Mkutano Mkuu
Kusonga Mbele
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2020


5:7

Kusonga Mbele

Kazi ya Bwana inasonga mbele bila kutetereka.

Akina kaka na dada zangu wapendwa, ni shangwe iliyoje kuwa nanyi wakati tunapoanza mkutano mkuu wa 190 wa Nusu Mwaka wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Ninapenda kujumuika nanyi katika nyumba zenu au popote mlipo kusikiliza pamoja jumbe za manabii, waonaji na wafunuzi na viongozi wengine wa Kanisa.

Tuna shukrani kubwa kwa sababu ya teknolojia ambayo inaturuhusu kuunganika kama mkusanyiko mmoja mkubwa ulimwenguni wa wafuasi wa Yesu Kristo. Mkutano Mkuu wa Aprili iliyopita ulitazamwa na watu wengi zaidi kuliko iliyowahi kupita, na tuna matarajio ya kila aina kwamba itakuwa hivyo tena.

Kwa kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, janga la ulimwenguni kote, moto wa nyikani, na majanga mengine ya asili yameugeuza ulimwengu wetu juu chini. Ninasikitika pamoja na kila mmoja wenu ambaye amempoteza mpendwa wake kwa wakati huu. Na ninaomba kwa ajili ya wote wanaoteseka sasa.

Kwa sasa, kazi ya Bwana inasonga mbele bila kutetereka. Katikati ya kujitenga kijamii, barakoa, na mikutano kupitia Zoom, tumejifunza kufanya baadhi ya vitu kwa utofauti na baadhi hata kwa ufanisi zaidi. Nyakati zisizo za kawaida zinaweza kuleta zawadi zisizo za kawaida.

Wamisonari wetu na viongozi wa misheni wamekuwa wenye kuleta tija, mashujaa na wa kushangaza. Ingawa wengi wa wamisionari walitakiwa kutafuta njia mpya, za kiubunifu za kufanya kazi yao, misheni nyingi zimeripoti kufundisha zaidi kuliko hapo awali.

Tulilazimika kufunga mahekalu kwa muda, na baadhi ya miradi ya ujenzi ilicheleweshwa kwa muda, lakini sasa vyote vinaendelea. Katika kalenda ya mwaka 2020, tutakuwa na sherehe za kuchimba ardhi kwa ajili ya mahekalu mapya 20!

Kazi ya historia ya familia imeongezeka mara dufu. Kata nyingi na vigingi vipya vimeundwa. Na tumeridhishwa kuripoti kwamba Kanisa limetoa misaada ya kibinadamu kwa janga lililoenea kwenye miradi 895 katika nchi 150.

Ongezeko la kujifunza injili nyumbani linaongoza kwenye kuwepo kwa shuhuda imara na mahusiano imara ya familia. Mama mmoja aliandika: “Tunahisi ukaribu zaidi na watoto na wajukuu zetu sasa kwamba tunakutana kupitia Zoom kila Jumapili. Kila mmoja huchukua zamu ya kushiriki mawazo yao kwenye Njoo, Unifuate. Maombi kwa ajili ya wanafamilia yamebadilika kwa sababu tunaelewa vyema kile wanachohitaji.”

Ninaomba kwamba sisi kama watu tunatumia wakati huu maalum kukua kiroho. Tuko hapa duniani ili kujaribiwa, kuona kama tutachagua kumfuata Yesu Kristo, kutubu kila mara, kujifunza na kukua. Roho zetu zinatamani kukua. Na tunafanya vyema zaidi katika hilo kwa kubaki katika njia ya agano.

Katika yote, Baba yetu wa Mbinguni na Mwanawe, Yesu Kristo, wanatupenda! Wanatujali! Wao na malaika Zao watakatifu wanatulinda. 1 Ninajua kwamba hilo ni kweli.

Wakati tunapokusanyika kusikiliza maneno ambayo Bwana amewatia msukumo wa kiungu watumishi Wake kuyasema, ninawaalika kutafakari ahadi ambayo Bwana aliitoa. Alitangaza kwamba “yeyote atakaye angelishikilia neno la Mungu, ambalo ni jepesi na lenye nguvu, ambalo litaangamiza ujanja … na hila za ibilisi, na kumwongoza [mfuasi] wa Kristo katika njia nyembamba na iliyosonga.” 2

Ninaomba kwamba mtachagua kulishikilia neno la Mungu kama linavyotangazwa wakati wa mkutano huu mkuu. Na ninaomba kwamba muweze kuhisi upendo mkamilifu wa Bwana kwa ajili yenu, 3 katika jina takatifu la Yesu Kristo, Amina.