Ninaamini katika Malaika
Mwokozi anafahamu changamoto unazokabiliana nazo. Anakujua, Anakupenda, na ninakuahidi, Atakutumia malaika wakusaidie.
Akina kaka na dada, ninaamini katika malaika, na ningependa kushiriki nanyi uzoefu wangu kuhusiana nao. Kwa kufanya hivyo, natumaini na ninaomba kwamba tutatambua umuhimu wa malaika katika maisha yetu.
Haya ni maneno ya Mzee Jeffrey R. Holland kutoka mkutano mkuu uliopita: “Tunapozungumzia kuhusu wale ambao ni vyombo katika mkono ya Mungu, tunakumbushwa kwamba si malaika wote wanatoka upande wa pili wa pazia. Wengine wao tunatembea nao na kuongea nao—hapa, sasa, kila siku. Baadhi yao wanaishi kwenye ujirani wetu. … Hakika, mbingu hazijawahi kuwa karibu zaidi kama pale tunapoona upendo wa Mungu ukionekana katika ukarimu na kujitoa kwa watu wazuri na wasafi kiasi kwamba malaika ndio neno pekee linalokuja akilini” (“Huduma ya Malaika” Liahona, Nov. 2008, 30).
Ni kuhusu malaika katika upande huu wa pazia ninaotaka kuwaongelea. Malaika wanaotembea kati yetu katika maisha yetu ya kila siku ni wenye nguvu za kutukumbusha upendo wa Mungu kwetu.
Malaika wa kwanza nitakaowataja ni wadada wawili wamisionari walionifundisha injili nilipokuwa mvulana, Dada Vilma Molina na Dada Ivonete Rivitti. Dada yangu mdogo na mimi tulialikwa kwenye shughuli ya Kanisa ambapo ndipo tulipokutana na hawa malaika wawili. Sikuwahi kufikiria kwa kiasi gani shughuli hiyo nyepesi ingebadili maisha yangu.
Wazazi na ndugu zangu hawakupendelea kujifunza zaidi juu ya Kanisa kwa wakati huo. Hawakupenda hata kuwa na wamisionari nyumbani kwetu, hivyo nilijifunza masomo ya wamisionari katika jengo la Kanisa. Chumba kile kidogo katika kanisa kwangu kilikuwa “kichaka kitakatifu.”
Mwezi mmoja baada ya hawa malaika kunieleza juu ya injili, nilibatizwa. Nilikuwa na umri wa miaka 16. Kwa bahati mbaya, sina picha ya tukio hili takatifu, lakini nina picha ya dada yangu na mimi tuliposhiriki katika shughuli ile. Nitahitaji kufafanua nani ni nani katika picha hii. Mimi ni huyo mrefu upande wa kulia.
Kama unavyoweza kufikiria, kubakia mshiriki kamili Kanisani ilikuwa ni changamoto kwa kijana ambaye mfumo wa maisha ulibadilika na ambaye familia yake walikuwa hawafuati njia moja.
Wakati nilipokuwa najaribu kuingia katika maisha mapya, utamaduni mpya, na marafiki wapya, nilijihisi kuwa nje ya mfumo. Nilijisikia mpweke na kukata tamaa mara nyingi. Nilijua Kanisa lilikuwa la kweli, lakini nilikuwa na wakati mgumu kujisikia kama sehemu yake. Wakati sina amani wala utulivu nilipokuwa nikijaribu kuendana na dini yangu mpya, nilipata ujasiri wa kushiriki katika mkutano wa siku tatu wa vijana, ambao nilifikiri ungenisaidia kupata marafiki wapya. Hapa ndipo nilipokutana na malaika mwingine wa uokoaji, aitwaye Mônica Brandão.
Alikuwa ni mgeni katika eneo, akiwa amehamia toka sehemu nyingine ya Brazil. Kwa haraka alishika hisia zangu na, bahati kwangu, alinikubalia kama rafiki. Nadhani aliniangalia zaidi kwa ndani kuliko kwa nje.
Kwa sababu alinifanya kuwa rafiki yake, alinitambulisha kwa rafiki zake, ambao pia wakawa rafiki zangu kadiri tulivyofurahia shughuli nyingi za vijana nilizohudhuria. Shuguli hizi zilikuwa mahususi kwa ajili ya kujumuika katika maisha haya mapya.
Rafiki hawa wazuri walileta mabadiliko makubwa, ila bila ya injili kufundishwa nyumbani kwetu pamoja na familia inayoniunga mkono bado iliweka uogofu wangu katika hatari. Uhusiano wangu wa injili Kanisani ulikuwa ni wa muhimu zaidi katika ukuaji wangu wa uongofu. Kisha malaika wawili zaidi walitumwa na Bwana kusaidia.
Mmojawapo alikuwa Leda Vettori, mwalimu wangu wa seminari ya asubuhi. Kupitia upendo wake wa kunikubali na darasa la kuhamasisha, alinipa kila siku kiwango cha “maneno mazuri ya Mungu” (Moroni 6:4), ambayo yalihitajika katika siku yangu yote. Hii ilinisaidia kupata nguvu za kiroho za kuniwezesha kusonga mbele.
Malaika mwingine aliyetumwa kwangu kunisaidia alikuwa ni rais wa Wavulana, Marco Antônio Fusco. Pia alipangiwa kuwa mwenza wangu mkubwa katika mafundisho ya nyumbani. Licha ya kutokuwa na uzoefu na tofauti ya mwonekano, alinipa kazi ya kufundisha katika mikutano yetu ya akidi ya ukuhani na ualimu wa nyumbani. Alinipa nafasi ya kutenda na kujifunza na si kuwa tu mtazamaji wa injili. Aliniamini, kuliko nilivyojiamini mwenyewe.
Asante kwa malaika hawa wote, na wengine wengi niliokutana nao wakati wa miaka hiyo muhimu ya mwanzo, nilipata nguvu za kutosha za kubakia kwenye njia ya agano kadiri nilivyopata ushuhuda wa kiroho wa ukweli.
Pamoja na yote, yule binti mdogo malaika, Mônica? Baada ya sote kutumikia misheni, alikuwa mke wangu.
Sifikirii kama ilikuwa ni bahati nasibu tu kwamba marafiki wazuri, majukumu ya Kanisa, na kulishwa kwa neno zuri la Mungu vilikuwa ni sehemu ya mchakato huo. Rais Gordon B. Hinckley kwa busara alifundisha: “Si jambo rahisi kufanya mabadiliko kwa ghafla kujiunga na Kanisa hili. Inamaanisha kuvunja mahusiano ya kale. Inamaanisha kupoteza marafiki. Inaweza kumaanisha kuweka pembeni imani ulizozithamini. Inaweza kuhitaji mabadiliko ya tabia na kuzuia matamanio. Katika hali nyingi inamaanisha upweke na hata hofu ya visivyojulikana. Lazima kuwepo na kulelewa na kuimarishwa wakati wa kipindi hiki kigumu cha maisha ya muumini mpya” (“There Must Be Messengers,” Ensign, Oct. 1987, 5).
Baadae alifundisha,“Kila mmoja wao anahitaji vitu vitatu: rafiki, jukumu, na kulishwa kwa ‘neno zuri la Mungu’” (“Converts and Young Men,” Ensign, May 1997, 47).
Kwa nini ninashiriki uzoefu huu nanyi?
Kwanza, ni kutuma ujumbe kwa wale wote wanaopitia katika hali sawa na hiyo kwa sasa. Labda wewe ni muumini mpya, au unarudi Kanisani baada ya kuhangaika huko kwa muda, au unajaribu kuwa sehemu ya. Tafadhali, tafadhali, usikate tamaa katika jitihada zako za kuwa sehemu ya familia hii kubwa. Ni Kanisa la kweli la Yesu Kristo!
Inapohusu furaha yako na wokovu, daima ni jambo la thamani kuendelea kujaribu. Ni jambo la thamani kurekebisha mfumo wa maisha yako na tamaduni. Mwokozi anafahamu changamoto unazokabiliana nazo. Anakujua, Anakupenda, na ninakuahidi, Atakutumia malaika wakusaidie.
Kwa maneno yake mwenyewe Mwokozi alisema: “Nitakwenda mbele ya uso wenu. Nitakuwa mkono wenu wa kuume na wa kushoto, … na Roho wangu atakuwa [mioyoni] mwenu, na malaika zangu watawazingira, ili kuwabeba juu” (M&M 84:88).
Shabaha yangu ya pili kushiriki uzoefu huu ni kutuma ujumbe kwa waumini wote wa Kanisa—kwetu sisi sote. Tunapaswa kukumbuka kwamba sio rahisi kwa waumini wapya, marafiki wanaorudi kanisani, na wale wenye mfumo tofauti wa maisha kwa haraka kuchangamana. Bwana anajua changamoto wanazokabiliana nazo, na Anatafuta malaika walio tayari kusaidia. Bwana daima anatafuta walio tayari kujitolea kuwa malaika katika maisha ya wengine.
Akina kaka na dada, mgependa kuwa chombo katika mikono ya Bwana? Ungependa kuwa mmojawapo wa malaika hawa? Kuwa mjumbe, aliyetumwa kutoka kwa Mungu, kutoka upande huu wa pazia, kwa mtu ambaye Bwana ana wasiwasi naye? Anakuhitaji. Wanakuhitaji.
Ndiyo, tunaweza kuwategemea wamisionari wetu. Daima wapo, ni wa kwanza kujisajili kwenye kazi hii ya malaika. Ila hawatoshi.
Kama ukiangaza kwa umakini, utagundua wengi wanahitaji usaidizi wa malaika. Watu hawa sio lazima wawe wamevaa shati nyeupe, gauni, au vazi lolote stahiki la Jumapili. Wanaweza kuwa wamekaa peke yao, nyuma ya kanisa au darasa, wakati mwingine wakihisi kuwa hawaonekani. Labda mtindo wa nywele zao umepitiliza kiwango au msamiati wao ni tofauti, lakini wapo, na wanajaribu.
Wengine wanaweza kujiuliza: “Niendelee kuhudhuria? Je, niendelee kujaribu? Wengine wanaweza kujiuliza kama siku moja watahisi wamekubaliwa na kupendwa. Malaika wanahitajika, hivi sasa, malaika walio tayari kuacha starehe zao kuwakumbatia wao; “[Watu walio] wazuri na safi kwamba umalaika ndio neno pekee ambalo huja katika fikra ili [kuwaelezea]” (Jeffrey R. Holland, “Huduma ya Malaika,” 30).
Akina kaka na dada, naamini katika malaika! Sote tuko hapa leo, kundi kubwa la malaika tukiwa tumetengwa kwa ajili ya siku hizi za mwisho, kuhudumia wengine kama mwendelezo wa mikono ya Muumba mwenye upendo. Ninaahidi kwamba kama tu radhi kutumikia, Bwana atatupatia fursa za kuwa malaika wahudumu. Anajua nani anahitaji msaada wa kimalaika, na Atawaweka katika njia zetu. Bwana huwaweka wale wanaohitaji msaada wa kimalaika katika njia zetu kila siku.
Ninashukrani kwa ajili ya malaika wengi ambao Bwana amewaweka katika njia yangu kipindi chote cha maisha yangu. Walihitajika. Ninashukrani kwa ajili ya injili Yake inayotusaidia kubadilika na kutupa fursa ya kuwa wazuri zaidi.
Hii ni injili ya upendo, injili ya kuhudumia. Juu ya hili ninashuhudia katika jina la Yesu Kristo, amina.