Mkutano Mkuu
Mtafuteni Kristo katika Kila Wazo
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2020


14:47

Mtafuteni Kristo katika Kila Wazo

Kupambana dhidi ya majaribu kunachukua juhudi na uaminifu wa maisha yote. Lakini tafadhali fahamuni kwamba Bwana yuko tayari kutusaidia.

Katika wimbo wake wa zaburi wa sifa, Mtunga Zaburi alitamka:

“Ee Bwana, umenichunguza, na kunijua.

“Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu, umelifahamu wazo langu tokea mbali.

“Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu, umeelewa na njia zangu zote.”1

Katika shairi hili lenye mfanano wa kisemantiki, Mtunga Zaburi anatukuza sifa za kiungu za yeye mwenye maarifa yote kwa sababu hakika Yeye anajua kila kipengele cha nafsi zetu.2 Kujua yote ambayo ni muhimu kwetu sisi katika maisha haya, Mwokozi anatualika sisi kumtafuta Yeye katika kila wazo na kumfuata Yeye kwa moyo wetu wote.3 Hii inatupa sisi ahadi kwamba tunaweza kutembea katika nuru yake na kwamba mwongozo Wake unazuia nguvu ya giza katika maisha yetu.4

Kumtafuta Kristo katika kila wazo na kumfuata Yeye kwa moyo wetu wote kunahitaji kwamba tufungamanishe mawazo na matamanio yetu Kwake.5 Maandiko yanarejelea mfungamano huu kama “[kusimama] imara katika Bwana.”6 Mwenendo huu wa matendo unadokeza kwamba sisi daima tunaendesha maisha yetu sambamba na injili ya Kristo na kufokasi kila siku kwenye kila kitu ambacho ni chema.7 Hapo ndipo tunaweza kupata “amani ya Mungu, ipitayo akili zote” na ambayo itahifadhi mioyo [yetu] na nia zetu katika Kristo Yesu.”8 Mwokozi mwenyewe aliwapa maelekezo wazee wa Kanisa mnamo Februari 1831, “Yatunzeni mambo haya katika mioyo yenu, na taadhima ya milele iwe akilini mwenu.”9

Licha ya jitihada zetu endelevu za kumtafuta Bwana, mawazo yasiyo sahihi yanaweza kupenya akili zetu. Mawazo ya jinsi hii yakiruhusiwa na hata kualikwa kukaa, yanaweza kuyapa umbo matamanio ya mioyo yetu na kutuongoza kwenye kile tutakachokuwa katika maisha haya na hatimaye kwenye kile tutakachorithi milele.10 Mzee Neal A. Maxwell wakati mmoja alisisitiza kanuni hii kwa kusema, “Matamanio … huamua viwango katika matokeo, ikijumuisha kwa nini ‘wengi huitwa, lakini wateule ni wachache.’”11

Manabii wetu wa kale na wa sasa daima wametukumbusha sisi kuepuka majaribu ili kuepuka kupoteza mwenendo wetu wa kiroho na kuwa tuliokanganyikiwa, tusiojifahamu, na tuliokata tamaa katika maisha.

Nikiongea kwa mfano, kujiachia katika majaribu ni sawa sawa na kuikaribia sumaku ukiwa na kifaa cha chuma. Nguvu isiyoonekana ya sumaku hukivuta kifaa cha chuma na kukishikilia kwa nguvu. Sumaku itapoteza nguvu yake juu ya kifaa hicho wakati tu kifaa hicho cha chuma kitakapowekwa mbali na sumaku. Kwa hiyo, kama vile ambavyo sumaku haiwezi kutumia nguvu zake juu ya kifaa cha chuma kilicho mbali, tunapoepuka majaribu, yanafifia mbali na kupoteza nguvu yake kwenye akili na moyo wetu na, kwa hivyo, kwenye matendo yetu.

Analojia hii inanikumbusha juu ya uzoefu mmoja ambao muumini mmoja wa Kanisa aliye mwaminifu sana alinisimulia miaka kadhaa iliyopita. Muumini huyu aliniambia kwamba wakati alipoamka asubuhi ya siku moja, wazo lisilo sahihi ambalo kamwe hakuwahi kulipata kabla pasipo kutegemea liliingia akilini mwake. Ingawa lilimjia pasipo kutarajia kabisa, yeye alipinga hali hiyo ndani ya sekunde chache, akijiambia mwenyewe na kwa wazo hilo, “Hapana!” na akalibadilisha kwa kitu chema ili kuiepusha akili yake kutokana na wazo lile ambalo halikukaribishwa. Aliniambia kwamba alipotumia haki yake ya kujiamulia kimaadili kwa haki, lile wazo hasi, lisilo la hiari punde likatoweka.

Wakati Moroni alipowataka watu kuamini katika Kristo na kutubu, aliwasihi sana waje kwa Kristo kwa mioyo yao yote, wakijivua wenyewe kutokana na uchafu wote. Zaidi ya hayo, Moroni aliwaalika kumwomba Mungu, kwa kusudi imara, ili wasiangukie katika majaribu.12 Kufanyia kazi kanuni hizi katika maisha yetu kunahitaji zaidi tu ya kuamini; kunahitaji kurekebisha akili zetu na mioyo yetu kwenye kanuni hizi za kiungu. Marekebisho ya jinsi hii yanahitaji juhudi binafsi endelevu za kila siku, katika kuongezea kwenye utegemezi wetu kwa Mwokozi, kwa sababu miinamo yetu ya kidunia haitatoweka yenyewe. Kupambana dhidi ya majaribu kunachukua juhudi na uaminifu wa maisha yetu yote. Lakini tafadhali jua kwamba Bwana yuko tayari kutusaidia katika jitihada zetu binafsi na anaahidi baraka kubwa kama tutavumilia hadi mwisho.

Katika wakati mgumu hasa wakati Joseph Smith na wafungwa wenzake katika Jela ya Liberty hawakuwa na uhuru katika chochote isipokuwa wa mawazo yao, Bwana alitoa ushauri wenye msaada na ahadi kwao ambavyo vinatolewa kwetu sisi sote:

“Na moyo wako pia uwe umejaa hisani kwa wanadamu wote, na kwa jamaa ya waaminio, na wema uyapambe mawazo yako bila kukoma; ndipo kujiamini kwako kutakuwa imara katika uwepo wa Mungu; na mafundisho ya ukuhani yatatonatona juu ya roho yako kama umande utokao mbinguni; …

“Roho Mtakatifu atakuwa mwenzi wako daima, na fimbo yako ya kifalme fimbo isiyobadilika ya haki na ukweli.”13

Katika kufanya hivyo, mawazo matakatifu daima yatazipamba akili zetu na matamanio safi yatatuongoza kwenye matendo ya haki.

Moroni pia aliwakumbusha watu wake wasiteketee kwa tamaa zao mbaya.14 Neno tamaa mbaya linamaanisha hamu kubwa isiyo sahihi na ya muda mrefu ya kitu fulani.15 Inajumuisha mawazo yoyote ya giza au tamaa mbaya ambazo zinasababisha mtu kufokasi kwenye desturi za kichoyo au milki za kiulimwengu badala ya kutenda mema, kuwa mkarimu, kutii amri za Mungu, na kadhalika. Mara nyingi inajidhihirisha kupitia hisia kali zaidi za kimwili za nafsi. Mtume Paulo aliziainisha baadhi ya hisia hizi, kama vile “uchafu, uasherati, … chuki, … hasira, ugomvi, … wivu, … na mambo yanayofanana na hayo.”16 Kando na vipengele vyote viovu vya tamaa mbaya, hatuwezi kusahau kwamba adui anaitumia kama silaha ya siri na ya udanganyifu dhidi yetu sisi wakati anapotujaribu tufanye jambo baya.

Wapendwa kaka zangu na dada zangu, ninashuhudia kwamba tunapotegemea juu ya mwamba wa wokovu, Mwokozi wa nafsi zetu, na kufuata ushauri wa Moroni, uwezo wetu wa kudhibiti mawazo yetu utaongezeka kuwa wa maana. Ninaweza kuwahakikishieni kwamba ukomavu wetu kiroho utakua na kuongezeka kasi, ukibadilisha mioyo yetu, ukitufanya kuwa zaidi kama Yesu Kristo. Zaidi ya hayo, ushawishi wa Roho Mtakatifu utakuwa imara zaidi na endelevu katika maisha yetu. Ndipo majaribu ya adui, kidogo kidogo, yatapoteza nguvu yake juu yetu sisi, ikiongoza kwenye maisha ya furaha zaidi na masafi na yaliyowekwa wakfu.

Kwa wale ambao, kwa sababu yoyote ile, wanaangukia majaribuni na kukaa kwenye matendo yasiyo ya haki, ninawahakikishieni kwamba kuna njia ya kurudi, kwamba lipo tumaini katika Kristo. Miaka michache iliyopita, nilipata fursa ya kuongea na muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ambaye alikuwa amepitia wakati mgumu sana katika maisha yake baada ya kufanya kosa kubwa la uvunjaji wa sheria. Nilipomwona mara ya kwanza, niliweza kuona huzuni machoni mwake, iliyoambatana na mwangaza wa tumaini katika uso wake. Mwonekano wake uliakisi moyo mnyenyekevu na moyo uliobadilika. Yeye alikuwa Mkristo aliyejitoa kwa dhati na alikuwa amebarikiwa sana na Bwana. Hata hivyo, aliliachia wazo moja tu lisilo sahihi kuvamia akili yake, ambalo kisha liliongoza kwenye mengine. Kadiri alivyokuwa akiendelea zaidi na zaidi kuwa mwenye kuruhusu mawazo haya, punde yakaota mizizi katika akili yake na yakaanza kukua moyoni mwake. Mwishowe akayafanyia kazi matamanio haya yasiyostahili, ambayo yalimwongoza kwenye kufanya maamuzi dhidi ya kila kitu ambacho kilikuwa cha thamani kubwa katika maisha yake. Aliniambia kwamba kama asingelipa nafasi wazo lile la kipumbavu lilipoanza, asingelikuwa muhanga na mwenye kuathirika kwa urahisi kwa majaribu ya adui—majaribu ambayo yalileta huzuni nyingi katika maisha yake, angalau kwa kipindi cha muda.

Kwa bahati nzuri, kama mwana mpotevu katika mfano ule maarufu unaopatikana katika injili ya Luka, “alizingatia moyoni mwake” na kuamka kutoka kwenye jinamizi lile.17 Alifanya upya tumaini lake katika Bwana na akajisikia kupondeka kweli na akawa na hamu ya hatimaye kurudi katika zizi la Bwana. Siku ile sote wawili tulihisi upendo ukomboao wa Bwana kwa ajili yetu sisi. Mwishoni mwa maongezi yetu mafupi, sote tulizidiwa kwa hisia, na hadi siku hii ya leo, ninakumbuka shangwe nzuri katika uso wake wakati alipoondoka ofisini kwangu.

Wapendwa rafiki zangu, wakati tunapoepuka majaribu madogo, ambayo mara nyingi huja pasipo kutarajiwa katika maisha yetu, tunakuwa tumejiandaa vyema zaidi kuzuia dhambi kubwa zaidi. Kama Rais Spencer W. Kimball alivyosema: “Aghalabu sana mtu kuingia katika uvunjaji sheria mkubwa pasipo kwanza kujiingiza kwenye mdogo, ambao huufungulia mlango ule mkubwa. … ‘Shamba safi [haliwezi] ghafla tu [kuwa] magugu.’”18

Wakati akijitayarisha kumaliza misheni yake takatifu hapa duniani, Mwokozi Yesu Kristo alitolea mfano umuhimu wa uthabiti wa kupinga kila kitu ambacho kinaweza kutushawisi sisi tusitambue lengo letu la milele. Baada ya mashambulizi kadhaa yasiyo na mafanikio ya adui, ambaye alijaribu kumuondoa kutoka kwenye misheni Yake, Mwokozi kwa kipekee alimfukuza adui kwa kusema: “Nenda zako, Shetani. … Kisha ibilisi akamwacha, na, tazama wakaja malaika wakamtumikia.”19

Je, mnaweza kufikiria, kaka na dada zangu, kile ambacho kingetokea kama tungekuwa tunaweza kuzalisha nguvu na ujasiri kutoka kwa Mwokozi na kusema “Hapana” na “Nenda zako” kwa mawazo yasiyostahili ambayo kwa mara ile ya kwanza yanakuja akilini mwetu? Je, kungekuwa na matokeo gani juu ya matamanio ya mioyo yetu? Je, ni kwa jinsi gani matokeo ya matendo yetu yangetuweka karibu na Mwokozi na kuruhusu ushawishi endelevu wa Roho Mtakatifu katika maisha yetu? Ninajua kwamba kwa kufuata mfano wa Yesu, tutaepuka majanga mengi na tabia zisizotakiwa ambazo zingeweza kusababisha matatizo ya kifamilia na kutokubaliana, hisia hasi na mwinamo, zinazofanya kuwepo na kukosekana kwa haki na unyanyasaji, kufanywa watumwa wa uraibu mbaya, na kila kitu kingine ambacho kingekuwa kinyume na amri za Mungu.

Katika ujumbe wake wa kihistoria na wenye kugusa wa Aprili mwaka huu, Rais Nelson alifanya ahadi kwamba wale wote walio tayari “kumsikiliza Yeye” na kutii amri Zake “watabarikiwa kwa nguvu ya ziada ya kupambana na majaribu, mahangaiko, na udhaifu” na kwamba uwezo wetu wa kuhisi shangwe utaongezeka, hata wakati wa ongezeko la ghasia hizi za sasa.20

Ninawashuhudieni kwamba ahadi za mpendwa nabii wetu ni ahadi zinazotolewa na Mwokozi Mwenyewe. Ninawaalika sote kati yetu “kumsikiliza Yeye” katika kila wazo na kumfuata Yeye kwa moyo wetu wote ili kupata nguvu na ujasiri wa kusema “Hapana” na “Ondoka hapa” kwa mambo yote ambayo yanaweza kutuletea kukosa furaha katika maisha yetu. Kama tunafanya hivyo, ninaahidi kwamba Bwana atatuma ongezeko la Roho wake Mtakatifu ili kutuimarisha na kutufariji na tunaweza kuwa watu kwa mfano wa moyo wa Bwana mwenyewe.21

Ninatoa ushahidi wangu kwamba Yesu Kristo yu hai na kwamba kupitia Yeye, tunaweza kushangilia juu ya ushawishi mwovu wa adui na kustahili kuishi milele na Bwana na katika uwepo wa Baba yetu mpendwa wa Mbinguni. Ninashuhudia juu ya kweli hizi kwa upendo wangu wote juu yenu na kwa Mwokozi wetu mzuri, ambaye jina lake ninalipa utukufu, heshima na sifa milele zote. Ninasema mambo haya katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.