2010–2019
Kuwa Mchungaji
Oktoba 2018


Kuwa Mchungaji

Ninatumaini wale mnaowahudumia watawaona kama rafiki na kutambua kwamba, ndani yenu, wanaye mshindi na mwandani.

Mwaka mmoja uliopita, mtoto wa Msingi niliyekutana naye Chile alileta tabasamu kwenye uso wangu. “Habari,” alisema, “Naitwa David. Je, utaongea kuhusu mimi kwenye mkutano mkuu?”

Katika muda mtulivu, nimetafakari salamu isiyotarajiwa ya David. Sisi sote tunataka kujulikana. Tunataka kuthaminiwa, kukumbukwa, na kujisikia kupendwa.

Akina dada na akina kaka, kila mmoja wenu ni wa thamani. Hata kama huongelewi kwenye mkutano mkuu, Mwokozi anakujua na anakupenda. Ikiwa unajiuliza kama hiyo ni kweli, unahitaji tu kutafakari kwamba “Amekuandika [wewe] kwenye viganja vya mikono [Yake].”1

Kujua kwamba Mwokozi anatupenda, tunaweza kujiuliza, ni kwa jinsi gani tunaweza kuonyesha upendo wetu Kwake?

Mwokozi alimuuliza Petro, “Je wanipenda …?”

Petro akajibu, “Ndio, Bwana; wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Lisha wana-kondoo wangu.”

Wakati alipoulizwa swali hili kwa mara ya pili na ya tatu, “Je wanipenda?” Petro, alihuzunika lakini alidhihirisha upendo wake: “Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa nakupenda. Yesu akamwambia, Lisha kondoo zangu.2

Kwani Petro hakuwa tayari amedhihirisha kuwa mwanafunzi mzuri wa Kristo? Tangu kukutana kwao kwa mara ya kwanza kwenye ufukwe, “mara moja” aliacha nyavu zake za uvuvi kumfuata Mwokozi.3 Petro akawa mvuvi wa kweli wa watu. Akafuatana na Mwokozi wakati wa huduma Yake na akasaidia kuwafundisha wengine injili ya Yesu Kristo.

Bali sasa Bwana aliyefufuka alijua hangeweza tena kuwa pembeni mwa Petro, akimwonyesha jinsi gani na wakati gani wa kutumikia. Bila ya uwepo wa Mwokozi, Petro angehitaji kupata mwongozo kutoka kwa Roho, kupokea maono mwenyewe, na kisha kuwa na ujasiri na imani ya kutenda. Akiwalenga kondoo Wake, Bwana alitaka Petro kufanya yale ambayo Angefanya kama Angekuwepo pale. Alimtaka Petro kuwa mchungaji.

Aprili iliyopita, Rais Russell M. Nelson alitoa mwaliko kama huo kwetu wa kuwalisha kondoo wa Baba yetu katika njia takatifu na kufanya hivyo kupitia kuhudumu.4

Ili kukubali kwa ufanisi mwaliko huu, tunapaswa kujenga moyo wa mchungaji na kuelewa mahitaji ya kondoo wa Bwana. Kwa hiyo tunawezaje kuwa wachungaji ambao Bwana anatuhitaji tuwe?

Kama ilivyo kwa maswali yote, tunaweza kumtazama Mwokozi wetu, Yesu Kristo—Mchungaji Mwema. Kondoo wa Bwana walijulikana na kuhesabika, walilindwa, na walikusanywa kwenye zizi la Mungu.

Kujulikana na Kuhesabika

Tukiwa tunajitahidi kufuata mfano wa Mwokozi lazima kwanza tuwajue na kuwahesabu kondoo Wake. Tumepewa watu na familia maalum kuwaangalia hivyo tuna uhakika kwamba kundi lote la Bwana linajulikana na hakuna mtu aliyesahaulika. Kuhesabu, hata hivyo, si hasa kuhusu idadi; ni kuhakikisha kila mtu anahisi upendo wa Mwokozi kupitia mtu fulani anayehudumu kwa ajili Yake. Kwa njia hiyo, wote wanaweza kugundua kwamba wanajulikana na Baba mpendwa wa Mbinguni.

Picha
Mwokozi na Mwanakondoo

Hivi karibuni nilikutana na msichana aliyepangwa kuhudumu kwa dada ambaye ana umri mara tano ya yeye. Kwa pamoja, wamegundua kupenda wote muziki. Wakati msichana huyu anapomtembelea, wanaimba nyimbo pamoja na wanashiriki wanazozipenda. Wameanzisha urafiki ambao hubariki maisha yao wote.

Ninatumaini wale mnaowahudumia watawaona kama rafiki na kutambua kwamba, ndani yenu, wanaye mshindi, na mwandani—mtu anayejua hali zao na kuwasaidia katika matumaini na matamanio yao.

Hivi karibuni nilipokea jukumu la kuhudumu kwa dada ambaye si mimi wala mwenza wangu tulimfahamu vizuri. Nikiwa nashauriana na Jess, mwenza wangu wa miaka 16, kwa busara alishauri, “Tunahitaja kumjua.”

Picha
Dada Cordon na mwenzi wake wa uhudumiaji

Mara moja tuliamua kwamba picha na maandishi ya utangulizi yalikuwa katika utaratibu. Nilishikilia simu, na Jess akabonyeza kitufe kupiga picha. Fursa yetu ya kwanza ya kuhudumu ilikuwa ni juhudi za pamoja.

Tulipotembelea kwa mara ya kwanza, tulimuuliza dada yetu iwapo kuna kitu chochote tunaweza kukijumuisha katika sala zetu kwa niaba yake. Alishiriki changamoto ororo binafsi na alisema angezikaribisha sana sala zetu. Uaminifu na ujasiri wake vilileta muunganiko wa upendo papo hapo. Ni fursa nzuri iliyoje kumkumbuka yeye katika sala zangu za kila siku.

Wakati unasali, utahisi upendo wa Yesu Kristo kwa wale unaowahudumia. Shiriki upendo huo pamoja nao. Ni njia gani nzuri ya kuwalisha kondoo Wake zaidi ya kuwasaidia kuhisi upendo Wake—kupitia wewe?

Kuangaliwa

Njia ya pili ya kuwa na moyo wa mchungaji ni kuwaangalia kondoo Wake. Kama waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, tunaweza kuondoa, kutengeneza, kurekebisha, na kujenga upya chochote. Ni wepesi kutimiza hitaji kwa mkono saidizi au sahani ya biskuti. Lakini je kuna zaidi?

Je, kondoo wetu wanajua tunawaangalia kwa upendo na tutachukua hatua ya kuwasaidia?

Katika Mathayo 25 tunasoma:

“Njooni, enyi mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme ulioandaliwa kwa ajili yenu … :

“Kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula: nalikuwa na kiu, mkaninywesha: nalikuwa mgeni, mkanikaribisha: …

“Ndipo wenye haki watakapomjibu, wakisema Bwana ni lini tulipokuona una njaa, tukakulisha? au una kiu tukakunywesha?

“Ni lini tulipokuona u mgeni, tukakukaribisha?”5

Akina kaka na kina dada, neno muhimu ni ona. Wenye haki waliwaona wale walio na mahitaji kwa sababu walikuwa wakiangalia na kutambua. Sisi pia tunaweza kuwa jicho la kuangalia ili kutoa msaada na kufariji, kusherehekea na hata kuota. Tunapotenda, tunaweza kuhakikishiwa ahadi katika Mathayo: “kadri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo … , mlinitendea mimi.”6

Picha
Mwokozi akimtunza kondoo

Rafiki—tutamwita John—alishiriki kile kinachoweza kutokea pale tunapoona hitaji la mwingine si muhimu: “Dada katika kata yangu alijaribu kujiua. Baada ya miezi miwili, niligundua hakuna yeyote katika akidi yangu aliyekwenda kwa mume wake kuzungumzia tatizo hili la kutisha. Kwa masikitiko, hata mimi sikufanya hivyo. Mwishowe, nilimwomba mume huyu kwenda kupata chakula cha mchana. Alikuwa ni mtu mwenye aibu, mara nyingi alijihifadhi. Na mara niliposema, ‘Mke wako alijaribu kujiua. Hilo linaweza kuwa jambo zito kwako. Je, unataka kuliongelea jambo hili?’ alilia wazi wazi. Tulikuwa na mazungumzo nyororo na ya karibu sana na tulianzisha urafiki wa karibu na uaminifu ndani ya dakika chache.”

John aliongeza,“Nadhani tabia yetu ni kuleta tu keki badala ya kujifunza jinsi ya kutembea ndani ya wakati huo kwa uaminifu na upendo.”7

Kondoo wetu wanaweza kuwa wanaumia, wamepotea, au hata kupotoka kimakusudi; kama wachungaji wao, tunaweza kuwa miongoni mwa watu wa kwanza kuona mahitaji yao. Tunaweza kusikiliza na kupenda bila ya kuhukumu na kutoa tumaini na kusaidia kwa utambuzi wenye mwongozo wa Roho Mtakatifu.

Akina dada na akina kaka, ulimwengu umejaa matumaini zaidi na furaha kwa sababu ya vitendo vya ukarimu mnavyovifanya. Mnapotafuta mwongozo wa Bwana juu ya jinsi ya kufikisha upendo Wake na kuona mahitaji ya wale mnaowahudumia, macho yenu yatafunguliwa. Jukumu lako takatifu la kuhudumu linakupa haki ya kiungu ya mwongozo. Unaweza kutafuta mwongozo huo kwa kujiamini.

Kukusanywa kwenye Zizi la Mungu

Tatu, tunataka kondoo wetu wakusanywe kwenye zizi la Mungu. Kufanya hivyo, sisi sharti tutathimini wako wapi kwenye njia ya agano na kuwa tayari kutembea pamoja nao katika safari yao ya imani. Hii ni fursa yetu takatifu ya kujua mioyo yao na kuwaelekeza kwa Mwokozi wao.

Picha
Kondoo wakimfuata Mchungaji Mwema

Dada Josivini huko Fiji alikuwa na ugumu kuona uelekeo wake kwenye njia ya agano—kiuhalisia. Rafiki yake aliona kwamba Josivini alihangaika kuona maandiko vizuri ili kusoma. Alimpa Josivini miwani mpya ya kusomea na kalamu ya kung’aa ya njano ili kuweka alama kila lilipotajwa jina Yesu Kristo katika Kitabu cha Mormoni. Kile kilichoanza kama tamaa rahisi ya kuhudumu na kusaidia kujifunza maandiko kimesababisha Josivini kuhudhuria hekaluni kwa mara ya kwanza miaka 28 baada ya kubatizwa.

Picha
Dada Josivini
Picha
Dada Josivini hekaluni

Hata kama kondoo wetu ni imara au wadhaifu, wakifurahi au kuumia, tunaweza kuamua kwamba hakuna mtu wa kutembea peke yake. Tunaweza kuwapenda popote walipo kiroho na kutoa msaada na kuwahimiza kwa hatua nyingine mbele. Tunaposali na kutafuta kujua mioyo yao, ninashuhudia kwamba Baba wa Mbinguni atatuongoza na Roho Wake atakwenda pamoja nasi. Tuna fursa ya kuwa “malaika wa kuwazunguka” Yeye akiwa amewatangulia mbele.8

Picha
Mchungaji Mwema na kondoo Wake

Bwana anatualika tuwalishe kondoo Wake, kulitunza kundi Lake kama vile ambavyo Yeye angefanya. Yeye anatualika tuwe wachungaji kwa kila taifa, kila nchi. (Na ndiyo, Mzee Uchtdorf, tunawapenda na tunawahitaji mbwa wa Kijerumani.) Na Anataka vijana Wake kujiunga na kazi hiyo.

Vijana wetu wanaweza kuwa baadhi ya wachungaji shupavu. Wao ni, kama Rais Russell M. Nelson alivyosema, “miongoni mwa wazuri ambao Bwana amewahi kuwaleta ulimwenguni.” Wao ni “roho nzuri,” “wachezaji wetu bora” wamfuatao Mwokozi.9 Je, unaweza kufikiria nguvu ambazo wachungaji kama hawa wataleta wanapokuwa wakitunza kondoo Wake? Kuhudumu bega kwa bega pamoja ya vijana hawa, tunaona maajabu.

Wavulana na wasichana, tunawahitaji! Ikiwa huna jukumu la kuhudumu, zungumza na rais wako wa Muungano wa Usaidizi wa Akina mama au akidi ya Wazee. Watafurahi kwa kukubali kwako kuhakikisha kwamba kondoo Wake wanajulikana na kuhesabika, wanalindwa, na wamekusanywa kwenye zizi la Mungu.

Wakati siku itakapofika kwamba tutapiga magoti mbele ya miguu ya Mwokozi wetu mpendwa, tukiwa tumelisha kundi Lake, naomba tuweze kujibu kama Petro alivyojibu: “Ndiyo, Bwana; wewe wajua kuwa nakupenda.”10 Hawa, kondoo Wako, wanapendwa, wako salama, na wako nyumbani. Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Chapisha