako mwenyewe kwamba Kitabu cha Mormoni ni neno la Mungu, kwamba Joseph Smith ni nabii, na kwamba hili ni Kanisa la Bwana. Licha ya kile wengine wanaweza kusema au kufanya, hakuna hata mmoja anayeweza kamwe kuutoa ushahidi uliotolewa kwenye moyo wako na akili kuhusu kilicho kweli.8
Wakati Yakobo alipoahidi kwamba Mungu “awapa wote, kwa ukarimu” wanaotafuta hekima9 pia alionya:
“Ila na aombe kwa imani, pasipo shaka. Maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku.
“Maana mtu kama yule asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa Bwana.
“Mtu wa nia mbili husita-sita katika njia zake zote.10
Mwokozi wetu kwa upande mwingine, alikuwa mfano mkamilifu wa uthabiti Alisema “Baba hakuniacha peke yangu; kwa sababu nafanya siku zote yale yampendezayo”11 Fikiria maelezo haya kutoka kwa maandiko juu ya wanaume na wanawake, kama Mwokozi, walikuwa imara na thabiti.
Walikuwa “waliogeukia imani ya kweli; na hawangeiacha, kwani walikuwa imara, na thabiti na wasiotingishika, na wanaotamani kwa bidii yote kutii amri za Bwana.”12
“Akili zao ni imara, na wanaweka matumaini yao kwa Mungu siku zote.”13
“Na tazama, mnajua wenyewe, kwani mmejionea, kwamba vile wengi wao wanaletwa kuelimishwa ukweli … wako imara na thabiti katika imani, na pia kitu ambacho kwacho wamefanywa huru.”14
“Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali.”15
Kuvumilia kuwa imara na thabiti kwenye imani ya Kristo kunahitaji kwamba injili ya Yesu Kristo iweze kupenya moyo na nafsi ya mtu, kumaanisha kuwa injili inakuwa si mojawapo ya athari katika maisha ya mtu bali kiini cha ufasili ya maisha na sifa yake. Bwana asema:
“Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama.
“Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda.
“Nanyi … mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu.”16
Hili ndilo agano tunaofanya katika ubatizo wetu na katika ibada za hekaluni. Lakini wengine bado hawajapata kikamilifu injili ya Yesu Kristo kwenye maisha yao Ingawa, kama Paulo asemavyo, “walizikwa pamoja naye [Kristo] kwa njia ya ubatizo,” bado wanakosa sehemu ambayo “kama Kristo alivyofufuka katoka kwa wafu … vivyo hivyo na sisi… tuenende katika upya wa uzima.”17 Injili bado haiwafasili. Bado hawajashikishwa tao katika Kristo. Wanachagua kuhusu mafundisho na amri watakayofuata na wapi na wakati watahudumu Kanisani. Kwa tofauti, ni kwa kuweka maagano yao kikamilifu ambapo wale “ambao ni wateule kulingana na agano”18 wanaepukana na udanganyifu na kubaki imara katika imani ya Kristo.
Wengi wetu tunajipata wakati kwenye mwendelezo kati ya ushiriki kwenye ibada zilizowekwa na jamii kwa upande mmoja na kujitoa kikamilifu kama Kristo kwa mapenzi ya Mungu kwa upande mwingine. Katika mahali fulani kwenye mwendelezo, habari njema ya injili ya Yesu Kristo huingia ndani ya mioyo yetu na kumiliki nafsi yetu. Inaweza kuwa isifanyike mara moja, lakini tunapaswa kuwa tunasonga mbele kuelekea hali hii iliyobarikiwa.
Ni changamoto lakini muhimu kubaki imara na thabiti tunapojipata tunasafishwa kwenye “tanuru ya mateso,”19 jambo ambalo huja mara au baadaye kwetu sote kwenye maisha ya duniani. Bila Mungu, uzoefu huu wa giza huelekea kwenye ukataji tamaa, kufa moyo na hata kuwa na machungu. Pamoja na Mungu, faraja huja badala ya uchungu, amani huja badala ya vurugu, na matumaini huja badala ya majonzi. Kusalia kuwa imara katika imani ya Kristo kutaleta neema itakayohimili na kusaidia na itabdilisha majaribu kuwa baraka20 Atabadilisha majaribu kuwa baraka na kwa maneno ya Isaya “wapewe taji ya maua badala ya majivu”21
Acha nitaje mifano mitatu ambayo kwayo mimi nina ufahamu wa kibinafsi:
Kuna mwanamke anayeumia kutokana na ugonjwa dondandugu unaodhoofisha licha ya matibabu, baraka ya ukuhani, kufunga na sala. Hata hivyo, katika nguvu za sala na uhalisi wa upendo wa Mungu kwake haujadidimia. Anajikaza akisonga mbele kila siku hadi siku (Na wakati mwingine saa hadi saa) akihudumu kama alivyoitwa Kanisani na, pamoja na mumewe, wakilea familia yao changa, akitabasamu awezavyo. Huruma yake ni ya kina, ikisafishwa na kuteseka kwake, na anajipoteza katika kuwahudumia wengine. Anaendelea kuwa thabiti, na watu wanahisi furaha kuwa karibu naye.
Mtu aliyekua Kanisani, akahudumu misheni ya wakati wote, na akamwoa mke mwema alishangaa wakati baadhi ya ndugu zake walipoanza kuzungumza kwa kukosoa Kanisa na Nabii Joseph Smith. Baada ya muda waliacha Kanisa na kujaribu kumshawishi kuwafuata. Kama ilivyo mara nyingi katika visa hivi, walimshambulia kwa insha, podkasti na video zilizotolewa na wakosoaji wa kanisa wengi ambao wenyewe walikuwa washiriki na kupoteza upendo kwa Kanisa. Ndugu zake walikashifu imani yake wakimwambia alikuwa amedanganywa na kupotoswa. Hakuwa na majibu kwa madai yao, na imani yake ikaanza kutikisika chini ya upinzani usiokoma. Alishangaa kama aache kuhudhuria kanisani. Alizungumza na mke wake. Alizungumza na watu aliowaamini. Alisali. Alitafakari katika hali ya usumbufu wa akilini mwake, alikumbuka nyakati ambapo alihisi Roho Mtakatifu na kupokea ushuhuda kwa Roho. Alihitimisha “Nikiwa mkweli kwangu mwenyewe, ni lazima nikubali kuwa Roho amenigusa zaidi ya mara moja na ushuhuda wa Roho ni halisi.” Ana hisia mpya ya furaha na amani inashirikiwa na mke wake na watoto.
Mume na mke ambao kidesturi na kwa furaha wamefuata ushauri wa akina Ndugu maishani mwao wamehuzunishwa na ugumu waliopata kwa kupata watoto. Walitumia fedha nyingi wakifanya kazi na madaktari waliohitimu, na baada ya muda, wao walibarikiwa na mwana. Kwa masikitiko hata hivyo, mtoto alikuwa mwathirika na ajali ambayo haikuwa kosa la mtu yeyote, ilimwacha akiwa bila fahamu pamoja na kuharibika kwa kiasi kikubwa kwa ubongo. Amepokea tunzo bora lakini madaktari hawawezi kutabiri jinsi mambo yatakavyokuwa hapo mbele. Mtoto ambaye wenzi walifanya kazi sana na kusali kwa bidii kumleta duniani kwa njia nyingine amechukuliwa na hawajui kama atarejeshwa kwao. Wanajitahidi sasa wanashughulikia mahitaji yake huku wakifanya majukumu yao mengine. Katika wakati huu mgumu sana, wamemgeukia Bwana. Wanategemea “mkate wa kila siku” wanaopokea kutoka kwake. Wanasaidiwa na marafiki na wanafamilia wenye huruma na kuimarishwa na nguvu za ukuhani. Wamesogeleana karibu, na umoja wao sasa una kina na mkamilifu kuliko pengine jinsi ingewezekana.
Mnamo Julai 23 1837 Bwana aliagiza ufunuo kuelekezwa kwa aliyekuwa wakati huo-Rais wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, Thomas B. Marsh. Ilijumuisha yafuatayo:
“Na uwaombee ndugu zako Kumi na Wawili. Waonye kwa nguvu kwa ajili ya jina langu, na acha waonywe kwa ajili ya dhambi zao zote, na muwe waminifu mbele zangu kwa jina langu.
Na baada ya majaribu yao, na taabu nyingi, tazama, Mimi, Bwana, nitawatafuta, na kama hawakuishupaza mioyo yao, na kuzikaza shingo zao dhidi yangu, wataongolewa, nami nitawaponya.22
Ninaamini kanuni kutoka kwa maisha yake zinatumika kwetu sote. Majaribu na mateso tunayokumbana nayo, pamoja na kujaribiwa ambako Bwana anaona vyema kutuwekea kunaweza kupelekea uongofu mkamilifu na uponyaji. Lakini hii hufanyika, ikiwa, na ikiwa tu, hatutafanya mioyo yetu kuwa migumu au wenye shingo ngumu dhidi yake. Tukisalia imara na thabiti kwa vyovyote vile, tunapata uongofu ambao Bwana alikusudia alipomwambia Petro: “Nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako,”23 uongofu mkamilifu ambao haiwezi kubadilishwa. Uponyaji ulioahidiwa ni usafishaji na atakasaji ya nafsi zetu zilizojeruhiwa na dhambi ili kutufanya watakatifu.
Ninakumbuka ushauri wa mama zetu: “Kula mboga yako, itakufaidi.” Akina mama ni sahihi na kwenye muktadha wa uthabiti katika imani “kula mboga zenu” ni kuomba kila mara, kula kutoka kwa maandiko kila siku, kuhumu na kuabudu Kanisani, kushiriki sakramenti ipasavyo kila wiki, kumpenda jirani yako na kuchukua msalaba wenu kwa utiifu kwa Mungu kila siku.24
Kumbuka kila wakati ahadi ya mema yajayo, sasa na baada ya hapa, kwa wale walio imara na thabiti katika imani ya Kristo. Kumbuka “maisha ya milele, na furaha ya watakatifu.”25 “Ee nyinyi nyote mlio safi moyoni, inueni vichwa vyenu na kupokea neno la kupendeza la Mungu, na kusherekea upendo wake; kwani mnaweza, kama mawazo yenu yatakuwa imara, daima.26 Katika jina la Yesu Kristo, amina.