Macho ya Kuona
Kwa kupitia nguvu za Roho Mtakatifu, Kristo atatusaidia kujiona sisi wenyewe na kuwaona wengine kama Yeye anavyowaona.
Kuona Mkono wa Bwana
Ninaipenda hadithi ya Agano la Kale ya kijana mdogo aliyekuwa mtumishi wa nabii Elisha. Mapema asubuhi moja kijana huyo aliamka, akatoka nje, na kukuta mji ukiwa umezingirwa na kikosi kikubwa chenye nia ya kuwaangamiza. Alikimbia kwa Elisha: “Ole wetu! Bwana wangu, tufanyeje?”
Elisha alijibu, “Usiogope; maana walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao.”
Elisha alitambua kwamba mtumishi huyo alihitaji zaidi ya uhakika wa kumtuliza; alihitaji ono. Kisha “Elisha akaomba, … Bwana, … mfumbue macho yake, apate kuona. Bwana akafumbua macho ya yule mtumishi; naye akaona; na tazama, kile kilima kilikuwa kimejaa farasi na magari ya moto yaliyomzunguka Elisha pande zote.” 1
Kunaweza kuwa na nyakati ambapo, kama mtumishi, utajikuta unapata ugumu kutambua jinsi Bwana anavyofanya kazi katika maisha yako—nyakati ambapo wewe utahisi umezingirwa—wakati ambapo mateso ya maisha yatakufanya udhoofike. Subiri na amini katika Mungu na katika muda Wake, kwa sababu unaweza kuamini moyo Wake kwa moyo wako wote. Lakini kuna somo la pili hapa. Wapendwa dada zangu na kaka, nyie, pia, mnaweza kuomba ili Bwana afungue macho yenu kuona mambo ambayo kwa kawaida msingeyaona.
Tujitazame kama vile Mungu Angetutazama
Huenda vitu vya muhimu sana kwetu sisi kuviona vyema ni Mungu ni nani na sisi ni akina nani hasa—wana na mabinti wa wazazi wa mbinguni wenye “asili ya uungu na takdiri ya milele.” 2 Muombe Mungu afunue kweli hizi kwako, pamoja na jinsi Anavyohisi kuhusu wewe. Kadiri unavyoelewa kuhusu utambulisho wako na lengo lako halisi, ndani ya nafsi yako, ndivyo itakavyochangia kila kitu katika maisha yako.
Kuwaangalia Wengine
Kwa kuelewa jinsi Mungu anavyotuangalia huandaa njia ya kutusaidia kuwaangalia wengine kama Yeye anavyowaangalia. Mwandishi wa makala David Brooks alisema: “Baadhi ya matatizo makubwa ya jamii zetu hutokana na watu kuhisi kutokuonwa au kutambulika. … Kuna sifa … kuu ambayo sote tunayo tunayohitaji kuifanya vyema, ni sifa ya kuangaliana kwa kina na kwa kina kuonwa.” 3
Yesu Kristo huwaangalia watu kwa kina. Huwaangalia watu , mahitaji yao, na kile watakachokuwa. Ambapo wengine waliona wavuvi, wenye dhambi, au watoza ushuru, Yesu aliona wanafunzi; ambapo wengine waliona mwanaume akiwa na pepo, Yesu aliangalia kupita dhiki za nje, akamtambua, na kumponya. 4
Hata katika maisha yetu yenye shughuli nyingi, tunaweza kufuata mfano wa Yesu na kuwaangalia watu—mahitaji yao, imani yao, changamoto zao, na wenye kuweza kuwa nani. 5
Kadiri ninavyosali ili Bwana afungue macho yangu nione vitu ambavyo kwa kawaida siwezi kuviona, mara kwa mara najiuliza maswali mawili na kuwa makini kwa hisia zinazokuja: “Je, ninafanya nini ambacho natakiwa kuacha kufanya?” na “Je, sifanyi nini ambacho natakiwa kuanza kukifanya?” 6
Miezi iliyopita, wakati wa sakramenti, nilijiuliza mwenyewe maswali haya na nilishangazwa na hisia zilizonijia. “Acha kuangalia simu yako wakati ukiwa kwenye foleni ukisubiri.” Kuangalia simu yangu kwenye foleni kumekuwa takribani otomatiki; naona ni muda mzuri wa kufanya kazi nyingi, kuangalia barua pepe, kuangalia vichwa vya habari, au kupitia taarifa za mitandao ya kijamii.
Asubuhi iliyofuata, nilijikuta nikisubiria kwenye foleni ndefu katika duka la bidhaa. Nilitoa simu yangu na kisha nikakumbuka hisia niliyoipokea. Nilirudisha simu yangu na kuanza kuangaza. Nilimuona kwa mbele yangu mwanaume mzee kwenye foleni. Kikapu chake kilikuwa tupu isipokuwa makopo machache ya chakula cha paka. Nilihisi vibaya kidogo, lakini nilisema kitu mahiri kweli kama, “naona una paka.” Alisema kwamba tufani lilikuwa linakuja, na hakutaka kukutwa bila chakula cha paka. Tuliongea kwa ufupi, na kisha akanigeukia na kusema, “Unajua, sijamwambia yeyote hili, lakini leo ni siku yangu ya kuzaliwa.” Moyo wangu ulilainika. Nilimtakia kheri ya kuzaliwa na kutoa ombi la siri la shukrani kwamba sikuwa kwenye simu yangu na kukosa fursa ya kuona na kuunganika na mtu mwingine ambaye alikuwa anaihitaji.
Kwa moyo wangu wote sitaki kuwa kama kuhani wa kilawi aliyekuwa njiani kwenda Yeriko—aliyetazama na kupita kando. 7 Lakini mara kwa mara nadhani nimekuwa kama kuhani huyo.
Kuiona Huduma ya Mungu Kwangu
Hivi karibuni nimejifunza somo lenye thamani kuhusu kuangalia kwa kina kutoka kwa msichana aitwaye Rozlyn.
Hadithi ilisimuliwa kwangu na rafiki yangu ambaye alikuwa amechanganyikiwa pale mume wake aliyedumu naye kwa miaka 20 alipomuacha. Na watoto wakigawa muda wa kuwaona wazazi wao, matarajio ya kuhudhuria kanisani peke yake yalionekana yenye kikwazo. Anasimulia:
“Katika kanisa ambapo familia ina umuhimu mkubwa, kukaa peke yako kunaweza kuwa kuchungu. Jumapili hiyo ya kwanza niliingia kanisani nikiomba kwamba asiwepo mtu wa kunisemesha. Kwa shida nilijikaza, na machozi yalikuwa karibu kunitiririka. Nilikaa kwenye nafasi yangu niliyoizoea, nikitumaini hakuna hata mmoja atagundua jinsi gani benchi lilionekana tupu.
Msichana katika kata yetu aligeuka na kuniangalia. Nilijifanya kutabasamu. Na akanitabasamia pia. Ningeweza kuona shaukuku katika uso wake. Kwa utulivu nilimuomba kwamba asije kuongea nami—sikuwa na kitu chanya cha kusema na nilijua kwamba ningelia. Niliangalia chini kwenye paja langu na kuepuka mgongano wa macho.
“Wakati saa lililofuatia, niligundua alikuwa akiniangalia hapa na pale. Na mara mkutano ulipokwisha, kwa haraka alisonga kwangu. ‘Habari Rozlyn,’ nilinong’ona. Alinikumbatia na kusema, ‘Dada Smith, naweza kusema leo ni siku mbaya kwako. Pole. Ninakupenda.’ Kama nilivyotabiri, machozi yalinitoka aliponikumbatia tena. Lakini nilipokuwa nikiondoka, nilitafakari, ‘Baada ya yote huenda naweza kufanya hili.’
“Yule msichana mrembo wa miaka 16, nusu kidogo ya umri wangu, alinitafuta kila Jumapili kwa mwaka huo ili kunikumbatia na kunisalimia, ‘Habari yako?’ Ilifanya nihisi tofauti kuhusu kuhudhuria kanisani. Ukweli ni kwamba nilianza kutegemea kwenye kumbatio hizo. Mtu mmoja alinigundua. Mtu mmoja alijua nilikuwa hapo. Mtu mmoja alinijali.”
Kama kwa vipaji vyote ambavyo Baba kwa dhati hutupatia, vinatuhitaji sisi kwa dhati Kumuomba Yeye—na kisha kutenda. Omba ili uwaone wengine kama Yeye anavyowaona—wana na mabinti Zake wenye uwezo usio na mwisho na wa kiungu. Kisha tenda kwa kupenda, kutumikia, na kuthibitisha ustahiki na uwezo wao kama utakavyoongozwa na Roho. Hii ikiwa ni mwenendo wa maisha yetu, tutajikuta tunakuwa “wafuasi wa kweli wa … Yesu Kristo.” 8 Wengine wataweza kuiaminisha mioyo yao kwa mioyo yetu. Na katika mwenendo huu tutagundua pia utambulisho wetu wa kweli na dhumuni.
Rafiki yangu alisimulia uzoefu mwingine akiwa amekaa katika lilelile benchi tupu, peke yake, akijiuliza kama juhudi za miaka 20 ya kuishi injili katika nyumba yake ilikuwa ni bure. Alihitaji zaidi ya uhakika wa kumtuliza; alihitaji ono. Alihisi swali likisumbua moyo wake: “Kwa nini ulifanya vitu hivyo? Je, ulivifanya kwa ajili ya tuzo, kutukuzwa na wengine, au matokeo yaliyokuwa yanategemewa?” Alisita kwa muda, akachunguza moyo wake, na kisha akaweza kujibu kwa ujasiri, “nilivifanya kwa sababu nampenda Mwokozi. Na pia naipenda injili Yake. Bwana alifungua macho yake ili kumsaidia kuona. Ono hili japo la kawaida lakini lenye badiliko kubwa lilimsaidia kuendelea kusonga mbele kwa imani katika Kristo, bila kujali hali yake.
Ninashuhudia kwamba Yesu Kristo anatupenda na anaweza kutupatia macho ya kuona—hata ambapo ni vigumu, hata ambapo tumechoka, hata ambapo tu wapweke, na hata ambapo matokeo yako kinyume na matarajio yetu. Kwa kupitia neema Zake, Atatubariki na kukuza uwezo wetu. Kwa kupitia nguvu za Roho Mtakatifu, Kristo atatusaidia kujiona sisi wenyewe na kuwaona wengine kama Yeye anavyowaona. Kwa msaada Wake, tunaweza kutambua ni nini cha umuhimu sana. Tunaweza kuanza kuona mkono wa Bwana ukitenda katika na kupitia vitu vya kawaida vya maisha yetu—kisha tutaona kwa kina.
Na kisha, katika siku hiyo kuu “kwamba wakati atakapoonekana tutakuwa kama yeye, kwani sisi tutamwona vile alivyo; ili tuwe na tumaini hili” 9 ni ombi langu katika jina la Yesu Kristo, amina.