Amini, Penda, Tenda
Tunapata uzima tele kwa kuwa wafuasi wa kweli wa Yesu Kristo—kwa kufuata njia Zake na kuifanya kazi Yake.
Akina kaka na kina dada wapendwa, ni fursa ya miujiza jinsi gani kuwa pamoja nanyi katika hiki kikao cha mkutano mkuu wa ajabu leo: kusikiliza jumbe zenye mwongozo; kusikiliza hii kwaya ya wamisionari ya ajabu na kushangaza ikiwakilisha maelfu ya wamisionari kote ulimwenguni—mabinti zetu, wana wetu—na hasa kuwa tumeunganika katika imani leo, kumkubali Rais na nabii wetu mpendwa, Rais Russell M. Nelson, Urais wa Kwanza, na Maafisa wa Wakuu wa Kanisa. Ni siku ya furaha jinsi gani kuwa pamoja nanyi leo?
Mfalme wa kale Sulemani alikuwa mmoja wa watu wenye mafanikio makubwa ya kuonekana katika historia.1 Alionekana kuwa na kila kitu—pesa, mamlaka, heshima, umaarufu. Lakini baada ya miongo ya kujiendekeza na anasa, ni kwa jinsi gani Mfalme Sulemani alihitimisha maisha yake?
“Mambo yote ni ubatili,”2 alisema.
Mtu huyu, aliyekuwa na vyote, aliishia kukata tamaa, bila rajua, na mwenye huzuni, licha ya kila kitu alichokuwa nacho.3
Kuna neno la Kijerumani, Weltschmerz. Kwa maana rahisi, linamaanisha huzuni inayoletwa na wasiwasi kuhusu jinsi ulimwengu ulivyo duni kuliko vile tunavyodhani unapaswa kuwa.
Pengine kuna Weltschmerz kidogo ndani yetu sote.
Wakati simanzi isiyoonekana inapotambaa kwenye kona za maisha yetu. Wakati huzuni inapojaza mchana wetu na kuleta kiza kinene kwenye usiku wetu. Wakati majonzi na udhalimu unapoingia kwenye ulimwengu unaotuzunguka, ikiwemo kwenye maisha ya wapendwa wetu. Wakati tunaposafiri kupitia njia yetu binafsi ya upweke na taabu, na maumivu yanafifisha uthabiti wetu na kuvunja utulivu wetu—tunaweza kushawishika kukubaliana na Sulemani kwamba maisha ni ubatili na hayana maana.
Tumaini Kuu
Habari njema ni kwamba, lipo tumaini. Kuna suluhisho kwenye utupu, ubatili, na Weltschmerz za maisha. Kuna suluhisho hata kwenye kukosa tumaini kabisa, na kukata tamaa unakoweza kuhisi.
Tumaini hili hupatikana katika nguvu ya kufanya upya ya injili ya Yesu Kristo na katika nguvu ya ukombozi ya Mwokozi kutuponya kutokana na ugonjwa wetu wa nafsi.
“Mimi nalikuja,” Yesu alitangaza, “ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.”4
Tunapata uzima huo wa milele siyo kwa kuzingatia kwenye mahitaji yetu wenyewe au kwenye mafanikio yetu bali kwa kuwa wafuasi wa kweli wa Yesu Kristo—kwa kufuata njia Zake na kuifanya kazi Yake. Tunapata uzima tele kwa kujikana sisi wenyewe na kujihusisha katika kusudi kuu la Kristo.
Na ni nini kusudi la Kristo? Ni kuamini katika Yeye, kupenda kama alivyopenda, na kutenda kama Yeye alivyotenda.
Yesu “alizunguka huko na huko akitenda kazi njema.”5 Alitembea kati ya maskini, wenye shida, wagonjwa na walioteseka. Aliwahudumia wasio na uwezo, wadhaifu, na wasio na rafiki. Alitumia muda pamoja nao; Alizungumza nao. “Na Akawaponya wote.”6
Kila Alipokwenda, Mwokozi alifundisha “habari njema”7 ya injili. Alishiriki kweli za milele ambazo ziliwaweka watu huru kiroho na pia kimwili.
Wale wanaojitolea nafsi zao kwenye kusudi la Mwokozi wanagundua ukweli wa ahadi ya Mwokozi: “Mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona.”8
Sulemani hakuwa sahihi, kaka zangu na dada zangu wapendwa—maisha siyo “ubatili.” Kinyume chake, yanaweza kujaa lengo, maana, na amani.
Mikono ya uponyaji ya Yesu Kristo inawafikia wote wanaomtafuta Yeye. Nimekuja kujua bila shaka kwamba kumwamini na kumpenda Mungu na kujitahidi kumfuata Kristo kunaweza kubadili mioyo yetu,9 kupunguza maumivu yetu, na kujaza nafsi zetu kwa “shangwe kuu.”10
Amini, Penda, Tenda
Ndiyo, lazima tutende zaidi ya kuwa tu na uelewa makini wa injili ili iwe na ushawishi huu wa uponyaji katika maisha yetu. Lazima tuiunganishe katika maisha yetu—kuifanya sehemu ya utambulisho wetu na kile tunachokifanya.
Acha nipendekeze kwamba ufuasi huanza na maneno matatu rahisi:
Amini, penda, na tenda
Kumuamini Mungu hupelekea kuwa na imani Kwake na kujenga uaminifu kwenye maneno Yake. Imani husababisha mioyo yetu kuvimba na kukua katika upendo wetu kwa Mungu na kwa wengine. Upendo huo unapokua, tunapata msukumo wa kumfuata Mwokozi tunapoendelea na safari yetu kuu kwenye njia ya ufuasi.
“Lakini,” unasema, “hiyo inaonekana kidogo rahisi. Shida za maisha, bila shaka shida zangu, ni changamani zaidi kwa maagizo rahisi kama hayo. Huwezi kutibu Weltschmerz kwa maneno matatu rahisi: Amini, Penda, Tenda.”
Siyo maneno ya hekima ambayo hutibu. Ni upendo wa Mungu ambao huokoa, hurejesha, na kuhuisha.
Mungu anakujua. Wewe ni mtoto Wake. Yeye anakupenda.
Hata wakati unapohisi kwamba hupendeki, Yeye anafika kwako.
Siku hii hasa—kila siku—Yeye anakufikia, akitamani kukuponya, kukuinua, na kujaza utupu katika moyo wako kwa shangwe ya kudumu. Anatamani kutupilia mbali kiza chochote kinachofunika maisha yako na kukijaza kwa nuru takatifu na angavu ya utukufu Wake usio na mwisho.
Nimepata uzoefu wa hili mimi mwenyewe.
Na ni ushahidi wangu kama Mtume wa Bwana Yesu Kristo kwamba wale wote wanaokuja kwa Mungu—wote ambao hakika wanaamini, wanapenda, na kutenda—wanaweza kuwa na uzoefu kama huo.
Tunaamini
Maandiko yanatufundisha kwamba “pasipo imani haiwezekani kumpendeza [Mungu]: kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko.”11
Kwa wengine, tendo la kuamini ni gumu. Kiburi chetu kinakua kizuizi. Pengine tunadhani kwamba kwa sababu sisi ni wenye akili, wenye elimu, au wenye uzoefu, hatuwezi kabisa kumwamini Mungu. Na tunaanza kuitazama dini kama utamaduni wa kipumbavu.12
Katika uzoefu wangu, kuamini siyo hasa kama mchoro wa kuvutia ambao tunautazama na kuupenda na ambao tunaujadili na kuutolea nadharia. Ni zaidi kama jembe tunaloenda nalo shambani na, kwa jasho la uso wetu, tunatengeneza matuta katika ardhi ambayo huotesha mbegu na kuzaa matunda ambayo yatabaki.13
Mkaribieni Mungu, Naye atawakaribia ninyi.14 Hii ni ahadi kwa wale wote wanaotafuta kuamini.
Tunapenda
Maandiko yanafunua kwamba kadiri tunavyompenda Mungu zaidi pamoja na watoto Wake, ndivyo tunavyokuwa zaidi wenye furaha.15 Upendo Yesu aliongelea hili, hata hivyo, siyo upendo wa kadi ya zawadi ya kutupa, endelea na mambo mengine. Siyo upendo ambao huzungumziwa na kisha kusahaulika. Siyo aina ya upendo wa “nijulishe kama kuna kitu chochote naweza kufanya”.
Upendo ambao Mungu anauzungumzia ni ule ambao huingia mioyoni mwetu tunapoamka asubuhi, hukaa nasi mchana wote, na huvimba ndani ya nafsi zetu tunapotoa sala zetu usiku.
Huu ndio upendo usioelezeka Baba wa Mbinguni alionao kwetu.
Ni huruma huu usiyo na mwisho ambayo huturuhusu vizuri zaidi kuwaona wengine kwa vile walivyo. Kupitia lenzi ya upendo msafi, tunawaona viumbe wasiokufa wenye uwezo usio na kikomo na wa thamani na wana na mabinti wapendwa wa Mwenyezi Mungu.
Pale tunapoona kupitia lenzi hiyo, hatuwezi kumpuuza, kumdharau, au kumtenga yeyote.
Tunatenda
Katika kazi ya Mwokozi, mara nyingi ni “kupitia kwa vitu vilivyo vidogo na rahisi” kwamba “vitu vikubwa hutendeka.”16
Tunajua kwamba inahitaji mazoezi ya kujirudia kuwa mzuri kwenye kitu chochote. Iwe ni kupiga zumari, kupiga mpira nyavuni, kurekebisha gari, au hata kurusha ndege, ni kupitia kufanya mazoezi ndipo tunakuwa wazuri zaidi na zaidi.17
Mfumo Mwokozi wetu aliouweka duniani—Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho—hutusaidia sisi kufanya hilo hasa. Unatoa mahali pa kufanyia mazoezi kuishi jinsi Yeye alivyofundisha na kuwabariki wengine jinsi Yeye alivyobariki.
Kama waumini wa Kanisa, tunapewa miito, majukumu, na fursa za kufikia kwa huruma na kuwahudumia wengine.
Hivi karibuni, Kanisa limeweka msisitizo mpya kwenye kuwahudumia, au kuwatumikia wengine au kuwapenda wengine. Hadhari kubwa ilichukuliwa kuamua jina tunalopaswa kuupa msisitizo huu maalumu.
Moja ya jina lililofikiriwa ni kuchunga, rejeo linalofaa kwenye mwaliko wa Kristo wa: “Lisha kondoo wangu.”18 Hata hivyo, lilikuwa na angalau kasoro moja: kutumia neno hilo kungenifanya mimi mbwa wa Kijerumani. Kwa hivyo, naridhika sana na neno kuhudumu.
Kazi Hii ni ya Kila Mtu
Ndiyo, msisitizo huu si mpya. Inatoa tu fursa mpya na iliyorekebishwa kwetu kufanyia mazoezi amri ya Mwokozi ya “,mpendane”19 katika njia iliyorekebishwa na kufanyia mazoezi kusudi la Kanisa .
Kama vile tu kazi ya umisionari; ushupavu, unyenyekevu, na ujasiri wa kushiriki injili ni mfano mzuri wa kuhudumia mahitaji ya kiroho ya wengine, iwe ni kina nani.
Au, kufanya kazi ya hekalu—kutafuta majina ya mababu zetu na kuwapatia baraka za milele? Ni njia takatifu iliyoje ya kuhudumu.
Fikiria kitendo cha kuwatafuta masikini na wenye uhitaji, kunyoosha mikono iliyolegea, au kuwabariki wagonjwa na wanaoteseka. Je, haya si matendo hasa ya huduma safi Bwana aliyofanya wakati Alipotembea duniani?
Kama wewe si muumini wa Kanisa, ninakualika “njoo uone.”20 Njoo, na ujiunge nasi! Kama wewe ni muumini wa Kanisa lakini kwa sasa hushiriki kikamilifu, ninakualika: tafadhali rudi. Tunakuhitaji!
Njoo, ongeza nguvu yako kwenye yetu.
Kwa sababu ya vipaji vyako, uwezo, na hulka ya kipekee, utatusaidia kuwa wazuri zaidi na wenye furaha zaidi. Kama malipo, tutakusaidia kuwa mzuri zaidi na mwenye furaha vilevile.
Njoo, tusaidie kujenga na kuimarisha utamaduni wa kuponya, ukarimu, na rehema kwa watoto wote wa Mungu. Kwani sote tunajitahidi kuwa viumbe wapya ambapo “ya kale yamepita” na “mambo yote … yamekuwa mapya.”21 Mwokozi anatuonyesha uelekeo wa kwenda—mbele na juu. Anasema, “Mkinipenda, mtazishika amri zangu.”22 Acha sote tufanye kazi pamoja kuwa watu Mungu anaohitaji tuwe.
Huu ndiyo aina ya utamaduni wa injili tunatamani kuujenga kote katika Kanisa la Yesu Kristo. Tunatafuta kuliimarisha Kanisa kama mahali ambapo tunasameheana. Ambapo tunaepuka majaribu ya kutafuta makosa, umbeya, na kuwadharau wengine. Ambapo, badala ya kuonyesha dosari, tunainuana na kusaidiana kuwa bora kadiri tunavyoweza.
Acha niwaalike tena. Njoo uone Jiunge nasi. Tunawahitaji ninyi.
Watu Wasiowakamilifu
Utagundua kwamba Kanisa hili limejaa watu wazuri ulimwengu huu unapaswa kuwa nao. Ni wakaribishaji, wenye upendo, wakarimu, na wa kweli. Wana bidii ya kazi, wanafanya dhabihu, na hata mashujaa wakati mwingine.
Wao pia wana mapungufu ya kuhuzunisha.
Wanafanya makosa.
Mara kwa mara wanasema mambo wasiyopaswa kusema. Wanafanya mambo wanayotamani wasingefanya.
Lakini wana sifa hii ya pamoja—wanataka kubadilika na kusogea karibu na Bwana, Mwokozi wetu, hata Yesu Kristo.
Wanajaribu kufanya ipasavyo.
Wanaamini. Wanapenda. Wanatenda.
Wanataka kutokuwa wabinafsi, wenye huruma zaidi, wastaarabu zaidi, zaidi kama Yesu.
Mpango kwa ajili ya Furaha
Ndiyo, maisha yanaweza kuwa magumu wakati mwingine. Hakika sote tuna nyakati zetu za kukata tamaa na kuvunjika moyo.
Lakini injili ya Yesu Kristo hutoa tumaini. Na, katika Kanisa la Yesu Kristo, tunaungana na wengine wanaotafuta mahali ambapo tutahisi tuko nyumbani—mahali pa kukua ambapo, kwa pamoja, tunaweza kuamini, kupenda, na kutenda.
Bila kujali tofauti zetu, tunatafuta kukumbatiana kama wana na mabinti wa Baba yetu mpendwa wa Mbinguni.
Nina shukrani isiyo kifani kuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho na kujua kwamba Mungu anawapenda watoto Wake vya kutosha kuwapa mpango wa furaha na maana katika maisha haya na njia ya kupata uzoefu wa shangwe ya milele ndani ya kumbi za utukufu katika maisha yajayo.
Nina shukrani kwamba Mungu ametupatia njia ya kupona ugonjwa wa nafsi na Weltschmerz za maisha.
Ninashuhudia na kuwaachia baraka zangu kwamba pale tunapoamini katika Mungu, tunapompenda Yeye na tunapowapenda watoto Wake kwa mioyo yetu yote, na tunapojitahidi kutenda kama Mungu alivyotuelekeza, tutapata uponyaji na amani, furaha na maana. Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.