Nyamaza, Utulie
Mwokozi anatufundisha jinsi ya kujisikia amani na utulivu hata wakati upepo unapovuma vibaya kutuzunguka sisi na kusukuma mawimbi yenye kutishia kuzamisha matumaini yetu.
Wakati watoto wetu wakiwa wadogo, familia yetu ilikaa siku chache karibu na ziwa zuri. Mchana baadhi ya watoto walivaa jaketiokozi kabla ya kuruka kutoka kwenye sehemu ya kurukia na kuingia kwenye maji. Binti yetu mdogo alitizama kwa kusita, kwa makini akiwachunguza ndugu zake. Kwa ujasiri wote alioweza kuwa nao, aliziba pua yake kwa mkono mmoja na kuruka. Punde alijitokeza juu gafla akiwa na hamaki kidogo katika sauti yake na kupiga kelele, “Nisaidie! Nisaidie!”
Sasa, hakuwa katika hatari yoyote ya kimwili, jaketi lake okozi lilikuwa linafanya kazi yake na alikuwa akielea salama. Tungeweza kumfikia na kumtoa na kumvuta nyuma kwenye sehemu ya kurukia kwa jitihada kidogo tu. Bado, kutokana na mtizamo wake, yeye alihitaji msaada. Labda ilikuwa ni baridi ya maji au upya wa uzoefu. Kwa njia yoyote, alipanda juu mpaka kwenye sehemu ya kurukia, ambapo tulimzungushia taulo kavu na kumsifia kwa ujasiri wake.
Iwe sisi ni wazee au vijana, wengi wetu tumo, katika nyakati za hofu, ikitamkwa kwa maneno ya dharura kama “Nisaidie!” “Niokoe!” au “Tafadhali, jibu sala yangu!”
Tukio kama hili liliwatokea vile vile wafuasi wa Yesu wakati wa Huduma Yake duniani. Katika Marko tunasoma kwamba Yesu “alianza tena kufundisha kandokando mwa bahari: na walikusanyika kwake watu wengi.”1 Umati ulikuwa mkubwa kiasi kwamba Yesu “aliingia kwenye mashua”2 na kuongea akiwa kwenye staha yake. Kwa siku yote nzima aliwafundisha watu kwa mafumbo wakiwa wamekaa mwaloni.
“Na … wakati [jioni] ilipowadia,” Aliwaambia wanafunzi Wake, “Na tuvuke mpaka ng’ambo. Na wakati walipo uruhusu umati kwenda mbali,”3 waliondoka ukingoni mwa bahari na walikuwa wakivuka Bahari ya Galilaya. Alipopata nafasi nyuma ya mashua,Yesu alilala chini na haraka alipatwa na usingizi. Punde “palitokea dhoruba kuu na upepo, na mawimbi yakapiga chombo, hata [kikaanza] kujaa”4 maji.
Wanafunzi wengi wa Yesu walikuwa wavuvi wazoefu na walijua namna ya kushughulikia mashua nyakati za dhoruba. Walikuwa wanafunzi Wake walio waaminifu—ndiyo, wafuasi Wake—wapendwa. Waliacha kazi, matakwa yao binafsi, na familia ili kumfuata Yesu. Imani yao Kwake ilishuhudiwa na uwepo wao kwenye mashua. Na sasa mashua yao ilikuwa katikati ya dhoruba na katika hatari ya kuzama.
Hatujui ni kwa muda gani walipigana kuiweka mashua ielee kwenye dhoruba, ila walimwamsha Yesu wakiwa na taharuki kidogo katika sauti zao, wakisema:
“Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia?”5
“Bwana, tuokoe: tunaangamia.”6
Walimwita Yeye “Bwana,” na kwamba Ndiye. Na pia ni Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, Baba wa mbingu na dunia, Muumba wa vitu vyote tangu mwanzo.”7
Kutoka sehemu Aliyokuwa kwenye mashua,Yesu alisimama na kuukemea upepo na kuiambia bahari “Nyamaza, utulie. Na upepo [ulitulia], na kulikuwepo na utulivu mkubwa.”8 Akiwa Bwana na Mwalimu, Yesu tena aliwafundisha wanafunzi Wake kupitia maswali mawili mepesi lakini kwa upendo. Aliwauliza.
“Mbona mmekuwa waoga?”9
“Imani yenu iko wapi?”10
Kuna tabia ya kimwili, na hata jaribu, pale tunapojikuta katikati ya majaribu, matatizo, au mateso kiasi cha kulia, “Bwana, hujali kuwa naangamia? Niokoe mimi.” Hata Joseph Smith alisihi kutoka kwenye gereza baya, “Ee Mungu, uko wapi?” Na ni wapi lilipo hema lifichalo mahali pako pa kujificha?”11
Hakika, Mwokozi wa dunia anaelewa ukomo wetu wa kimwili, kwani Yeye hutufundisha namna ya kujisikia amani na utulivu hata kama upepo utavuma kwa nguvu kutuzunguka na kusukuma mawimbi yakitishia kuzamisha matumaini yetu.
Kwa wale wenye imani iliyothibitika, au hata chembe ndogo ya imani,12 Yesu anaalika, akisema: “Njooni kwangu.”13 “Amini kwa jina langu.”14 “Jifunze kwangu, na sikiliza maneno yangu.”15 Kwa upole anaamuru, “Tubuni na [mka] batizwe katika jina langu,”16 “pendaneni; kama mimi nilivyo wapenda ninyi”17 na “Daima mnikumbuke.”18 Yesu anatuhakikishia tena, akieleza, “Haya mambo nimeyaongea kwenu, ili ndani yangu mpate kuwa na amani. Ulimwenguni mtakuwa na dhiki: lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.”19
Naweza kufikiria kuwa wafuasi wa Yesu ndani ya mashua iliyokuwa ikipigwa na dhoruba, walilazimika, kuwa na shughuli ya kuangalia mawimbi yakigonga kwenye staha yao na wao wakiyatoa nje. Naweza kuvuta taswira ya wao wakishikilia tanga wakijaribu kuweka mlingano wa kuongoza mashua yao ndogo. Fokasi yao ilikuwa kwenye kupona wakati huo, na ombi kwa ajili ya msaada lilikuwa la dharura na la dhati.
Wengi wetu hatuko tofauti katika siku yetu. Matukio ya hivi karibuni katika Ulimwengu na katika nchi zetu, jumuiya, na familia yametutafuna kwa majaribu yasiyotabirika. Katika nyakati za matatizo imani yetu inaweza kuhisi imefikia kikomo cha uvumilivu na uelewa wetu. Mawimbi ya woga yanaweza kutusumbua, kutusababisha tusahau wema wa Mungu, hivyo kuacha mtizamo wetu kutoona-mbali na nje ya fokasi. Na bado ni ndani ya mwendo huu mgumu wa safari yetu ndipo imani yetu inapoweza kujaribiwa na kuimarishwa.
Bla kujali hali zetu, tunaweza kwa makusudi kufanya juhudi ya kujenga na kuongeza imani yetu katika Yesu Kristo. Inaimarishwa tunapo kumbuka kwamba sisi ni watoto wa Mungu na Anatupenda. Imani yetu inakua tunapojaribiwa katika neno la Mungu kwa matumaini na unyenyekevu, tukijaribu kwa uwezo wetu wote kufuata mafundisho ya Yesu Kristo. Imani yetu huongezeka tukichagua kuamini kuliko kutia shaka, tunaposamehe badala ya kuhukumu, tunapotubu badala ya kuwa wakaidi. Imani yetu inatakaswa wakati bila kukoma tunategemea huruma na rehema na neema ya Masiya Mtakatifu.20
“Wakati imani si maarifa kamili,” Mzee Neal A. Maxwell alisema, “inaleta mategemeo ya kina katika Mungu, ambaye maarifa yake ni makamilifu!”21 Hata katika nyakati za matatizo, imani katika Bwana Yesu Kristo ni ya uvumilivu na thabiti. Inatusaidia kupita vizuizi visivyo vya muhimu. Inatutia moyo tuendelee kusonga mbele katika njia ya maagano. Imani hutuvusha kupita ukataji tamaa na huturuhusu kukabiliana na nyakati zijazo tukiwa na azimio na utayari. Ina tushawishi kuomba uokozi na msaada tuombapo kwa Baba katika jina la Mwanawe. Na wakati maombi yetu yanapoonekana kutojibiwa, imani yetu imara katika Yesu Kristo huzaa subira, unyenyekevu, na uwezo kwa utulivu kutamka maneno, “Mapenzi yako yatimizwe.”22
Rais Russell M. Nelson amefundisha:
“Hatuhitaji kuruhusu hofu yetu ichukue nafasi ya imani yetu. Tunaweza kukabiliana na hofu hizo kwa kuimarisha imani yetu.
“Anzeni na watoto wenu. … Acha waone imani yenu, hata kama majaribu makali yanakuja juu yenu. Acha imani ielekezwe kwa Baba yetu mpendwa wa Mbinguni na Mwanaye Mpendwa, Bwana wetu Yesu Kristo. Mfundishe kila mvulana au msichana aliye wa thamani kwamba wao ni watoto wa Mungu, waliumbwa katika mfano Wake, wakiwa na lengo takatifu na uwezekano wa kuwa. Kila mtu amezaliwa na changamoto za kuzishinda na imani ya kukuza.”23
Hivi karibuni nilisikia watoto wawili wa umri wa miaka minne wakishiriki imani yao katika Yesu Kristo walipojibu swali “Yesu Kristo anakusaidiaje wewe?” Mtoto wa kwanza alisema,“Najua Yesu ananipenda kwa sababu alikufa kwa ajili yangu. Vile vile anawapenda wakubwa.” Mtoto wa pili alisema, “Ananisaidia ninapokuwa kwenye machungu au mwenye hasira. Ananisaidia pia ninapokuwa nazama.”
Yesu alitamka, “Kwa hiyo, yeyote anayetubu na kuja kwangu kama mtoto mdogo yeye, nitampokea, kwani hivyo ndivyo ulivyo ufalme wa Mungu.”24
“Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanaye wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.”25
Hivi karibuni, Rais Nelson aliahidi “kwamba hofu iliyopungua na imani iliyoongezeka vitafuata” wakati “tunapoanza upya kwa dhati kusikiliza, kufuata, na kutii maneno ya Mwokozi.”26
Akina dada na kaka, hali za changamoto zetu za sasa sio kikomo cha safari yetu ya milele. Kama waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, tumejichukulia juu yetu jina la Yesu Kristo kwa maagano. Tuna imani katika nguvu zake za kukomboa na matumaini katika ahadi Zake kubwa na za thamani. Tuna kila sababu ya kushangilia, kwa sababu Bwana na Mwokozi wetu anafahamu kwa makini matatizo yetu, hali, na masikitiko yetu. Kama vile Yesu alivyokuwa na wafuasi wake wa zamani, Yupo katika mashua yetu! Ametoa uhai Wake ili mimi na wewe tusiangamie. Na tumwamini Yeye, tutii amri Zake, na kwa imani tumsikilize akisema, “Nyamaza, utulie.”27 Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.