2010–2019
Ono la Ukombozi wa Wafu
Oktoba 2018


Ono la Ukombozi wa Wafu

Ninashuhudia ya kwamba ono alilopokea Rais Joseph F. Smith ni la kweli. Ninashuhudia ya kwamba kila mmoja anaweza kupata ufahamu ya kwamba ni la kweli.

Kaka na dada zangu, hotuba yangu ilitayarishwa muda mrefu kabla ya kifo cha mke wangu, mpendwa Barbara. Familia yangu pamoja nami tunawashukuru kwa ajili ya upendo wenu na uwezo wenu wa kufikia wa ukarimu. Ninaomba Bwana atanibariki ninapoongea nanyi asubuhi hii.

Mnamo Oktoba 1918, miaka 100 iliyopita, Rais Joseph F. Smith alipokea ono tukufu. Baada ya karibu miaka 65 ya huduma ya kujitolea kwa Bwana katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, na wiki chache tu kabla ya kifo chake Novemba 19, 1918 alikuwa ameketi katika chumba chake akitafakari dhabihu ya upatanisho ya Kristo akiwa anasoma maelezo ya Mtume Paulo kuhusu huduma ya Mwokozi karika dunia ya Roho baada ya Kusulubiwa Kwake.

Aliandika: “Nilipokuwa nikisoma. … Nilipokuwa nikitafakari juu ya mambo haya … , macho yangu ya ufahamu yakafunguliwa, na Roho wa Bwana akatulia juu yangu, na nikaona jeshi la waliokufa wote”1 Maandishi kamili ya ono hilo yamenukuliwa katika Mafundisho na Maagano sehemu ya 138.

Acha nitoe usuli kiasi ili tuweze kufahamu vyema zaidi kujitayarisha kwa Joseph F maisha yake yote kwa ajili ya kupokea ufunuo huu.

Picha
Joseph na Hyrum Smith juu ya farasi

Wakati alipokuwa Rais wa Kanisa, alitembea kule Nauvoo mwaka wa 1906 na kutafakari juu ya kumbukumbu aliyokuwa nayo akiwa tu na umri wa miaka tano. Alisema: “Hapa ndipo hasa mahali pale nilipokuwa nimesimama wakati [Joseph, mjomba wangu, na baba yangu, Hyrum] walipita wakielekea kule Carthage. Bila ya kushuka kutoka kwenye farasi wake mrefu baba aliinama akiwa katika tandiko lake na kuniinua juu kutoka chini. Alinibusu kwaheri na kuniweka chini tena na nikamuona akienda.”2

Wakati Joseph F. aliwaona tena, mamake, Mary Fielding, alimuinua juu kuwaona mashahidi wakiwa wamelala upande kwa upande baada ya kuuwawa kinyama katika jela ya Carthage mnamo Juni 27, 1844.

Miaka miwili baadaye, Joseph F., pamoja na familia yake na mamake mwaminifu, Mary Fielding Smith, waliondoka nyumbani kwao kule Nauvoo kuelekea Winter Quarters. Ingawaje hakuwa amefikisha miaka minane, Joseph F. alihitajika kuendesha moja kati ya mkokoteni uiovutwa na kundi la ng’ombe kutoka Montrose, Iowa, hadi Winter Quarters na kisha kuelekea katika Bonde la Salt Lake, wakiwasili akiwa karibu na miaka 10. Natumai ya kwamba nyinyi wavulana wadogo na wavulana wakubwa mnasikiliza na mtagundua jukumu na matarajio yaliyowekwa juu ya Joseph F. katika wa ujana wake.

Miaka minne tu baadaye, katika mwaka wa 1852, wakati alikuwa na miaka 13, mama yake mpendwa aliaga—na kumuacha Joseph na ndugu zake mayatima.3

Joseph aliitwa kuhudumu misheni katika visiwa vya Hawaii mnamo Juni 1854 alipokuwa na umri wa miaka 15. Misheni hii, iliyochukua zaidi ya miaka mitatu, ilikuwa chanzo cha maisha ya huduma Kanisani.

Baada ya kurudi kule Utah, Joseph F. alifunga ndoa mwaka wa 1859.4 Kwa muda wa miaka michache iliyofuata, maisha yake yalijawa na kazi, majukumu ya kifamilia, na misheni mbili za ziada. Mnamo Julai 1, 1866, akiwa na umri wa miaka 27, maisha ya Joseph F. yalibadilika milele wakati alipotawazwa kama Mtume na Rais Brigham Young. Oktoba ya mwaka uliofuata, alichukua nafasi katika Baraza la Kumi na Wawili.5 Alihudumu kama mshauri wa Brigham Young, John Taylor, Wilford Woodruff, na Lorenzo Snow kabla ya yeye Mwenyewe kuwa Rais mwaka wa 1901.6

Joseph F. na mkewe Julina walimkaribisha mtoto wao wa kwanza, Mercy Josephine, katika familia.7 Alikuwa tu na umri wa miaka miwili na nusu wakati alipofariki. Muda mfupi baadaye, Joseph F. Aliandika: “Ni mwezi mmoja kufikia jana tangu … mpenzi wangu Josephine alipoaga. Ee! ningeweza kumuokoa aweze kukua katika uanamke. Ninamkosa kila siku na ninajihisi mpweke. … Mungu nisamehe upungufu wangu ikiwa ni makosa kuwapenda watoto wangu jinsi ninavyowapenda.”8

Maishani mwake, Rais Smith alimpoteza babake, mamake, kaka mmoja na dada wawili, wake wawili, na watoto kumi na watatu. Alifahamu vyema huzuni na kupoteza wapendwa.

Wakati mwana wake Albert Jesse alifariki, Joseph F. alimwandikia dadake Martha Ann kwamba alikuwa amemsihi Bwana amuokoe na akauliza, “Kwa nini iko hivyo? Ee,, Mungu ni kwa nini ilitokea hivi?”9

Licha ya sala zake kwa wakati ule, Joseph F. hakupokea jibu lolote kuhusu swali hili.10 Alimwelezea Martha Ann kwamba “mbingu [ilionekana kuwa kama] shaba juu ya vichwa vyetu” kuhusu swala la kifo na ulimwengu wa roho. Hata hivyo, imani yake katika ahadi za milele za Bwana ilikuwa imara na yenye imani.

Katika wakati mwafaka wa Bwana, majibu ya ziada, faraja, na uelewa wa kuhusu ulimwengu wa roho alivyotafuta vilimjia Rais Smith kupitia ono la ajabu alilopokea mnamo Oktoba 1918.

Mwaka huo hasa ulikuwa wenye uchungu mwingi kwake. Aliomboleza juu ya vifo vya watu katika Vita Vikuu vya Dunia ambavyo viliendelea kuongezeka kuwa zaidi ya watu milioni 20 walio uawa. Kando na hayo, homa ya kuenea kote ilikuwa ikisambaa kote duniani ikiwaua watu milioni 100.

Picha
Mzee Hyrum Mack Smith

Katika mwaka huo pia, Rais smith aliwapoteza wanafamilia watatu wapendwa. Mzee Hyrum Mack Smith wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, mwanawe wa kwanza na babu yangu, walifariki ghafla kutokana na kupasuka kwa kidole tumbo.

Rais Smith aliandika: “Nimekosa la kusema—[nimeganda] kwa huzuni!… Moyo wangu umevunjika; na unahangaika kwa ajili ya maisha! … Ee! Nilimpenda! … Nitampenda milele. Na hivyo ndivyo ilivyo na daima itakavyokuwa na wana na mabinti wangu wote, lakini yeye ni mwana wangu wa kwanza, wa kwanza kuniletea shangwe na tumaini la jina la kudumu, lenye heshima miongoni mwa watu. Kutoka kina cha nafsi yangu ninamshukuru Mungu kwa ajili yake! Lakini … Ee! Nilimhitaji! Sote tunamhitaji! Alikuwa mwenye usaidizi mkubwa kwa Kanisa. … Na sasa … Ee! mimi ninaweza kufanya nini! … Ee! Mungu nisaidie!”11

Mwezi uliofuata, Shemeji yake Rais Smith, Alonzo Kesler, alifariki katika ajali ya kusikitisha.12 Rais Smith aliandika katika shajara yake, “Ajali hii mbaya zaidi na yenye kuvunja moyo kwa kusababisha kifo, tena imetanda huzuni juu ya familia yangu yote.”13

Miezi saba baadaye, mnamo Septemba 1918, Shemeji wa Rais Smith na bibi yangu, Ida Bowman Smith, alifariki baada ya kujifungua mtoto wake wa tano, mjomba wangu Hyrum.14

Na basi ikawa hivyo, mnamo Oktoba 3, 1918 akiwa amepitia huzuni mkubwa juu ya mamilioni ambao walikuwa wamefariki duniani kutokana na vita na magonjwa na vile vile vifo vya wanafamilia wake, Rais Smith alipokea ufunuo kutoka mbinguni unaojulikana kama “ono la ukombozi wa wafu.”

Picha
Rais Joseph F. Smith

Alidokezea ufunuo huo siku iliyofuata katika kikao cha kufungua mkutano mkuu mwezi wa Oktoba. Afya ya Rais Smith ilikuwa ikidhoofika, na bado alizungumza kwa ufupi: “Sitafanya, sitathubutu, sitajaribu kuingilia mambo mengi ambayo yako akilini mwangu asubuhi ya leo, na nitaahirisha hadi wakati fulani katika siku zijazo, Bwana akipenda, jaribio langu la kuwaelezea baadhi ya mambo ambayo yako akilini mwangu, na yaliyo moyoni mwangu. Sikuwa naishi peke yangu miezi hii mitano [iliyopita]. Nimeishi katika roho ya maombi, ya maombolezo, ya imani na ya dhamira; na nimekuwa na mawasiliano ya kuendelea na Roho wa Mungu.”15

Ufunuo huu aliupokea mnamo Oktoba 3 ulifariji moyo wake na kumpa majibu ya mengi kati ya maswali yake. Sisi pia tunaweza kufarijiwa na kujifunza zaidi kuhusu siku zetu za usoni wakati sisi na wapendwa wetu tutakapofariki na kwenda katika ulimwengu wa roho kupitia kujifunza ufunuo huu na kutafakari umuhimu wake katika jinsi tunavyoishi maisha yetu kila siku.

Miongoni mwa vitu vingi ambavyo Rais Smith aliona ilikuwa ni matembezi ya Mwokozi kwa roho waaminifu katika ulimwengu wa roho baada ya kifo chake msalabani. Kutoka katika ono ninadondoa:

“Bali tazama, kutoka miongoni mwa wenye haki, aliunda jeshi lake na akawateua wajumbe, waliovikwa uwezo na mamlaka, na akawapa mamlaka ya kwenda na kupeleka nuru ya injili kwa wao ambao walikuwa gizani, hata kwa roho zote za wanaume [na wanawake];16 na hivyo ndivyo injili ilivyohubiriwa kwa wafu. …

“Hawa walifundishwa imani katika Mungu, toba ya dhambi, ubatizo unaofanywa kwa niaba ya wafu kwa ajili ya ondoleo la dhambi, kipawa cha Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono,

“Na kanuni nyingine zote za injili ambazo zilikuwa muhimu kwao kuzijua ili kujithibitishia wenyewe kwamba waweze kuhukumiwa kulingana na wanadamu katika mwili, lakini waishi kulingana na Mungu katika roho. …

“Kwani wafu waliotazamiwa kwa muda mrefu kutokuwepo kwa roho zao kutoka kwenye miili yao kama ni utumwa.

“Hizi Bwana alizifundisha, na kuzipa uwezo wa kutoka, baada ya ufufuko wake kutoka kwa wafu, ili kuingia katika ufalme wa Baba yake; ili kuvikwa kutokufa na uzima wa milele,

“Na kuendelea kutoka saa hiyo kufanya kazi zao kama ilivyoahidiwa na Bwana, na kuwa washiriki wa baraka zote ambazo zilishikiliwa kwa akiba kwa ajili yao waliompenda yeye.”17

Picha
Sanamu ya Joseph na Hyrum Smith

Katika ono hilo, Rais Smith alimwona babake, Hyrum, na Nabii Joseph Smith. Ilikuwa miaka 74 tangu awaone akiwa mvulana mdogo kule Nauvoo. Tunaweza tu tukafikiria shangwe aliyokuwa nayo kwa kuwaona baba na mjomba wake wapendwa. Ni lazima alikuwa ametiwa msukumo na kufarijiwa kujua ya kwamba roho zote husalia na sura za mili yao ya maisha ya muda na kwamba zinasubiri kwa hamu siku iliyoahidiwa ufufuo wao. Ono hilo lilifunua zaidi kina na upana wa mpango wa Baba wa Mbinguni kwa ajili ya watoto Wake na upendo wa ukombozi wa Kristo na uwezo wa Upatanisho Wake usiolinganishwa.18

Katika maadhimisho haya maalum ya 100, ninawaalikeni msome ufunuo huu kabisa na kwa makini. Mnapofanya hivyo, Mungu na awabariki muweze kuelewa vyema zaidi na kuwa na shukrani kwa ajili ya upendo wa Mungu na mpango Wake wa wokovu na furaha kwa ajili ya watoto Wake.

Ninashuhudia ya kwamba ono alilopokea Rais Joseph F. Smith ni la kweli. Ninashuhudia ya kwamba kila mmoja anaweza kulisoma na kupata ufahamu ya kwamba ni la kweli. Wale ambao hawapokei ufahamu huu katika maisha haya hakika watakuja kujua ukweli wake wakati kila mmoja atawasili katika ulimwengu wa roho. Huko, kila mmoja atamsifu Mungu na Bwana Yesu Kristo kwa ajili ya mpango mkuu wa wokovu na baraka ya ufufuko ulioahidiwa wakati mwili na roho vitaunganishwa tena na kamwe kutotenganishwa tena.19

Picha
Dada Barbara Ballard

Nina shukrani jinsi kujua pale kipenzi changu Barbara yuko na kwamba tutakuwa pamoja tena na familia yetu milele. Na amani ya Mungu iweze kutuhimili sasa na daima ndiyo maombi yangu ya unyenyekevu katika jina la Bwana Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Mafundisho na Maagano 138:6, 11.

  2. Joseph F. Smith, katika Preston Nibley, Marais wa Kanisa (1959), 228.

  3. Joseph Fielding Smith, Maisha ya Joseph F. Smith (1938), 13.

  4. Alimuoa Levira Clark mwaka wa 1859, Julina Lambson mwaka wa 1866, Sarah Richards mwaka wa 1868, Edna Lambson mwaka wa 1871, Alice Kimball mwaka wa 1883, na Mary Schwartz mwaka wa 1884.

  5. Joseph F. Smith aliitwa kama mshauri wa ziada katika Urais wa Kwanza (Brigham Young, Heber C. Kimball na Daniel H. Wells). Pia alihudumu kama mshauri wa pili katika Urais wa Kwanza kwa Marais watatu wa Kanisa, ikijumuisha Marais John Taylor, Wilford Woodruff, na Lorenzo Snow.

  6. Joseph F. Smith alihudumu kama mshauri katika Urais wa Kwanza himaya ya Brigham Young’s na akahudumu kama mshauri wa Pili katika Urais wa Kwanza wakati wa himaya za John Taylor, Wilford Woodruff, na Lorenzo Snow. Alikuwa Rais wa Kwanza wa Kanisa aliyekuwa amehudumu katika Urais wa Kwanza kabla ya kuitwa kama Rais.

  7. Mercy Josephine, mtoto wa kwanza wa Joseph F., alizaliwa mnamo Agosti 14, 1867, na akafariki mnamo Juni 6, 1870.

  8. Shajara ya Joseph F. Smith, Julai 7, 1870, Maktaba ya Historia ya Kanisa, Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, Mjini Salt Lake, Utah.

  9. Joseph F. Smith to Martha Ann Smith Harris, Aug. 26, 1883, Church History Library; see Richard Neitzel Holzapfel and David M. Whitchurch, My Dear Sister: The Letters between Joseph F. Smith and His Sister Martha Ann (2018), 290–91.

  10. Nyakati nyingi, Bwana alimwelekeza Joseph F. Smith katika maisha yake binafsi na katika huduma yake kama Mtume na Rais wa Kanisa kupitia ndoto zenye mwongozo, mafunuo, na maono Mara nyingi vipawa hivi vya thamani kutoka kwa Bwana vimeandikwa kwenye shajara zake, mahubiri, makumbusho na kumbukumbu rasmi za Kanisa.

  11. Joseph F. Smith, journal, Jan. 23, 1918, Church History Library; spelling and capitalization modernized; see Joseph Fielding Smith, Life of Joseph F. Smith, 473–74.

  12. Ona “A. [P.] Kesler Is Killed in Fall from a Building,” Ogden Standard, Feb. 5, 1918, 5.

  13. Shajara ya Joseph F. Smith, Jan. 4, 1918, Maktaba ya Historia ya Kanisa.

  14. “Ida Bowman Smith,” Salt Lake Herald-Republican, Sept. 26, 1918, 4.

  15. Joseph F. Smith, katika Ripoti ya Mkutano Mkuu,Okt. 1918, 2.

  16. Ona marejeo ya “mtukufu Mama yetu Hawa” na “mabinti waaminifu ambao … wakimwabudu Mungu wa kweli na aliye hai” (Mafundisho na Maagano 138:39).

  17. Mafundisho na Maagano 138:30, 33–34, 50–52.

  18. Maandishi ya ono kwa mara ya kwanza yalionekana katika toleo la Deseret News mnamo Novemba 30, 1918 siku 11 baada ya kufariki kwa Rais Smith, mnamo Novemba 19. Lilichapishwa katika Improvement Era ya Desemba na katika matoleo ya Januari 1919 ya Relief Society Magazine, Utah Genealogical na Historical Magazine, Young Women’s Journal, na Millennial Star.

  19. Ingawaje wana wa upotevu watafufuliwa, huenda wasionyeshe upendo na kumsifu Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo kama watakavyofanya wale watakaopokea ufalme wa utukufu. Ona Alma 11:41; Mafundisho na Maagano 88:32–35.

Chapisha