Mmoja katika Kristo
Washirika wenzangu wapendwa katika kazi ya Bwana, naamini kuwa tunaweza kufanya bora zaidi na tunapaswa kufanya bora kwa kuwakaribisha marafiki wageni Kanisani.
Habari za mchana, kina kaka na kina dada wapendwa. Jinsi tunavyosema katika lugha yangu ya kiasili ya Kireno cha Brazili, “Boa tarde!” Ninajisikia nimebarikiwa kukusanyika pamoja nanyi katika mkutano huu mkuu wa ajabu wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho chini ya usimamizi wa nabii wetu mpendwa, Rais Russell M. Nelson. Ninastaajabishwa na nafasi kuu ambayo kila mmoja wetu aliyo nayo kuisikiliza sauti ya Bwana kupitia watumishi wake duniani katika siku hizi za mwisho tunazoishi.
Nchi yangu ya kuzaliwa Brazili ina maliasili nyingi mno. Mojawapo ni Mto wa Amazoni ambao ni maarufu, mojawapo ya mito mikubwa na mirefu zaidi ulimwenguni. Unaumbwa na mito miwili tofauti, Solimões na Negro. Cha kupendeza, yote inatiririka pamoja kwa maili kadhaa kabla ya maji hayo kuchanganyika, kwa sababu ya mito hiyo ina vyanzo tofauti, kasi, halijoto, na michanganyiko ya kemikali tofauti. Baada ya maili kadhaa, maji hayo hatimaye yanachanganyika, na kuwa mto tofauti na sehemu zake. Ni baada tu ya hizi sehemu kuchanganyika, ndipo Mto Amazon unakuwa na nguvu sana kwamba wakati unapofika katika Bahari ya Atlantiki, unasukuma maji ya bahari kiasi kwamba maji baridi yanaweza kupatikana maili nyingi ndani ya bahari.
Kwa njia sawa na vile mito ya Solimões na Negro inavyotiririka pamoja kuunda Mto Amazoni, watoto wa Mungu huja pamoja katika Kanisa la urejesho la Yesu Kristo kutoka tabaka, desturi na tamaduni mbali mbali kutengeneza jamii hii ya ajabu ya Watkatifu katika Kristo. Hatimaye, tunapotia moyo, kusaidiana, na kupendana, tunaungana kutengeneza ushawishi mkubwa kwa ajili ya wema duniani. Kama wafuasi wa Yesu Kristo, tukitiririka kama wamoja katika mto huu wa wema, tutaweza kupeana “maji baridi” ya injili kwa dunia inayohisi kiu.
Bwana amewaongoza manabii Wake watufundishe jinsi tunavyoweza kusaidiana na kupendana, ili tuweze kuungana katika imani na lengo katika kumfuata Yesu Kristo. Paulo, Mtume Katika Agano Jipya, alifundisha kwamba wale ambao “mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo … : maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu.”1
Wakati tunapoahidi wakati wa ubatizo kumfuata Mwokozi, tunashuhudia mbele ya Baba kwamba tuko radhi kujichukulia juu yetu jina la Kristo.2 Huku tukijitahidi kuwa na sifa zake takatifu maishani mwetu, tunakuwa tofauti na jinsi tulivyokuwa, kupitia Upatanisho wa Kristo aliye Bwana, na upendo wetu kwa watu wote unaongezeka kwa urahisi.3 Tunahisi kujali kwa kweli kwa ajili ya ustawi na furaha ya kila mmoja. Tunachukuliana kama kaka na dada, kama watoto wa Mungu wenye asili, sifa, na uwezo mtakatifu. Tunatamani kumjali kila mmoja na kubeba mizigo ya kila mmoja.4
Hiki ndicho kile ambacho Paulo alielezea kuwa hisani.5 Mormoni, nabii wa Kitabu cha Mormoni, aliifafanua kama “upendo msafi wa Kristo,”6 ambao ni aina tukufu, adili, na wenye nguvu zaidi ya upendo. Nabii wetu wa sasa, Rais Russell M. Nelson, hivi karibuni alielezea kudhihirika kwa upendo huu msafi kama utumishi, ambayo ni njia iliyolengwa na takatifu zaidi ya kuwapenda na kuwajali watu wengine jinsi alivyofanya Mwokozi.7
Basi tuzingatie kanuni hii ya upendo na kujali, jinsi alivyofanya Mwokozi, katika mazingira ya kutia moyo, kusaidia, na kuwasahidia wale walioongoka hivi karibuni na wale wanaoanza kuonyesha hamu ya kutaka kushiriki ibada zetu za Kanisani.
Wakati marafiki hawa wanatoka duniani na kuikubali injili ya Yesu Kristo, kuungana na Kanisa Lake, wanakuwa wafuasi Wake, wakizaliwa upya kupitia Kwake.8 Wanaiacha dunia ambayo waliifahamu vizuri na kuchagua kumfuata Yesu Kristo, kwa moyo wa lengo moja, wakijiunga na “mto” mpya kama ule Mto mkubwa wa Amazoni—mto ambao ni nguvu jasiri ya wema na haki ambao unatiririka kuelekea kwa uwepo wa Mungu. Mtume Petro anauelezea kama “mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu.”9 Wakati marafiki hawa wageni wanapoungana na mto huu mpya na wasioufahamu vyema, wanaweza kuhisi kama kwamba wamepotea mwanzoni. Marafiki hawa wageni wanajipata wakichanganyika na mto ulio na vyanzo vya kipekee, halijoto, na mchanganyiko wa kemikali tofauti—mto ulio na desturi, tamaduni, na msamiati yake. Maisha haya mapya katika Kristo yanaweza kuonekana kuwashinda. Hebu fikiria kidogo jinsi wanavyoweza kuwa wakihisi wanaposikia matamshi kama “FHE” “BYC”, “Jumapili ya mfungo,” “ubatizo kwa ajili ya wafu,” “muungano wa utatu,” na kadhalika.
Ni rahisi kuona ni kwa nini wanahisi si wenyeji. Katika hali kama hizi, wanaweza kujiuliza, “Je, kunayo nafasi kwangu mimi mahali hapa? Je, mimi ni mwenye kufaa katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho? Kanisa linanihitaji? Nitawapata marafiki wapya ambao wako radhi kunisaidia na kutegemeza?”
Marafiki zangu wapendwa, katika nyakati kama hizi, wale kati yetu ambao tuko katika sehemu tofauti katika safari hii ndefu ya uanafunzi ni lazima tunyooshe mkono wa ushirika kwa marafiki zetu wapya, tuwakubali pale walipo, na tuwasaidie, tuwapende na kuwashirikisha katika maisha yetu. Hawa marafiki wapya wote ni wana na mabinti wa Mungu wenye thamani kubwa.10 Hatuwezi kumpoteza hata mmoja tu kwa sababu, kama Mto Amazoni ambao unategemea mito ingine kuingia ndani yake, tunawahitaji jinsi tu wanavyotuhitaji ili kuwa nguvu kubwa ya wema duniani.
Marafiki wetu wageni huja na vipaji kutoka kwa Mungu, furaha, na wema ndani yao. Shauku yao kwa injili yaweza kuwa ya kuambukiza, na hivyo basi kutusaidia kutia nguvu tena shuhuda zetu. Pia wao huleta mitazamo mipya kwa uelewa wetu wa maisha na injili.
Tumefundishwa kwa muda mrefu jinsi tunavyoweza kuwasaidia marafiki zetu wageni kuhisi wamekaribishwa na wanapendwa katika Kanisa la Yesu Kristo la urejesho. Wanahitaji vitu vitatu ili kubakia imara na waaminifu maishani mwao mwote:
Kwanza, wanahitaji kina kaka na akina dada Kanisani ambao kihalisia na kwa ukweli wana hamu ya kuwajua, ni marafiki wa kweli na waaminifu ambao wanaweza kila mara kuwategemea, ambao watatembea nao, na watakaojibu maswali yao. Kama waumini, daima tunapaswa kuwa makini na kutafuta nyuso mpya wakati tunapohudhuria shughuli na mikutano ya Kanisa, bila ya kujali wajibu, majukumu, au wasiwasi huenda tukawa nao. Tunaweza kufanya vitu rahisi kuwasaidia hawa marafiki zetu wageni kuhisi wamekubalika na kukaribishwa Kanisani, kama vile kuwasalimia kwa furaha, kutabasamu kwa kweli, kuketi pamoja tunapoimba na kuabudu pamoja, kuwatambulisha kwa waumini wengine, na kadhalika. Tunapofungua mioyo yetu kwa marafiki zetu wageni katika baadhi ya njia hizi, tunatenda katika roho wa utumishi. Wakati tunapowatumikia kama Mwokozi alivyofanya, hawatahisi kama “wageni ndani ya lango letu.” Watahisi kama kuwa wao wanakubalika na kuwa na marafiki wapya, na muhimu zaidi, watauhisi upendo wa Mwokozi kupitia kujali kwetu kwa kweli.
Pili, marafiki wapya wanahitaji jukumu—nafasi ya kuwatumikia wengine. Huduma ni mojawapo ya busara kuu ya Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Ni mchakato ambao kupitia kwake imani yetu inaweza kukua imara. Kila rafiki mpya anahitaji nafasi hiyo. Huku askofu na baraza la kata wakiwajibika kutoa miito, hakuna kinachotuzuia kuwaalika marafiki zetu wapya kutusaidia kuwatumikia wengine kwa njia zisizo rasmi kupitia miradi ya huduma.
Tatu, marafiki wapya ni lazima “[wa]lishwe kwa neno jema la Mungu.”11 Tunaweza kuwasaidia wapende na kufahamu maandiko vyema tunaposoma na kujadiliana mafundisho hayo pamoja nao, tukiwafahamisha mazingira kuhusu hadithi hizo na kufafanua maneno magumu. Tunaweza pia kuwafundisha jinsi ya kupokea maongozi ya kibinafsi kupitia kujifunza kwa maandiko kila siku. Kando na hayo, tunaweza kuwatembelea marafiki zetu wapya manyumbani kwao na kuwaalika nyumbani kwetu wakati mwingine nje ya wakati ulioratibiwa kwa kawaida kwa ajili ya mikutano na shughuli za Kanisa, kuwasaidia kuungana na mto mkuu wa jamii ya Watakatifu.
Kutambua marekebisho na changamoto marafiki zetu wapya wanafanya kwa ajili ya kuwa washiriki wa familia ya Mungu, kama kaka na dada zetu, tunaweza kushiriki jinsi ambavyo tumeweza kushinda changamoto sawa na hizo maishani mwetu. Hii itawasaidia kujua ya kwamba hawako peke yao na kwamba Mungu atawabariki wanapokuwa na imani katika ahadi Zake.12
Wakati mito ya Solimões na Negro inapochanganyika, Mto wa Amazoni unakuwa mkubwa na wenye nguvu. Katika mtindo sawa na huo, wakati sisi pamoja na marafiki zetu tunapoungana kweli, Kanisa la urejesho la Yesu Kristo linakuwa imara na thabiti zaidi. Mpenzi wangu, Rosana, pamoja nami tuna shukrani nyingi kwa wale wote ambao walitusaidia kuchanganyika katika mto huu mpya miaka mingi iliyopita, wakati tulipoikubali injili ya Yesu Kristo katika nchi yetu ya kuzaliwa ya Brazil. Kwa kipindi cha miaka mingi, hawa watu waaminifu kwa hakika wametutumikia na wametusaidia kuendelea kutiririka katika haki. Tunatoa shukrani nyingi sana kwao.
Manabii waliokuwa Amerika Kaskazini na Kusini walifahamu vyema jinsi ya kuwadumisha marafiki wapya wakitiririka pamoja kwa uaminifu katika mto huu mpya wa wema kuelekea maisha ya milele. Kwa mfano, akiwa ameona siku zetu na akifahamu kwamba tungekumbwa na changamoto sawa,13 Moroni alijumuisha baadhi ya hatua hizo muhimu katika maandishi yake katika Kitabu cha Mormoni.
“Na baada ya hao kupokewa kwenye ubatizo, na kupokelewa na kusafishwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, walihesabiwa miongoni mwa watu wa kanisa la Kristo; na majina yao yalichukuliwa ili wakumbukwe na kulishwa na neno nzuri la Mungu, kuwaweka kwa njia nzuri, kuwaweka waangalifu siku zote kwenye sala, wakitegemea tu katika nguvu ya wokovu wa Kristo, ambaye alikuwa mwanzilishi na mtimizaji wa imani yao.
“Na kanisa lilikutana pamoja mara kwa mara, kufunga na kuomba, na kuzungumza mmoja na mwingine kuhusu ustawi wa nafsi zao.”14
Washirika wenzangu wapendwa katika kazi ya Bwana, naamini kuwa tunaweza kufanya bora zaidi na tunapaswa kufanya bora kwa kuwakaribisha marafiki wageni Kanisani. Ninawaalikeni mfikirie kile tunachoweza kufanya ili kuwa wenye kuwakumbatia, kuwakubali, na kuwasaidia zaidi, kuanzia Jumapili hii ijayo. Kuwa mwangalifu usije ukakubali wajibu wako Kanisani kukuzuia kuwakaribisha marafiki wageni katika mikutano na shughuli za Kanisa. Hata hivyo, nafsi hizi ni zenye thamani machoni mwa Mungu na ni muhimu zaidi kuliko programu na shughuli. Ikiwa tutawatumikia marafiki zetu wapya na mioyo yetu iliyojaa upendo msafi jinsi alivyofanya Mwokozi, ninakuahidi, katika jina Lake, kwamba Atatusaidia katika juhudi zetu. Tunapotenda kama watumishi waaminifu, jinsi alivyofanya Mwokozi, marafiki zetu wapya watapata msaada wanaohitaji kuendelea kuwa imara, wenye kujitolea kwa dhati, na waaminifu hadi mwisho. Wataungana nasi tunapokuwa watu wakuu wa Mungu na watatusaidia kuleta maji safi kwa dunia ambayo inahitaji kwa dharura baraka za Injili ya Yesu Kristo. Hawa watoto wa Mungu watahisi kama kwamba wao “si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu.”15 Ninaahidi ya kwamba watatambua uwepo wa Mwokozi wetu, Yesu Kristo, katika Kanisa Lake. Wataendelea kutiririka nasi kama vile mto kuelekea chemichemi ya wema wote hadi watakapopokelewa na mikono iliyonyooka na Bwana wetu Yesu Kristo; na kumsikia Baba akisema, “Mtapokea uzima wa milele.”16
Ninakualikeni mtafute usaidizi wa Bwana katika kuwapenda wengine jinsi ambavyo Amekupenda. Na wote tufate ushauri uliotolewa na Mormoni: “Kwa hivyo, ndugu [na dada] zangu wapendwa, ombeni kwa Baba kwa nguvu zote za moyo, kwamba mjazwe, na upendo huu, ambao ametoa kwa wote ambao ni wafuasi wa kweli wa Mwana wake, Yesu Kristo” (17). Juu ya kweli hizi, mimi nashuhudia na ninafanya hivyo katika jina la Yesu Kristo, amina.