Jipeni Moyo
Imani yetu imara katika mafundisho ya injili iliyorejeshwa ya Yesu Kristo inaongoza hatua zetu na kutupatia shangwe.
Katika siku za mwisho za maisha Yake hapa duniani, Yesu Kristo aliwaambia Mitume Wake juu ya mateso na dhiki watakazopitia. 1 Alihitimisha kwa hakikisho hili kubwa: “Ulimwenguni mnayo dhiki: lakini jipeni moyo; Mimi nimeushinda ulimwengu” (Yohana 16:33). Huo ni ujumbe wa Mwokozi kwa watoto wote wa Baba wa Mbinguni. Hiyo ni habari nzuri sana kwa kila mmoja wetu katika maisha yetu ya hapa duniani.
“Jipeni moyo” lilikuwa pia hakikisho lililohitajika katika ulimwengu ambao Kristo aliyefufuka aliwatuma Mitume Wake. “Pande zote twadhikika,” Mtume Paulo baadaye aliwaambia Wakorintho, “bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa; twaudhiwa, bali hatuachwi; twatupwa chini, bali hatuangamizwi” (2 Wakorintho 4:8–9).
Miaka elfu mbili baadaye sie pia “twadhihakiwa pande zote”, nasi pia twahitaji ujumbe sawa na ule wa kutokata tamaa bali tujipe moyo. Bwana ana upendo na uhusiano maalumu kwa ajili ya mabinti zake wapendwa. Anajua kuhusu matakwa yenu, mahitaji yenu, na hofu zenu. Bwana ni mwenye uwezo mkubwa. Mwamini Yeye.
Nabii Joseph Smith alifundishwa kwamba “kazi, na mipango, na malengo ya Mungu hayawezi kubatilishwa, wala hayawezi kuwa kazi bure” (Mafundisho na Maagano 3:1.) Kwa watoto Wake wanaohangaika, Bwana alitoa mahakikisho haya makuu:
“Tazama, hii ni ahadi ya Bwana kwenu, Enyi watumishi wangu.
“Kwa hiyo, changamkeni, na msiogope, kwani Mimi Bwana nipo pamoja nanyi, na nitasimama karibu yenu; nanyi mtanishuhudia, hata Yesu Kristo, kuwa Mimi ndimi Mwana wa Mungu aliye hai” (Mafundisho na Maagano 68:5–6).
Bwana anasimama karibu yetu, na Yeye amesema:
“Na sasa, amini ninawaambia, na lile nisemalo kwa mmoja nasema kwa wote, muwe na furaha, watoto wadogo; kwani mimi nipo katikati yenu, na sijawasahau” (Mafundisho na Maagano 61:36).
“Kwani baada ya taabu kubwa huja baraka” (Mafundisho na Maagano 58:4).
Akina dada, ninashuhudia kwamba ahadi hizi, zilizotolewa katikati ya mateso na majanga binafsi, hutumika kwa kila mmoja wenu katika hali zenu za matatizo leo. Ni za thamani na hutukumbusha kila mmoja wetu kujipa moyo na kuwa na furaha katika utimilifu wa injili wakati tunaposonga mbele kupitia changamoto za hapa duniani.
Taabu na changamoto ni uzoefu wa kawaida wa duniani. Upinzani ni sehemu muhimu ya mpango mtukufu kwa ajili ya kutusaidia sisi kukua, 2 na katikati ya mchakato huo, tuna hakikisho la Mungu kwamba katika mtazamo mrefu wa milele, upinzani hautaruhusiwa kutushinda. Kwa msaada Wake na uaminifu wetu na uvumilivu, tutashinda. Kama vile maisha ya duniani ambayo hayo ni sehemu yake, taabu zote ni za muda. Katika mabishano ambayo yalitangulia vita ya maafa, Rais wa Marekani Abraham Lincoln kwa hekima alikumbusha hadhira yake juu ya hekima ya kale kwamba “hili pia, litapita.” 3
Kama mnavyojua, dhiki za hapa duniani ambazo ninazizungumzia—ambazo zinafanya iwe vigumu kujipa moyo—wakati mwingine huja kwetu kwa namna inayofanana na ya wengine wengi, kama mamilioni wanaohangaika sasa kupitia baadhi ya athari nyingi za kuhuzunisha za maradhi yaliyoenea ulimwenguni kote ya COVID‑19. Vilevile, ndani ya Marekani mamilioni wanateseka kupitia kipindi cha uadui na mabishano ambayo siku zote yanaonekana kuambatana na chaguzi za urais lakini kipindi hiki ni makali mno kiasi kwamba wengi wetu tulio wakubwa tutakumbuka daima.
Kwa kiwango binafsi, kila mmoja wetu anahangaika kibinafsi kwa baadhi ya dhiki nyingi za duniani, kama vile umasikini, ubaguzi wa rangi, afya mbaya, upotevu wa kazi au kukata tamaa, watoto watukutu, ndoa mbaya au kutokuwa na ndoa, na athari za dhambi—zetu wenyewe au za wengine.
Bado, katikati ya hivi vyote, tunao ushauri ule wa kimbingu wa kujipa moyo na kupata furaha katika kanuni na ahadi za injili na matunda ya kazi zetu. 4 Ushauri huo umekuwa hivyo siku zote, kwa manabii na kwa ajili yetu sote. Tunajua hili kutokana na uzoefu wa watangulizi wetu na kile Bwana alichosema kwao.
Kumbuka hali za Nabii Joseph Smith. Yakitazamwa kupitia lenzi ya dhiki, maisha yake yalikuwa ya umasikini, kuteswa, kukata tamaa, huzuni za familia na hatimaye kifo cha kishahidi. Wakati akiteseka kifungoni, mke wake na watoto na Watakatifu wengine waliteseka taabu nyingi wakati walipofukuzwa kutoka Missouri.
Wakati Joseph aliposihi kwa ajili ya msaada, Bwana alijibu:
“Mwanangu, amani iwe katika nafsi yako; taabu yako na mateso yako yatakuwa kwa muda mfupi;
“Na halafu, kama utastahimili vyema, Mungu atakuinua juu; nawe utawashinda maadui zako wote” (Mafundisho na Maagano 121:7–8).
Huu ulikuwa ushauri binafsi wa milele, ambao ulimsaidia Nabii Joseph Smith kudumisha hulka yake ya uchangamfu na upendo na uaminifu wa watu wake. Sifa sawa na hizi ziliwaimarisha viongozi na waasisi waliofuatia na zinaweza kuwaimarisha ninyi pia.
Wafikirie waumini wale wa mwanzo! Tena na tena, walifukuzwa kutoka sehemu moja hadi nyingine. Mwishowe walikabiliana na changamoto ya kuanzisha makazi yao na Kanisa nyikani. 5 Miaka miwili baada ya kundi la waasisi wa mwanzo kuwasili katika bonde la Great Salt Lake, mshiko imara kwenye kuendelea kuishi kwa watakatifu katika eneo lile lenye uadui ulikuwa bado hatari. Waumini wengi walikuwa bado njiani wakivuka uwanda au wakihangaika kupata nyenzo za kufanya hivyo. Lakini bado viongozi na waumini walikuwa bado na tumaini na walijipa moyo.
Japokuwa Watakatifu hawakuwa wamejiimarisha katika nyumba zao mpya, kwenye mkutano mkuu wa Oktoba 1849 wimbi jipya la wamisionari lilitumwa Scandanavia, Ufaransa, Ujerumani, Italia, na Pacific ya Kusini. 6 Kwa kile ambacho kingeweza kufikiriwa kuwa kiwango chao cha chini kabisa, waasisi waliinuka kufikia viwango vipya vya juu kabisa. Na punde miaka mitatu baadaye, wengine 98 waliitwa pia kuanza kukusanya Israeli iliyotawanyika. Mmoja wa viongozi wa Kanisa alielezea kwamba misheni hizi “kwa kawaida, sio za kuwa ndefu sana; huenda kuanzia miaka 3 mpaka 7 ndiyo utakuwa muda wa mtu kutokuwepo kwenye familia yake.” 7
Akina Dada, Urais wa Kwanza una wasiwasi kuhusu changamoto zenu. Tunawapenda na kuomba kwa ajili yenu. Wakati huo huo, mara kwa mara tunatoa shukrani kwamba changamoto zetu za kimwili—mbali na matetemeko ya nchi, moto, mafuriko, na vimbunga—mara nyingi ni ndogo kuliko waasisi walizokabiliana nazo.
Katikati ya dhiki, hakikisho la kiungu daima ni “changamkeni, kwa kuwa nitawaongoza. Ufalme ni wenu na baraka zake ni zenu na utajiri wa milele ni wenu” (Mafundisho na Maagano 78:18). Ni kwa jinsi gani hili hutokea? Je, hili lilitokeaje kwa waasisi? Je, ni kwa jinsi gani itatokea kwa wanawake wa Mungu leo? Kwa kufuata kwetu mwongozo wa kinabii, “milango ya kuzimu haitashinda dhidi [yetu],” Bwana alisema kupitia ufunuo mnamo Aprili 1830. “Ndiyo,” Alisema, “… Bwana Mungu atazitawanya nguvu za giza kutoka mbele zako, naye atasababisha mbingu zitetemeke kwa ajili yenu, na kwa utukufu wa jina lake” (Mafundisho na Maagano 21:6). “Msiogope, enyi kundi dogo; tendeni mema; acha dunia na jahanamu ziungane dhidi yenu, kwani kama mmejengwa juu ya mwamba wangu, haziwezi kuwashinda.” (Mafundisho na Maagano 6:34).
Pamoja na ahadi za Mungu, “tunainua” [mioyo yetu] na kushangilia” (Mafundisho na Maagano 25:13), na “kwa nyuso zenye furaha” (Mafundisho na Maagano 59:15), tunasonga mbele kwenye njia ya agano. Wengi wetu hatukabiliani na maamuzi yenye uwiano mkubwa sana, kama kuacha nyumba zetu ili kuwa waasisi kwenye nchi isiyojulikana. Maamuzi yetu kwa kawaida yapo katika utaratibu wa kila siku wa maisha, lakini kama Bwana alivyotuambia, “Msichoke kutenda mema, kwa kuwa mnaijenga misingi ya kazi kubwa. Na kutokana na mambo madogo huja yale yaliyo makuu” (Mafundisho na Maagano 64:33).
Kuna nguvu isiyo na mipaka katika mafundisho ya injili ya urejesho ya Yesu Kristo. Imani yetu imara katika mafundisho hayo huongoza hatua zetu na kutupatia furaha. Inaangaza akili zetu na inatoa nguvu na ujasiri kwenye matendo yetu. Mwongozo huu na mwangaza na nguvu ni tuzo zilizoahidiwa ambazo tumepokea kutoka kwa Baba yetu wa Mbinguni. Kwa kuelewa na kupatanisha maisha yetu na mafundisho hayo, pamoja na zawadi tukufu ya toba, tunaweza kujipa moyo tunapojiweka kwenye njia kuelekea kwenye hatma yetu ya milele—kuungana tena na kuinuliwa pamoja na wazazi wetu wa mbinguni wenye upendo.
“Unaweza kuwa unakabiliana na changamoto ngumu,” Mzee Richard G. Scott alifundisha. “Wakati mwingine zinakuwa nyingi, zisizokoma, kwamba unaweza kuhisi ziko nje ya uwezo wako kuzidhibiti. Usikabiliane na ulimwengu peke yako. “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe’ [Mithali 3:5]. … Ilikusudiwa kwamba maisha yawe yenye changamoto, si kwamba uweze kushindwa, bali kwamba uweze kufanikiwa kupitia kushinda.” 8
Hii yote ni sehemu ya mpango wa Mungu baba na Mwanaye, Yesu Kristo, ambao juu yao ninashuhudia, ninapoomba kwamba sote tuendelee mpaka ukomo wa mbinguni, katika jina la Yesu Kristo, amina.