Akina Dada katika Sayuni
Mtakuwa nguvu muhimu katika kuikusanya Israeli na katika kutengeneza watu wa Sayuni.
Dada zangu wapendwa, nimebarikiwa kuzungumza katika kipindi hiki cha wakati mzuri katika historia ya ulimwengu. Kila siku, tunasogea karibu na wakati mtukufu ambapo Mwokozi Yesu Kristo, atarudi duniani tena. Tunafahamu kitu juu ya matukio ya kuogofya yatakayo tangulia ujio Wake, lakini bado mioyo yetu inavimba kwa shangwe na kujiamini pia kwa kujua ahadi tukufu ambazo zitatimizwa kabla ya Yeye kurudi.
Kama mabinti wapendwa wa Baba wa Mbinguni, na kama mabinti wa Bwana Yesu Kristo katika ufalme Wake, 1 mtakuwa na sehemu muhimu kwenye nyakati tukufu zijazo. Tunafahamu kwamba Mwokozi atakuja kwa watu waliokusanywa na kutayarishwa kuishi kama vile watu walivyofanya katika mji wa Henoko. Watu huko walikuwa wameungana katika imani katika Yesu Kristo na walikuwa wasafi kikamilifu kwamba walinyakuliwa juu mbinguni.
Hapa ni maelezo ya Bwana yaliyofunuliwa ya kile ambacho kingetokea kwa watu wa Henoko na ambacho kitatokea katika kipindi hiki cha mwisho cha utimilifu wa nyakati:
“Nayo siku yaja ambayo dunia itapumzika, lakini kabla ya siku ile mbingu zitatiwa giza, na pazia la giza litaifunika dunia; na mbingu zitatikisika, na dunia pia; na dhiki kubwa itakuwa miongoni mwa watoto wa watu, lakini watu wangu nitawalinda;
“Na haki nitaishusha kutoka mbinguni; na ukweli nitaueneza kutoka duniani, ili kutoa ushuhuda juu ya Mwanangu wa Pekee; ufufuko wake kutoka kwa wafu; ndio, na pia ufufuko wa watu wote; na haki na ukweli nitasababisha ziifagie dunia kama kwa gharika, ili kuwakusanya wateule wangu kutoka robo nne za dunia, kwenda mahali ambapo nitapatayarisha, Mji Mtakatifu, kwamba watu wangu wapate kufunga viuno vyao, na wawe wakitazamia wakati wa kuja kwangu; kwani huko litakuwa hema langu, napo pataitwa Sayuni, Yerusalemu Mpya.
“Na Bwana akamwambia Henoko: Halafu wewe na mji wako wote mtakutana nao huko, nasi tutawapokea kifuani mwetu, nao watatuona; nasi tunawaangukia shingoni mwao, nao wataanguka shingoni mwetu, nasi tutapigana busu;
“Na huko kutakuwa na makao yangu, nayo itakuwa Sayuni, ambayo itajitenga kutoka kwa viumbe vyote nilivyovifanya; na kwa kitambo cha miaka elfu dunia itapumzika.” 2
Ninyi akina dada, mabinti zenu, wajukuu zenu, na wanawake mlio walea watakuwa katika kiini cha kujenga jamii hiyo ya watu ambao watajiunga katika ushirika mtukufu pamoja na Mwokozi. Mtakuwa nguvu muhimu katika kuikusanya Israeli na katika kutengeneza watu wa Sayuni ambao wataishi kwa amani katika Yerusalemu Mpya.
Bwana, kupitia manabii Wake, ametoa ahadi kwenu. Katika siku za mwanzo za Muungano wa Usaidizi, Nabii Joseph Smith alisema kwa akina dada, “Ikiwa mtaishi kustahili fursa zenu, malaika hawawezi kuzuiliwa kuwa washirika wenu.” 3
Uwezekano huo wa ajabu upo ndani yenu, na ninyi mnaandaliwa kwa ajili ya hilo.
Rais Gordon B. Hinckley alisema:
“Ninyi akina dada … hamshikilii nafasi ya pili katika mpango wa Baba yetu kwa ajili ya furaha ya milele na ustawi wa watoto Wake. Ninyi hakika ni sehemu muhimu ya mpango huo.
“Bila ninyi mpango usingefanya kazi. Bila ninyi mpango wote wa wokovu ungevurugika. …
“Kila mmoja wenu ni binti wa Mungu, aliyevikwa haki ya uzaliwa ya kiungu. 4
Nabii wetu wa sasa, Rais Russell M. Nelson, ametoa ufafanuzi huu juu ya sehemu mliyonayo katika kujitayarisha kwa ajili ya ujio wa Mwokozi:
“Haitawezekana kupima ushawishi ambao … wanawake wanao, si tu kwa familia lakini pia katika Kanisa la Bwana, kama wake, akina mama, na akina bibi; kama akina dada na mashangazi; kama walimu na viongozi; na hususani kama mifano na walinzi wa dhati wa imani.
“Hii imekuwa kweli katika kila kipindi cha injili tangu siku za Adamu na Hawa. Na bado wanawake wa kipindi hiki ni tofauti na wanawake wa vipindi vingine kwa sababu kipindi hiki ni tofauti na vingine. Tofauti hii huleta vyote fursa na majukumu.” 5
Kipindi hiki cha maongozi ya Mungu ni tofauti kwa sababu Bwana atatuongoza kuwa waliojitayarisha ili kuwa kama Mji wa Henoko. Yeye amefafanua kupitia mitume na manabii Wake kile ambacho badiliko hilo la kuwa watu wa Sayuni humaanisha.
Mzee Bruce R. McConkie alifundisha:
“Siku ya [Henoko] ilikuwa ya uovu na mbaya, siku ya giza na uasi, siku ya vita na ukiwa, siku iliyoongoza kwenye kusafishwa kwa dunia kwa maji.
“Henoko, hata hivyo, alikuwa mwaminifu. ‘Alimwona Bwana,’ na kusema naye ‘uso kwa uso’ kama vile mtu asemavyo na mwingine. (Musa 7:4.) Bwana alimtuma kutangaza toba kwa ulimwengu, na kumpa mamlaka ya ‘kubatiza katika jina la Baba, na la Mwana, aliyejaa neema na ukweli, na la Roho Mtakatifu, awashuhudiaye Baba na Mwana.’ (Musa 7:11.) Henoko alifanya maagano na kuleta pamoja mkusanyiko wa waaminio wa kweli, ambao wote walikuwa waaminifu sana kiasi kwamba ‘Bwana alikuja na kukaa pamoja na watu wake, nao walikaa katika haki,’ na walibarikiwa kutoka juu. ‘Na Bwana akawaita watu wake Sayuni, kwa sababu wao walikuwa wa moyo mmoja na wazo moja, na waliishi katika haki; na hapakuwa na maskini miongoni mwao.’ (Musa 7:18.) …
“Baada ya Bwana kuwaita watu wake Sayuni, maandiko yanasema kwamba Henoko ‘alijenga mji ambao uliitwa Mji Mtakatifu, hata Sayuni;’ na kwamba Sayuni ‘ikatwaliwa juu mbinguni’ ambapo ‘Mungu aliipokea kifuani mwake yeye mwenyewe; na “kutokea hapo ukaenea uvumi ukisema, Sayuni imekimbia.’ (Musa 7:19, 21, 69.) …
“Sayuni hii iliyotwaliwa juu mbinguni itarejea … wakati Bwana atakaporejesha tena Sayuni, na wakaao ndani yake wataungana na Yerusalemu mpya, ambayo itajengwa kwa wakati huo.” 6
Ikiwa yaliyopita ni sehemu muhimu ya yajayo, wakati wa kurudi kwa Mwokozi, mabinti ambao wana msimamo wa kina kwenye maagano yao na Mungu watakuwa zaidi ya nusu ya wale ambao wamejitayarisha kumkaribisha Yeye wakati Atakapokuja. Lakini bila kujali idadi, mchango wenu katika kujenga umoja kati ya watu waliojitayarisha kwa ajili ya Sayuni hiyo utakuwa mkubwa zaidi ya nusu.
Nitawaambia kwa nini ninaamini hilo litakuwa hivyo. Kitabu cha Mormoni kinatoa maelezo ya watu wa Sayuni. Mnakumbuka kwamba ilikuwa ni baada ya wao kufundishwa, kupendwa, na kubarikiwa na Mwokozi aliyefufuka kwamba “hakukuwa na ubishi katika nchi, kwa sababu ya mapenzi ya Mungu ambayo yaliishi katika mioyo ya watu.” 7
Uzoefu wangu umenifundisha kwamba mabinti wa Baba wa Mbinguni wanayo karama ya kuondoa ubishi na kukuza haki kwa upendo wao kwa Mungu na kwa upendo wa Mungu wanawasaidia wale wanaowatumikia.
Niliona hilo katika ujana wangu wakati tawi letu dogo lilipokutana katika nyumba yangu ya utotoni. Mimi na kaka yangu ndiyo pekee tuliokuwa na Ukuhani wa Haruni, baba yangu pekee mwenye Ukuhani wa Melkizedeki. Rais wa Muungano wa Usaidizi kwenye tawi alikuwa muongofu ambaye mumewe hakufurahia huduma yake kwa Kanisa. Waumini walikuwa akina dada wakubwa wote wasio na ukuhani katika nyumba zao. Nilimtazama mama yangu pamoja na akina dada hao wakipendana, kuinuana, na kujaliana wao kwa wao bila kuchoka. Ninatambua sasa kwamba nilipewa mapema kuiona Sayuni kidogo tu.
Mafunzo yangu kwenye ushawishi wa wanawake waaminifu yaliendelea katika tawi dogo la Kanisa huko Albuquerque, New Mexico. Niliwatazama mke wa rais wa tawi, mke wa rais wa wilaya, na rais wa Muungano wa Usaidizi wakigusa moyo wa kila mgeni na muongofu. Jumapili niliyoondoka Albuquerque, baada ya miaka miwili ya kutazama ushawishi wa akina dada huko, kigingi cha kwanza kiliundwa. Sasa Bwana ameweka hekalu huko.
Nilihamia jirani na Boston, ambapo nilitumikia katika urais wa wilaya ambao ulisimamia matawi madogo yaliyosambaa kwenye majimbo mawili. Kulikuwa na mabishano ambayo kwa zaidi ya mara moja yalitatuliwa na wanawake wenye upendo na wenye kusamehe ambao walisaidia kulainisha mioyo. Jumapili niliyoondoka Boston, mshiriki wa Urais wa Kwanza alianzisha kigingi cha kwanza huko Massachusetts. Kuna hekalu huko sasa, karibu na ambapo rais wa wilaya alikuwa akiishi. Alikuwa ameletwa kwenye shughuli ya Kanisa na baadaye aliitwa kutumikia kama rais wa kigingi na kisha kama rais wa misheni, akishawishiwa na mke wake mwaminifu na mwenye upendo.
Akina dada, mlipewa baraka ya kuwa mabinti wa Mungu wenye karama maalum. Mlileta pamoja nanyi katika maisha haya uwezo wa kiroho wa kulea wengine na kuwainua juu kuelekea upendo na usafi ambao utawastahilisha wao kuishi pamoja katika jamii ya Sayuni. Si kwa bahati mbaya kwamba Muungano wa Usaidizi, kikundi cha kwanza cha Kanisa maalum kwa mabinti wa Baba wa Mbinguni, kina kauli mbiu yake “Hisani Haikosi Kufaulu Kamwe.”
Hisani ni upendo msafi wa Kristo. Na ni imani katika Yeye na matokeo kamili ya Upatanisho Wake usio na mwisho ambavyo vitakustahilisha wewe, na wale unaowapenda na kuwatumikia, kwa ajili ya zawadi ya mbinguni ya kuishi katika ujamaa wa Sayuni iliyotazamiwa na kuahidiwa. Huko mtakuwa akina dada katika Sayuni, mkipendwa binafsi na Bwana pamoja na wale mlio wabariki.
Ninashuhudia kwamba ninyi ni raia wa ufalme wa Bwana hapa duniani. Ninyi ni mabinti wa Baba wa Mbinguni mwenye upendo, ambaye amewaleta ulimwenguni mkiwa na vipawa vya kipekee ambavyo mliahidi kuvitumia ili kuwabariki wengine. Ninawaahidi kwamba Bwana atawapa mwongozo na usaidizi, kupitia Roho Mtakatifu. Atawatangulia mbele wakati mnapomsaidia Yeye kuwatayarisha watu Wake kuwa Sayuni Yake iliyoahidiwa. Ninashuhudia hivyo, katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.