Mkutano Mkuu
Tunazungumza Kuhusu Kristo
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2020


15:1

Tunazungumza Kuhusu Kristo

Kwa kuwa ulimwengu unamzungumzia Yesu Kristo kwa uchache, acha sisi tuzungumze zaidi juu Yake.

Ninatoa upendo wangu kwenu, rafiki zetu wapendwa na waumini wenzetu. Nimevutiwa na imani yenu na ujasiri wenu katika miezi hii iliyopita, kwani janga hili la ulimwenguni kote limevuruga maisha yetu na kuwapoteza wanafamilia na marafiki wapendwa.

Katika kipindi hiki cha mashaka, nimehisi shukrani zisizo za kawaida kwa ajili ya uelewa wangu wa uhakika na yakini kwamba Yesu ndiye Kristo. Je, ninyi mmehisi hivyo? Kuna shida ambazo zinamuelemea kila mmoja wetu, lakini kila mara mbele yetu yupo Yeye aliyetangaza kwa unyenyekevu, “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima.”1 Wakati tunavumilia kipindi cha kujitenga mbali na wengine, kamwe hatuhitaji kuvumilia kipindi cha kujitenga kiroho kutoka Kwake Yeye ambaye kwa upendo anatuita, “Njooni kwangu.”2

Kama vile nyota inayoongoza katika anga angavu, lenye kiza, Yesu Kristo anaangaza njia yetu. Alizaliwa duniani katika hori nyenyekevu. Aliishi maisha ya ukamilifu. Aliponya wagonjwa na kufufua wafu. Alikuwa rafiki kwa waliosahaulika. Alitufundisha kutenda mema, kutii, na kupendana. Alisulubiwa msalabani, akafufuka kwa utukufu siku tatu baadaye, na kuturuhusu sisi na wale tunaowapenda kuishi baada ya maisha haya ya duniani. Kwa rehema na neema Yake isiyo na kifani, alijichukulia juu Yake dhambi na mateso yetu, akileta msamaha pale tunapotubu na amani katika dhoruba za maisha. Tunampenda Yeye. Tunamwabudu Yeye. Tunamfuata Yeye. Yeye ni nanga ya nafsi zetu.

Cha kushangaza, wakati usadikisho huu wa kiroho unaongezeka ndani yetu, kuna wengi duniani ambao wanajua kidogo sana juu ya Yesu Kristo, na katika sehemu zingine za ulimwengu ambapo jina Lake limetangazwa kwa karne nyingi, imani katika Yesu Kristo inafifia. Watakatifu hodari huko Ulaya wameona imani ikififia katika nchi zao kwa miongo kadhaa.3 Kwa masikitiko, hapa Marekani imani inapungua pia. Utafiti wa hivi karibuni ulidhihirisha kuwa katika miaka 10 iliyopita, watu milioni 30 nchini Marekani wameacha kuamini katika uungu wa Yesu Kristo.4 Ukiangalia ulimwenguni kote, utafiti mwingine unatabiri kuwa katika miongo ijayo, zaidi ya mara mbili ya wengi wataacha Ukristo kuliko wale ambao wataukubali.5

Sisi, kwa kweli, tunaheshimu haki ya kila mmoja kuchagua, lakini Baba yetu wa Mbinguni alitangaza, “Huyu ni Mwanangu mpendwa: Msikilize Yeye.”6 Ninashuhudia kwamba siku yaja ambapo kila goti litapigwa na kila ulimi utakiri kuwa Yesu ndiye Kristo.7

Je, tunapaswa kujibu vipi kwa ulimwengu wetu unaobadilika? Wakati wengine wanapuuza imani yao, wengine wanatafuta ukweli. Tumejichukulia juu yetu jina la Mwokozi. Tunapaswa kufanya nini zaidi?

Matayarisho ya Rais Russell M. Nelson

Sehemu ya jibu letu inaweza kuja tunaporejea jinsi Bwana alivyomfundisha Rais Russell M. Nelson katika miezi kabla ya wito wake kama Rais wa Kanisa. Akihutubia mwaka mmoja kabla ya wito wake, Rais Nelson alitualika tujifunze kwa undani zaidi marejeleo 2,200 ya jina Yesu Kristo yaliyoorodheshwa kwenye Mwongozo wa Mada.8

Rais Nelson akisoma maandiko

Miezi mitatu baadaye, katika mkutano mkuu wa Aprili, alizungumzia jinsi, hata kwa miongo yake ya ufuasi wa kujitolea, kujifunza huku kwa kina kuhusu Yesu Kristo kulimuathiri sana. Dada Wendy Nelson alimuuliza juu ya matokeo yake kwake. Alijibu, “Mimi ni mtu tofauti!” Alikuwa mtu tofauti. Katika Umri wa miaka 92, mtu tofauti? Rais Nelson alifafanua:

“Tunapowekeza muda katika kujifunza juu ya Mwokozi na dhabihu Yake ya upatanisho, tunavutwa [Kwake]. …

“… Fokasi yetu [inakuwa] imeelekezwa kwa Mwokozi na injili Yake.”9

Mwokozi alisema, “Nitegemeeni katika kila wazo.”10

Katika ulimwengu wa kazi, wasiwasi, na juhudi zinazostahili, tunaweka moyo wetu, akili yetu, na mawazo yetu Kwake Yeye ambaye ndiye tumaini na wokovu wetu.

Ikiwa kujifunza upya juu ya Mwokozi kulisaidia kumtayarisha Rais Nelson, je, hakuwezi kusaidia kututayarisha sisi pia?

Rasi Russell M. Nelson

Katika kusisitiza jina la Kanisa, Rais Nelson alifundisha, “Kama … tutataka kufikia nguvu ya Upatanisho wa Yesu Kristo—ili kututakasa na kutuponya, ili kutuimarisha na kutukuza, na hatimaye kutuinua—ni lazima tumtambue Yeye bayana kama chanzo cha nguvu hiyo.”11 Rais Nelson alitufundisha kwamba kwa kutumia jina sahihi la Kanisa kila mara, kitu ambacho kinaweza kuonekana kuwa kitu kidogo, siyo kidogo kabisa na kitaipa umbo kesho ya ulimwengu.

Ahadi kwa Matayarisho Yako

Ninawaahidi kwamba mnapojitayarisha wenyewe, kama Rais Nelson alivyofanya, ninyi pia mtakuwa tofauti, mkifikiria zaidi juu ya Mwokozi, mkimzungumzia Yeye zaidi mara kwa mara na bila kusita hata kidogo. Mnapokuja kumjua na kumpenda Yeye kwa undani zaidi, maneno yenu yatatiririka vizuri zaidi, kama yanavtotiririka wakati mnapomzungumzia mmoja wa watoto wenu au rafiki mpendwa. Wale wanaowasikiliza hawatahisi kama ni mdahalo au kuwaondosha na zaidi watahisi kujifunza kutoka kwenu.

Wewe na mimi tunazungumza kuhusu Yesu Kristo, lakini pengine tunaweza kufanya vizuri zaidi. Kama ulimwengu utazungumza machache kumhusu Yeye, ni nani atazungumza mengi kuhusu Yeye? Ni sisi! Pamoja na Wakristo wengine waliojitolea!

Kuzungumza kuhusu Kristo katika Nyumba Zetu

Je! Kuna picha za Mwokozi katika nyumba zetu? Je! Tunazungumza mara nyingi na watoto wetu juu ya mifano ya Yesu? “Hadithi za Yesu [ni] kama upepo uvumao kwenye makaa ya imani katika mioyo ya watoto wetu.”12 Wakati watoto wako wanapokuuliza maswali, fikiria kwa uangalifu kufundisha kile Mwokozi alichofundisha. Kwa mfano, kama mtoto wako anauliza, “Baba, kwa nini tunasali?” Unaweza kujibu, “Hilo ni swali zuri. Je, unakumbuka wakati Yesu aliposali? Hebu tuzungumze kuhusu kwa nini Alisali na Alisali vipi.”

“Tunazungumza kuhusu Kristo, tunafurahia katika Kristo … ili watoto wetu wajue asili ya kutegemea msamaha wa dhambi zao.”13

Kuzungumza kuhusu Kristo Kanisani

Andiko hilihili linaongezea kwamba “tunahubiri kuhusu Kristo.”14 Katika ibada zetu, acha tufokasi kwa Mwokozi Yesu Kristo na zawadi ya dhabihu Yake ya upatanisho. Hii haimaanishi kwamba hatuwezi kusimulia uzoefu kutoka kwenye maisha yetu wenyewe au kushiriki mawazo kutoka kwa wengine. Wakati mada yetu inaweza kuhusu familia au huduma au mahekalu au misheni ya hivi karibuni, kila kitu katika ibada zetu kinapaswa kuelekezwa kwa Bwana Yesu Kristo.

Miaka thelathini iliyopita, Rais Dallin H. Oaks alizungumzia barua ambayo aliipokea “kutoka kwa mtu ambaye alisema alikuwa amehudhuria mkutano wa [sakramenti] na alisikiliza shuhuda kumi na saba bila kusikia Mwokozi akitajwa.”15 Kisha Rais Oaks alisema, “Labda maelezo hayo yametiwa chumvi [lakini] nayanukuu kwa sababu yanatoa ukumbusho dhahiri kwetu sote.”16 Kisha alitualika kuzungumza zaidi kuhusu Yesu Kristo katika mahubiri na mijadala ya darasa. Nimegundua kwamba tunafokasi zaidi na zaidi juu ya Kristo katika mikutano yetu ya Kanisa. Kwa umakini acha tuendelee na juhudi hizi chanya.

Kuzungumza kuhusu Kristo kwa Wengine

Kwa wale wanaotuzunguka, acha tuwe wawazi zaidi, wenye utayari zaidi kuzungumza kuhusu Kristo. Rais Nelson alisema, “Wafuasi wa kweli wa Yesu Kristo wako tayari kujitokeza, kuzungumza kwa ukakamavu, na kuwa tofauti na watu wa ulimwengu.”17

Wakati mwingine tunafikiri kuwa mazungumzo na mtu yanahitaji kusababisha wao waje kanisani au kukutana na wamisionari. Acha Bwana awaongoze kama wanavyotaka, wakati tunafikiria zaidi juu ya jukumu letu la kuwa sauti kwa ajili Yake, wenye kujali na kuwa wawazi kuhusu imani yetu. Mzee Dieter F. Uchtdorf ametufundisha kwamba wakati mtu anapotuuliza kuhusu wikiendi yetu, tunapaswa kuwa tayari kujibu kwa furaha kwamba tulipenda kusikia watoto wa Msingi wakiimba “Ninajaribu kuwa kama Yesu.”18 Acha kwa wema tushuhudie imani yetu katika Kristo. Kama mtu atashiriki tatizo alilonalo katika maisha yake binafsi, tunaweza kusema, “John, Mary, unajua kwamba ninaamini katika Yesu Kristo. Nimekuwa nikifikiria juu ya kitu Alichokisema ambacho kinaweza kukusaidia.”

Kuwa muwazi zaidi katika mitandao ya kijamii katika kuzungumza kuhusu uaminifu wako kwa Kristo. Wengi wataheshimu imani yako, lakini ikiwa mtu anapuuza wakati unazungumza kuhusu Mwokozi, jipe moyo katika ahadi Yake: “Heri ninyi watakapowashutumu … kwa ajili yangu. … Kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni.”19 Tunajali zaidi kuwa wafuasi Wake kuliko “kupendwa” na wafuasi wetu wenyewe. Petro alishauri, “Mwe tayari siku zote kutoa jibu [kwa ajili ya] tumaini lililo ndani yenu.”20 Acha tuzungumze kuhusu Kristo.

Kitabu cha Mormoni ni ushuhuda wenye nguvu wa Yesu Kristo. Karibu kila ukurasa hushuhudia juu ya Mwokozi na misheni Yake ya kiungu.21 Uelewa wa Upatanisho na neema Yake vimejaa kurasa zake. Kama mwenzi wa Agano Jipya, Kitabu cha Mormoni kinatusaidia kuelewa vizuri zaidi kwa nini Mwokozi alikuja kutuokoa na jinsi tunavyoweza kuja Kwake kwa dhati.

Baadhi ya Wakristo wenzetu, wakati mwingine, hawana uhakika juu ya imani na nia zetu. Acha tushangilie kwa dhati pamoja nao katika imani yetu ya pamoja katika Yesu Kristo na katika maandiko ya Agano Jipya ambayo sisi sote tunayapenda. Katika siku zijazo, wale wanaomwamini Yesu Kristo watahitaji urafiki na msaada wa kila mmoja.22

 Nuru ya Ulimwengu

Wakati ulimwengu unamzungumzia Yesu Kristo kwa uchache, acha sisi tuzungumze zaidi juu Yake. Kadiri rangi zetu halisi kama wafuasi Wake zinavyojidhihirisha, wengi wanaotuzunguka watakuwa tayari kusikiliza. Tunaposhiriki nuru tuliyoipokea kutoka Kwake, nuru Yake na nguvu Yake kuu ya kuokoa itawaangazia wale walio radhi kufungua mioyo yao. Yesu alisema, “Mimi nimekuja … [kama] nuru ya ulimwengu.”23

Kuinua Matamanio Yetu ya Kuzungumza Kuhusu Kristo

Hakuna kitu kinachoinua matamanio yangu ya kuzungumza kuhusu Kristo kuliko kupata picha ya ujio Wake tena. Japo hatujui Atakuja lini, matukio ya kurudi Kwake yatakuwa ya kustaajabisha! Atakuja katika mawingu ya mbinguni kwa utukufu na ufalme pamoja na malaika Zake wote watakatifu. Siyo tu malaika wachache, bali malaika Zake wote watakatifu. Hawa si makerubi wenye mashavu mekundu waliochorwa na Raphael wanaopatikana kwenye kadi zetu za siku ya wapendanao. Hawa ni malaika wa karne nyingi, malaika waliotumwa kufunga vinywa vya simba,24 kufungua milango ya gereza,25 kutangaza kuzaliwa kwake kulikosubiriwa kwa muda mrefu,26 kumfariji huko Gethsemane,27 kuwahakikishia wanafunzi wakati wa Kupaa Kwake,28 na kufungua urejesho mtukufu wa injili.29

Ujio wa Pili

Unaweza kufikiria kwamba umenyakuliwa kukutana Naye, iwe upande huu au upande mwingine wa pazia?30 Hiyo ndiyo ahadi Yake kwa wenye haki. Uzoefu huu wa kustaajabisha utaacha alama kwenye nafsi zetu milele.

Tuna shukrani iliyoje kwa nabii wetu mpendwa, Rais Russell M. Nelson, ambaye ameinua matamanio yetu ya kumpenda Mwokozi na kutangaza uungu Wake. Mimi ni shuhuda wa mkono wa Bwana juu yake na kipawa cha ufunuo kinachomuongoza. Rais Nelson, tunasubiri ushauri wako kwa shauku kubwa.

Rafiki zangu wapendwa ulimwenguni kote, acha tuzungumze kuhusu Kristo, tukitumainia ahadi Yake tukufu: “Kila … atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri … mbele za Baba yangu.”31 Ninashuhudia Yeye ni Mwana wa Mungu. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Yohana 14:6.

  2. Mathayo 11:28

  3. Ona Niztan Peri-Rotem, “Religion and Fertility in Western Europe: Trends across Cohorts in Britain, France and the Netherlands,” European Journal of Population, May 2016, 231–65, ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC4875064.

  4. “[Asilimia sitini na tano] ya watu wazima wa Kiamerika wanajitanabaisha kama Wakristo wanapoulizwa kuhusu dini yao, anguko la asilimia 12 ikilinganishwa na muongo uliopita. Kwa sasa, idadi ya watu wasiojihusisha na dini, ikijumuisha watu wanaotoa utambulisho wa dini zao kama wakana Mungu, wakataa habari za Mungu au ‘wasio na jina maalum,’ sasa wanafikia 26%, ongezeko kutoka 17% mwaka 2009” (Pew Research Center, “In U.S., Decline of Christianity Continues at Rapid Pace,” Oct. 17, 2019, pewforum.org).

  5. Ona Pew Research Center, “The Future of World Religions: Population Growth Projections, 2010–2050,” Apr. 2, 2015, pewforum.org.

  6. Marko 9:7; Luka 9:35; ona pia Mathayo 3:17; Joseph Smith—Historia ya 1:17.

  7. Ona Wafilipi 2:9–11.

  8. Russell M. Nelson, “Manabii, Uongozi, na Sheria Takatifu” (worldwide devotional for young adults, Jan. 8, 2017), broadcasts.lds.org.

  9. Russell M, Nelson, “Kuvuta Nguvu ya Yesu Kristo kwenye Maisha Yetu,” Liahona, Mei 2017, 40–41.

  10. Mafundisho na Maagano 6:36.

  11. Russell M. Nelson, “Jina Sahihi la Kanisa”,” Liahona Nov. 2018, 88.

  12. Neil L. Andersen, “Tell Me the Stories of Jesus,” Liahona, Mei 2010.

  13. 2 Nefi 25:26.

  14. 2 Nefi 25:26.

  15. Dallin H. Oaks, “Another Testament of Jesus Christ” (Brigham Young University fireside, June 6, 1993), 7, speeches.byu.edu.

  16. Dallin H. Oaks, “Witnesses of Christ,” Ensign, Nov. 1990, 30.

  17. Russell M, Nelson, “Kuvuta Nguvu ya Yesu Kristo kwenye Maisha Yetu,” 40.

  18. Ona Dieter F. Uchtdorf, “Kazi ya Umisionari: Shiriki Yaliyo Moyoni Mwako,” Liahona, Mei 2019, 17; “I’m Trying to Be like Jesus,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 78.

  19. Mathayo 5:11–12.

  20. 1 Petro 3:15.

  21. “Kama [waandishi wa kinabii wa Kitabu cha Mormoni] walivyoandika shuhuda zao za masiya aliyeahidiwa, walitaja aina kadhaa za majina yake kwa wastani kwenye kila mistari 1.7. [Wao] walimwita Yesu Kristo, kiuhalisia, kwa majina tofauti yapatayo 101. … Tunapotambua kwamba mstari mara zote una sentensi moja, inaonekana kwamba hatuwezi, kwa wastani, kusoma sentensi mbili katika Kitabu cha Mormoni bila kuona aina fulani ya jina la Kristo” (Susan Easton Black, Finding Christ through the Book of Mormon [1987], 5, 15).

    “Wakati maneno patanisha au upatanisho, katika kila aina yake, yanaonekana mara moja tu katika tafsiri ya Agano Jipya ya King James, maneno hayo yanaonekana mara 35 kwenye kitabu cha Mormoni. Kama ushuhuda mwingine wa Yesu Kristo, kinatoa nuru ya thamani katika Upatanisho Wake” (Russell M. Nelson, “The Atonement,” Ensign, Nov. 1996.)

  22. Wale wanaoachana na Ukristo hapa Marekani ni vijana. “Zaidi ya waumini nane kati ya kumi wa Kizazi kilicho Kimya (wale waliozaliwa kati ya 1928 na 1945) wanajitanabaisha kama Wakristo (84%), kama ilivyo kwa robo tatu ya Watoto Wachanga (76%). Katika tofauti ya wazi, nusu ya wale waliozaliwa mwanzoni mwa karne ya 21 (49%) wanajitanabaisha kama Wakristo; wanne kati ya kumi ‘hawana’ dini, na mmoja kati ya kumi ya wazawa wa karne ya 21 wanajitanabaisha kwa wale wasio na imani ya Kikristo” (“In U.S., Decline of Christianity Continues,” pewforum.org).

  23. Yohana 12:46.

  24. Ona Danieli 6:22.

  25. Ona Matendo ya Mitume 5:19.

  26. Ona Luka 2:2–14.

  27. Ona Luka 10:42–43.

  28. Ona Matendo ya Mitume 1:9–11.)

  29. Ona Mafundisho na Maagano 13; 27:12–13; 110:11–16; Joseph Smith—Historia ya 1:27–54.

  30. Ona 1 Wathesolanike 4:16–17; Mafundisho na Maagano 88:96–98.

  31. Mathayo 10:32.